Zanzibar, nchi kwanza, Katiba mpya baadaye

Wanafunzi wa vyuo vikuu wakisikiliza mjadala kuhusu katiba mpya huko katika chuo cha ualimu Beit Al Raas Mjini Unguja

Kinachobainika sasa Maalim atahamsisha hoja hiyo katika Mikutano yake inayoendelea mwishoni mwa wiki katika Majimbo ya Wingwi, Micheweni na Mgogoni Mkoa wa Kaskazini, Pemba.

Zanzibar, nchi kwanza, Katiba mpya baadaye *Maalim Seif azidi kuwasha moto

Na Mwandishi Wetu
Joto la kudai nchi na mfumo mpya wa muungano linazidi kupanda Zanzibar.
Kinachobainika hivi sasa ni kuwa, wakati katika Tanzania (Bara) kilio ni kutaka katiba mpya, kwa Zanzibar zoezi hilo linaonekana halina maana kama halitarejesha heshma ya visiwa hivyo ya kuwa nchi na Dola kamili.

Kwa kuisoma na kuielewa hali hiyo, Makamu wa Kwanza wa serikali ya Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, ametoa wito kwa Wazanzibari kuitumia vyema fursa ya mjadala wa katiba mpya ili kuhakikisha kuwa yote wanayoyataka yanapatikana.

Maalim amekuwa akitoa wito huo katika ziara zake anazoendelea kuzifanya katika mikoa na wilaya za Unguja.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amewataka Wazanzibari waungane na kuwa na kauli moja wakati wa kutoa maoni juu ya Katiba mpya ili kupata mfumo wa Muungano wanaoutaka.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema hayo juzi wakati akihutubia mkutano wa hadhara Donge Mchangani katika Wilaya ya Kaskazini B Unguja.

Maalim Seif amesema hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, atateua wajumbe wa Tume ya Kuchukua Maoni kwa wananchi juu ya Katiba mpya wanayoitaka ambapo wananchi wa Zanzibar na wa Tanzania Bara watapata fursa sawa za kutoa maoni yao.

Akasema, katika hatua hiyo iwapo Wazanzibari watakuwa na kauli moja kuhusu mambo wanayotaka yawemo au yasiwemo kwenye Katiba hiyo, Tanzania Bara hawatokuwa na njia nyingine isipokuwa kukubaliana na maoni ya Wazanzibari.

Alifafanua kuwa iwapo Wazanzibar watatofautiana na kukosa msimamo, inaweza kuwaathiri kupata kile wanachokihitaji.

“Hii ni fursa adhimu kwa Wazanzibari kupata mambo wanayoyataka ndani ya Jamhuri ya Muungano ikiwemo mfumo wa Muungano wenye maslahi kwa Zanzibar,” alisema Maalim Seif.

Maalim Seif ambaye pia alitembelea majimbo ya Kitope na Bumbwini, amesisitiza kuwa hiyo ni fursa pekee kwa Wazanzibari kuamua hatima ya nchi yao.

Kinachobainika sasa Maalim atahamsisha hoja hiyo katika Mikutano yake inayoendelea mwishoni mwa wiki katika Majimbo ya Wingwi, Micheweni na Mgogoni Mkoa wa Kaskazini, Pemba.

Kwa upande mwingine, Maalim Seif aliwataka wananchi kuendelea kuhifadhi mazingira ili kuvirithisha vizazi vijavyo nchi yenye misitu na neema.

Alisema iwapo juhudi za makusudi hazitochukuliwa, kuna hatari kwa vizazi vijavyo kurithishwa nchi ikiwa jangwa, hali ambayo itazorotesha shughuli zao za maendeleo.

Aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuacha kabisa tabia ya ukataji miti ovyo na kuongeza juhudi katika upandaji wa miti mbalimbali ikiwemo ya matunda ili

kuimarisha rasilimali ya misitu ambayo ni hazina muhimu kwa maendeleo ya Taifa. Alisema kuwepo kwa miti mingi kutasaidia kwa kikasi kikubwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa yakiathiri visiwa vya Zanzibar kwa kukosa mvua kwa wakati, kuathiri vyanzo vya maji na kupoteza rutuba na haiba ya visiwa vya Zanzibar.

Akizungumzia kuhusu dawa za kulevya, Maalim Seif aliwataka wananchi kuvihifadhi vijiji vyao na tatizo hilo, kwa vile athari zake zinakuwa kubwa hasa kwa vijana na kupelekea kupoteza nguvu kazi ya taifa.

“Wenyewe wanavijiji tukiamua kudhibiti dawa za kulevya haziingii. Kweli, uongo,” alihoji Maalim Seif.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari, Uenezi, Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani amewasisitiza wananchi wa maeneo hayo kufuatilia vitambulisho vya Uzanzibari ukaazi, ili kuhakikisha kuwa wanavipata na kuvitumia kwa shughuli mbalimbali za siasa na kimaendeleo.

Kwa mujibu wa Bimani, wananchi wengi hasa wa Jimbo la Bumbwini hawajachukua vitambulisho vyao, licha ya vitambulisho hivyo kuweko katika mamlaka zinazohusika na vitambulisho hivyo
Wadadisi wa mambo wanasema kuwa, kinachobainika sasa ni mwelekeo wa kauli moja kwa wananchi wa Zanzibar kusimama juu ya madai ya kupigania kuirejesha Dola yao huru kabla ya hata mijadala ya Mabadiliko ya Katiba.

Msimamo huu unaonekana kupitia majukwaa mbali mbali ya mijadala ya hivi karibuni likiwamo Kongamano la Ukumbi wa Zamani wa Baraza la Wawakilishi, Mnazi Mmoja Mjini hapa.

Katika kongamano hilo, viongozi wa itikadi na vyama tafauti vya siasa walisimama na kwa kauli moja waliamua kuhamasisha utetezi wa nchi kulikoni majadiliano ya muundo wa muungano.

“Nawaomba pamoja na sera zetu za vyama waheshimiwa tusahau yote hayo muhimu tunahitaji Wazanzibari wote tudai Dola yetu huru, hapa hatuhitaji muungano kwanza”, alisema Bw. Massoud Juma mmoja wa Viongozi wa Ngazi za Juu wa CHADEMA Zanzibar, katika kauli iliyoungwa mkono na Naibu Katibu wake Mkuu Hamad Mussa, upande wa ZanzibaR.

Msimamo kama huo ulitolewa hivi karibuni na Waziri wa Katiba wa Zanzibar, Abubakar Khamis Bakar, akitoa ufafanuzi hapa juu ya umuhimu wa Wazanzibari kushikamana katika kudai maslahi ya nchi yao sasa.

Kinachoonekana sasa madai haya yataendelea na kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi yatamfikia Rais Kiwete wakati atakapokutana na Manaibu Katibu wa CUF Taifa Ismail Jussa na Julius Mttatiro, Ikulu Dar es Salaam.

Chanzo Gazeti la Ann.Nuur

Advertisements

One response to “Zanzibar, nchi kwanza, Katiba mpya baadaye

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s