Muswada wa Katiba bungeni kuanza leo

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Neville Meena, Dodoma
MVUTANO mkali unatarajiwa kuibuka bungeni kuanzia leo wakati wa mjadala wa muswada wa Sheria ya Mapitio na Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011 utakapowasilishwa.Dalili za kuwepo kwa mvutano zilianza kujitokeza juzi Jumamosi wakati wabunge walipokutana kwenye semina kuhusu muswada huo, kubwa likiwa ni kile upande wa upinzani unachoidai kuwa ni madaraka makubwa aliyopewa Rais katika mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya.

Jana, Kamati ya Bunge ya Katiba Sheria na Utawala ilikutana ikiwa ni siku ya tano mfululizo kukamilisha taarifa ya maoni yake ambayo yatasomwa bungeni ‘kuunga mkono hoja’ itakayokuwa imewasilishwa awali na Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Pindi Chana alisema jana kuwa kamati yake ilikuwa imekamilisha kujadili muswada huo na kwamba tayari taarifa ya kukamilika kwake imewasilishwa kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda.

“Kamati imekamisha kazi yake na tayari tumemwandikia Spika, kwa hiyo kama muswada huu utasomwa kwa mara ya pili kesho kama ilivyo kwenye ratiba, basi sisi tupo tayari kutoa maoni yetu,” alisema Chana kwa simu jana.
Hata hivyo, habari zilizopatikana zinadai kuwa juzi katika kikao ambacho kilifanyika baada ya semina, wajumbe wa kamati hiyo waliendelea kutokubaliana katika baadhi ya maeneo hasa yale yanayohusu mamlaka ya Rais.

Kadhalika, watendaji wa sekta ya sheria serikalini wakiongozwa na Waziri Kombani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, jana walishinda kwenye vikao wakifanya maandalizi ya mwisho ili kuwezesha uwasilishwaji wa muswada huo bungeni leo.

Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema muswada huo utasomwa kwa mara ya pili bungeni leo na hakuna mabadiliko ya ratiba licha ya kutohitimishwa Ijumaa iliyopita kwa muswada wa Sheria ya Ununuzi wa Umma wa mwaka 2011 ambao utahitimishwa leo.

Kwa kauli ya Joel, huenda muswada wa Katiba ukasomwa katika kikao kitakachoanza saa 11.00 jioni na mjadala wake kwa mujibu wa ratiba ya mkutano wa tano, utaendelea hadi keshokutwa Jumatano.

Kanuni za Bunge toleo la 2007, zinasema vikao vyote vya Bunge lazima vianze kwa kipindi cha maswali na majibu, kwa maana hiyo ni dhahiri muswada wa Ununuzi wa Umma utaanza kuhitimishwa baada ya kipindi hicho na kukamilika kabla ya mapumziko ya mchana leo.

Mvutano wa wabunge
Juzi wakati wa semina, wabunge wa CCM walionekana kutofautiana na wa upinzani kimawazo.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Chiku Abwao alijikuta akizomewa na wabunge wa CCM pale alipojaribu kutambua mchango wa wana harakati katika mchakato wa kuwezesha kupatikana kwa Katiba Mpya.Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR – Mageuzi), David Kafulila alisema: “Madaraka ya Rais ni makubwa mno katika mchakato mzima,” hivyo kushauri yapunguzwe.

Kauli ya Kafulila ambaye ni mmoja wa wabunge walioteuliwa na Spika Makinda kuongeza nguvu kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ilikinzana na ya mjumbe mwenzake, Christopher Ole Sendeka wa Simanjiro (CCM), ambaye alibeza mawazo ya wale walioonekana kuukosoa muswada huo.

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alisema miongoni mwa kasoro zilizopo ni mchakato wa kura ya maoni kuratibiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi hali Watanzania wengi wakiwa hawana imani nayo, hivyo matokeo yake yanaweza kuzua mgogoro siku zijazo.

Uchambuzi wa Kafulila
Akizungumzia hoja yake katika semina hiyo jana, Kafulila alinukuu kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Mon akisema “Tatizo kwa nchi maskini duniani siyo nakisi ya bajeti, bali ni nakisi ya imani ya umma kwa watawala,” akisema na kwa Tanzania, tatizo hilo ndiyo msingi wa kuhitajika kwa Katiba Mpya.

“Ibara ya 5 ya Muswada inaeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar ndiye mwenye mamlaka ya Kuunda Tume. Mimi nashauri Rais apendekeze majina ya wajumbe wa Tume yatangazwe katika Gazeti la Serikali uwepo muda wa umma kutafakari, kisha yapitishwe na Bunge,” alisema na kuongeza:

“Pia kwenye kuwaondoa (wajumbe wa tume) isiwe kama inavyotamkwa, tuweke mchakato mgumu kama ilivyo kwa majaji, kwamba Rais atoe pendekezo na kiwepo chombo cha kupitia pendekezo hilo.”

Alisema Rais pia anapewa madaraka katika Ibara ya 8(1) ya Muswada huo kwa kutoa hadidu za rejea kwa Tume ya Kukusanya maoni huku Ibara ya 13(2) ikimpa Rais wajibu wa kuteua Katibu wa Sekretarieti ya Tume.

“Hiki (sekretarieti) ni chombo cha kiutendaji chini ya mamlaka ya Tume. Kama Tume itapatikana kwa namna nilivyoeleza, nashauri sekretarieti iteuliwe na tume yenyewe ila iwajibike kwa tume na kuepusha nguvu na mamlaka za Rais katika shughuli za utendaji,” alisema.

Aliitaja kasoro nyingine kuwa ipo kwenye Ibara ya 13(5) ambayo inampa Waziri mamlaka ya kuwalipa wajumbe wa sekretarieti kadri atakavyoamua kulingana na sheria na kanuni za nchi na kwamba hali hiyo inaweza kukwaza uhuru na uwazi wa wajumbe hao.

Alishauri kuwa viwango na utaratibu wa malipo viwekwe wazi na kuondoa uwezekano wa Serikali kuamua mwelekeo wa kiutendaji wa Tume kwa kuwa majaaliwa ya utendaji yamefungwa mikononi mwa wizara.
Kafulika pia alikosoa Ibara 18(1) inayohusu uwasilishaji wa ripoti ya tume, kwamba kipengele hicho kinampa Rais mamlaka ya kuamua Katiba iwe ya namna gani.

“Bunge likipitisha Katiba inayopendekezwa, haifai Rais tena aboreshe na badala yake Katiba inayopendekezwa inapaswa kupelekwa kwa wananchi. Baada ya Tume kukamilisha kazi yake haipaswi kuwasilisha ripoti kwanza kwa Rais, inapaswa iwasilishwe kwa wananchi kwa kuchapwa kwenye gazeti na uwepo muda umma kujiridhisha kama hicho kilichochapwa ndiyo maoni yao,” alisema.

Alisema Mwenyekiti wa Tume ndiye anayepaswa kuwasilisha ripoti ya Tume kwenye Bunge la Katiba badala ya Waziri kwa kuwa ripoti hiyo haitakuwa ya Serikali, bali ya Tume.

Kasoro nyingine kwa mujibu wa mbunge huyo zipo kwenye Ibara ya 20(1) inayompa Rais mamlaka ya kuunda Bunge la Katiba pia Ibara ya 20(4) ambayo Rais anateua wajumbe 116 wa Bunge hilo kutoka taasisi mbalimbali za kijamii.

“Kama haiwezekani kuendesha mchakato wa uchaguzi kupata wabunge wa Bunge la Katiba, wajumbe waliobainishwa kutoka taasisi hizo wasiteuliwe na Rais moja kwa moja, badala yake taasisi tajwa zipewe mamlaka ya kuchagua wajumbe wake.”

Muswada ulikotoka
Muswada huo ulisomwa kwa mara ya kwanza Bungeni Aprili 5, mwaka huu lakini ukarejeshwa serikalini ili kufanya marekebisho kadhaa na kuandikwa kwa Kiswahili kabla ya kurejeshwa tena bungeni.

Kutokana na hali hiyo, Serikali ilipata upinzani mkali kutoka kwa wabunge na wanaharakati ambao walidai kwamba ulipaswa usomwe kwa mara ya kwanza kutokana na kufanyiwa marekebisho mengi.

Miongoni mwa wanaharakati ambao wanapinga muswada huo kusomwa kwa mara ya pili ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Jukwaa la Katiba.

Chanzo ni MWANANCHI

Advertisements

One response to “Muswada wa Katiba bungeni kuanza leo

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s