Kamata kamata Al Shabaab yatua Mwanza

Kijana mdogo akiwa ni miongoni mwa kikundi kinachodaiwa kuwa ni cha Al Shabab kikifanya mazoezi ya kijeshi ya utumiaji wa silaha dhidi ya wapinzani wao

*Vijana 4 wa Kiislamu wakamatwa Mwanza,*Yahofiwa wanateswa ‘Guantanamo’ Somalia
*Mbinu za ki-FBI zatumika, kanda zasambazwa, *Makachero wajifanya mujahidina Misikitini

Na Mwandishi Wetu
Vijana wanne (4) wa Kiislamu wamekamatwa jijini Mwanza wakituhumiwa kuwa ni Al Shabaab. Vijana hao ambao walikamtwa katika muda na mahali tofauti, wa kwanza akikamtwa Jumatatu huku wawili wakikamatwa Jumanne na mwingine akikamatwa juzi Jumatano.Waliokamatwa wametajwa kuwa ni Hassan Jumanne Hassan mkazi wa Igogo na mfanyabiashara ndogo ndogo katika eneo la Mlango mmoja.


Wengine ni Omar, maarufu Osamah, Said na Idd, wote wakazi wa Nyakato.Hadi tunakwenda mitamboni, haikuwa imefahamika vijana hao walifichwa katika kituo gani cha polisi au katika gereza gani na walikuwa hawajafikishwa mahakamani.Kwa mujibu wa taarifa za ndugu wa Waislamu hao, kila kituo cha polisi walichopita kutaka kujua iwapo ndugu zao wamefikishwa hapo na wanakabiliwa na tuhuma gani, waliambiwa hawapo na hakuna askari aliyekuwa tayari kuzungumzia suala hilo.

Hali hiyo ya kutokujulikana walipo vijana hao, imeleta wasiwasi isije ikawa wamepelekwa au wapo njiani kupelekwa ‘Guantanamo’ kuteswa katika kambi za mateso za CIA Somalia.Inaelezwa kuwa kamata kamata hiyo ilitanguliwa na kilichoonekana kuwa mtego na mchezo wa kupanga ambapo kijana mmoja aliyejitambulisha kutoka Uganda alifika katika msikiti wa Buzuruga, Nyakato akitaka kusaidiwa kama msafiri aliyeharibikiwa.

“Mimi ni Ibn Sabil, msafiri niliyeharibikiwa naomba msaada wenu Waislamu niweze kuendelea na safari kurudi Uganda”, baadhi ya waumini wanamnukuu alivyojieleza.Kijana huyo alidai kuwa alikuwa akitokea Somalia na aliharibikiwa na hivyo kutaka sadaka za Waislamu ili aweze kuendelea na safari kurudi nyumbani, Uganda. Baadhi ya Waislamu walitoa sadaka kumpa, hata hivyo ikawa fedha hazikutosha.

Baadhi ya taarifa zinasema kuwa kijana huyo alijitaja kama mtaalamu wa masuala ya kijeshi na ufundi wa aina mbalimbali, ila hakufafanua utaalamu huo alikuwa akiutumia vipi huko Somalia. Baada ya kupata sadaka kutoka kwa waumini wa Buzuruga, kijana huyo aliingia mitaani akidai kuwa fedha alizopata hazitoshi nauli ya kumrejesha Uganda kwa hiyo akaomba kibarua ili apate fedha.

Mpasha habari wetu anafahamisha kuwa kiasi wiki moja iliyopita kijana huyo alipata kazi ya kuchomelea au kuunga chuma (Welder) Nyegezi na alionekana kuwa fundi hasa. Kwa upande mwingine kwa jinsi alivyojiweka na Waislamu na kuonekana kama mwana-Da’wah, kijana mmoja Omar, maarufu Osamah wa Nyakato alimkaribisha akae nyumbani kwake kwa muda.

Hata hivyo, ghafla kijana huyo alitoweka na kamata kamata ikaanza kuwakamata waliokuwa marafiki na waliomfadhili kijana huyo wa Uganda. Hayo yakijiri, zimesambazwa kanda zikidaiwa za Al Shabaab zikionesha hali ilivyo katika uwanja wa mapambano. Na kwa upande mwingine kanda na CD hizo huonesha darsa zinazodaiwa kuwa za Al Shabaab wanazofanya wakiwa porini katika uwanja wa mapambano.

Darsa hizo pamoja na zile zinazopatikana katika CD za darsa za Sheikh Abdu Rogo wa Mombasa, zinawahamasisha Waislamu kushika silaha kupambana na makafiri. CD na kanda hizo zimeenea zaidi Mwanza na Bukoba. Baadhi ya masheikh na wazee wa Mwanza wameelezea tukio hilo kama jambo la kupangwa ili kupata sababu ya kuwahujumu vijana wa Kiislamu na kukoleza kitisho cha Al Shabaab.

“Ukiangalia ujio wa kijana huyu aliyedai kutoka Uganda na jinsi matukio yalivyofuatana, huu ni mchezo wanachezewa Waislamu na bahati mbaya vijana wetu wamekuwa watu wa jazba badala ya kufuata kanuni ya Qur’an ya kutafiti na kuchunguza mambo.” Amesema mzee mmoja akiongea na mwandshi. “Vipi mtu atoke Somalia badala ya kwenda Uganda kupitia Kenya aje kwanza Tanzania, vipi katika hali hii ya vita na kusakwa Al Shabaab, kijana huyo asiogope bali aone fahari kujitaja hadharani kuwa ni mtaalamu wa kijeshi, ni Mganda Muislamu, anarejea kutoka Somalia?” Alihoji Mzee huyo aliyejitaja kwa jina moja la Hussein.

Akaongeza kuwa haiwezekani ikawa kwamba polisi na vyombo vya usalama vilikuwa havijui kuingia kwa kijana huyo toka amejitangaza Msikitini mpaka anafanya kazi Nyegezi. “Mi naamini kuwa vyombo vyetu vya usalama ni makini, na vilijua ujio wa kijana huyo mtaalamu wa kijeshi anayetokea Somalia toka siku ile aliposimama msikitini kujitangaza na kuomba sadaka, swali ni je, kwa nini hakukamatwa mpaka akaingia mitaani na kufanya kazi kwa siku kadhaa? Kwa nini ilingojewa akajenga mahusiano na baadhi ya watu, kisha akatoweka ndio vyombo vya usalama vistuke na kuanza kukamata watu? Haiwezekani vyombo vya usalama wa nchi vikafanya uzembe wa kiwango hicho, tafsiri pekee sahihi ni kuwa walimjua na walijua anachokisema na hawakuwa na wasiwasi naye. Walimjua na walijua kinachoendelea.” Alihoji na kusema.

Hayo yakijiri jijini Mwanza, zimepatikana habari kuwa serikali ya Marekani inaendesha kambi za siri za mateso nchini Somalia.Katika makala yake aliyoipa jina “Obama administration operates illegal torture compound in Somalia”, mwandishi Tom Carter (19 July 2011) anasema kuwa serikali ya Obama imekuwa ikitesa watu wasio na hatia katika makambi ya siri ya utesaji ndani ya Somalia.

Katika ufafanuzi wake anasema kuwa, watu hao hukamatwa wakituhumiwa kuwa ni Al Shabaab, kisha bila ya kufikishwa mahakamani huwekwa katika kambi hizo za mateso na kuteswa. Tom anatoa mfano wa kijana Ahmed Abdullahi Hassan, raia wa Kenya, ambaye alikamatwa bila ya kosa akabambikwa u-Alshabaab akaweka katika kambi ya mateso kwa zaidi ya mwaka na miezi saba.

“They put a bag on my head, Guantanamo style. They tied my hands behind my back and put me on a plane. In the early hours we landed in Mogadishu. The way I realized I was in Mogadishu was because of the smell of the sea―the runway is just next to the seashore. The plane lands and touches the sea. They took me to this prison, where I have been up to now. I have been here for one year, seven months. I have been interrogated so many times. Interrogated by Somali men and white men. Every day. New faces show up. They have nothing on me. I have never seen a lawyer, never seen an outsider. Only other prisoners, interrogators, guards. Here there is no court or tribunal.”

Anasema Hassan akisimulia yaliyomkuta baada ya kukamatwa Kenya na kupelekwa Somalia. Kwa kuwepo kwa makambi haya ya mateso Somalia na kwa utaratibu huu wa kupeleka watuhumiwa kuteswa katika makambi ya mateso ya CIA ndani ya Somalia, kuna wasiwasi isije ikawa watuhumiwa hawa wa Mwanza nao wasije kujikuta mikononi mwa watesaji wa CIA.

Wakati huo huo, hadithi ya kijana huyu mtaalamu wa kijeshi na mujahidina wa Uganda inakuja wakati kashfa ya kupanga vitendo vya kigaidi inazidi kuiandama Idara ya ukachero ya Marekani-FBI. Kwa mujubu wa taarifa iliyoandikwa na gazeti la Guardian (Uingereza) la Novemba 16, 2011, mchezo huu wa FBI umemkumba David Williams ambaye amejikuta akihukumiwa kifungo cha miaka 25 jela kwa kosa la kutaka kufanya kitendo Cha kigaidi kulipua hekalu la Mayahudi New York pamoja na kulipua ndege ya kijeshi kwa kombora.

Kwa mujibu wa makala hiyo ya Guardian iliyoandikwa na Paul Harris, mtego huu wa kuwanasa watu katika ugaidi wa kupanga unawalenga zaidi Waislamu, ila wakati mwingine huingia na akina Willium, Wamarekani Weusi. Anasema Paul Harris katika habari yake katika Guardian aliyoipa jina Fake terror plots, paid informants: the tactics of FBI ‘entrapment’ questioned” kuwa kumekuwa na mchezo wa kuwatega Waislamu na kuwaingiza katika mtego wa kufanya au kutaka kufanya vitendo vya kigaidi na kisha kuwakamata.

Katika mchezo huo, makachero hupewa fedha na kutumwa miskini na mitaani ambapo hujifanya kuwa wachamungu na wanaharakati. Wakishakubalika, huanza kuwatega baadhi ya watu kwa kupenyeza fikra za jihad na kulipiza kisasi kwa makafiri.

Wakishafanikiwa kunasa shabaha, makachero hao huwa wafadhili wa mpango kwa fedha na silaha. Usanii ukikamilika kwa shambulio kufanyika au kiasi tu cha kuwaunganisha na mtu anayedaiwa kuwa Al Shabaab au gaidi kama ilivyokuwa kwa yule mtaalamu wa kijeshi wa Uganda anayetokea Somalia na kutua Masjid Buzuruga, Nyakato, polisi huingia na kuanza kukamata waliokuwa naye.

Ikifikia hapo kachero ama hutoweka au huwa shahidi na hata kuhukumiwa pamoja na vijana walionaswa, lakini baadae huachiwa. Katika taarifa nyingine, inaelezwa kuwa sababu ya kuandaa usanii na mchezo huu wa kunasa magaidi feki, ni katika kukoleza kitisho cha ugaidi ili kutoa sababu ya kuendeleza vita hiyo na kuipa sababu serikali ya Marekani kuendeleza agenda yake ya kujenga na kusambaza utando wa kijeshi katika maeneo inayotaka.
Chanzo: Gazeti la An-nuur

Jinamizi la Al Shabaab

Na Omar Msangi

Katika taarifa moja ya Al Jazeera ya Novemba 15, 2006, mpasha habari Mohammed Adow akiwa Mogadishu akisimulia hali ya mji huo alisema kuwa “kabla ya Umoja wa Mahkama za Kiislamu kukamata mji huo, hali ilikuwa ya kutisha. Ilikuwa vurugu mitaani, risasi zikivurumishwa kutoka kila mtaa na kila kona. Lakini tahamaki hali imekuwa shwari.”

Wababe wa kivita walikuwa wamesalimu amri na hali ya kawaida ya maisha ilikuwa ikirejea Somalia. Mauwaji, uporaji na ubakaji ulikuwa umesita na wananchi wakishukuru na kutoa kila msaada kwa “Islamic Courts Union” (ICU).

Hayo yalithibitishwa pia na Tony Burns, aliyekuwa mkurugenzi wa taasisi isiyokuwa ya kiserikali (NGO) SAACID, akionesha katika taarifa yake hali ilivyokuwa tofauti kabla na baada ya kuingia ICU.

Hata hivyo, hali ilibadilika baada ya Marekani na Ethiopia kuingia na kuwaondoa ICU. Hali ya vita, mauwaji na vinavyodaiwa kuwa vitendo vya kigaidi vinavyoendelea hivi sasa, ni matokeo ya uvamizi wa Ethiopia na uingiliaji wa Marekani katika masuala ya Somalia.

Nini lengo la Marekani katika uingiliaji huu? Marekani yenyewe inadai kuwa ni kuleta amani ya Somalia na eneo lote la Pembe ya Afrika. Hata hivyo, wanazuoni mbalimbali na wachambuzi wa siasa za Marekani wanasema kuwa hicho ni kisingizio tu. Lakini lengo hasa ni kulichafua eneo la Pembe ya Afrika na Afrika Mashariki, kuondoa hali ya amani iliyopo na kisha kujenga kisingizio cha kuingia kusaidia masuala ya kiusalama na hivyo kupata fursa ya kulidhibiti eneo hilo kijeshi kulinda masilahi ya Marekani.

Hivi karibuni mwandishi Joe Penney ameandika maoni yake aliyoyapa kichwa cha habari, Clinton, counter-insurgency and hegemony.

Joe Penney aliandika maoni hayo kufuatia ziara ya hivi karibuni ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton katika nchi ya Philippines. Mwandishi anakumbusha kuwa mwaka 1951, kiasi miaka 60 iliyopita, Philippines iliwekeana mkataba wa ulinzi na Marekani ulioitwa  The Mutual Defence Treaty.

Kutokana na mkataba huo, Marekani ilijaza vikosi vyake, kambi za kijeshi na silaha katika Philippines. Hata hivyo, uwepo wa majeshi na kambi za kijeshi, hakujawaletea amani Wafilipino. Kinyume chake, umekuwa uwanja wa vita wakiuliwa na kuteswa wananchi kwa zaidi ya nusu karne.

Kwa upande mwingine, Marekani imefanya nchi hiyo kama koloni lake ambapo askari wa Marekani huingia bila ya kuitaka idhini ya serikali ya Philippines, lakini kwa upande mwingine, Wafilipino hawana uwezo wa kuweka jeshi Marekani wala kwa raia wake kuingia Marekani wapendavyo.

Philippines imekuwa na historia ya kuwa na viongozi madikiteta, katili na mafisadi. Kutokana na hali hiyo, kumekuwa kukitokea makundi ya wananchi wakitaka mabadiliko, wakitaka demokrasia na kupigania haki za binadamu na hata mengine kufikia kutaka kujitenga kutokana na uonevu wanaofanyiwa na watawala.

Hata hivyo, kwa vile watawala hao fisadi wamekuwa wakitekeleza matakwa ya Marekani, wamekuwa wakilindwa na kupewa silaha zaidi kwa ajili ya polisi na askari wake wanaokabiliana na makundi ya kiraia na wale wenye silaha wanaotaka kujitenga.

Hali hiyo imefanya Ufilipino kuwa nchi isiyo na amani kwa muda mrefu. Kwa mujibu wa taarifa za taasisi za kutetea haki za binadamu za kimataifa kama Human Rights Watch, polisi na idara za usalama zimekuwa zikifanya mauwaji ya kikatili na hata vitendo vya kigaidi na kisha kuwasingizia watu wapinzani wa serikali. Hata taarifa ya Umoja wa Mataifa, kitengo cha Haki za Binadamu, iliyowasilishwa na Philip Alston (2008), imeeleza wazi jinsi vyombo vya usalama na jeshi linavyofanya mauwaji na mateso kwa raiya kinyume na sheria.

Hao ni wanajeshi na makachero ambao kila mwaka serikali ya Marekani huwamiminia fedha, silaha na kuwapa mafunzo katika kile kinachoitwa “joint exercises”, kama ambavyo hivi sasa mazoezi hayo hufanyika Tanzania na eneo lote la Afrika Mashariki.

Kwa hiyo, moja linalotakiwa kufahamika na mapema ni kuwa kuwepo kwa vikosi vya Marekani kwa kisingizio cha kulinda amani, hakuleti amani bali kuchafua. Na pili, kwa uzoefu wa Ufilipino, nchi nyingine zilizotutangulia katika hiki kinachoitwa “joint exercises”, baina ya askari wa Marekani na majeshi na polisi wetu, si kwa lengo la kulinda amani ya nchi na masilahi ya watu wetu; bali kutengeneza askari wa kuuwa, kutesa na kupambana na wananchi wanaoonekana kuhatarisha masilahi ya Marekani ikiwa ni pamoja na kuwakataa viongozi katili na madikiteta lakini wanaopendwa na Washington kwa ukibaraka wao.

Chemia na mahesabu ya uhusiano huu wa Washington na viongozi dikiteta na vibaraka wa Ufilipino yapo hivi. Kama ilivyofichuliwa katika taarifa mbalimbali ikiwemo ile ya WikiLeaks, lengo la Marekani ni kuitumia Philippines kama uwanja wake na ngome ya kulinda masilahi yake katika eneo lote la Asia ya Kusini. Na masilahi haya yapo ya namna mbili. Moja ni fursa ya kudhibiti, kuvuna na kuhodhi mali asili za ndani ya Philippines na maeneo yanayozunguka nchi hiyo. Pili, kuzuiya China isizikamate nchi hizo.

Sasa maadhali ushirikiano huu ni wa masilahi ya kibeberu ya upande mmoja, Philippines inajikuta inaumia. Ndio maana wananchi wanakuja juu kupinga, wakipinga, viongozi wa serikali wanawakandamiza kwa nguvu za kipolisi na kijeshi. Wanakuwa madikiteta katili. Marekani inawalinda kwa kuwapa misaada ya kijeshi na kutoa mafunzo kwa askari watakao kuwa na kazi ya kuwakandamiza wananchi.

Hii ndio ile counter-insurgency and hegemony, katika Philippines anayozungumzia mwandishi Joe. Joe anasema:

 “During Operation Enduring Freedom-Philippines, scores of innocent Muslims have been arrested, tortured and held without charge on suspicion of terrorist activity. The military was also accused of indiscriminate shelling against civilians during its multiple all-out wars against the MILF and the NPA.”

Kwamba katika kupambana na makundi yanayopinga serikali inayotumikiaWashington, wananchi wasio na hatia wamekuwa wakiuliwa na kuteswa kwa kisingizio cha kupambana na magaidi.

Hali hiyo ndiyo inayolazimishwa Somalia, Kenya, Uganda na Tanzania. Ugaidi wa Al Shabaab unachochewa ili ifike mahali ionekane kwamba tunahitaji usaidizi wa kudumu wa askari wa Marekani kulinda amani. Na tayari Kenya imeomba msaada wa Israel. Israel ndiyo Marekani.

Tusichojua ni kwamba hiyo amani tunayoililia haitakuwepo. ItakuwaPhilippinesnaAfghanistannyingine.

Kwa mujibu wa utafiti na uchambuzi uliofanywa na Profesa Horace Campbell na kupewa jina “Somalia: Global war on terror and the humanitarian crisis”, inachofanya Marekani Somalia sio kujenga taifa na kuleta amani ya nchi hiyo; bali kuisambaratisha na kujenga mazingira ya vurugu na vita isiyokwisha na kwa kutumia hali hiyo, kujipa fursa ya kukaa kijeshi katika eneo la Pembe ya Afrika na kisha kushuka hadi Afrika ya Mashariki.

Katika kufanya hivyo, Profesa Campbell anasema, Marekani inataka kudhibiti eneohiloambalo ni muhimu kwa biashara ya mafuta Mashariki ya Kati. Pili, kudhibiti utajiri waSomaliaambayo nayo inakisiwa kuwa na mafuta na madini mengine. Tatu, kuondoa uwezekano waChinakuingia na kuwa na ushawishi katika eneohiloikiwa ni pamoja naSomaliayenyewe,Ethiopiana Djibout. Nne, kwa kutumia kisingizio cha ugaidi wa Al Shabaab na kuzishinikiza Uganda, Kenya, Burundi (na pengine Tanzania) kuingia vitani, itasambaza vita (proxy wars) hadi eneo la Maziwa Makuu na hivyo kupata pia mwanya na fursa nyingine ya kujizatiti kijeshi katika eneo hilo. Na kupitia mlango huo, hata Africom itaingia na kukaa bila ya kipingamizi.

Profesa Horace Campbell anasema kuwa ili kukoleza kitisho cha ugaidi wa Al Shabaab na kujenga hoja ya Kenya na nchi nyingine za Afrika Mashariki kuingia vitani, Marekani imekuwa ikitumia baadhi ya mashirika mashuhuri kwa kupiga propaganda, ikiwa ni pamoja na Bell Pottinger, kuipa Al Shabaab umaarufu wa kupanga na kukoleza kitisho cha jinamzi la ugaidi wa Al Shabaab kama ilivyokuwa kwa kile kitisho cha kupanga cha Al Qaida na Usamah Bin Laden.Yote hii inafanyika ili kutafuta kizingizio cha kuendeleza mradi wake kusambaza makucha yake ya kijeshi- (militarism and World Hegemony).

Ni ubeberu kupitia mtutu wa bunduki. Na katika kukamilisha mkakati huo huo, vyombo vya habari vimekamatwa na kutumiwa kuimba habari potofu. Kwa bahati mbaya nasi tumetumbukia katika maigizo hayo. Polisi wanaimba Al Shabaab magaidi, Waziri Nahodha anaimba Al Shabaab, wahariri nao wanaimba Al Shabaab. Tunajisokotea kitanzi na kujivisha.

Hivi sasa katika uwanja wa soka kuna mzozo mkubwa kutokana na kauli ya Rais wa FIFA, Sepp Blatter. Hii ni kutokana na kauli yake aliposema kuwa hakuna vitendo vya ubaguzi, Weusi kubaguliwa na Weupe.

Mzozo unakuja kwa sababu, upo ushahidi kwamba wachezaji kutoka Afrika wanaochezea vilabu mashuhuri vya Ulaya wamekuwa wakibaguliwa na kutukanwa wakati mwingine wakiitwa nyani. Inatolewa mifano kuwa, yapo matukio ambapo mchezaji hutupiwa ndizi, hii ikiashiria kuwa anatukanwa kwamba yeye ni sawa na nyani na wenzao tumbili na kima.

Sasa kwa Blater kusema hakuna ubaguzi, inatafsiriwa kuwa anawatetea wanaowabagua na kuwatukana wachezaji Weusi. Kwa tafsiri nyingine ni kuwa na yeye ni mbaguzi.

Mtu akikuita nyani, hamaanishi umbo tu, lakini kubwa zaidi ni kuwa anakuona kuwa huna akilikamayeye. Kwamba japo na wewe ni binadamu, lakini akili yako na uwezo wako wa kufikiri sio sawa na ule wa Mzungu. Huu ndio mtizamo wa wanaowatukana watu Weusi na kuwafananisha na nyani.

Wale wachezaji wa Kiafrika wanaochezea vilabu mashuhuri vya Ulaya, ni kwamba katika uwanja wa soka wameonesha uwezo mkubwa kiasi kwamba Wazungu pamoja na ubaguzi wao wamewakubali.

Sasa hii inatarajiwa kuwa katika kila eneo, tuweze kuwaonesha Wazungu hawa wabaguzi kwamba mawazoyaoni potofu. Sisi ni binadamukamawao, sote tumeumbwa na Mungu yule yule aliyewaumba wao na tumepewa akili sawa na wao. Ndio maana tuna maprofesa wasomikamaakina Profesa Ali Mazrui ambao hugombewa katika Vyuo Vikuu vya Ulaya na Marekani vyenye hadhi.

Kwamba ukiwa na Profesa Mazrui katika chuo chako, basi unakipa sifa chuo na utakuwa kimbilio la wanafunzi na kufanya biashara kubwa za kitafiti, kandarasi na ushauri.

Kama ilivyo kwa wasomi, ni matarajio yetu kwamba hata katika uwanja wa siasa, wanasiasa wetu na wanausalama wataonesha umahiri wa kutambua masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa na kuchukua hatua ambazo zitakuwa na manufaa kwa nchi zetu na watu wetu.

Lakini ikitokea vinginevyo, wasiwasi ni kuwa tutakuwa tunawapa hoja na mashiko wale wabaguzi wanao tudharau wakafikia kuturushia ndizi.

Lazima tujiulize, leo sisi tunapotangaza kupambana na Al Shabaab, tunapambana nayo vipi na uwanja wenyewe wa vita uko wapi? Je, na sisi tunakusudia kupeleka jeshiSomalia? Au tumeweka mkakati wa kuwakamata akina Ahmed na kuwatesa na wengine kuwakabidhi katika ile ‘Guantanamo’ iliyopo Somalia?

Na tusisahau, mabeberu hawa wana uwezo wa kufanya tupigwe kweli ili kitisho cha Al Shabaab kikolee. Badala ya kuhangaika na shida zetu za mgawo wa umeme, tuhangaike na zimwi tuliloanza kulibuni wenyewe vichwani.

Advertisements

One response to “Kamata kamata Al Shabaab yatua Mwanza

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s