Upinzani mkubwa Zanzibar kwa wenye kutaka serikali moja

 

Vijana kutoka taasisi mbali mbali wakifuatilia majadala wa mchakato wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huko Zanzibar

Na Ahmed Rajab
KWA vile Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba umepitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, muswada huo utatekelezwa mara tu utapomalizika mchakato wa kuufanya uwe sheria kamili.Muswada huo ambao ni muhimu sana kwa watu wa Tanganyika na wa Zanzibar kwa vile utaamua mustakabali wa nchi zao mbili, utatekelezwa kwa mujibu wa ratiba au jedwali itayowekwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kati ya taasisi zote zitazoundwa katika utekelezwaji wa mchakato wa kuiandika upya Katiba mpya ya Muungano, iliyo na umuhimu mkubwa ni ile tume ya wajumbe 30 itakayokuwa na idadi sawa ya wawakilishi kutoka Tanganyika na Zanzibar.

Hii ndiyo taasisi itayoongoza kupanga na kusimamia huo mchakato mzima. Hali kadhalika itatoa mapendekezo itayokuwanayo juu ya misingi ya mizingo au vigezo na miongozo itayotangazwa na Rais wa Muungano baada ya kushauriana na Rais wa Zanzibar na pia kupata ridhaa yake.

Miongoni mwa majukumu muhimu sana ya tume au kamisheni hiyo itakuwa ni kazi ya kuuongoza mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi katika ngazi za chini kabisa za taifa hili. Huko Zanzibar kazi hiyo itafanyika katika ngazi ya shehia ambapo Wazanzibari watatakiwa watoe maoni yao kuhusu mwelekeo ujao wa nchi yao na pia kuhusu Muungano na Tanganyika.

Kwa mfano, wale watakaohudhuria mikutano itakayofanywa kwenye shehia zao huko Zanzibar au wataopeleka taarifa zao kwa maandishi kwenye kamisheni au kwa wao wenyewe kuhudhuria mbele ya kamisheni watakuwa na uwezo wa kutoa maoni yao kwa uhuru kabisa bila ya hofu.

Hali ya mambo haitokuwa tena kama zamani ambapo kaka mkubwa alikuwa akiongoza, akiangalia na hatimaye akijiamulia kuhusu ya sasa na yajayo ya Jamhuri ya Muungano. Kwa kufanya hivyo, kaka mkubwa alikuwa akiamua kuhusu mustakabali wa Tanganyika na ule wa Zanzibar, nchi huru zilizoungana mwaka 1964.

Vifungu vya muswada huu vinavyotaka pawepo na uwakilishi ulio sawa na ushiriki ulio sawa katika kufikia uamuzi katika mchakato huu vinaitambua ile kanuni ya kimsingi ya uhuru na mamlaka ya nchi hizo mbili pamoja na usawa wao. Utambuzi huo ni juu ya msingi wa kanuni za sheria za kimataifa pamoja na sheria za taifa hili.

Ninasema hivi kwa sababu Hati za Muungano ni mkataba wa kimataifa. Nathubutu pia kuongeza kwamba Hati hizo za Muungano ndizo nyaraka zilizo muhimu kushinda zote zilizotajwa kuhusika na historia ya utungwaji wa Katiba nchini Tanzania.

Tuwe wakweli pia na tukumbuke kwamba utungwaji wa Katiba nchini humu umeihusisha zaidi Tanganyika. Historia inakanushwa kwa kupuuzwa kama haipo ile Katiba ya Uhuru wa Zanzibar ya mwaka 1963, iliyopatikana baada ya mashauriano huko Lancaster House mjini London kati ya vyama; Zanzibar Nationalist Party na Afro-Shirazi Party.

Hali kadhalika, siku ya uhuru wa Zanzibar — Desemba 10, mwaka 1963 — baada ya miaka 70 ya ukoloni wa Uingereza haitambuliwi ingawa siku ya uhuru wa Tanganyika inaadhimishwa na kusherehekewa kuwa ni Sikukuu ya Kitaifa ya Tanzania.

Katika kuizingatia ripoti yake kamisheni inapaswa kuyatia maanani “maoni yanayolingana na yanayokinzana katika sehemu zote mbili za Jamhuri ya Muungano” (yaani Tanganyika na Zanzibar) kuhusu mustakabali wa Muungano.

Itapoangalia dhana nzima ya Muungano ama muundo wake itaona kwamba kuna ukinzani mkubwa kati ya wanachodai Wazanzibari na msimamo rasmi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Kwa bahati mbaya ni taabu kuutaja msimamo wa Watanganyika kuhusu Muungano, na iwapo wanapendelea waendelee nao au wauvunje. Ni taabu kwa sababu inavyoonyesha ni kwamba msimamo rasmi na wa wengi huko Bara katika muda wote huu wa miaka 47 ya Muungano ni kuwa Zanzibar ni mzigo kwa Tanganyika.

Tusisahau kwamba hali hiyo ilikuwa na ukweli katika kipindi kifupi sana cha historia ya Visiwani pale ilipokuwa kawaida kwa wanadamu kuwatesa wanadamu wenzao, pale wananchi walipokuwa wakinyimwa uhuru wao wa kimsingi na pale nchi hiyo ilipokuwa ikiongozwa na mtu mmoja. Kwa hakika, yaliyokuwa yakitokea Zanzibar kabla ya mwaka 1972 yameutia dosari uungwana na utu wa Mwalimu Julius Nyerere na pia yameitia dosari Tanzania.

Kamisheni yenye jukumu la kuichunguza na kuirekebisha Katiba imepewa mamlaka makubwa na lazima pachukuliwe hadhari wanapoteuliwa wajumbe wake na uongozi wake. Ni muhimu kwamba iwe huru na isifungamane na Serikali. Pia itambue kwamba itakabiliwa na changamoto nyingi kabla ya kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Atapoipata Rasimu hiyo, Rais ataunda Bunge la Katiba kwa masharti yaliyomo kwenye Muswada wa Mabadiliko ya Katiba. Zanzibar itakuwa na asilimia 30 ya wajumbe kwenye Bunge hilo. Muhimu ni kwamba wajumbe wa Tanganyika na wale wa Zanzibar watapiga kura mbalimbali si kwa pamoja. Na kila upande utahitaji upate ridhaa ya wingi wa theluthi mbili ya wajumbe wake ili rasimu hiyo ya Katiba iweze kufikishwa kwa wananchi watoe uamuzi wao kwenye kura ya maoni.

Kwa Zanzibar hiyo kura ya maoni itasimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na rasimu ya Katiba itapita endapo Wazanzibari wengi wataikubali.
Panaweza pakazuka mgogoro wa kisiasa ikiwa, kwa mfano, upande mmoja utaikataa hiyo rasimu ya Katiba mpya. Mgogoro huo utaweza kutanzuliwa kwa vile Katiba ya kale (yaani hii ya sasa) ya mwaka 1977, itaendelea kufanya kazi.

Hatua hiyo itakuwa ni ya suluhisho la kisheria tu kwani matatizo ya kisiasa kuhusu mustakbali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yatabidi yatanzuliwe kwa njia ya kirafiki kati ya Tanganyika na Zanzibar, tukikumbuka kwamba katika demokrasia ni matakwa ya watu yaliyo juu na yenye kutawala.
Inapaswa pia wakubwa wakumbuke ya kuwa kinyume cha miaka ya nyuma watu hawana tena hofu visiwani Zanzibar. Vilevile kinyume cha miaka ya nyuma vyama vya kisiasa vyenye matawi yao Zanzibar haviwezi tena kuwafukuza wenzao wa Visiwani au kuwatisha. Wala wale wenye kutokubaliana na msimamo rasmi wa kisiasa au wa kiitikadi hawafikiriwi tena kuwa ni wahaini wa Taifa la Tanzania.

Hivyo inatia moyo kuona kwamba Wazanzibari kwa mara ya kwanza katika historia yao ndani ya Muungano na Tanganyika, wamepewa haki yao ya kuwa washirika sawa. Pongezi ni kwa Wazanzibari wote na hasa viongozi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, na wale wenye kuhusika na mambo ya kikatiba na kisheria ambao kwa mara ya kwanza wametoa mapendekezo yanayolinda maslahi ya nchi yao.

Kuna hofu Zanzibar kuhusu namna kura ya maoni itavyoendeshwa na jinsi orodha ya kudumu ya wapigaji kura itavyotumiwa. Pia kuna manung’uniko mengi kuhusu kutolewa kwa vitambulisho vya ukaazi. Hofu iliyopo ni kwamba wasio Wazanzibari huenda pia wakashiriki kwenye kura ya maoni ijapokuwa sheria inasema wazi kwamba kutakuwa na kura mbili za maoni: moja kwa Watanganyika na nyingine kwa Wazanzibari.

Msimu wa kampeni umekwishaanza na kuna wengi Visiwani ambao wamekwishafikiria masharti magumu kuhusu Muungano na muundo wake wa baadaye na iwapo uendelee kama ulivyo sasa au la. Hili linapingwa na Wazanzibari wengi lakini inavyoonyesha ni kwamba viongozi wa Tanganyika wangependelea uendelee ulivyo, na pengine, hata baadaye, kuitimiza ndoto yao ya kuwa na serikali moja tu kwa sehemu zote mbili za Muungano, yaani Tanganyika na Zanzibar.

CHANZO: RAIA MWEMA

3 responses to “Upinzani mkubwa Zanzibar kwa wenye kutaka serikali moja

 1. Kuhusu kusherehekewa / Kutosherehekewa kwa kushushwa kwa bendera ya Uigereza tarehe 10 disember 1963.
  Ni wazi kabisa serikali ya Mapinduzi Zanzibar,kutoutambua uhuru wa siku hiyo kwa sababu ya “WIZI WA UGAWAJI
  WA MAJIMBO NA IDADI YA WAPIGGAJI KURA WA UHAGUZI WA MWISHO”.Afro-Shirazi ilishinda kwa wingi wa kura
  za wananchi,ugawaji wa majimbo yalipendelea ZNP , na kwa hivyo ,Uhalali wa Utawala wa ZNP/ZPPP haujakubalika
  na wale waliokuwa wengi na ndio moja wapo wa sababu nyingi za MAPINDUZI ya january 12 ,1964.

  Kwa hivyo ,kinyume na Uhuru wa Tanganyika tarehe 9 Disemba- Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kusherehekea
  kushushwa kwa bendera ya Uingereza na kule kupandishwa bendera ya ZNP-Usultani , itakuwa kama unawambia
  wananhi wa Zimbabwe – kusherehekea UDI -ya Ian Smith au Wapelestina kusherehekea 1948 wakati Mazionists
  kukubaliana na Uingereza kuigawa Palestina na kukubaliwa rasmi kwa Israel katika Umoja wa Mataifa, au kuwaambia
  akina Nielson Mandela na wananchi wa South Africa kusherehekea1913 au 1948 wakati Boers/Makaburu wa huko
  walipo tangaza rasmi umoja /Union of South Africa au siku ya utangazaji wao wa siasa ya Apartheid .

  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,endapo itasherehekea Disemba 10,1963 -itakuwa nisawa na kunajinisha uchukuwaji
  wa madaraka na Mapinduzi ya 1964. Atakae fanya hayo ni nani Shani ,Seif Sharif au Baraza la Wawakilishi na ndoto
  hiyo lini itaweza kukamilishwa ?

 2. ZANZIBAR BILA YA KUPATA UHURU HAIWEZI KUENDELEA. Jee viongozi wa smz wanafanya nini kila siku bungeni wazanzibari wanatukanwa na kuambiwa ZANZIBAR SI NCHI. Hakika muungano hauna faida kwa wazanzibar.

 3. Suala la kua :Zanzibar ni nchi au sio nchi?
  Kwa kweli ni maneno ya kiuhokozi,na maneno hayo husemwa aidha na Wanasiasa au na Wapinzaani wa Muungano kwa sababu mbali mbali.

  Baadhi ya Watanganyika nao,wanajiuliza Tanganyika ipo au haipo ? Wanasema hivyo
  kwa sababu wanajiuliza .(a) Mbona Zanzibar inayo Rais ,Serikali,Mawaziri wake,inayo
  bendera yake,inayo wimbo wa dola lakini Tanganyika haina ?
  (b) Kwa nini Rais wa Zanzibar ana nguvu sawa na Rais wa Tanzania (Muungano) katika
  kuamua mambo ya ndani ya Tanganyika wakati Tanaganyika haina Rais wake ?
  (c) Kwa nini pasiwe na Marais na Serikali tatu ?

  Inasemekana kwamba mara tu baada ya Mzee Abeid Amani Karume ,na Mwalimu Julius
  Kambarage Nyerere,kutia sahihi hati ya kuunganisha nchi mbili huru ,yaani Zanzibar na
  Tanganyika – na kua Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Mstaaafu Aboud Jumbe,
  alimuuliza Marehemu Karume ” Mbona Zanzibar inayo serikali na Rais wake,lakini wenzetu
  Tanganyika hawana ?”.
  Mzee Karume ,alijibu kwa kusema “Ikiwa hawataki,si shauri yao”.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s