Barza zina historia kubwa katika siasa

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad akiwa akiongea na wajumbe wa baraza za mazungumzo huko Kilimahewa maarufu (Rarza ya Radio One) Mkoa wa Mjini Magharibi

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad ameanza utekelezaji wa mpango wake wa kutembelea baraza za mazungumzo (Barza) kwa lengo la kuwa karibu zaidi na wananchi na pia kutoa wito kwa wananchi kuhuisha baraza zao kwani zina mchango mkubwa katika harakati za kisiasa nchini.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar ameanza ziara hiyo katika barza ya Radio One huko Mtaa wa Darajabovu  nje kidogo na Mji wa Zanzibar na kuongea na wajumbe wa baraza hiyo ambayo imejizolea umaarufu mkubwa katika harakati za kisiasa tokea kuanza kurejeshwa kw amfumo wa vyama vingi vya siasa nchini Tanzania.

Katika baraza hizo wananchi hukutana na kuzungumza mambo mbali mbali yanayohusu maendeleo yao na taifa na yanayowakabili kila siku pamoja na kupashana habari zinazotokea katika nchi yao kwa jumla.

Akiongea katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na wananchi kadhaa wa eneo hilo Maalim Seif alitaja lengo la ziara hiyo katika Barza hiyo kwa kuelewa historia yake katika historia za siasa za upinzani hapa Zanzibar na jinsi ilivyotoa mchango mkubwa katika siasa.

“Nimeamua nianzie barza zangu hapa Radio One kwa kuelewa historia na na umuhimu wa barza hii katika ulingo wa siasa zetu”, alisema Maalim Seif.

Ziara hiyo inatoa changamoto kwa baadhi ya viongozi wa majimbo ambao wamekuwa wakilalakiwa kwa kukimbia majimboni mwao na hatimaye kuwa mbali na wananchi, jambo ambalo linawafanya wapiga kura wao kutoamini kile kinachotokea baada ya viongozi hao kuchaguliwa.

Mara kwa mara Maalim Seif amekuwa akiwahimiza viongozi wa majimbo kufanya bajeti ya muda ili kutenga muda kwa ajili ya kutembelea barza za mazungumzo na kushiriki shughuli za kijamii zikiwemo mazishi na harusi.

Katika mazungumzo hayo Maalim Seif alielezea juhudi zinazochukuliwa na serikali katika kuwakwamua na ukali wa maisha, licha ya kuonekana hali kuwa tofauti na hivyo kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa mbali mbali hasa vyakula.

Amesema serikali inatambua hali inayowakabili wananchi lakini inafanya juhudi kuona kuwa matatizo ya wananchi yanapatiwa ufumbuzi muafaka katika kipindi kifupi kijacho.

“kipindi cha mwaka mmoja uliopita serikali ilikuwa inajipanga kuangalia namna ya kukabiliana na matatizo haya, lakini nna matumaini kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ijayo hali itakuwa tofauti kabisa Insha-Allah”, alisema Maalim Seif.

Amesema serikali inafanya juhudi za kuwaalika wawekezaji kuja kuwekeza Zanzibar sambamba na kuimarisha huduma za kilimo na uvuvi kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Katika hatua nyengine Maalim Seif Sharif Hamad amezitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhakikisha Sheria ya Gharama za Uchaguzi iliyotungwa nchini, inafuatwa na kutekelezwa kivitendo ili uchaguzi unaofanyika uwe huru na haki na usiotawaliwa na rushwa.

Maalim Seif alisema hayo jana huko Makao Makuu ya CUF Zanzibar, Mtaa wa Mtendeni mjini Unguja wakati alipotembelewa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Rajab Baraka katika ziara yake ya kawaida ya kuvitembelea vyama hivyo.

Alisema pamoja na kutungwa sheria hiyo, baadhi ya vyama vya siasa vimekuwa vikiikiuka hadharani kwa kutoa rushwa bila kificho pamoja na kukiuka kima kilichowekwa cha gharama za uchaguzi wa jimbo, bila ya kuchukuliwa hatua zozote na mamlaka husika.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alitoa mfano wa ukiukwaji mkubwa wa sheria hiyo ni matukio yaliyojiri wakati wa Uchaguzi Mdogo wa Igunga mkoani Tabora, Oktoba mwaka huu.

Alieleza kuwa wakati wa uchaguzi huo, Sheria ya Gharama za Uchaguzi ilifumbiwa macho kwa sababu licha ya sheria hiyo kuweka bayana kima cha juu cha gharama za uchaguzi wa jimbo kisizidi Sh milioni 80, kuna chama kilitangaza kwenye vyombo vya habari kitatumia Sh milioni 400 katika uchaguzi huo.

“Yaliyotokea Igunga ni uthibitisho wa ukiukwaji wa sheria hii, rushwa ilikuwa ikitolewa nje nje, Takukuru wapo wanaona, sasa kama tumeamua kutunga sheria basi tuzifuate sote,” Maalim Seif alimueleza Naibu Msajili wa Vyama.

Katika hatua nyingine, Maalim Seif ameitaka ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuwasaidia wananchi wanaokosa haki zao kwa kunyimwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkazi kwa kuzishitua mamlaka zinazowawekea vikwazo wananchi hao ziache tabia hiyo kwa sababu ni kuwanyima haki zao na kuleta ubaguzi.

Alimueleza Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa hivi sasa kuna wananchi wengi wa Zanzibar wanazungushwa na kukoseshwa fomu za kuomba vitambulisho hivyo, kwa sababu za kisiasa, hali inayowasababishia wakose haki zao nyingi za msingi, mbali na shughuli za uchaguzi.

Kwa upande wake, Naibu Msajili huyo wa vyama vya siasa alisema amesikia malalamiko hayo na atayafanyia kazi, kwa nia ya kuinua hali ya demokrasia nchini. Alivitaka vyama vya siasa ambavyo havifanyi kazi zake ipasavyo viache tabia hiyo kwa sababu haisaidii kukuza uhai wa vyama na pia inadumaza demokrasia.

Habari na Hassan Hamad na Salmin Said

2 responses to “Barza zina historia kubwa katika siasa

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s