Zanzibar inahitaji ukombozi ili kufika, maridhiano yanastahiki kulindwa

Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Maalim Seif Sharif Hamad wakisalimiana siku ya Eid El Fitri 2009

Na Mohammed Ghassany

Uumini wangu kwa Maridhiano ya Wazanzibari hautetereki au hauporomoki. Niliyaamini yalipozaliwa miaka miwili iliyopita na ninayaamini leo yakiwa yamefanikisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUKZ) iliyodumu madarakani kwa mwaka mzima sasa. Nitayaamini kesho, keshokutwa na milele.
Hata hivyo, niweke wazi kwamba siyachukulii Maridhiano hayo kuwa ndilo lengo la Wazanzibari; badala yake nayachukulia kuwa ni njia ya kufikia lengo. Lengo ni Ajenda ya Zanzibar.Nakusudia kuwa, Wazanzibari waliporidhiana hawakufanya hivyo kwa sababu wapate kuridhiana. Bali waliridhiana ili waikomboe nchi yao. Je, Zanzibar inahitaji ukombozi? Hapa tunaweza kutafautiana kujibu swali hilo na hasa katika maana ya ‘ukombozi wa Zanzibar‘, lakini juu ya kilele cha tafauti yetu, tunaweza kukubaliana kuwa, kwa ilivyo sasa, Zanzibar haiko huru; inahitaji ukombozi – na Maridhiano ni njia ya kufikia huko.

Kwa hivyo, tunalazimika kuisafisha njia tunayopita ili kurahisisha safari yetu kuelekea kwenye lengo letu. Na hili ni suala la wajibu wala si la hiyari kwetu. Maana kama njia ni chafu, safari itakuwa ngumu kufikia mwisho, na huenda hata isikamilike.

Wengine tumeanza kuiona njia hii ikianza kuchafuliwa, ikiwa ni mwaka mmoja tu baada ya kuundwa kwa SUKZ, miaka miwili baada ya Rais Amani Karume kukutana na Maalim Seif Sharif kwenye Ikulu ya Zanzibar. Tumeuona uundwaji na utendaji kazi wa SUKZ.

Hapana. Tumeiona tabia ya uundwaji na ufanyaji kazi huo. Katikati yake tunamuona Rais Ali Mohammed Shein, ambaye ukiwacha Baraza lake kubwa la Mawaziri kuwa na sura ya Umoja wa Kitaifa, baki ya serikali yake haiko hivyo. Kuanzia makatibu wakuu wa mawizara hadi masheha wa shehia.

Na mwenyewe, anajiona kuwa ana hoja ya kisheria kwa hayo ambayo wengine tunayaita ni mapungufu ya kimantiki, panapohusika Maridhiano na Umoja wa Kitaifa. Kwamba, muongozo wa Katiba ya Zanzibar unamtaka kuweka sura ya Umoja wa Kitaifa katika ngazi ya mawaziri tu, na sio nje ya hapo.

Lakini hoja hiyo inasahau ukweli wa kimantiki. Kwamba serikali ya Umoja wa Kitaifa ni matokeo ya Maridhiano. Hata kama Maridhiano haya baadaye yalipelekwa kwenye Baraza la Wawakilishi kuundiwa sheria, yakawa sehemu ya Katiba, lakini msingi wa chochote kinachokuja juu yake hakitakiwi kiyavunje, bali kiyaimarishe.

Kimantiki – na katika kiwango ambacho Umoja wa Kitaifa unahusika – utekelezaji wa Maridhiano haupaswi kukiukwa kwa kisingizio cha Katiba. Juu ya yote, Katiba haikumzuia Rais Shein kuteua makatibu wakuu, manaibu wao, wakurugenzi, wakuu wa mikoa na wilaya na hata masheha, kwa kutumia moyo wa Maridhiano.

Hadi sasa hajateua wakuu wa mikoa, wilaya wala masheha wapya, lakini uzoefu katika nafasi za watendaji wa serikali yake, tayari unatabiri nini atakifanya, kama atafanya uteuzi mpya: ataweka mvinyo ule ule kwenye chupa mpya!
Moyo wa Maridhiano pia unamtaka Rais Shein kuwa karibu sana (tena sana kabisa) na Makamo wake wa Kwanza, Maalim Seif Sharif Hamad, kuhakikisha kuwa njia ya Maridhiano inasafishwa dhidi ya uchafu wowote ule. Hata kama halazimishwi kufanya hivyo na Katiba, lakini Maridhiano na Umoja wa Kitaifa unampa wajibu huo. Maana, kwa uhakika hasa, Dk. Shein si rais wa kikatiba, bali rais wa Maridhiano. Huo ndio ukweli, tukitaka kuwa wakweli.

Siandiki haya kwa kuwa na uhakika kuwa Maalim Seif hashirikishwi kwenye maamuzi mbalimbali ya Rais Shein, lakini pua zetu waandishi zina nguvu zaidi ya kunusa uovu kuliko wema. Baada ya kusoma kauli ya Maalim Seif iliyochapishwa na vyombo vya habari akiwa kwenye ziara ya mwishoni mwa wiki huko Tumbatu, Kaskazini Unguja, nimenusa kudhoofika kwa umoja ndani ya serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Katika kauli hiyo, Maalim Seif amezungumzia suala tete la vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (ZAN-ID). Ukweli ni kuwa kuna kundi kubwa la Wazanzibari, ambalo halijapatiwa vitambulisho hivyo hadi sasa. Na hii ingawa si kesi mpya, maana serikali ya sasa imeirithi kutoka iliyopita, hilo halihalalishi kuwepo kwake. Ilikuwa haramu wakati ule, ni haramu leo, na ni haramu kesho. ZAN-ID ni haki ya kila Mzanzibari.

Hivi sasa Zanzibar imo kwenye kipindi muhimu sana katika historia yake. Baada ya miaka karibuni 50 ya kuwekwa chini ya Muungano, ambao kwa wengi ni aina nyengine ya ukoloni, vuguvugu la mageuzi liko juu. Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar yamechochea mchakato wa Katiba Mpya kwa Jamhuri ya Muungano. Matokeo ya mchakato huo, itakuwa ni wananchi wa pande zote mbili – Tanganyika na Zanzibar – kuulizwa maoni yao kuhusiana na hatima ya Jamhuri ya Muungano.

Maoni hayo yatapatikana kwa kura, na kura itapigwa na wenye sifa, ambapo kwa Zanzibar ZAN-ID ni sharti muhimu (baadhi ya wakati la pekee). Mamia kwa maelfu ya Wazanzibari ambao hadi sasa hawajapatiwa vitambulisho hivyo, hawatashiriki kura hiyo. Itakayopoteza itakuwa ni Zanzibar.

Lakini, kwa kuwa wengi wa hao ni wale wanaoonekana kukiunga mkono Chama cha Wananchi (CUF), mmoja wa mwenza muhimu katika SUKZ na Maridhiano, mtu anaweza kuiona makusudi kwa kila sura yake kwenye hili. Makusudi ya kuichafua njia ya Maridhiano. Makusudi ya kuturudisha tulikotoka, bali mbali zaidi ya hapo. Pale tulipokosa nguvu kwa sababu ya kugawika kwetu.

Rais Shein ana nguvu kamili za kuizuia Zanzibar isirudi ilikotoka. Anaweza kuendesha gari hii ya SUKZ kwenye njia ya Maridhiano kuelekea kwenye lengo letu – ukombozi wa kweli wa Zanzibar. Lakini hilo litafanyika ikiwa yeye mwenyewe ni muumini wa kweli wa Maridhiano, ikiwa ni mfuasi wa umoja wa kweli, na ana ndoto ile ile waliyonayo waumini wengine wa Maridhiano – Ajenda ya Zanzibar. Nguvu zilizotumiwa na watangulizi wake kuyalinda Mapinduzi, azitumie yeye kulinda Maridhiano, lau dhamira ya kweli anayo!

Makala hii imechapishwa leo gazeti la An-nuur

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s