Sitavumilia Wazanzibari kubaguliwa-Seif

Makamu wa kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad akiwa ndani ya boti ndogo kuelekea Kisiwani Tumbatu kwa ziara ya siku moja ya kufuatlia uhai wa chama chake

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad amesema cha chake hakiwezi kukubali kuona baadhi ya wazanzibari wanaendelea kunyimwa haki yao ya kupatiwa vitambulisho vya uzanzibari ukaazi.

Amesema kuwanyima vitambulisho hivyo ni kuwanyima haki yao ya kisheria, jambo ambalo linakwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu, jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa na chama chake.

Maalim Seif ambaye pia ni makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar ametoa indari hiyo katika kisiwa cha Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja alipofanya ziara ya siku moja kisiwani humo kuangalia uhai na maendeleo ya chama chake.

“Hatuwezi kukubali nchi ikaendeshwa katika njia za ubaguzi namna hii, tumefikia maridhiano ili kusudi kila mwananchi apatiwe haki zake za kisheria, iweje leo wengine wapewe, wengine wanyimwe haki hizo”, alifoka Maalim Seif akibainisha kuwepo kwa baadhi ya vijana kutoka Tanzania bara ambao hupewa vitambulisho huku Wazanzibari wengine wenye sifa wakinyimwa.

“Naiambia serikali yangu, namwambia rais wangu kwamba kwa hili hatukubali hata siku moja, na nawambia wananchi kuwa hili nimelivalia njuga”, aliongeza kiongozi huyo wa CUF.

Amesema licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana tangu kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, ikiwa ni pamoja na kusimamia amani na utulivu uliopo nchi, lakini changamoto iliyopo kwa sasa ni kwa baadhi ya watendaji kutotekeleza majukumu yao ipasavyo kwa wananchi wakiweka mbele itikadi za vyama vyao.

“Bado wapo watendaji hasa katika ngazi ya shehia wanawahudumia wananchi kwa itikadi za vyama, nakwambieni masheha hivyo sivyo, na tukayembaini akifanya hivyo tutamchukulia hatua za kisheria.

Akielezea umuhimu wa vitambulisho hivyo Maalim Seif alisema baadhi ya watu wanalichukulia suala hili kisiasa zaidi lakini suala hilo lina umuhimu katika nyanja zote za maisha ya wazanzibari.

“Mbali na vitambulisho hivyo kutumika zaidi kwa ajili ya kura lakini kama huna Zan ID huwezi kupata ajira, huwezi kuendelea na elimu ya juu na kama polisi wanafuata sheria basi wanao uwezo kisheria wa kukusimamisha njiani na kukuomba kitambulisho, ikiwa huna inakuwa kosa la jinai”, alifahamisha.

Maalim Seif aliongeza kuwa wakati Taifa linajiandaa kuchukua maoni ya wananchi juu ya Katiba mpya wanayoitaka, kila Mzanzibari lazima awe na kitambulisho cha Ukaazi, ili aweze kushiriki kikamilifu na kulinda maslahi ya Zanzibar.

Amesema wakati wa kutoa maoni hayo juu ya mfumo wa Muungano wananchi wa Tanzania Bara na Wazanzibari kila upande utatakiwa kutoa maoni yao, ambapo kwa Zanzibar kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi kitakuwa kigezo cha kumjua Mzanzibari na hatimaye kuweza kushiriki katika kura ya maoni.

Akizungumzia nyanja za maendeleo, Makamu wa kwanza wa Rais alisema serikali inakusudia kuziendeleza sekta za uvuvi na kilimo ili ziweze kuleta tija kwa wananchi na kuongeza kipato chao, sambamba na kuongeza nafasi za ajira kwa wananchi.

Alisema viwanda vya usindikaji wa matunda na mazao ya baharini vitajengwa ambapo viwanda vya aina hiyo na vyengine vitachangia kutoa ajira kwa vijana.

“Ni matumaini yangu kuwa kutokana na mipango imara ya serikali ya umoja wa kitaifa, katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, zaidi ya nusu ya vijana wa Zanzibara watakuwa tayari wamepata ajira za kuendesha maisha yao”, alisema.

Aidha alisema serikali inaendelea kufanya mazungumzo na makampuni ya ununuzi wa mwani ili kuangalia uwezekano wa kuongeza bei kufikia angalau shilingi 1000 kwa kilo, sambamba na kuwawezesha wavuvi ili waweze kuvua katika bahari kuu.

Hassan Hamad (OMKR)

Advertisements

One response to “Sitavumilia Wazanzibari kubaguliwa-Seif

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s