Al Shabab bandia aponza Waislam

Kijana huyo Hassan Jumanne Hassan ndiye alionekana kama mtuhumiwa mkuu kwa sababu ndiye alimpokea kijana kutoka Uganda ambaye alidai kuwa anatokea Somalia akiwa mtaalamu wa masuala ya kijeshi.

Al Shabab bandia aponza Waislam

*Imam afikishwa matesoni Kigoso, Kirumba
*Waislamu wapongeza Polisi kwa umakini

Vijana wa Kiislamu waliokuwa wamekamatwa wakihusishwa na harakati za Al Shabaab wameachiwa huru.
Wameachiwa baada ya kugundulika kuwa, hawana wanachojua kuhusu Al Shabaab ila ni watu mashabiki tu ambao walinaswa na mtego wa ‘Al Shabaab bandia’ kutoka Uganda.

Hata hivyo, haikuwa kazi nyepesi kwani mmoja wa watuhumiwa hao alifikishwa hadi kituo cha mahojiano kinachotajwa kwa utesaji, Kigoso, Kirumba akitakiwa kueleza uhusiano wake na Al Shabaab.Kijana huyo Hassan Jumanne Hassan ndiye alionekana kama mtuhumiwa mkuu kwa sababu ndiye alimpokea kijana kutoka Uganda ambaye alidai kuwa anatokea Somalia akiwa mtaalamu wa masuala ya kijeshi.

Hassan ni Khatib katika msikiti wa Buzuruga, Nyakato na mara kadhaa huwa mawaidha yake hugusia masuala ya Al Shabaab.Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana kutoka Mwanza, polisi wamewaachia vijana hao baada ya kugundua hawana uhusiano wowote, wala hawana wanalojua juu ya Al Shabaab zaidi ya taarifa wanazopata juu ya suala hilo kupitia vyombo vya habari.

Imeelezwa kuwa upo wasiwasi mkubwa kuwa yule Mganda aliyedai kuwa aliharibikiwa akitokea Somalia, huenda ni Al Shabaab wa kupandikiza aliyetumiwa kuwanasa vijana wa Kiislamu. “Mazingira ya kufika kijana yule na alivyojitambulisha kuwa anatoka Somalia akiwa mtaalamu wa kijeshi na alivyotoweka, kuna kila sababu ya kuamini kuwa kulikuwa na mchezo, kulikuwa na usanii wa kuwanasa Waislamu na kuwapachika u-Al Shabaab”, amesema mzee mmoja wa jijini Mwanza.

Akijibu ni kwa nini ilionekana mtego uletwe katika msikiti wa Buzuruga alisema kuwa, kijana Hassan aliyekamatwa huwa ana kawaida ya kutoa mawaidha akizungumzia harakati za makafiri kuhujumu Uislamu na baadhi ya wakati akigusia masuala ya Al Shabaab na Al Qaida.

“Nahisi, ikiwa ni kweli ilikuwa mchezo, ilionekana kuwa Khatibu yule ni katika watu wanaoweza kwa wepesi kabisa kuwakubali na kuwapokea watu watakaojitambulisha kuwa ni wanaharakati kama Al Shabaab.” Alisema.Hata hivyo Mzee huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Khalid alisema kuwa anawapongeza polisi kwa kufanya kazi yao kwa uhodari na umakini mkubwa.

“Kama ni mchezo, naamini kuwa polisi wetu hawapo katika mchezo ule, vinginevyo vijana wetu wasingeachiwa, lakini inavyoonekana kuwa watu wanataka kututosa katika tope la Al Shabaab, polisi wamefanya kazi yao kitaalamu kabisa, hili ni jambo la kushukuru.” Aliongeza.

“Naamini polisi na vyombo vyetu vya usalama ni makini, walichosema wakiwaachia vijana wale, ndio ukweli wenyewe, vijana wale hawana wanalojua zaidi ya haya wanayosoma na kusikia katika televisheni na redio.”

Habari zaidi zinaonesha kuwa ujio wa kijana yule aliyejitangaza kuwa ni msafiri aliyeharibikiwa na kutaka msaada kwa Waislamu, unaacha maswali mengi na kitendawili ambacho hakijapatiwa jibu la uhakika.

Hata hivyo, kila watu wakitafakari alivyokuja na aliyosema Msikitini na alivyoingia mitaani na kisha kutoweka baada ya kujizoesha na kujikurubisha kwa Hassan ambaye baadae alikamatwa kama mtuhumiwa namba moja, inaleta shaka kuwa huenda alikuja kuweka mtego.

Kutokana na wasiwasi huo, baadhi ya watu wamesema kuwa kuna haja ya vijana na jamii ya Kiislamu kwa ujumla kuwa makini zaidi. Swali ambalo bado Waislamu wa Mwanza hawajalipatia jawabu ni je, kama ni kutumwa, Mganda yule Al Shabaab bandia katumwa na nani?

Wiki iliyopita gazeti hili liliripoti kukamatwa vijana wanne wa Kiislamu wakituhumiwa kuhusika na kundi la Al Shabaab.
Habari hiyo ilisema kuwa kamata kamata hiyo ilitanguliwa na kilichoonekana kuwa mtego na mchezo wa kupanga ambapo kijana mmoja aliyejitambulisha kutoka Uganda alifika katika msikiti wa Buzuruga, Nyakato akitaka kusaidiwa kama msafiri aliyeharibikiwa.

Kijana huyo alidai kuwa alikuwa akitokea Somalia na aliharibikiwa na hivyo kutaka sadaka za Waislamu ili aweze kuendelea na safari kurudi nyumbani, Uganda. Taarifa zaidi zilisema kuwa kijana huyo alijitaja kama mtaalamu wa masuala ya kijeshi na ufundi wa aina mbalimbali, ila hakufafanua utaalamu huo alikuwa akiutumia vipi huko Somalia.
Kwa upande mwingine kwa jinsi alivyojiweka na Waislamu na kuonekana kama mwana-Da’wah, kijana mmoja Omar, maarufu Osamah wa Nyakato alimkaribisha akae nyumbani kwake kwa muda.

Hata hivyo, ghafla kijana huyo alitoweka na kamata kamata ikaanza kuwakamata waliokuwa marafiki na waliomfadhili kijana huyo wa Uganda. Zaidi habari hiyo ilisema kuwa, hadithi ya kijana huyu mtaalamu wa kijeshi na mujahidina wa Uganda inakuja wakati kashfa ya kupanga vitendo vya kigaidi inazidi kuiandama Idara ya ukachero ya Marekani-FBI.
Kwa mujubu wa taarifa iliyoandikwa na gazeti la Guardian (Uingereza) la Novemba 16, 2011, mchezo huu wa FBI umemkumba David Williams ambaye amejikuta akihukumiwa kifungo cha miaka 25 jela kwa kosa la kutaka kufanya kitendo Cha kigaidi kulipua hekalu la Mayahudi New York pamoja na kulipua ndege ya kijeshi kwa kombora.

Kwa mujibu wa makala hiyo ya Guardian iliyoandikwa na Paul Harris, mtego huu wa kuwanasa watu katika ugaidi wa kupanga unawalenga zaidi Waislamu, ila wakati mwingine huingia na akina Willium, Wamarekani Weusi.

Anasema Paul Harris katika habari yake katika Guardian aliyoipa jina Fake terror plots, paid informants: the tactics of FBI ‘entrapment’ questioned” kuwa kumekuwa na mchezo wa kuwatega Waislamu na kuwaingiza katika mtego wa kufanya au kutaka kufanya vitendo vya kigaidi na kisha kuwakamata.

Katika mchezo huo, makachero hupewa fedha na kutumwa misikini na mitaani ambapo hujifanya kuwa wachamungu na wanaharakati. Wakishakubalika, huanza kuwatega baadhi ya watu kwa kupenyeza fikra za jihad na kulipiza kisasi kwa makafiri.

Wakishafanikiwa kunasa shabaha, makachero hao huwa wafadhili wa mpango kwa fedha na silaha. Usanii ukikamilika kwa shambulio kufanyika au kiasi tu cha kuwaunganisha na mtu anayedaiwa kuwa Al Shabaab au gaidi kama ilivyokuwa kwa yule mtaalamu wa kijeshi wa Uganda anayetokea Somalia na kutua Masjid Buzuruga, Nyakato, polisi huingia na kuanza kukamata waliokuwa naye.

Ikifikia hapo kachero ama hutoweka au huwa shahidi na hata kuhukumiwa pamoja na vijana walionaswa, lakini baadae huachiwa. Tuliwahi kutahadharisha juu ya suala hili la Al Shabaab kuwa maadhali Israel iliyofuzu na yenye uzoefu wa kutosha katika masuala ya ufaidi wa kupanga, imealikwa kusaidia kupambana na Al Shabaab, basi watu wawe makini.
Tukasema kuwa yaweza kufanyika mashambulizi ya kutisha kama ilivyowahi kufanyika katika “Operation Cynide”, kashfa ya Lavon (Lavon Affair in 1954) na Operation Trojan.

Lakini kwa upande mwingine ni huu mchezo wa ‘entrapment’ ambapo makachero hutumwa misikitini na kwa Waislamu wakijifanya watu wema na wachamungu kisha huwatega na kuwakamatisha kwa tuhuma za ugaidi.

.Chanzo Fazeti la Annuur

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s