Sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011

Philemon Luhanjo

Sekretarieti 13.-(1) Kutakuwa na Sekretarieti ya Tume itakayoongozwa na katibu.
(2) Katibu atateuliwa na Rais baada ya kukubaliana na Rais wa Zanzibar. (3) Mtu atakuwa na sifa ya kuteuliwa kuwa katibu endapo mtu huyo ni mtumishi wa serikali na ana taaluma ya sheria na amefanya kazi hiyo kwa muda usiopungua miaka kumi na ana mwenendo na tabia nzuri. (4) Katibu atawajibika kwa Tume na atafanya kazi na kutekeleza majukumu ya Sekretarieti. (5) Watendaji wengine wa Sekretarieti watateuliwa na waziri kwa makubaliano na waziri mwenye dhamana ya mambo ya katiba wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. (6) Sekretarieti itakuwa na idadi ya watumishi wa umma kwa kadri itakavyohitajika kwa madhumuni ya utekelezaji bora wa majukumu na matumizi ya mamlaka ya Tume. Gharama za Tume 14.-(1) Gharama za shughuli za Tume wakati wa mchakato wa mapitio ya katiba kwa mujibu wa sheria hii zitalipwa kutoka mfuko mkuu wa Hazina. (2) Wajumbe wa Tume na Sekretarieti watalipwa kwa kadri waziri atakavyoamua kulingana na sheria na kanuni za nchi.

SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA YA MWAKA 2011

MPANGILIO WA VIFUNGU

Kifungu Maelezo

SEHEMU YA KWANZA
MASHARTI YA UTANGULIZI

1. Jina na kuanza kutumika
2. Matumizi
3. Tafsiri
SEHEMU YA PILI
MADHUMUNI
4. Madhumuni
SEHEMU YA TATU
UUNDAJI WA TUME
5. Uundaji wa Tume
6. Uteuzi wa wajumbe wa Tume
7. Muundo wa Tume
8. Hadidu za Rejea
9. Kazi za Tume
10. Uhuru wa Tume
11. Kiapo cha wajumbe na Katibu.
12. Ukomo wa ujumbe
13. Sekretarieti.
14. Gharama za Tume
15. Kinga kwa wajumbe wa Tume na Sekretarieti

SEHEMU YA NNE

UTARATIBU WA UTENDAJI KAZI WA TUME

16. Utaratibu wa utendaji kazi.
17. Ripoti ya Tume.
18. Uwasilishaji wa ripoti ya Tume.
19. Makosa na adhabu.

SEHEMU YA TANO

KUUNDWA BUNGE LA KATIBA
20. Kuundwa Bunge la katiba.
21. Spika na Naibu Spika wa Bunge la katiba.
22. Katibu na watumishi wa Bunge la katiba.
23. Mamlaka ya Bunge la katiba.
24. Masharti kuhusu Bunge la katiba.
25. Sheria za Bunge la katiba.
26. Ukomo wa mamlaka ya Bunge la katiba.

SEHEMU YA SITA

UHALALISHAJI WA KATIBA INAYOPENDEKEZWA

27. Utendeshaji wa kura ya maoni.
28. Swali la Kura ya maoni.
29. Taarifa ya uendeshaji wa kura katika kura ya maoni.
30. Haki ya kupiga kura katika kura ya maoni
31. Utaratibu wa kuendesha kura ya maoni
32. Matokeo ya Kura ya maoni.
33. Kuvunjwa kwa Tume.
34. Kuanza kutumia kwa katiba.

_____

MAJEDWALI
_____

____

TAARIFA
____
Muswada huu, utakaowasilishwa Bungeni ulichapishwa katika Toleo Maalum la Muswada Na.1 wa tarehe 11 March, 2011 na kusomwa mara ya kwanza Bungeni tarehe 5 Aprili, 2011. Muswada huu sasa unachapishwa tena kwa lugha ya Kiswahili na kiingereza kwa madhumuni ya kusomwa mara ya pili na kusomwa mara ya tatu.

Dar es Salaam, PHILLEMON L.LUHANJO,
9 Juni, 2011

MUSWADA
wa
Sheria kwa ajili ya kuunda Tume ya Mabadiliko ya katiba kwa madhumuni ya kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi juu ya katiba; kuainisha na kuchambua maoni ya wananchi;kuainisha masharti kuhusu mabaraza ya kuhalalisha masharti yaliyomo kwenye Rasimu ya katiba; kuweka masharti juu ya utayarishaji na uwasilishaji wa ripoti kuhusu maoni ya wananchi;kuweka utaratibu wa kuunda Bunge la katiba, uendeshaji wa kura ya maoni na kuweka Bunge la katiba, uendeshaji wa kura ya maoni na kuweka masharti yanayohusiana na mambo hayo.

IMETUNGWA Na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

SEHEMU YA KWANZA

MASHARTI YA UTANGULIZI

Jina na 1.-(1) Sheria hii itaitwa Sheria ya Mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011.
Sheria
Kuanza
Kutumia
(2) Sheria hii itaanza kutumika tarehe 1 Desemba, 2011.
Matumizi 2. Sheria hii itatumikaTanzania Bara na Tanzania Zanzibar

Tafsiri 3. Katiba Sheria hii, isipokua kama muktadha utahitaji vinginevyo:
“Katiba” maana yake ni sheria ya msingi, iliyoandikwa au isiyoandikwa, ambayo inaweka mfumo wa Taifa kwa kuanisha misingi ya taifa ambayo jamii italazimika kuifuata, mgawanyo wa madaraka na majukumu ya mihimili mikuu ya dola, kwa kuanisha muundo wa serikali, bunge na mahakama, usimamizi wake mgawanyo na ukomo wa mamlaka ya vyombo mbalimbali vya dola, na kwa kuanisha namna na taratibu za utekelezaji wa mamlaka yao;

Sura ya 2 ‘Katiba “maana yake ni Katiba ya Jamuhuri ya muungno wa Tanzania ya mwaka 1977;
“Katiba inayopendekezwa” maana yake ni Risimu ya katiba iliyopitishwa na Bunge la katiba kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni; “Katibu” maana yake ni katibu aliyetanjwa chini ya kifungu cha 13;
“Kura ya maoni” maana yake ni kura iliyopingwa na wananchi kwa mujibu wa masharti ya sheria hii kwa madhumuni ya kuridhia katiba inayopendekezwa;

“Mapitio ya Katiba “maana ni mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi juu ya kutunga upya katiba ya jamuhuri ya Muungano wa Tanzania; “Mabaraza” maana yake ni mikutano, mikusanyiko, hadhara au majadiliano huru na ya wazi yaliyotayarishwa au kuandaliwa na Tume kwa madhumuni ya kukusanya maoni ya wananchi juu ya Rasimu ya Muswada wa katiba;

“Maoni ya wananchi” maana yake ni mawazo, maoni, fikra, taarifa au mapendekezo yaliyokusanywa kotoka kwa wananchi kwa madhumuni ya mchakato wa mabadiliko ya katiba; Sura ya 2 “Rais” maana yake ni Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania; “Tume” maana yake ni Tume iliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mchakato wa mabadiliko ya katiba; “Waziri” maana yake ni Waziri wa serikali ya jamuhuri ya Muungano mwenye dhamana ya mambo ya katiba.

SEHEMU YA PILI

MADHUMUNI

Madhumuni 4. Madhumuni ya Sheria hii yatakuwa ni;
a) Kuweka utaratibu wa kuunda Tume itakayokusanya na kuratibu maoni ya wananchi;
b) Kuanisha viapo au yamini na kuweka taratibu kuhusu namna ya wajumbe wa Tume na Sekretarieti watakavyoapa au kula yamini;
c) Kuweka masharti kuhusu Hadidu za Rejea za Tume;
d) Kuweka masharti ya kuundwa kwa Sekretarieti ya Tume itakayoongozwa na katibu;
e) Kuweka utaratibu ambao utaruhusu wananchi kushiriki kwa mapema katika kutoa na kuwasilisha maoni yao kuhusu katiba;
f) Kuweka utaratibu ambao Tume itatumia katika kutayarisha na kuwasilisha ripoti;
g) Kuainisha majukumu na mamlaka ya Tume;
h) Kuweka utaratibu kuhusu namna ambayo Tume itakusanya maoni kutoka katika taasisi za umma na binafsi, vyama vya hiari na mashirika ya kidini;
i) Kuweka utaratibu utakaowezesha Tume kupata taarifa za kitaalam kutoka kwa wataalam elekezi;
j) Kwa ujumla, kuweka utaratibu utakaowezesha kujenga muafaka wa kitaifa katika masuala yenye maslahi kwa taifa wakati wa mchakato kukhusu katiba;
k) Kuweka utaratibu utakaoweza kuchambua Rasimu ya Muswada wa katiba;
l) Kuanzisha mfumo wa kisheria utakaomwezesha Rais kuunda Bunge La katiba;
m) Kuweka mfumo utakaowezesha uchaguzi wa spika na Naibu wa Bunge la katiba na kupatikana kwa katibu na watendaji wengine;
n) Kuweka mfumo wa sheria utakaowezesha kupiga kura ya maoni;na
o) Kuweka utaratibu wa namna katiba Mpya itakavyozinduliwa;

SEHEMU YA TATU

UUNDAJI WA TUME

Uundaji wa Tume 5. Rais, baada ya kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar, na kwa ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa serikali wa jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanasheria mkuu wa Zanzibar na kwa kuzingatia hali ya jamii, kisiasa na kiuchumi iliyopo katika jamuhuri ya muungano katika nyakati zote na kwa amri itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali ataunda Tume.

Uteuzi wa 6.-(1) Rais, baada ya kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar atateua wajumbe wa Tume
Wajumbe wa Tume
(2) Kwa kuzingatia masharti ya kifungu kidogo cha (3) muundo wa Tume utazingatia msingi wa kuwepo kwa uwakilishi ulio sawa kwa kila upande wa jamuhuri ya muungano.
(3) Katika kufanya uteuzi wa wajumbe wa Tume, Rais atazingatia masuala yafuatayo;
a) Uzoefu katika kufanya mapitio ya katiba na sifa za kitaalam za wajumbe kwenye mambo ya katiba, sheria , utawala , uchumi, fedha na sayansi ya jamii;
b) Jiohrafia na mtawanyiko wa watu katika jamuhuri ya muungano wa Tanzania;
c) Maslahi ya Umma;
d) Umri , jinsia na uwakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii; na
e) Vigezo vingine ambavyo Rais ataona vinafaa.
(4) Bila ya Kujali kifungu kidogo cha (3) , mtu hatakuwa na sifa za kuteuliwa kuwa mjumbe wa Tume endapo mtu huyo;
a) Ni mbunge , mjumbe wa Baraza la wawakilishi la Zanzibar, Diwani au Kiongozi wa chama cha siasa wa ngazi ya Taifa , Mkoa au Wilaya;
b) Ni mtumishi katika vyombo vya usalama;
c) Ni mtu aliyewahi kuhukumiwa kwa kutenda kosa au ni mtuhumiwa katika shauri lililopo mahakamani. linalohusu shitaka la kukosa uaminifu au maadili;au
d) Si raia wa Tanzania

Muundo wa Tume 7,-(1) Tume itakuwa na wajumbe kama ifuatayo:

a) Mwenyekiti;
b) Makamu Mwenyekiti; na
c) Makamishna wengine wasiozidi thelathini.
(2) Uteuzi wa Mwenyekiti na makamu mwenyekiti utafanyika kwa msingi kwamba iwapo mwenyekiti atatoka upande mmoja wa jamuhuri ya Muungano, basi Makamu mwenyekiti atakuwa mtu anayetoka upande mwingine wa jamuhuri ya Muungano.
(3) Wajumbe wa Tume watateuliwa kupitia amri itakayotangazwa kwenye Gazeti la serikali.
Hadidu za Rejea 8,-(1) Hadidu za rejea za Tume zitatolewa na Rais kwa makubaliano na Rais wa Zanzibar katika amri ile ile ambayo uteuzi wa wajumbe wa Tume utafanyika na kuanisha muda ambao Tume inatakiwa kukamilisha na kuwasilisha na kuwasilisha ripoti.
(2) Rais kwa makubaliano na Rais wa Zanzibar anaweza, kama hali itahitaji kufanya hivyo, kuongeza muda usiozidi miezi mitatu ili kuwezesha Tume, kukamilisha na kuwasilisha ripoti.
(3) Hazidu za rejea zitakuwa ni hati ya kisheria ambayo Tume itaizingatia katika utekelezaji wa majukumu na utumiaji wa mamlaka yake kwa mujibu wa sheria hii.
Kazi za Tume 9,-(1) Majukumu ya Tume yatakuwa ni-
a) Kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi;
b) Kupitia na kutafiti usahihi na ulinganifu wa masharti ya kikatiba yanayohusu mamlaka ya watu, mifumo ya kisiasa, demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora;
c) Kutoa mapendekezo kwa kila hadidu ya rejea;na
d) Kuandaa na kuwasilisha ripoti
(2) Katika kutekeleza masharti ya kifungu kidogo cha (1), Tume itazingatia misingi mikuu ya kitaifa na maadili ya jamii na kwa mantiki hiyo, kuhifadhi na kudumisha mambo yafuatayo:
a) Kuwepo kwa jamuhuri ya Muungano ;
b) Uwepo wa serikali, Bunge na Mahakama;
c) Mfumo wa kiutawala wa kijamuhuri;
d) Uwepo wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar;
e) Umoja wakitaifa,amani na utulivu;
f) Uchaguzi wa kidemokrasia wa mara kwa mara katika vipindi maalum kwa kuzingatia haki ya watu wote kupiga kura;
g) Ukuzaji na uhifadhi wa haki za binadamu;
h) Utu, usawa mbele ya Sheria na mwenendo wa sheria; na
i) Uhuru wa kuabudu na uvumilivu wa dini nyingine.

(3) Kwa madhumuni ya vifungu vya (1), (2) na kwa jambo lolote jingine muhimu kwa taifa, Tume itatoa fursa kwa watu kutoa maoni yao kwa uhuru kwa lengo la kuendeleza na kuboresha masuala hayo.
Mamlaka ya Tume 10. Tume itakuwa na mamlaka na uhuru kwa kadri itakavyokuwa muhimu kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu na matumizi ya mamlaka yak echini ya sheria hii na haitaingiliwa na mtu au mamlaka yoyote

Kiapo cha wajumbe na katibu 11. Kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yake, kila mjumbe wa Tume na katibu ataapa au kula yamini mbele ya Rais kwa namna ilivyoainishwa katika jedwali la kwanza la sheria hii.

Ukomo wa wajumbe 12. –(1) Mtu atakoma kuwa mjumbe wa Tume endapo litatokea tukio lolote kati ya matukio yafuatayo:
a) Kifo;
b) Kujiuzulu;
c) Kutokuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa sababu za kiafya;
d) Kuondolewa kwa makosa ya kukiuka kanuni za maadili;
e) Kutiwa hatiani kwa kosa ambalo adhabu yake ni kifungo gerezani kwa muda usiopungua mwezi mmoja;au
f) Kupoteza sifa ambazo kwazo aliteuliwa

(2) Kwa madhumuni ya utekelezaji bora wa majukumu ya Tume, kutakuwa na kanuni za maadili kama zilivyoainishwa katika jedwali la pili la sheria hii.
(3) Mjumbe wa Tume au sekretarieti ambaye atakiuka masharti ya kanuni za maadili atapoteza sifa za kuendelea kuwa mjumbe.
Sekretarieti 13.-(1) Kutakuwa na Sekretarieti ya Tume itakayoongozwa na katibu.
(2) Katibu atateuliwa na Rais baada ya kukubaliana na Rais wa Zanzibar.
(3) Mtu atakuwa na sifa ya kuteuliwa kuwa katibu endapo mtu huyo ni mtumishi wa serikali na ana taaluma ya sheria na amefanya kazi hiyo kwa muda usiopungua miaka kumi na ana mwenendo na tabia nzuri.
(4) Katibu atawajibika kwa Tume na atafanya kazi na kutekeleza majukumu ya Sekretarieti.
(5) Watendaji wengine wa Sekretarieti watateuliwa na waziri kwa makubaliano na waziri mwenye dhamana ya mambo ya katiba wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
(6) Sekretarieti itakuwa na idadi ya watumishi wa umma kwa kadri itakavyohitajika kwa madhumuni ya utekelezaji bora wa majukumu na matumizi ya mamlaka ya Tume.
Gharama za Tume 14.-(1) Gharama za shughuli za Tume wakati wa mchakato wa mapitio ya katiba kwa mujibu wa sheria hii zitalipwa kutoka mfuko mkuu wa Hazina.
(2) Wajumbe wa Tume na Sekretarieti watalipwa kwa kadri waziri atakavyoamua kulingana na sheria na kanuni za nchi.

Kinga kwa wajumbe wa Tume na Sekretarieti 15. Mjumbe wa Tume au Sekretarieti hatashitakiwa yeye binafsi kwa ushauri la madai au jinai kutokana na jambo lolote au kitu chochote atakachofanya au kutofanya kwa nia njema kama mjumbe wa Tume au Sekretarieti katika utekelezaji wa majukumu na utumiaji wa mamlaka yak echini ya sheria hii.

SEHMU YA NNE

UTARATIBU WA UTENDAJI KAZI WA TUME

Utratibu wa utendaji kazi 16.-(1) Tume itatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria hii na hadidu za rejea.
(2) Kwa madhumuni ya utekelezaji wa kifungu kidogo cha (1), Tume itafanya kazi zifuatazo:
a) Kuandaa na kuendesha programu za kuelimisha juu ya madhumuni na majukumu ya Tume;
b) Kuitisha na kusamamia mikutano au mabaraza katika sehemu na nyakati mbakimbali kama ambavyo itakavyoamua;
c) Kutathmini na kuchambua kwa kutofautiana maoni ya wananchi yanayokubaliana na yale yasiyokubaliana; na
d) Kutayarisha na kuwasilisha ripoti kwa kuzingatia hadidu za rejea.
(3) Tume yaweza kumtaka mtu yeyote atakaye hiari kufanya hivyo kwenda mbele ya Tume kufanya majadiliano, kwa mazungumzo au kuwasilisha nyaraka, kuhusu jambo lolote la kikatiba ambalo Tume inaona ni muhimu na linahusiana na mchakato wa mapitio ya katiba.
(4) Katika kutekeleza majukumu yak echini ya sheria hii, Tume itapitia au kuchambua michango, mawazo, maoni, taarifa na mapendekezo yaliyokusanywa na kufanyiwa tathmini siku za nyuma ikiwemo:
a) Muhtasari wa maoni ya wananchi wanayokubaliana na wasiyo kubaliana kwa pande zote mbili za jamhuri ya Muungano;
b) Nyaraka zote zinazowakilisha mawazo, maoni ya wananchi kwa ujumla katika waraka wa serikali Na.1 wa mwaka 1962 kuhusu kuanzishwa kwa jamhuri ya Tanganyika, Tume ya Rais kuhusu kuanzishwa kwa mfumo wa kidemokrasia wa chama kimoja, Mapendekezo ya Halmashauri kuu ya CCM ya jamhuri mwaka 1983 kuhusu mabadiliko ya katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na katiba ya Zanzibar ya mwaka 1979, Tume ya Rais ya mfumo wa chama kimoja au vyama vingi vya siasa Tanzania ya mwaka 1991 na kamati ya kukusanya maoni kuhusu katiba (Waraka wa serikali Na.1 wa mwaka 1998);
c) Katiba ya Uhuru wa Tanganyika ya mwaka 1961;
d) Katiba ya jamhuri ya Tanganyika ya mwaka 1962
e) Hati za Muungano wa Jamhuri YA Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar;
f) Katiba ya Mpito ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1965;
g) Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977;
h) Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1979;
j) Ripoti ya pamoja ya Tume ya Fedha na Ripoti ya Shellukindo juu ya Changamoto za muungano;
k) Ripoti ya Wangwe juu uharakishaji wa shirikisho la Afrika Mashariki;
i) Tafiti za kiuchambuzi na kitaalam zitakazofanywa na Tume; na
m) Nyaraka nyingine zozote ambazo Tume itaona ni muhimu.
5. Tume yaweza.
a) Kwa Tanzania Bara, kumtaka Mkuu wa wilaya, Afisa mtendaji wa kata au mtaa au Afisa mtendaji wa kijijij kuitisha mkutano wa wakazi wa mji, kata, mtaa au kijijij, kwa vyovyote itakavyo kuwa;na
b) Kwa Tanzania Zanzibar, kumtaka Mkuu Wa wilaya au sheha kuitisha mkutano wa wakazi wa mji au shehia mbalimbali.Kwa madhumuni ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu masuala ya katiba kama yalivyoainishwa kwenye hadidu za rejea.
(6) Kwa madhumuni ya kifungu hiki, kutakuwa na mabaraza ya maapitio ya katiba.
(7) Mabaraza ya katiba yataundwa na Tume kwa muda maalum kwa kuzingatia mgawanyiko wa kijiografia wa jamhuri ya muungano na yatashirikisha na kuwakutanisha wawakilishi toka makundi mbalimbali ya watu katika jamii.
(8) Mabaraza ya katiba yatatoa ushauri juu ya Rasimu ya Muswada wa katiba kupitia mikutano maalum itakayoandaliwa na Tume.
(9) Mabaraza yanayorejewa katika kifungu kidogo cha (6) na katika vifungu vingine vya sheria hii yatakuwa maalum kwa ajili ya, na yatahudhuriwa na raia wa Tanzania pekee.
(10) Ili kutekeleza majukumu yake Kwa ufanisi, Tume inaweza kuunda kamati na inaweza kuipatia kamati yoyote iliyoiunda kazi za jumla au kazi maalum za kufanya.
(11) Tume inaweza kumshirikisha mtu yoyote au kumtumia mtaalam mwelwkwzi yeyote kama itakavyokuwa lazima kwa ajili ya utekalazaji bora wa majukumu yake.
(12) Isipikuwa kama mazingira yatahitaji vinginevyo, katika utekelezaji wa majukumu yake Tume itabuni utaratibu unaofanana ambao utakao tumika katika kila upande wa Jamuhuri ya Muungano katika ukusanyaji na uchambuzi wa maoni ya wananchi, uendeshaji wa mabaraza na uandaaji wa ripoti.
Ripoti ya tume
7-(1) Kwa msingi wa mahojiano wa uchambuzi uliofanywa na kuzingatia kifungu cha 16, Tume itatayarisha ripoti itakayokuwa na:
a) muhutasari wa maoni ya wananchi kwa kila hadithi ya rejea;
b) mapendekezo ya Tume kwa kila hadithi ya rejea;
c)ripoti za wataalam welekezi ambao Tume iliwatumia;
d)Rasimu ya Maswada wa Katiba; na
e)Taarifa nyingine yeyote muhimu.
(2) Rasimu ya Muswada wa katiba itakuwa ni kiambatisho kwenye ripoti ya Tume.
Uwasilishaji wa ripoti ya tume
18-(1) Baada ya Tume kumaliza kazi yake, itawasilisha ripoti kwa Rais na Rais wa Zanzibar.
(2) Baada ya kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar na baada ya kukamilisha majadiliano kuhusu masuala ya kisera na taratibu za kiutendaji, Rais atamuagiza Waziri kuwasilisha Muswada wa Katiba katika Bunge la Katiba.
19-(1) Mtu atakayemkwamisha, kumkwaza aua kumzuia mjumbe wa. Tume au sekretarieti kutekeleza mujukumu au kutekeleka mamlaka ya Tume au sekretarieti atakuwa ametenda kosa.
(2) Mtu atakaepatikana na hatia kwa kosa la kuvunja masharti ya kifungu kidogo cha (1) atawajibika kulipa faini isiyozidi shilingi milioni tano au kutumikia kifungo cha kipindi kisichozidi miezi kumi na mbili.

SEHEMU YA TANO

KUUNDWA BUNGE LA KATIBA

Tamko la Bunge la Katiba. 20-(1) Rias, baada ya kukubaliana na Rais wa Zanzibarna kwa ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, kwa kupitia Tangazo la Serikali, ataunda Bunge la Katiba.
(2)Bila ya kuathiri masharti ya kifungu kidogo cha (1), Bunge la Katiba litakuwa na wajumbe wa aina zifuatazo, yaani:
(a) Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
(b) Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar;
(c) Mawaziri wenye dhamana ya mambo ya katiba wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
(d) Mwanasheria Mkuu wa Serikaliya Jamhuri ya Muungano na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar; na
(e) Wajumbe mia moja na kumi na sita watakao teuliwa kutoka:
i. Asai zisizokuwa za kiserikali;
ii. Asasi za kidini;
iii. Vyama vya siasa vilivyo na usajili wa kudumu;
iv. Taasisi za elimu ya juu; na
v. Makundi yenye mahitaji maalumkatika jamii.
(3) Kwa madhumuni ya kifungu kidogo cha (2), idadi wa wajumbe wa Bunge la katiba ya kutika Tanzania Zanzibar wataopatikana kwa mujibu wa aya ya (a) hadi (e) haitapungua theluthi moja ya Wajumbe wote wa Bunge la katiba.
(4) Rais atachapisha majina ya watu atakaowateuwa kuwa wajumbe wa Bunge la katiba pamoja na wajumbe waliotajwa katika kifungu kidogo cha (2) katika Tangazo la Serikali litakalochapishwa kwa mujibu wa masharti ya kifungu kidogo cha (1).
21-(1) Siku ya kwanza ya kikao cha Bunge la Katiba, watawachagua Spika na Naibu Spika wa Bunge la Katiba.
(2) Spika na Naibu Spika wa Bunge la katiba watachaguliwa kutoka miongoni mwa wajumbe wa Bunge la Katiba kwa msingi Kwamba endap Spika atatoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, basi Naibu Spika atatoka upande mwingine wa Jamhuri ya Muungano.
(3) Uchaguzi wa Spika na Naibu Spika ataendeshwa kwa kura ya siri na mshindi atachaguliwa kutokana na wingi wa kura.
(4) Kabla ya kushika madaraka, Spika na Naibu Spika wa Bunge la Katiba wataapa au kula yamini, vyovyote itakavyokuwa, mbele ya Bunge la Katiba kama ilivyoainishwa kwenye kanuni za kudumu za Bunge.
22-(1) Mara baada ya Rais kulitangaza Bunge laKatiba na kwa kizingatia masharti ya kifungu kidogocha (2), Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, kwa mujibu wa sheria hii, watakuwa katibu na Naibu Katibu wa Bunge la Katiba au kinyume chake.
(2) Katibu wa Bunge na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, watashika nyadhifa zao kwa msingi kwamba, endapo Spika atachaguliwa kutoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano basi Katibu wa Bunge la Katiba atatoka upande wa piliwa Jamhuri ya Muungano.
(3) Katibu ` wa Bunge la Katiba na Naibu Katibu wa Bunge la Katiba watatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa maelekezo wa Spika au Naibu Spika kadri itakavyokuwa.
(4) Katibu wa Bunge la katiba baada ya kushauriana na Naibu Katibu wa Bunge la katiba watateuwa watumishi kutoka kwenye Bunge na Baraza la Wawakilishi kwa idadi watayoona inafaa kwa ajili ya kutekeleza kwa ufanisi majukumu ya Bunge la katiba.
(5) Katibu na Naibu Katibu wa Bunge la katiba, kabla ya kushika madaraka yao wataapa au kula yamini mbele ya Rais kwa namna ilivyoainishwa mbele ya Jadweli la Taifa la Sheria hii.
23-(1) Bunge la katiba litakuwa na mamlaka na litatumia mamlaka hayo kutunga upya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutunga masharti yatokanayo, masharti ya mpito na vile vile kutunga na kuweka masharti mengine kama Bunge la katiba litakavyoona linafaa.
(2) Mamlaka ya Bunge la Katiba kutunga masharti ya katiba Musawda utakaowasilishwa na Waziri na kupitishwa na Bunge la Katiba.
24-(1) Bunge la katiba linaweza kuandaa kanuni kwa ajili ya kuendesha shughuli katika Bunge la Katiba.
(2) Bila ya kuathiri kifungu kidogo cha (1) na kwa kuzingatia marekebisho yatayolazimu, Bunge la Katiba linaweza kutumia kanunia za kudumu za Bunge na masharti yote yanayohusu upitishaji wa Miswada ya Sheria yanayotumiwa na Bunge.
(3) Ili masharti ya Mswada wa Katiba yapate kupitishwa katika Bunge la Katiba, yatahitaji kuungwa mkono kwa wingi theluthi mbili ya idadi ya Wajumbe wote wa Bunge la Katiba kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya idadi ya Wajumbe wote wa Bunge la Katiba kutoka Tanzania Zanzibar.
25-(1) Kwa kuzingatia masharti ya nsheria yoyote ya Bunge la Katiba, Sheria ya Tafsiri za sheria itatumika katika kutoa tafsiri kwa sheria ya Bunge la Katiba na kwamba rejea kwenye Sheria hiyo au Sheria nyingine yoyote, isipokuwa kama maktadha utahitaji vinginevyo, itajumuisha rejea kwenye sheria ya Bunge la Katiba.
(2) Kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge la Katiba, na kwa madhumuni hayo, masharti ya ibara 100 ya katiba na Sheria ya kinga, Madaraka na Haki ya Bunge, kwa kuzingatia marekebisho yatayolazimu, yatatumika katika Bunge la Katiba.
26-(1) Baada ya kutunga katiba, masharti yatokanayo, na masharti ya mpito yatakoma.
(2) Kuvunjwa na kukoma kwa mamlaka ya Bunge la Katiba hakutachukuliwa kuwa kunaondoa mamlaka ya Raia kuliitisha tene Bunge la Katiba lenye wajumbe wale wale siku zijazo kwa ajili ya kutunga masharti ya katiba kabla ya kuizindua katiba inavyopelekezwa kwa lengo la kurekebisha masharti yaliyomo katiba iliyopendekezwa.

SEHEMU YA SITA

UHALALISHAJI WA KATIBA INAYOPENDEKEZWA

27-(1) Kwa madhumuni ya kuyapatia uhalali masharti yaliyomo kwenye katiba, kutakuwa na kura ya maoni itakayoandaliwa, kuendeshwa na kusimamiwana Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirirkiana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
(2) Katika utekelezaji wa kifungu kidogo cha (1), Tume ya Uchaguzi Zanzibar itandaa, kuendesha na kusimamia upigaji wa kura ya maoni, kasha itawasilisha kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi matokeo ya kura zilizopigwa Tanzania Zanzibar kwa ajili ya kutangazwa.
28-(1) Ndani ya siki saba baada ya kuchapishwa kwa Katiba, Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar itatayarisha na kuchapisha kwenye Gazeti la Serikali swali litakaloamuliwa kwa kura ya maoni.
(2) Swali linalorejewa katika kifungu cha kidogo cha (1) litatayariswa baada ya mashauriano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano akishirikiana na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.
(3) Swali litakaloulizwa katika kura ya maonilitamtaka mpiga kura kuonyesha kuwa anaridhia au kutoridhia katiba hiyo na litatayarishwa kwa namna ambayo litamtaka mpiga kura kujibu ‘Ndio’ au ‘Hapana’.
(4) Upigaji kura ya maoniutakuwa wa siri.
29-(1) Ndani ya siku kumi na nne baada ya kuchapishwa kwa swali katika Gazeti la Serikali, Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar itaainisha:
(a) Siku ambayo kura ya maoni itafanyika;
(b) Muda wa upigaji kura ya maoni; na
(d) Muda wa kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu kuipigia kura ya maoni katiba inayopendekezwa, Tume italazimika, na vyama vya siasa na vyama vya kijamii vinaweza kutoa elimu ya uraia na kuhamasisha upigaji wa kura ya maoni.
(3)Ndani ya siku ishirini na moja baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza taarifa, msimamizi wa uchaguzi wa kila jimbo la uchaguzi atatoa taarifa kwa wananchi kuhusu utaratibu wa uendeshaji wa kura za maoni.
30.Mtu ambaye jina lake limeingizwa katika Daftari la kudumu la wapiga kuralililoanziswa chini ya sheria ya Taifa ya Uchaguzi na Daftari la Wakazi wa Zanzibar lililoanziswa chini ya sheria ya Uchaguzi Zanzibar ya mwaka 1984, atakuwa na haki ya kupiga kura isipokuwa kama mtu huyo atakuwa amezuiwa kupiga kura na sheria nyingine yoyopte.
31. Utaratibu wa uendeshaji wa Uchaguzi Mkuu chini ya sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibarya mwaka 1984 na sheria ya Uchaguzi wa Serikali ya Mitaa na kwa kufanya marekebisho yatakayolazimu, utatumika katika kuendesha kura ya maoni kwa mujibu wa sheria hii.
32-(1) Matokeo ya kura ya maoni yataamuliwa kutokana na wingi wa kura zote zilizopigwa kwa swali litakalopigiwa kura ya maoni na matokeo yatakayotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi yataheshimiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
(2) Matokeo ya kura ya maoni yataanuliwa kwa msingi mkono kwa asilimia inayozidi hamsini ya jumla ya kura zote zilizopigwa kutoka Tanzania Bara na asilimia inayozidi hamsini ya jumla ya kura zote zilizopigwa kutoka Tanzania Zanzibar.
(3) Endapo patakuwa na kulingana kwa kura za ‘DNIYO’ na ‘HAPANA’ katika swali linalopigiwa kura ya maoni, basi, kwa kupitia taarifa itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali na ndani ya siku thelathini baada ya kutangaza matokeo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi itateuwa siku nyingine ya kurudiwa kwa upigaji kura ya maoni na utaratibu wa kura ya maoni utaanza upya.
(4) Endapo wingi wa kura ya maoni utakuwa ni ‘HAPANA’, Katika Jamhuri ya Muunganoya mwaka 1977, itaendelea kutumika.
33-(1) Matokeo ya kura ya maoni kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Rais kwa kupitiwa amri iliyochapishwa kwenye Gazeti la Serikali, ataivunja Tume.
(2) Kuvunjwa kwa Tume kwa amri ya Rais kutakuwa na maana ya ukomo wa mamlaka ya Tume na Sekretarieti.
34-(1) Masharti ya Katiba Mpya yataanza kutumika tarehe itakayotajwa kwenye Katiba hiyo.
(2) Rais atazindua kwa namna atakayoona inafaa kuanza kutumika kwa Katiba Mpya.
(3) Baada ya kuzinduliwa kwa Katiba Mpya, sheria hii itakuwa imemaliza matumizi yake na itapoteza nguvu ya kisheria.
(4) Katika matumizi ya sheria hii, toleo la lugha ya Kiswahili na toleo la lugha ya kiingereza yote ni sahihi.
_____
JADWELI LA KWANZA
_____
(Chini ya kifungu 11)
________

SEHEMU YA 1

KIAPO/YAMINIYA MJUMBE WA TUME

Mimi……………………………………………..nilikuwa nimeteuliwa na Rais kuwa………………………………………tarehe………………………….siku ya ……………………………………………..2011kufanya kazi mjumbe wa Tume,naapa/nathibitisha kwamba nitakuwa mtiifu na bila na bila kuwa naupendeleo na kwa kadri ya uwezo na ufahamu wangu, nitatimiza wajibu wangu na kufanya kazi zinazonihusu kama Mjumbe wa Tume.
Ewe Mungu nisaidie.
…………………….
Mjumbe wa Tume

SEHEMU YA 11

KIAPO/ YAMINI YA KATIBU/ NAIBU KATIBU.

Mimi…………………………………nilikuwa nimeteuliwa na Rais kuwa………………………………….tarehe……………………….siku ya …………………….20………………..kufanya kazi ya kutibu, naapa/ nathibitisha kwamba nitakuwa mtiifu na bila ya upendeleo na kadri ya uwezo naufahamu wangu, nitatimiza wajibu wangu kufanyakazi zinazonihusu kama katibu,.
Ewe Mungu nisaidie.
……………………..
Katibu
______________
JADWELI LA PILI
_______________
(Chini ya kifungu 12(2))

KANUNI ZA MAADILI YA WAJUMBE WA TUME NA SEKRETARIETI

1. Kila mjumbe wa Tume / sekretarieti atapaswa kufanya kazi zake kwa uadilifu bila ya upendeleo na bila kuingiliwa na atafanya kazi za ofisi yake kwa nia njema na bila woga, upendekeo au chuki.
2. Mjumbe wa Tume / sekretarieti katika kipindi cha kutumikia yake, hatakuwa na sifa ya kuteuliwa au kuchaguliwa kwenye nafsi yoyote ya kisiasa.
3. Mjumbe wa Tume / sekretarieti.
(a) Kupitia ujumbe wake, hatoshiriki, hatatoa kauli, kufanya matendo au kwa namna yoyote ile kuhatarisha uhuru wa mjumbe au kuathiri hadhi, uadilifu, uhuru au hadhi ya Tume;au
(b) Kutumia kwa manufaa yake au kufaidika na taarifa yoyote ya siri akiwa kama mjumbe wa Tume.
_________________
JADWELI LA TATU
___________________
(Chini ya kifungu 22(4))
________________

KIAPO / YAMINI YA KATIBU WA BUNGE LA KATIBA

Mimi……………………………………….nilikuwa nimeteuliwa siku ya…………………….20…….kwa mujibu wa sheria kufanya kazi za katibu wa Bunge la katiba, naapa / nathibitisha kwamba nitakuwa mtiifu na bila upendeleo na kwa kadri ya uwezo na ufahamu wangu, nitatimiza wajibu wangu wa kufanya kazi zinazonihusu kama katibu wa Bunge la Katiba.
Ewe Mungu nisaidie.
……………………..
Katibu wa Bunge la Katiba

___________________
MADHUMUNI NA SABABU
_____________________
Muswada huu ambao umegawanyika katika sehemu sita unapendekezwa kutungwa kwa sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Nchi ya mwaka 2011. Mchakato wa mabadiliko ya Katiba pamoja na masuala mengine utaangalia chimbuko na mahusiano ya Katiba iliyopo kwa kuzingatia uhuru wa wananchi, mfumo wa siasa, demokrasia na utawala bora. Utaratibu wa kisheria unaopendekezwa utawahusisha na kuwashirikisha wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mchakato wa mabadiliko ya katiba ya nchi. Endapo Muswada huu utapitishwa na kuwa sheria, kutakuwa na utaratibu wa kisheria utakaomwezesha Rais kuunda Tume ya kukusanya maoni kuhusu katiba na kuunda Bunge la Katiba kwa madhumuni ya kutunga katiba mpya.

Awali, Muswada huu uliwasiliswa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano na kusomwa kwa Mara ya kwanza tarehe 5 mwezi Aprili 2011. Muswada uliwasilishwa kwenye kikao cha wadau kilichoandaliwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano na uliendeshwa kwa wakati mmoja katika miji ya Dododma, Dar-es-salaam na Zanzibar kuanzia tarehe 7 Aprili 2011 hadi tarehe 9 Aprili 2011. Muswada huu sasa umetangazwa kwa mara nyingine kwa kuchapiswa kwenye Gazeti la Serikali kwa lugha za Kiingereza na lugha ya Kiswahili kwa madhumuni ya kusomwa kwa Mara ya pili na kusomwa kwa mara ya tatu.

Sehemu ya kwanza inaweka masharti ya utangulizi ambayo inajumuisha jina la sheria inayopendekezwa, tarehe ya kuanza kutumika na matumizi ya sheria inayopendekezwa. Inaendelea kutoa tafsiri ya baadhi ya misamiati na maneno yoliyotumika na mamlaka zilizotajwa katika Muswada.

Sehemu ya pili inaweka masharti yanayohusu madhumuni ya Muswada. Sehemu hii inaainisha kwa undani madhumuni ya chimbuko la mcakato wa mabadiliko ya Katiba, ikijumuisha viapo vya yamini za Wajumbe wa Tume na Sekretarieti na utaratibu wa kuendesha mchakato wa mabadiliko ya katiba utakavyofanywa.

Sehemu ya tatu inaweka masharti kuanzishwa kwa Tume na kuainisha utaratibu na kukusanya maoni. Tume hii itaundwa na Rais wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Muungano na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Masharti mengine yaliyomo katika sehemu hii ni kuteuliwa kwa wajumbe wa Tume ambao watatoka katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano kwa idadi sawa na majina yaokutangazwa kwenye Gazeti la Serikali. Aidha sehemu hii pia inaweka masharti kuhusu mambo ambayo yanapaswa kuzingatia na kilindwa katika mchakato wa kukusanya maoni kutokana na umuhimu na uzito wake katika Taifa letu na inaweka masharti na inaweka masharti ya utaratibu wa Tume kuwasilisha taarifa na kinga kwa wajumbe wa Tume na Sekretarieti.

Sehemu ya nne inaweka masharti kuhusu utaratibu wa wa utendaji kazi wa Tume pamoja na kuanisha kazi, wajibu wa mamlaka ya Tume. Sehemu hii pia inaitaka Tume kutayarisha ripoti ambayo itaambatisha rasimu ya Muswada wa katiba na kiwasilisha kwa Rais na Rais wa Zanzibar.

Sehemu ya tano inaweka masharti ya kuundwa kwa Bunge la Katiba ambapo Rais atashauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar baada ya kupata ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa serikali ya Muungano na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wataunda Bunge la Katiba. Utaratibu wa kuwapata Wajumbe wa Bunge la Katiba, utaratibu wa kuwapata spika Naibu Spika, katibu na Naibu Katibu wa Bunge la katiba na jinsi watakavyoapishwa umeaminishwa. Aidha, mamlaka ya Bunge la katiba na masharti kuhusu Bunge la Katkba pia yameelezwa kwa lina.
Masharti mengine yaliyomo ni namna ya kuwapata makatibu Wasaidizi wa Bunge la Katiba, masharti yatokanayo na masharti ya mpito, sheria na kanuni zitakazotumika katika kuongoza Bunge la Katiba na kuvunjwa kwa Bunge la katiba.

Sehemu ya sita inahusu uhalalishaji wa katiba inayopendekezwa kwa utaratibu wa kura ya maoni, utaratibu wa uendeshaji wa kura ya maoni itakavyotolewa, ikiwa ni pamoja na haki ya wananchi kupiga kura ya maoni kama inavyoelekezwa na sheria ya Taifa ya Uchaguzi na sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Wakati wa mchakato wa kura ya maoni, wananchi watahamasishwa kupitia vipindi maalum vitakavyoendeshwa na vyama vya kiraia, vyama vya siasa na Tume. Kura ya maoni itaendeshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kutumia Daftari la kudumu la Wapiga kura, kwa upande wa Tanzania Bara na Daftari la Wakazi, kwa upande wa Tanzania Zanzibar.

Katiba Mpya itabainisha tarehe ya kuanza kutumika na namna Rais atakavyoizindua na kuanza kutumika. Sheria hii inayopandekezwa , ambayo kimsingi sasa itakoma kutumika na masharti yake yatapoteza nguvu ya kisheria mara tu Baada ya kuzinduliwa kwa Katiba Mpya.

Dar es salaam, CELINA O. KOMBANI,
8 Machi,2011 Waziri wa katiba na sheria

.(2) Katika utekelezaji wa kifungu kidogo cha (1), Tume ya Uchaguzi Zanzibar itandaa, kuendesha na kusimamia upigaji wa kura ya maoni, kasha itawasilisha kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi matokeo ya kura zilizopigwa Tanzania Zanzibar kwa ajili ya kutangazwa.

Advertisements

One response to “Sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s