Uongozi si ujana ni uadilifu…


Na Ahmed Rajab

SIKU mbili hizi tumeshuhudia matukio mawili makubwa barani Afrika. Tumeiona hatima ya kuhuzunisha ya Kanali Muammar Qadhafi nchini Libya huko Afrika ya Magharibi na huku kwetu Afrika ya Mashariki tumeiona Kenya ikijitutumua na kujiingiza kijeshi nchini Somalia.

Yanayojiri nchini Libya na Somalia ni mavuno ya ukosefu wa utawala bora na wenye uadilifu. Ukosefu huo umekuwa kama laana kwa nchi hizo.

Libya imeukosa utawala bora tangu mapinduzi ya mwezi Septemba, mwaka 1969, yaliyofanywa na Qadhafi na vijana wenzake wa kijeshi. Somalia nayo imeukosa utawala huo tangu mapinduzi yaliyofanywa na Mohammed Siyad Barre na wanajeshi wenzake mwezi Oktoba mwaka huo huo wa 1969. Qadhafi aliidhibiti nchi kwa muda wa miaka 42 na Siyad Barre kwa muda wa miaka 20.

Qadhafi akijiita ‘kiongozi’ (‘al qaid’ kwa Kiarabu’) na Barre akijiita ‘kiongozi aliyeshinda’ (‘guulwade’ kwa Kisomali). Tawala za viongozi wote hao wawili zilifurutu ada katika kuzikiuka haki za binadamu za wananchi wa nchi hizo. Hii leo nchi hizo mbili zimeingiliwa na madola ya magharibi.

Waliompindua na kumuua Qadhafi walisaidiwa pakubwa na Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (NATO) na Kenya, ingawa haisemwi, imeingia Somalia kwa msaada wa siri wa madola ya Magharibi.

Kinachosemwa ni kwamba lengo la Kenya ni kuwasaka na kuwatimua magaidi wa al-Shabbab wanaoutishia usalama na uchumi wa Kenya. Kinachofichwa ni ushauri unaotolewa na majasusi wa kijeshi wa Kimarekani na Kifaransa walio kwenye mpaka wa Kenya na Somalia.

Lau Qadhafi na Siyad Barre wangelikuwa na utawala bora yasingaliwafika yaliyowafika na nchi zao zisingefikwa na masaibu yaliyozikumba. Laiti wangeweza kutawala kama alivyotawala Pedro de Verona Rodrigues Pires, aliyekuwa rais wa Cape Verde na ambaye mapema mwezi huu alitunukiwa Tuzo ya Mo Ibrahim kwa kuwa na utawala bora.

Pires alikuwa mmoja wa viongozi wa Partido Africano da Independência da Guiné e CaboVerde(PAIGC), chama kilichokuwa kinaongozwa na Amilcar Cabral na kilichokuwa kikipigana na wakoloni Wakireno kikiwania uhuru wa Guinea-Bissau na Cape Verde.

Ingawa chama hicho cha PAIGC kikipigania uhuru wa nchi mbili, nyufa zilianza kujitokeza kwenye chama hicho baada ya Cabral kuuliwa na Wareno mjini Conakry, Guinea mnamo mwaka 1973 na miezi michache kabla ya kupatikana uhuru mwezi Septemba mwaka 1974.

Sababu kubwa iliyoibua mpasuko huo ni kuzuka kwa mivutano ya kieneo na kikabila ndani ya chama cha PAIGC. Kina João Bernardo‘Nino’Vieira walihisi kuwa Wacape Verde wanataka kuwakalia kichwani na kuwatawala wenzao wa Guinea-Bissau.

Hicho ndicho kilichokuwa chanzo cha mapinduzi ya Novemba mwaka 1980 yaliyomuangusha Rais wa kwanza wa Guinea-Bissau Luis de Almeida Cabral (ndugu wa baba mmoja na Amilcar Cabral).

Ingawa viongozi wa Cape Verde na wa Guinea-Bissau walikuwa na azma ya kuziunganisha nchi zao, mahusiano kati ya nchi hizo yalizidi kuharibika baada ya Luis Cabral kupinduliwa huko Bissau.

Cape Verde ikakata tamaa ya kuungana na Guinea-Bissau na wanasiasa wa huko Visiwani, akiwemo Pires, wakajiengua kutoka chama cha PAIGC na Januari mwaka 1981 wakaunda chama chao wenyewe walichokiita Partido Africano da Independência de Cabo Verde (PAICV) kikiongozwa na Aristides Pereira.

Ingawa kina Cabral walizaliwa Guinea-Bissau wazazi wao walitokea Cape Verde. Hivyo, kina ‘Nino’ na wenzake wa Guinea-Bissau wakiwachukulia kuwa si wazawa. Watu wakifikia kuwa na mawazo kama hayo ya kupalilia dhambi ya ubaguzi, chambilecho Mwalimu Nyerere dhambi hiyo huwapelekea wenyewe kwa wenyewe watafunane kwani haizuiliki kuenea.

Na hayo ndiyo yaliyotokea kwani ukabila na ubaguzi ukawaandama Waguinea-Bissau wenyewe waliokuwa kwenye ngazi za uongozi. Tunakumbuka yaliyomfika ‘Nino’ alipouliwa na wanajeshi waliokuwa watiifu kwa mkuu wa jeshi aliyeuliwa na ‘Nino’.

Yote hayo yalizuka kutokana na tafauti za kikabila ndani ya jeshi na serikali ya Guinea-Bissau. Na nchi hiyo tangu ipate uhuru nayo pia imekuwa kama iliyolaaniwa na sasa inatajwa kwa umaarufu wake wa kuwa kituo kikubwa cha mihadarati kutoka Amerika ya Kusini kuelekea nchi za Ulaya.

Wengi tuliwalaumu wanasiasa wa Cape Verde walipounda chama cha PAICV na kuwaacha mkono wenzao wa Guinea-Bissau. Tukiwaona kuwa wakiiua ile ndoto ya Amilcar Cabral ya kuzifanya nchi hizo mbili ziungane.

Lakini tukiangalia jinsi nchi hizo mbili zilivyo hivi sasa sina shaka tutakubaliana kwamba uamuzi wa wanasiasa wa Cape Verde ulikuwa uamuzi wa busara, hasa tukizingatia kwamba muungano wa nchi zozote haulazimishwi na kwamba unaimarika ikiwa unapata ridhaa ya wananchi wa nchi zinazohusika.

Hii leo Amilcar Cabral, mzaliwa wa Guinea-Bissau, anaenziwa zaidi Cape Verde kama ‘baba wa ukombozi’ lakini amesahaulika kwa kiasi kikubwa Guinea-Bissau, nje ya chama cha PAIGC. Hata ‘Nino’ alikuwa hamtaji kabisa mwanamapinduzi huyo.

Cape Verde anakoenziwa Cabral ni nchi ya mkusanyiko wa visiwa vidogo na ni mfano wa kuigwa katika suala zima la kuheshimu demokrasia, haki za binadamu na utawala bora.

Baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa mnamo mwaka 1990, chama cha PAICV kilishindwa kwenye uchaguzi uliofuata na kikayakubali matokeo. Aristides Pereira aliyekuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo akajiuzulu uongozi wa chama na Pires, aliyekuwa waziri wake mkuu, akashika hatamu za PAICV.

Pires akagombea uchaguzi uliofuata mwaka 2001 na akashinda. Alipata tena ushindi mwaka 2006 na mwaka huu alimaliza muda wake wa urais kwa mujibu wa katiba ya nchi.

Katika uchaguzi wa mwaka huu chama chake kilishinda kwa kupata viti vingi bungeni ingawa katika uchaguzi wa urais kilishindwa na Profesa Jorge Carlos Fonseca, mgombea urais wa chama cha Movimento para a Democracia (Vuguvugu la Demokrasia).

Chama cha PAICV kilishindwa kwenye uchaguzi wa urais kutokana na mvutano wa nani awe mgombea. Mwanasiasa mmoja wa chama hicho alifanya nongwa na akasimama akiwa mgombea wa kujitegemea na hivyo kuzigawa kura za wafuasi wa PAICV uchaguzi ulipoingia katika duru ya pili.

Wachambuzi wanayaona pia matokeo hayo kuwa yanadhihirisha kukomaa kisiasa kwa umma wa Cape Verde na hasa wafuasi wa PAICV ambao wamekipa funzo chama hicho baada ya hiyo mivutano ya ndani ya chama.

Pingine Cape Verde inaweza kuwa darasa la kisiasa kwa visiwa vilivyowahi kuwa na migogoro ya kisiasa kama vile Zanzibar na Comoro, ambako migogoro ilifikia kuwa sugu, au Madagascar ambayo hadi leo haijapata bado ufumbuzi. Badala yake, tunaziona Angola na Ufaransa, kila moja ikishindana na mwenziwe kuwa ndiye mfumbuzi wa matatizo ya Madagascar.

Kimaendeleo kuna kitu gani ambacho Cape Verde inaweza kujivunia kushinda Zanzibar? Cape Verde inategema utalii tu kwa sababu sehemu kubwa ya ardhi yake ni mawe wakati Zanzibar ina mengi yanayoweza kuufanya uchumi wake uwe bora zaidi.

Hata hivyo, uchumi bora utaweza tu kulinufaisha taifa endapo panakuwako pia utawala bora na demokrasia ya kweli — hayo mawili ni silaha kuu inayoua maovu katika jamii kama vile donda ndugu la rushwa na ufisadi.

Suala hapa si ukubwa au udogo wa nchi bali ni uadilifu. Ukipatikana uongozi wenye maadili mema basi katiba haiwezi kukiukwa na katiba inapoheshimika ndipo msingi wa utawala bora na demokrasia unapoimarika.

Kutokana na uadilifu wake, Pires leo ameifanya nchi yake iwe safu moja na Afrika ya Kusini, Botswana, Seychelles na Mauritius kuwa nchi tano bora za kuigwa barani Afrika.

Utawala wa Pires ulidhihirisha vilevile kwamba pamoja na Afrika kudai kizazi kipya cha uongozi, huo uongozi yaani uongozi ulio bora hautegemei ujana, sura za kupendeza wala tabasamu. Uongozi ulio bora unategemea uadilifu na ujasiri wa kupambana na maovu yaliyo katika jamii, ikiwa pamoja na ufisadi.

Wakati Meles Zenawi wa Ethiopia, Isaias Afewerki wa Eritrea, Paul Kagame wa Rwanda na hata Yoweri Museveni wa Uganda walipoingia madarakani walitajwa kuwa ‘matumaini ya Afrika’ na kwamba wanaanzisha enzi mpya ya uongozi barani humo. Matokeo yake ni kwamba kizazi kilichotarajia mageuzi kimevunjika moyo. Kinachotokea sasa Uganda, kwa mfano, ni sawa na kile Museveni alichokuwa akikipiga vita wakati wa utawala wa Milton Obote.

Kweli kumepatikana amani katika nchi zote hizo na hilo si jambo dogo na kweli kumepatikana maendeleo ya aina fulani, ya majumba marefumarefu na makampuni kemkem ya kigeni.

Lakini hayo majumba na makampuni ndio vigezo vya kweli vya maendeleo? Kipimo cha maisha ya mtu wa kawaida kikoje? Waheshimiwa wako mbali kiasi gani katika kujirundikizia mali na utajiri kwa kutumia vyeo vyao? Wameyatekeleza kwa kiasi gani waliyoahidi kutekeleza walipokuwa wanaingia madarakani?

Hayo ni baadhi ya maswali yanayohitaji kuulizwa tunapozingatia iwapo nchi ina utawala bora au muovu; iwapo itakuwa kama Cape Verde ama Somalia.

CHANZO: RAIA MWEMA

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s