Unaotakiwa ni ujabari kuwang’oa mafisadi wa CCM…

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mawazo mazito

Ahmed Rajab

SI kweli kwamba Bwana Mkubwa Kabisa nchini Tanzania ana sikio la kufa. Akitaka kusikia anasikia. Hivyo ndivyo alivyofanya baada ya kushauriwa na mawaziri wakuu wa zamani Jaji Joseph Warioba na Dk. Salim Ahmed Salim kuwa Serikali yake inapaswa ikutane na wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuzungumzia mustakbali wa mchakato wa kupata katiba mpya ya Tanzania. Ni muhimu maoni ya CHADEMA yasikilizwe kwa vile ni chama kikuu cha upinzani nchini.

Wazee hao wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM) walitoa rai yao baada ya CHADEMA kujitoa bungeni wakati wa mjadala kuhusu Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011.

Baada ya kelele nyingi za CHADEMA na ushauri wa akina Salim na Warioba hatimaye wiki iliyopita viongozi wa CHADEMA walikaribishwa Ikulu kutoa joto lao kuhusu mchakato wa katiba mpya. Zamu ya wawakilishi wa chama kingine cha upinzani cha Civic United Front (CUF) ikafuatia baadaye.

Baada ya kuyasikiliza maoni ya vyama hivyo vya upinzani kuhusu mchakato wa kuleta katiba mpya, mkazi wa sasa wa Ikulu aliutia saini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kitendo hicho kiliwafanya viongozi wa CHADEMA waruke na waanze kulalamika kwamba Bwana Mkubwa Kabisa ‘amewauza’. Kwa kusema hivyo waliashiria kuwa aliwaendea kinyume, kwamba alivyotenda sivyo walivyokubaliana.

Ikiwa shutuma hiyo ina ukweli basi inaonyesha kwamba Taifa hili lina kiongozi asiyeweza kutabirika na wengine watasema ‘wala asiyeweza kuaminika.’ Sijui kama hilo ni jema au la.

Ninawaachia wataalamu wa saikolojia ya kisiasa wakune vichwa na kushindana iwapo hizo ni sifa ama ni ila kiongozi wa kisiasa kuwa nazo. Siasa zinaweza kuwa mchezo mchafu na zinapokuwa hivyo mara nyingi ila hugeuka na kuwa sifa na uadilifu huwa ni sawa na laana.

Kuna sifa moja lakini ambayo kiongozi wa kisiasa aliye imara na mwenye kujiamini lazima awe nayo. Hiyo ni sifa ya kutokuwa na woga wa kukata maamuzi magumu pale maamuzi aina hiyo yanapohitajika. Bahati mbaya kwa Taifa hili wiki mbili hizi zilizopita ilionekana bayana kwamba Bwana Mkubwa ana taksiri ya kutokuwa jasiri katika kuwachukulia hatua wanaostahili kuchukuliwa hatua.

Hapa tunawakusudia wanaotuhumiwa kwa ufisadi na kuhusu hili si wanachama wa CCM peke yao bali Taifa zima linamtaka mwenyekiti wa chama hicho awachukulie hatua kama alivyoahidi. Taifa linataka wachukuliwe hatua kwa sababu wakorofi hao si nuksi kwa chama chao tu bali kwa nchi nzima.

Kuna uwekezekano kwamba labda mwenyekiti hakuwachukulia hatua kwa sababu anataka aonekana kwamba ni mtu asiyepuuza kanuni na utaratibu wa CCM. Kuna uwezekano aidha kwamba labda anazificha kucha zake kwa sasa na kwamba huenda baadaye akaja kutushangaza kwa hatua kali atazochukuwa dhidi ya wanaokipa jina baya chama chake na taifa zima kwa laana zao za ufisadi.

Hayo ni matumaini lakini ni matumaini tu na kwa kweli si wengi wenye kuyatarajia. Vikao vya vyombo vikuu vya CCM yaani Halmashauri Kuu ya Taifa na Kamati Kuu vilivyofanywa mnamo muda wa wiki mbili zilizopita huko Dodoma vimedhihirisha wazi kuwa mwenyekiti wa chama hicho hana ujabari au moyo wa kukata maamuzi magumu. Akhasi zaidi vimeonyesha kwamba anaweza akatikiswa na mahasimu zake na akatikisika, akaanza kuyumbayumba.

Hilo pengo kubwa la maamuzi ya ngazi ya juu kabisa ndani ya chama hicho limezusha kioja. Kilichotokea katika kadhia ya wale waliotakiwa kujivua gamba ni kwa vyombo hivyo vikuu vya CCM kutupiana mpira. Ilikuwa mithili ya mchezo wa ping pong. Mara mpira unarushwa huku, mara unarudishwa upande wa pili.

Yote hayo yasingalitokea laiti pangekuwa na uongozi imara, uongozi ulio jasiri, usio na woga na usiotetereka. Laiti pangelikuwako na uongozi kama wa Mwalimu Julius Nyerere, uongozi wa kuwa na ujasiri wa kuamua hata kama uamuzi huo usingeliwafurahisha wengi.

Uongozi sampuli hiyo ni uongozi mahiri, ni uongozi wa kubeba jukumu la dhamana aliyo nayo kiongozi kwa ujasiri. Hivyo ndivyo kiongozi anavyotakiwa awe. Aweze kukata uamuzi na ikihitajika awe tayari kujieleza kwa nini ameukata uamuzi unaohusika.

Nyerere alionyesha ujasiri aina hiyo alipowafukuza kutoka TANU akina Chifu Abdallah Fundikira na rafiki yake wa zamani Joseph Kasella-Bantu.

Haikunishangaza niliposikia kwamba Rais mstaafu Benjamin Mkapa ndiye aliyekuwa akituliza mambo wakati moto ulipopamba katika kikao kizito cha Halmashauri Kuu pale Bwana Mkubwa Kabisa alipokuwa akisulubishwa na aliyekuwa waziri mkuu na mbunge wa Monduli Edward Lowassa, mmoja wa wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Kwenye kikao hicho Bwana Mkubwa aligeuzwa chambo na kuwekwa rehani. Hakuweza kujitetea wala kukemea lolote. Alichofanya ni kumpa nafasi Mkapa na kumfanya kama mwenyekiti wake mwenza. Swali linalozuka ni: nani hasa mwenyekiti wa CCM na anawajibika kwa nani?

Nilijikuta nikitabasamu nilipokuwa nikisoma jinsi Mkapa alivyokuwa akiingiliaingilia kati kumuokoa Bwana Mkubwa. Nilikumbuka alipokuwa akiandamwa na magazeti kuhusu shtuma za kuhusika kwake na masuala kadha wa kadha yaliyoonekana kama ni ya ukiukaji wa maadili kwa kiongozi.

Kati ya masuala hayo ni pamoja na madai ya ununuzi wa mgodi wa makaa na hata kisa cha EPA. Mkapa alijaribu kuyapiga chenga magazeti kwa kusema kwamba sasa yeye anajihusisha na mambo ya Kanisa na hatozungumzia siasa. Kwa hivyo, nilitabasamu kuona ghafla ameibuka na mori wa siasa umemuingia tena kwa kuanza kumuongoza mwenyekiti wa chama chake katika vikao vyao vya wiki mbili zilizopita.

Inasemekana kwamba moja ya aliyoyafanya Mkapa ni kumshauri mwenyekiti awazuie wajumbe walionyosha mikono kutaka kuchangia katika mjadala huo. Hivyo Kingunge Ngombale-Mwiru aliyekuwa ubavuni mwa Lowassa wakati wote alinyimwa nafasi ya kuzungumza.

Walio jikoni wanasema kulikuwa na hofu kwamba mwanasiasa huyo mkongwe angempigia debe kijana wake Lowassa anayemfahamu vizuri kwani Ngombale ndiye aliyemlea kisiasa Lowassa pamoja na mwenyekiti wa sasa wa CCM walipokuwa katika Umoja wa Vijana.

Hofu iliyokuwako ni kwamba lau Ngombale angefungua mdomo wake angeongeza mafuta kwenye moto na kuupalilia, moto ambao mwenyekiti alionekana alishindwa kuuzima. Si kwamba hakuweza kuuzima lakini labda akiogopa.

Karata ya Mkapa ilikuwa turufu kwa wahusika wote; hali kadhalika aliitumia kujinusuru mwenyewe na wimbi lionalovuma linalotishia kuwagharikisha wanaotuhumiwa kwa ufisadi. Ndipo alipomalizikia kuwa pande zote mbili, mguu mmoja huku mguu mwingine huku.

Sina haja ya kujadili iwapo kweli Mkapa ni msafi safina, ‘Mr Clean’, kama alivyobatizwa na Nyerere au la. Ninachoweza kusema lakini ni kuwa lau Nyerere angecheza bahati nasibu kwa hilo basi angelipoteza dau lake. Inavyosemekana ni kwamba alipostaafu urais alhamdulillahi Mkapa hakuondokea patupu.

Hata hivyo, amestaafu akiandamwa na vivuli vya EPA, ununuzi wa migodi ya makaa na vya mazingaombwe mengine. Angalia hali binafsi ya Nyerere baada ya miaka 25 ya urais au ile ya rais aliyemfuatia Sheikh Ali Hassan Mwinyi baada ya miaka 10 ya kuwa Ikulu. Zilinganishe hali za hao wawili na zile za Mabwana Wakubwa waliowafuatia.

Suala la kujivua gamba ndani ya CCM — la kukisafisha chama hicho — lina umuhimu mkubwa kwa sababu hamna shaka yoyote kwamba namna litavyohitimishwa litatoa sura kamili ya kule CCM inakoelekea kufikia 2015. Ishara zilizopo ni kwamba inaelekea pabaya.

Huu mvutano unaoendelea sasa, na suala zima la chama hicho kutaka kijisafishe, ni duru ya mwanzo tu ya mchuano mrefu utaofikia kilele pale chama hicho kitapomchagua mgombea wake wa urais katika uchaguzi ujao wa mwaka 2015.

Si siri kuwa miongo miwili iliyopita baadhi ya wanaotikisa kibiriti cha CCM hivi sasa wakiwemo makamu mwenyekiti wa chama hicho Pius Msekwa na Lowassa walitajwa na Mwalimu Nyerere kuwa watu wasiofaa ilipoonekana kama wana tamaa ya kuuwania urais. Swali ni kwa nini Nyerere alikuwa na uhakika huo? Madaftari aliyokuwa nayo kuwahusu hao wasiofaa yalikuwa na maelezo gani?

Labda Nyerere aliwang’amua mapema na labda aliona mbali. Vyovyote ilivyokuwa kauli yake iliwafanya wasithubutu kufurukuta wakati wa uhai wake. Swali jingine linazuka. Nalo ni: ikiwa hawakufaa wakati ule kipi kinachowafanya wafae hivi sasa?

Chanzo ni Raia Mwema

.

One response to “Unaotakiwa ni ujabari kuwang’oa mafisadi wa CCM…

  1. siasa kila siku nimchezo mchafu nakuwa mwana siasa ukamaliza kwa amani umebahatika ndio mana viongozi wengi wanamalizia kuuwawa au kwenda jela kwa ccm viongozi wao wanaelekea huko huko kwa juu ya matamanio ya utawala na wizi wa mali za waajiri wao ,wananchi amkeni kama nyinyi ni waajiri ndio munaweza kuwatoa madarakani na kuwaajiri wengine kwa kuvoti kwa wapizani na kuwajiri kukufanyieni kazi lazima wananci muondoke na zana kuwa bila ccm tumekwisha laa na wapizani ni watanzania vile vile.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s