Tanzia: Buriani Badawi Qullatein, mtetezi wa wanyonge (11 Oktoba 1930 – 31 Oktoba 2011)

Badawi Qullatein zama za uhai wake

Na Ahmed Rajab

BADAWI Qullatein aliyefariki dunia Makkah Jumatatu asubuhi akiwa na umri wa miaka 81 alikuwa ni mtu wa vipaji vingi: mpigania haki za wafanya kazi, mwanamapinduzi, mhariri wa magazeti na mcha Mungu. Alikuwa mtu wa dhihaka nyingi na maskhara mengi ingawa baadhi ya nyakati akipandisha hamaki. Na ulipomwambia mbona umekasirika, akijibu: ‘Unanikasirisha, kwa nini nisikasirike? Sifa nyingine ya Badawi ilikuwa ya ukaidi.

Hata hivyo, atakumbukwa zaidi kwa jinsi alivyoutumia ujana wake kuwatetea walala hoi na kupigania haki zao. Yeye ni mfano mzuri wa mtu wa tabaka la wenye kujiweza aliyejitolea kuwapigania wasiojiweza. Hivyo ndivyo walivyokuwa wengi wa wafuasi wa Abdulrahman Babu waliojiengua kutoka chama cha Hizbu au Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na kuanzisha chama cha Umma Party mwaka 1963.

Wengine watamkumbuka Badawi kwa mchango wake katika Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964. Akiwa mmoja wa viongozi wakuu wa Umma, Badawi alikuwa na mahusiano mazuri na wanaharakati wa Afro-Shirazi Party (ASP). Kati yao walikuwa akina Seif Bakari, Hassan Nassor Moyo, Saleh Saadalla na Abdulaziz Twala, ambaye wakati mmoja akiishi pamoja naye. Wakimuamini; naye akiwaamini.

Siku moja Seif Bakari alimdokozea Badawi kwamba baada ya uhuru kutoka Uingereza watafanya fujo Unguja mjini na kutia moto majumba ya serikali. Badawi akamwambia: ‘La, lengo lisiwe kutia moto bali kuichukua serikali.’ Usiku wa manane wa kuamkia 12 Januari 1964, serikali ya Zanzibar ilipinduliwa. Miongoni mwa waliopindua walikuwa akina Seif Bakari, Yusuf Himidi, Said Washoto, Pili Khamisi, Ramadhani Haji, Said Idi Bavuai, Khamis Darweshi na Abdallah Said Natepe.

Baadaye Badawi aliwaita vijana wa Umma waliokuwa wamerudi kutoka Cuba walikopata mafunzo ya mbinu za kupindua serikali wawasaidie wapinduzi. Badawi hali kadhalika ndiye aliyekaa pamoja na ‘Field Marshal’ John Okello, Twala na Jumbe na kulipanga Baraza la Mapinduzi na lile la Baraza la Mawaziri.

Badawi aliwahi kuniambia kwamba walipokuwa wanapanga nani ashike wizara gani, Okello alimwambia: ‘Ile ya Ali Muhsin mpe Babu.’ Okello ama alisahau au hakujuwa ni wizara gani aliyokuwa nayo Sheikh Ali Muhsin, aliyekuwa kiongozi wa Hizbu. Ndipo Babu akatangazwa kuwa waziri wa mambo ya nje na biashara.

Kuna baadhi ya wafuasi wa Umma waliomlaumu Badawi kwa kutofanya jitihada ya kuwaingiza makomredi zaidi kwenye Baraza la Mapinduzi. Jibu lake lilikuwa kwamba hakutaka wana-Afro wadhanie kuwa makomredi walikuwa na uchu wa madaraka.

Hivyo, mbali na katibu wake, Salim Rashid, Baraza la Mapinduzi lilikuwa na makomredi wawili tu:Abdulrahman Babu na Khamis Abdallah Ameir. Badawi mwenyewe aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Utangazaji. Moja ya hatua alizochukua ni kulibadilisha gazeti la serikali la ‘Maarifa’ liwe ‘Kweupe’. Baadaye akateuliwa waziri mdogo.

Kama wengi waliokuwa wakiyaunga mkono Mapinduzi, baadaye Badawi akisikitika kuwa mapinduzi yaliendeshwa sivyo. Nakumbuka siku moja katika miaka ya 1990 nikitembea Dar es Salaam pamoja na mwandishi Mohamed Said wa Tanga na tukasadif kukutana na Badawi njiani. Nilipokuwa ninawajulisha watu wawili hao nilimwambia Mohamed kwamba akitaka kuyaandika ya Mapinduzi ya Zanzibar basi amwendee Badawi.

Papohapo Badawi akasema kwa masikitiko: ‘Mapinduzi gani, ilikuwa ni wanawake tu.’ Nilishangaa na kumuuliza alikusudia nini. Alijibu kwamba Mapinduzi yalifisidika na akanitajia visa vya watu waliofungwa gerezani na waliouliwa kwa sababu baadhi ya viongozi wa Mapinduzi wakiwataka ama wake zao ama hawara zao.

Comrade Badawi, ambaye jina lake kamili lilikuwa Ahmed bin Abubakar Shibli bin Omar Qullatein alizaliwa Malindi, Unguja, ingawa nyumba ya ukoo wake na alikolelewa ni Hamamni, Mji Mkongwe, hukohuko Unguja. Ametokana na ukoo wa kisharifu. Asili ya ukoo wa Qullatein imeanzia Tarim, Hadhramaut huko Yemen ya Kusini. Ukoo huo ni tawi la kabila la Al Nadhiri la huko Tarim ingawa Maqullatein wanapatikana Afrika ya Mashariki tu.

Kutoka Tarim mababu zake Badawi wakateremkia Somalia; kwanza Mogadishu na halafu Barawa na baadaye kwenye kisiwa cha Pate karibu na Lamu, Kenya, kabla ya kuishia Unguja ambako ndiko alikozaliwa babu yake, Sayyid Omar Qullatein. Bwana huyu ana umaarufu mkubwa katika historia ya tariqa ya Kisufi ya Qadiriya iliyoshamiri katika nchi nyingi za Afrika ya Mashariki.

Yeye alipewa ijaza ya kuwa khalifa yaani kiongozi wa tariqa hiyo na Sheikh Uweys bin Muhammed bin Bashir al Barawi kutoka Barawa, Somalia, aliyefika Zanzibar mnamo karne ya 19 na ambaye ndiye aliyeiasisi tariqa hiyo Afrika ya Mashariki. Tangu siku hizo hadi leo miongoni mwa makhalifa wa Qadiriya huko Zanzibar hupatikana mmoja kutoka ukoo wa Qullatein.

Huyo babu yake Badawi ndiye aliyelijenga hilo jumba la Hamamni la ukoo wao. Linaitwa Hamamni kwa sababu jumba hilo, ambalo sasa limeporomoka, limepakana na hamamu za Waajemi wa kale. Kwenye hamamu hizo waungwana wa zama hizo walikuwa wakienda kuoga, kukandwa na kusingwa.

Tunaweza, kwa kiwango fulani, kumfananisha Badawi na babu yake. Wote waliwakumbatia watu wa chini — Badawi katika medani ya kisiasa na babuye kwenye tariqa ya Qadiriya. Wala sitokosea nikisema kwamba hata huko kwenye dhikiri kulikuwa na siasa. Wafuasi wa Qadiriya walikuwa na mtandao wao ulioenea sana Tanzania Bara na kuwa kati ya wapinzani wa kwanza wa ukoloni huko.

Visiwani Zanzibar lakini hali ya mambo ilikuwa tafauti na siasa hazikuchanganywa na dhikiri za Qadiriya. Badawi alizivaa siasa licha ya kukatazwa na baba yake, Sayyid Shibli, aliyekuwa mara kwa mara akimkumbusha kwamba wao ni watu wa dini na ‘siasa si mambo yetu.’ Pingine ilikuwa rahisi kwa Badawi kuziingia siasa kwa vile Sayyid Shibli kwa muda wa miaka mingi alikuwa akifanya kazi katika eneo la Wasomali, kaskazini mwa Kenya.

Hadi leo jina la Sayyid Shibli ni maarufu sana katika eneo hilo. Alianzisha skuli Isiolo, Garissa na halafu Wajir ambako aliishi kwa miaka. Mwishomwisho wa ukaazi wake katika eneo hilo alikuwa na cheo cha Afisa wa Elimu na aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria la Kenya. Hivyo, Badawi akimuona babake kila mwezi wa Ramadhani alipokuwa akienda Unguja.

Baada ya masomo ya sekondari huko Unguja Badawi alipata kazi ya ukarani serikalini, kwanza akiwa karani wa Forodha na baadaye wa Idara ya Kazi(PWD). Mara alijiingiza katika harakati za wafanya kazi na kuwa mmoja wa waasisi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanya Kazi vya Kimaendeleo (FPTU). Akishirikiana na kina Ali Sultan Issa, Khamis Abdallah Ameir pamoja na Bwanakheri Musa, ambaye sasa anaishi Liverpool, Uingereza.

Lakini Badawi akifanya mambo yake chini kwa chini kwa vile alikuwa mtumishi wa serikali. Mnamo mwaka 1960 Badawi alitoroka kazini na kuelekea Ujerumani ya Mashariki ya Wakomunisti. Alibaki huko mwaka mzima akisomea uchumi na fani ya kuendesha vuguvugu la wafanya kazi.

Aliporudi Zanzibar alijitumbukiza moja kwa moja katika vuguvugu la wafanyakazi. Akiwa katika uongozi wa chama cha FPTU Badawi akishirikiana sana na viongozi wa shirikisho jingine la wafanya kazi, Zanzibar and Pemba Federation of Labour (ZPFL), la chama cha ASP. Hao walikuwa pamoja na Hassan Nassor Moyo, Adam Mwakanjuki na Mohammed Mfaume.

Badawi akisifika kuwa mchapa kazi hodari na kati ya shughuli zake ilikuwa kuhariri magazeti ya ‘Kibarua’ kwa Kiswahili na ‘The Worker’ kwa Kiingereza.

Mbali na Khamis Abdalla Ameir mtu mwingine aliyekuwa na ushawishi mkubwa kwa Badawi ni Ali Sultan Issa, sahibu yake toka utotoni. Watatu hao walipokuwa kwenye kamati kuu ya Umma Party ndio waliokuwa na uwezo wa kushindana kiitikadi na mwenyekiti wao Babu. Wote wanne walikuwa wafuasi wa siasa za Kimarx za Mwenyekiti Mao wa China.

Kuna siku wafuasi wa Hizbu walipakaa kinyesi kwenye nyumba ya Badawi iliyokuwa Malindi, kwenye shina la Hizbu. Ikabidi Badawi na makomredi wenzake wahamie Miti Ulaya kulikokuwa na wafuasi wengi wa ASP. Kitimbi hicho cha kutiliwa kinyesi nyumbani kwake hakijamzuia Badawi kuandika makala ya kumsifu Sheikh Ali Muhsin alipofariki.

Baada ya kuyatumikia Mapinduzi tangu 1964 Badawi, aliyekuwa waziri mdogo, na Ali Sultani, aliyekuwa waziri, waliondoshwa kwenye nyadhifa zao tarehe 20 Februari 1972. Wakati huo Babu alikuwa amekwishatolewa kwenye uwaziri katika serikali ya Muungano na Julius Nyerere. Badawi alikuwa miongoni mwa watu waliokamatwa, takriban wote wakiwa makomredi, kufuatia kuuliwa Rais wa Zanzibar Sheikh Abeid Karume tarehe 7 Aprili, 1972. Alihukumiwa kifo.

Hatimaye aliachiwa huru mwaka 1978 na akahamia Dar es Salaam. Jijini humo haikumchukua muda kuanza kuishi maisha ya mtu wa kawaida. Alijiingiza katika biashara mbalimbali na mwishowe akaishia kuuza duka la nguo huko Kariakoo. Huko Dar pia akihudhuria darsa za Sharif Abdulkader Junayd katika Msikiti wa Ijumaa wa Kitumbini. Akifuata wasia wa babake kwamba awe akimtumikia Sharif Junayd. Hali kadhalika akiswali sana katika Msikiti wa Makonde.

Unyenyekevu na ucha Mungu wake ulizidi muda wote huo. Aliwahi kuonekana Makkah miaka mingi iliyopita akifagia katika Msikiti Mkuu wa Haram Sharif. Akiwa mzima, siku moja au mbili kabla ya kufariki alimwambia mwanawe Mohammed aliyekuwa naye kwamba angelipenda maisha yake yamalizikie huko katika mji mtakatifu.

Jumatatu asubuhi alifanya tawaf ya mwisho (kuzunguka Kaaba) katika Haram Sharif na aliporudi nyumbani pumzi zikampanda na akatutoka.

Baruapepe: ahmed@ahmedrajab.com

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Ma’alim nakushukuru, tiba ya zako fikira
Mwanadamu hukufuru, Mola mwenza maghafira
Hata nazi ya bufuru, hwenda ika’aunika!

Haya yote kwa hakika, kwa vilema na viwete
Si ajabu kufanyika, ushupavu na utete
Zanzibar na Tanganyika, watu kupigwa mateke!

Ya maovu tusiweke, uwerevu si siyari
Wetu Mola ni Mpweke, sijitie uhodari
Wenzio usiwacheke, M’Ngu ndo mwenye khiari!

Hoja za mtu hodari: si kejeli, simbulio
Hata uwe mwanamwari, kukengua na vilio
Na unywe yote Bahari, ugwiji ni masikio!

Kusoma ni kwenda mbio, sijigambe na uungu
Burahima na wenzio, wenye mawazo ya juu
Jitengeni na vitisho, yalopita ni ya M’Ngu!

Qulateni ni wa juu, mapinduzi hakuponya
Nchi ya Mwinyi Mkuu, makubeli kawaonya
Watunze yao miguu, makabwela si vipanya!

Wastahiki heshima, kwa nasaha za Mtume
Zanzibar ipate hima, Kichunjuu na Karume
Tufani hawakupima, kubomoa yetu Chumbe!
———————–
Wakatabahu bil yadii,
Salim H. M. Bwanatosha
8-10, rue Saint Sauveur
75002, PARIS
France/EU
            +336-63731703      

Assalamu alaykum,

Sayyid Ahmad-Badawy bin Shibly bin Omar Qulatayn bin Mudh-hir bin Abubakar Al-Nadhiry ni mtu aliyetokana na ukoo wa Masharifu, kutoka Tarim, Yemen, wengi wao wakiwa wasomi wa Dini ya Kiislamu na wacha-Mngu. Hadithi yao ni ndefu na inahitajia kikao mbali kukizungumzia. Ukoo wake wa karibu ulitokea Tarim na kuishi Barawa, ambako kulikuwa na vyuo vikubwa vya Dini na kutoa Mashkhe wengi, na kwa ilimu yao wengi walipewa Uqadhi kuanzia wakati wa Sayyid Majid mpaka kunofolewa Banadir (Mwambao wa Somalia) kutokana na mamlaka ya Zanzibar na kutiwa katika ukoloni wa Kitaliana. Kutokea Banadir walipitia Mwambao na baadaye kuja kuishi Zanzibar. Babake Syd Shibly alikuwa ni mwana chuoni na mcha Mgu wa kupigiwa mfano na kadhalika alikuwa ni mwalimu aliyesomesha shule za  serekali mjini Zanzibar na Garisa, Keya kwa mika mingi. Ami yake Syd Ali Kulatyn na mababu zake  walikuwa ni wana vyooni wajulikaniwao Mwambao mzima. Jina lake tunayemzungumza alipewa kwa kutabaruku na jina la Mwanachuoni, Sharifu na mcha Mgu kutoka mji wa Lamu, Sayyid Ahmad Badawy bin Habib Saleh Jamalilyl.

 

Almarhum na  tumbo lake lote lajulikana kwa laqb “Qulatyn” kuanziya Mogadisho, Barawa na Mwambao mzima kutokana babu yao Sayyid Omar Qulatyn ambaye alikuwa karimu, aliyekuwa akiwasaidia watu kwa hali na mali, msafi wa umbo na tabiya, Mwanachuoni na mcha Mngu wa kusifiwa  kwa kila sifa njema kama “maji yalofika kiwango cha ‘Qulatayni.’  

 

Cha muhimu hapa ni kuwa Sayyid Ahmad-Badawy tunayemzungumza alipata masomo ya msingi au tuseme makapi ya msimamo wa Kiislamu katika kutetea haqi za wanyonge na ndio imani na mtizamo huo ambao uliompelekea kupigania haqi za wanyonge na walalahoi. Haya yameshaelezwa kwa kiasi na Salim Msoma na pia Ahmed Rajab. Kuna na wengine pia walioangalia maisha ya Sayyid Ahmad-Badawy kidoto kukhusiana na yale yaliyokuwa ni muhimu kwao. Ni ya kama hadithi ya vipofu na wasifa wa tembo. Kila mmoja akatoa swifa za tembo kwa kile alichoweza kukikamata kwa mikono yake. Aliyeushika mkia akasema tembo ni kama ufagio. Aliyeshika mkonga akaelezea kuwa tembo ni kama chatu; aliyeupapasa mguu wa ndovu akasema tembo ni kama nguzo; mradi kila mmoja na mtizamo wake. Na mimi pia ninao mtizamo wangu pengine ni wa kidoto zaidi kuliko wa hao niliowazungumzia.

 

Walilokuwa hawakulielezea waandishi hao wawili niliowataja kwa majina ni ule msingi wake Sayyid Ahmad-Badawy uliompelekea kurudi kulekule alikoanzia, nako ni katika Dini ya Kiislamu na maagizo ya Mwenye-enzi Mngu Subhanah waTaala na ya Mtume wake Muhammad Swala ‘lLahu alayhi waSalam. Kwa mtizamo wangu naamini kuwa kuna jambo moja ambalo Makomred wetu wa Zanzibar limewapita, nalo ni kuwa kwa upungufu wao mkubwa wa wengi wao, kama si wote, kuyaelewa ya Dini yao, basi pia wamepitwa na kufahamu kuwa hakuna nidhamu (system) iliokuwa ya kijamaa (hata kisosialisti) kuliko Uislamu, na tafauti na huo ujamaa wa akina Max na Nyerere na wengineo, Uislamu si ujamaa wa kutoana roho kwa dhulma wala kuwanyang’anya watu mali zao kwa dhulma. Inaonesha kuwa awali Sayyid Ahmad-Badawy pia hakulielewa hili na akaona kuwa nidhamu ya ujamaa wa kisosialisti ndiyo iloyo bora. Jambo lililokuja kumgutua ni kule kuja kuwaona wengi ya wanyonge walewale waliokuwa watetewe, waliuliwa bure, wengi walikuja kuadhibiwa bure na kufungwa bila ya sababu na kushuhudia mengi ya dhulma na ya uchafu. Ahmed Rajab anatuelezea haya yafuatayo:

 

“Kama wengi waliokuwa wakiyaunga mkono Mapinduzi, baadaye Badawi akisikitika kuwa mapinduzi yaliendeshwa sivyo. Nakumbuka siku moja katika miaka ya 1990 nikitembea Dar es Salaam pamoja na mwandishi Mohamed Said wa Tanga na tukasadif kukutana na Badawi njiani.  Nilipokuwa ninawajulisha watu wawili hao nilimwambia Mohamed kwamba akitaka kuyaandika ya Mapinduzi ya Zanzibar basi amwendee Badawi.” 
“Papohapo Badawi akasema kwa masikitiko: ‘Mapinduzi gani, ilikuwa ni wanawake tu.’ Nilishangaa na kumuuliza alikusudia nini.  Alijibu kwamba Mapinduzi yalifisidika na akanitajia visa vya watu waliofungwa gerezani na waliouliwa kwa sababu baadhi ya viongozi wa Mapinduzi wakiwataka ama wake zao ama hawara zao.”

 

Lakini si mapinduzi ya Zanzibar (ambayo kwa hakika hayakuwa mapinduzi) pekee ndiyo yaliyokuwa na matatizo. Bali ni ule mfumo mziwa wa kutaka kuleta mabadiko kwa kutunia njia zilizokatazwa na Uislamu zenye kumpeleka muubwa motoni milele, kwa mujibu wa qauli yake Subhana waTaala katika Qur’ani Tukufu. Baada ya kuyashuhudia maovu na maonevu hayo Sayyid Ahmad-Badawy alijijutia na alikwenda kumwangukia baba yake na baba yake akamwambie arejee kwa Mwenye-enzi Mungu upesi sana na kwanza ende Umra na akirudi aanze kusoma upya juu ya Uislamu na sharia zake. Akampeleka kwa Sheikh Suleiman Al-Alawy na akakaa upya na kusomea Uislamu kwa kituo. Alipofariki Sheikh Suleiman akaenda kwa Sayyid Abdulqadir Juneidy na kuendelea kujiilimisha. Kila alipozidi kuuelewa zaidi Uislamu ndipo alipozidi kutubia kwa aliyoyaamini ujanani.

 

Imani yake na Maisha yake ya ukubwani yalikuwa tafauti kabisa na alivyokuwa kabla ila katika hamu yake ya kuwasaidia wanyonge.  Na ndipo Bwana Mtume ( S.A.W.) aliposema “Amali za mtu ni za mwisho wake.” Sayyid Ahmad Badawy, alikuja kuelewa vizuri sana kabla ya mwisho wa maisha yake, kuwa usoshalisti ulioanzia Ulaya ni wa dhulma tupu na hauna mlingano wowote wa maana na ujamaa wa haqi uliomo katika Uislamu.

 

Ni mazishi na masikitiko mapevu sana ukiwaangalia masoshalisti kutoka makwetu. Huku hawako wala kule hawako, wameula huu. Sayyid Ahmad-Badawy alijiilimisha upya na akafanikiwa katika kuona ukweli wa mambo yalivyo na hikma za Mwenye-enzi Mungu aliyotuteremshia katika Dini yake. Sayyid Ahmad-Badawy alitubia tawban nasuha na naamini Mola Karimu Rahimu alimkubalia. Kwanza, hakushiriki katika mauwaji wala kumfunga mtu bure ingawa alikuwa na uwezo wa kuyatenda hayo. Pili, alikuja kulaani yaliyotokea Zanzibar kwa moyo wake na kwa maneno na vitendo vyake. Tatu, alipata radhi ya baba yake mzazi. Nne, watu walikuja kumpenda na kumwombea dua njemanjema wakati yuhai na baada ya kufariki. Huu ni mfano wa tafauti baina ya wale walioongoka na wale ambao bado wamo kutafakhari na dhulma na uchafu walioufanya.

 

La kusikitisha katika maandishi ya baadhi ya waandishi ni juu ya kuwa Sayyid Ahmad-Badawy amebadilika na kubadilisha itiqadi na msimamo wake na kuendelea mbele na kumwelekea Mwenye-enzi Mungu na kutubia, lakini katika maandishi yao hao waandishi sehemu hii wameiacha na kug’ang’ania palepale kuwa Sayyid Ahmad-Badawy ni Komredi mwenzao ilihali alitokana nao zamani sana na kuwa mtu mwingine kabisa. Ndipo jana nipotoa mfano wa Sayyidna Omar. Niliandika kwa mukhtasari haya:

 

“Kuna Sayyidna Omar ibn Khatab wawili. Yule aliyeyezaliwa katika ujahiliya akamzika mwanawe akiwa yuhai na yule Sayyidna Omar aliyesilimu na akabashiriwa pepo.”

 

“Wengine tunamzungumzia Sayyid Ahmad-Badawy aliyetubia na wengine wanamzungumza yule aliyefuata siasa za Kikomunisti katika ujana wake. Wewe fuata akili yako inavyokuelekeza!”

 

Nakutakia kila la kheri,

Professa Ibrahim Noor

Advertisements

8 responses to “Tanzia: Buriani Badawi Qullatein, mtetezi wa wanyonge (11 Oktoba 1930 – 31 Oktoba 2011)

 1. Mashallah Ingawa nina huzuni kubwa kwa msiba wa mjomba wangu mpenzi nimefurahi kuona article hii. Mzee Badawy alikuwa mjomba rafiki na akimpenda sana Mungu amrahamu babangu syd Umar qullatein(alie hamia Mombasa).
  Tunawaombea maghfira wazee wetu wote walotangulia na sisi Mungu atupe husnul khatimma.

 2. Masha’allah mi ni mtoto wake wa mwisho..’kitinda mimba’ nina huzni kubwa mno..lakini sina jinsi zaidi ya kumshukuru mola wetu maana kazi yake haina makosa na kashatuambia.,’kullu nafsu dhaaikatul maut’ Alhamdulilah babangu kaondoka njia nzuri ilokua bora kila mmoja wetu anaitaka hiyo…na alhamdulilah hali ya kua alikua hajapata tabu ya ugonjwa wowote japo umri wake ulikua mkubwa…Alhamdulilah! Alikua zaidi ya baba kwangu..bali babu na zaidi RAFIKI mkubwa kwangu kwani tulikua tunataniana sana….Alhamdulilah! Allahuma ghfirlahu warhamhu…

 3. i will miss youuuuu babuuuuuuu…. ‘:(
  he was a great grandpa,great father,great brother,great friend and amazing person.you are truely loved by everyone..and you will surely be missed..

 4. Ahsante kwa kutuletea habari za Komred Badawi. Tunamuombea Mungu amuwkeke pahala anapo stahiki.
  • Kama anovotuambia Komred Ahmed Rajab kwamba Komred Badawi alikuwa na mahusiano mazuri na wanaharakati wa Afro-Shirazi Party (ASP). Kati yao walikuwa akina Seif Bakari, Hassan Nassor Moyo, Saleh Saadalla na Abdulaziz Twala. Jambo ambalo hakutuambia ni nani aliyemjuilisha Badawi na akina Seif Bakari, Yusuf Himidi, Said Washoto, Pili Khamisi, Ramadhani Haji, Said Idi Bavuai, Khamis Darweshi na Abdallah Said Natepe? Kwa hakika mtu huyo alikuwa ni mzungu maarufu sana kwa vitimbi vyake kupinga wananchi zama hizo anaitwa Bwana Stringer.
  • Sisi hatumsahau Badawi kwa mchango wake katika Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964. Yeye ndie aliekuwa ni kifungo baina ya wanamapinduzi wa Afro-Shirazi na makomred waliopandiya mapinduzi baadae. Mwnyewe Ahmed Rajab anakiri kwamba “Baadaye Badawi aliwaita vijana wa Umma waliokuwa wamerudi kutoka Cuba walikopata mafunzo ya mbinu za kupindua serikali wawasaidie wapinduzi.”
  • Pia hatumsahau Badawi hali kadhalika aliyekaa pamoja na ‘Field Marshal’ John Okello, Twala na Jumbe na kulipanga Baraza la Mapinduzi na lile la Baraza la Mawaziri.
  • Komred Rajab anataka tusimsahau Badawi “kwa jinsi alivyoutumia ujana wake kuwatetea walala hoi na kupigania haki zao. Yeye ni mfano mzuri wa mtu wa tabaka la wenye kujiweza aliyejitolea kuwapigania wasiojiweza. Hivyo ndivyo walivyokuwa wengi wa wafuasi wa Abdulrahman Babu.”
  Hapa niteleza hadithi fupi ya kumfahamu nani alikuwa Badawi. Baada ya mapinduzi ya 1964, na baada ya Badawi kuwa waziri mdogo wa serikali ya mapinduzi, Komred Badawi alioa mke na alichongesha fanicha (furniture) yake kwa sarumalla wa ki-Bohora aliekuwa na duka lake huko Baghani Mjini Zanzibar. Bohora huyo alikuwa akifanya kazi yeye na wanawe hapo dukani kwake. Mmoja katika wanawe alikatika vidole kwa msumeno. Komred Badawi alipokuwa anadaiwa malipo ya fanicha alimzungusha yule sarumalla kwa muda mrefu. Siku moja alimuahid kumlipa, na alipofika yule Bohora ofisi yake Badawi huko Beitlajaibu Badawi alimtolea bastola yule Bohora na akmuambia: “sitaki kukuona tena hapa unakuja kudai, nikikuona nitukupiga risasi. Nyie Wahind mabepari kazi yenu kunyoya watu tu. Toka hapa.”
  Huyu ndie Badawi ati anaewatetea walala hoi na kupigania haki zao. Hivyo ndivyo walivyokuwa wengi wa wafuasi wa Abdulrahman Babu.

  Ramadhan Madafu

 5. mimi mohd badawy mtoto wa pili wa mzee qullatein..nashukuru sana kwa kutukumbusha deni la mzee lakini nakumbuka tuna jua mzee alipotoka jela baba yake alimletea pesa kulipa madeni na yeye aliuza mazuliya yake ya persei kulipa hiyo deni.ila tunamuomba mola na wewe ukifa mola atowe mtu akumbushe mambo yako..ramadhan madafu! Nb from hamid to bwana ramadhan KUMAMAMAMAMAMAMAMAMAMAMAMMAMAMAMAMAMLAMAMAMAMAMAMAMAMAMAMAMAMAMAMAYAKOOOOOOOOOOOOOOOOO….MBWA WEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEE

 6. Bwana Ramadhan….. Kwanza tafadhali tueleze hizi habari umetowa wapi kwa huyo bohora ? Na kama bado anamdai huyo bohora aonane na Mohd Badawy face to face , na kudaiwa si aibu kuiba ndo aibu. U’v made a very serious accusation tht he wanted to kill someone ,na yeye bin adam hajakamilika everyone makes mistakes. Almuhim huyo bohora should contact his son Mohammed Badawy regarding this issue. Thank you.

 7. Ramadhan Madafu…… hatujafahamu bado point yako ni nini, na kama Mzee wetu Badawy alifanya makosa hakuna binadam alokamilika. Lakini hapa umejionyesha choyo chako kwa sifa anazopewa mzee wetu ,kwani mtu akifa hutajwaa na kukumbukwa kwa mazuri yake na sio kumkashif kwa upungufu wake. Kwa hivo ningeomba uende ukatafute mwisho wa hadisi yako na uje kama huyo bohora alilipwa. Ukihadisia kitu uhadisie kwa ukamilifu na kwa hadhar utelezi wa ulimi ni hatari.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s