SUK na changamoto zake

Dk Ali Mohammed Shein

 

Na Ally Saleh

Ilikuwa ni siku njema kwa hakika kwa waandishi wa habari wa Zanzibar na Tanzania Bara kukaa na Dk Ali Muhammed Shein kwa zaidi ya saa tano ndani ya mjengo wa Ikulu ya Zanzibar ambao mara nyingi wengi wetu huwa tunaiona paa tu.Si aghlabu viongozi wa Kiafrika kukubali kukaa na waandishi wa habari kuzungumza nao juu ya uendeshaji wananchi, ambao kikatiba wana wajibu wa kuwaarifu wananchi juu ya kitu gani kinaendelea kila baada ya muda.

Imemchukua Dk Shein mwaka mzima kuwapa waandishi wa habari haki hiyo na kwa maana hiyo pia kuwapa haki raia kujua kwa undani Serikali yake inafanya nini, na tunasema kuwa umekuwa ni upungufu katika uendeshaji wa Serikali yake.

Na kwa hilo akajaribu kutupigia muziki katika masikio yetu kwa kusema kuwa anakusudia kuanzisha utaratibu wa kuzungumza na waandishi kila miezi mitatu na pia kuwa Makamo wake wawili na mawaziri pia watalazimika kuzungumza na waandishi wa habari juu ya majukumu walionayo.

Matamshi ya kufungua milango kwa waandishi yametetema midomoni mwa Dk Shein mara kadhaa ikiwa ni pamoja na katika hotuba yake ya kulizindua Baraza la Wawakilishi na pia tukamsikia wakati wa ziara yake ya mwanzo kutembelea Wilaya zote za Zanzibar.

Na kwa hivyo hizi hazikuwa habari mpya. Ni habari ambazo hazikutekelezwa katika hali ya uhakika kwa muda wa mwaka mmoja wa uongozi wake, kwa kuwa hilo alikwisha kusema, na wakati mwengine kwa ukali kidogo, lakini bado halikutelekezwa.

Hata yeye mwenyewe Dk Shein hakuwa mfano mzuri katika hili. Na ndio maana kiu ya waandishi ilikuwa kubwa sana walipoitwa Ikulu Novemba 3, kusherehekea mwaka mmoja wa utawala wake ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Ingawa hajakutana na waandishi wa habari kwa mwaka mzima wa uongozi wake, kwa maana ya mkutano wa waandishi wa habari, na sio mkutano wa kiwanja cha ndege akirudi katika ziara za nje, fursa hiyo waandishi waliitumia fursa hiyo kikamilifu.

Ilidhihirika kuwa hata hivyo Dk Shein ni mfuatiliaji wa vyombo vya habari, kwa kudhihirika ni msomaji mzuri wa magazeti lakini pia kumbe huwa hata na muda wa kutizama televisheni na kama alivyoonyesha ni mtizamaji wa kituo cha televisheni cha Zanzibar Broadcasting Corporation ZBC.

Kwa mfano alikuwa na taarifa ya karibuni kabisa ya michezo pale aliposema aliona mwenye habari ya timu ya soka ya Malindi kukipeleka Chama cha Soka Zanzibar ZFA katika shauri la kupinga kushushwa daraja kwa madai ya kufanyika Ligi Ndogo iliyodai ni kinyume na taratibu kwa kukosa kanuni yake wenyewe.

Lakini alionyesha kuwa ni msomaji wa magazeti pale aliposema kuwa baadhi ya wakati hukereka na yanayoandikwa na vyombo hivyo na kutoa mfano juu ya uteuzi wake wa wajumbe wa Kamati ya Uchunguzi ya kuzama kwa meli ya MV Spice Islander.

“Wakati mwengine nakereka, lakini sina haja ya kujibu,” alisema na nukuu hii ikionyesha upande mmoja kuwa na ustahamilivu na upande mmoja kukosa ustahamilivu kwa sababu kama kiongozi angepaswa kujua mpaka siku atakayoondoka madarakani vyombo vya habari vitaandika juu ya kazi na utumishi wake kwa maana yeye ndio kioo kikubwa cha jamii yake na Serikali anayoiongoza.

Lakini kwa sababu ya washauri wake, na kwa sababu ya kile yeye mwenyewe alichokiita kuchukua fursa hiyo kuzungumza na waandishi wa habari moja kwa moja, mazungumzo na waandishi wa habari basi yalitanguliwa na utangulizi mrefu wa zaidi ya saa moja na nusu.

Utangulizi huo ilikuwa ni hotuba yake ambayo alipitia sekta mbali mbali kwa ajili ya kueleza utekelezaji wa Serikali lakini kwa hakika ilituchosha waandishi wengi na hata mwenyewe Dk Shein alijua hilo.

Na alisema kuwa katika mkutano mwengine ataokuwa na waandishi wa habari hilo halitatokea kwa maana waandishi wa habari watakuwa na muda wa kutosha nae kumuuliza masuala na kupata ufafanuzi.

Lakini pia ilidhihirika wazi kuwa waandishi hawakuzingatia sana hotuba yake hiyo, ambayo pengine wangeipata kabla ingekuwa vyema, na ndio maana takriban masuala yote hayakutokana na hotuba yake hiyo ya utangulizi kwa sababu waandishi walikuja na masuala yao yanayotokana walichotumwa na wananchi kuuliza au kutumwa na hali wanavyoiona katika mwaka mmoja wa SUK.

Na mwaka mmoja wa SUK ni uchumi, ni uhaba wa ajira, ni kupanda kwa maisha, ni uwajibikaji, ni mzunguko wa fedha, ni usalama wa raia, ni usalama katika usafiri na mengi ya maisha ya kila siku.

Kwao waandishi si takwimu za idadi ya shule zilizojengwa na madarasa yake, bararaba zilizojengwa na kilomita zake, uwanja wa ndege utaojengwa na ndege zake, bandari itayojengwa na meli zake iwapo yote hayo hayakuhusishwa na ajira na maisha ya kila siku.

Na waandishi walimsikia Dk Shein akisema Serikali inaweza kuajiri watu kwa kiasi fulani tu na wakati huo huo akisita kusema idadi ya wafanyakazi wote wa Serikali, lakini hawakumsikia ni ajira ngapi zimetengenezwa katika kipindi hiki cha mwaka mmoja nje ya Serikali.

Pia waandishi walimsikia Dk Shein akisema kuwa kutekeleza Katiba ni ndani ya wakati wake (at his own pleasure) na kwa hivyo haoni kuwa anavunja Katiba kwa kutoteua Wakuu wa Wilaya na Mikoa hadi leo.
oDk. Shein hajatanabahishwa kuwa hilo si la hiari na kama halijafanywa ni kuvunja Katiba kwa sababu mara baada ya kuundwa SUK, Ma DC na Ma RC hawakutakiwa kuwa ni wanasiasa, na hilo halina mjadala kuwa wote ni wanasiasa na sio watendaji ( technocrats).

Waandishi wakamsikia Dk Shein asivyo na taarifa za kutosha juu ya suala la Vitambulisho vya Mzanzibari; asivyorifiwa vya kutosha juu ya suala la udhamini wa pombe katika michezo na hasa soka lakini ikadhihirika pia kuwa wakati taarifa alonayo juu ya mishahara mipya na posho kumbe huku nje hali si shwari kama ilivyodhihirika Novemba 4 wakati wafanyakazi wa Wizara ya Afya walivyogoma kwa saa kadhaa.

Lakini hata ndani ya taarifa yake alipozungumzia juu ya kutengwa mamilioni kujenga studio ya kurekodia nyimbo, hakuwa akijua kuwa studio zilioko Radio Zanzibar ni bora kuliko popote Afrika Mashariki na kwa hivyo hakuna haja ya kujenga nyengine mpya bali ni kuimarisha iliyopo na kama kujengwa kitu kipya basi ni nyumba ya maigizo ambayo hatunayo kabisa hapa Zanzibar, kama vile tunaishi dunia yetu wenyewe.

Nayasema haya kwa kuonyesha mambo mawili. Kwanza Rais kukaa muda mrefu bila ya kuzungumza na waandishi wa habari kunatengeneza umbwe kubwa ambalo kujazwa kwake hakutoshi kwa kukutana nae kwa saa moja au mbili.

Pili, ingefaa Dk Shein akawa na utaratibu wa kukutana na wahariri kwa maana ya kubadilishana nao fikra (for a cup of coffee) tu kwa sababu kama nilivyomwambia kuwa kwa kukutana na watu wale kwa wale kila mara anatengeneza kitu kinachoitwa mawazo feki na kwa hivyo anajengwa kuamini kinachosemwa na watu wake bila ya mjazo mpya kutoka nje ya duru yake.

Mwisho wa yote nchi ni yetu. Kama alivyo Rais na wajibu kwa wananchi na kwa hivyo anahitaji kuwafikia na njia bora ni kupitia vyombo vya habari, na waandishi pia wana dhima kwa wananchi na njia bora ya kupata undani wa utekelezaji wa Serikali ni kupitia mtendaji mkuu kwa sababu Rais wa Zanzibar pia ni mtendaji.

Hapana shaka SUK imetenda makubwa katika muda iliokuwa madarakani lakini makubwa zaidi yatakuja kwa kuendeleza ushirikiano na vyombo vya habari na kuepusha kabisa mivutano baina ya pande hizi na njia mojawapo Dk Shein anaweza kulihimiza hilo na kusukuma miswada miwili ya vyombo vya habari iliyopendekezwa na Baraza la Habari la Tanzania MCT.

Dk Shein muulize Waziri wako wa Habari, Abdillahi Jihad, mchakato wa miswada hii umefikia wapi hadi sasa ili kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari?

Source: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s