Tamasha la busara linaakisi utamaduni wa Mzanzibari lilindwe

Mkurugenzi wa Taasisi ya Busara Promotion, Yussuf Mahmoud kisalimiana na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad wakati wa uzinduzi wa tamasha la Busara huko Hoteli za Beach Resort, kulia ni Ismail Mohammed Mwenyekiti wa Busara Promotion.

Na Ally Saleh

Wiki iliyopita wengi wetu tuliokuwa katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort tulipata mshtuko kutokana na matamshi ya Mkurugenzi wa taasisi ya Busara Promotion, Yussuf Mahmoud. Yussuf Mahmoud ni raia wa Uingereza aliyehamia Zanzibar yapata miaka 10 iliyopita na anavyoniambia ni kuwa ameamua maisha yake yatamalizia hapa hapa Zanzibar kwa maana hana nia ya kurudi tena Ulaya.

Mkurugenzi Mahmoud ameongoza taasisi ya Busara Promotion kwa miaka 8 sasa akiwa ni mtaalamu maarufu katika fani ya muziki, ambayo ndio kazi kubwa inayofanywa na Tamasha la Busara ambalo hufanyika kila mwezi wa Februari.

Matamasha mengine hapa Zanzibar ni pamoja na lile la Filamu la ZIFF, tamasha la Mzanzibari linalosimamiwa na Serikali, tamasha jipya la Sanaa na muziki wa jazz na pia tamasha jengine jipya la sanaa za maonyesho la Mswahili.

Tamasha la Busara sasa limekuwa kalenda maarufu katika rubaa za kiutamaduni hapa Zanzibar na kwa hakika Afrika Mashariki na vile vile Afrika nzima. Taarifa zinasema kuwa tamasha hili kwa sasa ni la 5 kwa ukubwa Barani Afrika.

Halikadhalika ripoti zinaonyesha Tamasha la Busara limeingia katika kalenda ya kiutalii ya dunia na hivi sasa utajapo tamasha hilo basi ina maana unataja kuvutia watalii.

Kuna ushahidi wa kutosha katika hili. Kwanza ni kwamba wazo la tamasha kufanyika mwezi wa Februari lilikuwa ni kwa ajili ya kujaza pengo au umbwe la watalii katika miezi ya Januari mpaka April ambayo huwa na mvua kubwa na kwa hivyo watalii hawaji Zanzibar.

Ushahidi unaonyesha kuwa utalii wakati huo katika miaka 8 ya tamasha umeongezeka kwa asilimia 500. Wakati kipindi hicho hoteli nyingi zilikuwa zikifungwa na wenyewe kufanya usafi na matengenezo sasa imekuwa wakati huo ni wakati wa machumo kama ilivyo kwa miezi ya Juni mpaka Septemba.

Lakini sio hilo tu wakati wa tamasha nyumba binafsi pia hukodiwa kwa ajili ya kukaa wageni, maduka hutononoka kwa manunuzi, madereva wa taxi hufaidika na pia kila sekta nyengine kama mikahawa nayo hupata kitu kidogo.

Tuliambiwa kuwa Tamasha la Bushfire la Swaziland limefanyiwa hesabu na kugungulika kuwa kila dola moja inayowekezwa basi huzalisha dola 40 na kwa hivyo hali hiyo inaweza kuwa pia kwa Tamasha la Busara.

Lakini pia, washiriki wa kongamano la siku moja liloandaliwa na Busara Promotion kwa ajili ya kutafuta mbinu za kuungwa mkono na wafanyabiashara, liliambiwa kuwa nchi ya Misri ina matamasha 720 kwa mwaka kwa hivyo nchi na raia kufaidika kwa njia kadhaa wa kadhaa.

Zanzibar haina haja ya matamasha yote hayo, wala nusu yake, na hata robo yake. Hata haya matamasha machache yaliopo kama yataendeshwa vyema basi faida yake ni kubwa kama nilivyokwisha kuonyesha kwa mfano wa Tamasha la Bush Fire la Swaziland.

Tamasha la Busara pia hutoa fursa za ajira 150 na pia huibua vipaji mbali mbali ambavyo huendelezwa na kwa hivyo kugeuza muziki wenyewe kuwa ni ajira kinyume na dhana iliyopo hivi sasa.

Pale mwanzoni nilisema kuwa tulishitushwa na kauli ya Mkurugenzi Mahmoud ambaye alisema kwa ajili ya kukosa kuungwa mkono na makampuni, mashirika na makampuni ya Kizanzibari wanafanya fikra kuhamisha tamasha hilo kwenda Dar es salaam.

Aliyeshituka pamoja nasi alikuwa ni Maalim Seif Shariff Hamad, Makamo wa Kwanza wa Rais aliyekuja kufungua mkutano huo na akasema wazi wazi hilo halipendi hata kama tamasha hilo litapelekwa “ kwa ndugu zetu wa Tanganyika.”

Ukumbi mzima ulishituka na ukasema kuwa wako tayari kufanya lolote lile ilimradi tamasha libakie Zanzibar kwa sababu kwa sasa limeshakuwa alama “brand” ya Zanzibar dunia nzima na linawezwa kuuzwa na jina la Zanzibar katika biashara na hata utalii.

Busara imesema inaona aibu kuendelea kutembeza bakuli kwa balozi za kigeni ziliopo Tanzania kuomba fedha za ufadhili na udhamini au kuomba makampuni ambayo yako Dar es salaam.

Pamoja na hayo Tamasha lilitoa shukurani kwa makampuni hayo, lakini viongozi wake walisema wakati umefika kwa Wazanzibari kuona fahakhari kulimiliki tamasha hilo kwa ajili ya kuungwa mkono na vyanzo vya ndani.

Walisema wafadhili wa ndani wanahitaji kulipia tamasha hilo kwa vile linasadia kuibeba Zanzibar kama vile ambavyo Serikali ya Zanzibar ina wajibu wa kusaidia tamasha hilo kwa vile linafanya kazi ambayo vyovyote vile ingepaswa kufanywa na Serikali.

Maalim Seif alikiri hilo na akatoa wito wa Tamasha la Busara na matamasha mengine kukutana na kupanga mikakati yao ya kipi wanahitajia Serikali kisha kukaa na Wizara ya Habari na Utamaduni. Pamoja na Serikali huko nyuma kuyaunga mkono, Maalim Seif alisema bado kuna nafasi ya kutoa msaada zaidi.

Maalim Seif alisema kuna mashirika mengi ya kiserikali ya Zanzibar kama ZRB, ZSSF, Bandari, Bima, PBZ, Bima na mengineyo ambayo kama yataelezwa vyema na kuonyeshwa faida ambao na wao watapata bila ya shaka wataweza kutoa mchango wao.

Pia kama mahoteli yanafaidika basi hayana budi pia kurudisha kiasi cha faida zao kwa matamasha hayo, kama ambavyo ilivyo kanuni ya kurudisha fedha kwa jamii kutokana na faida ya mashirika.

Maalim Seif aliuunga mkono wazi la kuwa na Mfuko wa Utamaduni ambalo sio geni. Wadau walipendekeza njia moja wapo ya kuutunisha mfuko huo ni kuwekeza kila dola mbili anazotumia mgeni akiwa Zanzibar kuingia katiak mfuko huo ambao utengezewe sheria na menejimenti inayoaminika.

Kutokana na kukiri kuwa nchi yoyote haiwezi kuendelea bila kuulinda utamaduni wake, basi ikakubalika na wadau wengi kwamba kuna haja ya kuwa na mkakati wa kueleweka kuhusu kusaidia matamasha.

Lakini pia wadau wakalaumu Busara kwa kutotoa nafasi kubwa kwa wasanii wa ndani lakini pia kwa kutolipeleka tamasha kwa wananchi na ndipo ikapendekezwa kuwa kuwe na kitu cha zaidi ili wananchi wafaidike kwa tamasha kufika karibu yao.

Ila pia ikaelezwa kuna haja kubwa ya kutoa elimu ya umiliki. Umiliki wa tamasha uwe ni wa umma kwa maana ya kila aone ni lake na hilo linakuja kwa Busara yenyewe kukubali kuwa tamasha sio lao peke yao.

Washiriki wengi walipongeza uamuzi wa Busara kuzindua juu ya uwezekano wa matamasha kama lao na mengine kuweza kukwama kwa kukosa ufadhili bila ya kujifikiria watu tu.

Hisia hizo zilivutia watu wengi kwa kuwa kumewekwa uzalendo leo. Na dhana ya jumla ikawa ukawa kuendesha matamasha ni uzalendo maana yake yanasaidia kulinda utamaduni na pia kuongoza kuingiliana na tamaduni nyengine katika njia njema zaidi ni sio ya hasara.

Utamaduni wa Zanzibar ni karne kadhaa. Umeingiliwa na Wareno, Wayunani, Waajemi, Washirazi, Waingereza, Waomani, Wamalay na wengine wengi, lakinii bado uko imara. Na kila Mzanzibari yuko tayari kwa lolote lile kuulinda ili aviachie vizazi vyake utamaduni bora na bora zaidi, ijapo utakuwa umechanganyika, maana ni jambo la lazima.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s