Shein atakiwa kuhoji Majeshi ya Kanisa Katoliki


Rais Shein atakiwa kuhoji Majeshi ya Kanisa Katoliki

*Aombwa kukata kitanzi kinachoinyonga ZNZ     *Kisa cha “mbwa” immigration chafafanuliwa

 

Viongozi wa Zanzibar wametakiwa kuhoji ile Tume ya Majeshi ya Kanisa Katoliki ili kujua kazi yake na ni nani hao wanaounda jeshi hilo.

Wito huo umetolewa huku ikikumbushwa jinsi Zanzibar wakati wa uchaguzi ilivyokuwa ikijazwa askari toka Bara mithili ya nchi iliyovamiwa kijeshi ambapo matokeo yake yalikuwa kuuliwa watu, wanawake kubakwa, mali kuporwa na wengi kutiwa vilema.

Kwa upande mwingine kile kisa cha mbwa immigration kule Sumbawanga kimefafanuliwa upya ikilinganishwa na mauwaji ya Waislamu Mwembechai kama kielelezo cha kuonesha jinsi Waislamu walivyodhalilishwa na kudunishwa.

Hayo na mengine mengi ni katika jumla ya mambo yaliyozunguzwa katika kongamano juu ya Mfumo Kristo lililofanyika katika viwanja vya Lumumba, Zanzibar Jumapili iliyopita, Oktoba 9, 2011.

Akizungumza katika kongamano hilo Sheikh Ilunga Hassan Kapungu amesema kuwa mwaka 1990 alipokuja kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki, Pope John Paul II, Kanisa lilitoa ripoti yake ya kazi ambapo pamoja na mambo mengine walisema kuwa wamefanikiwa kuwa na Tume ya Majeshi ya Kivita (Commission of Armed Forces).

Akifafanua nini maana ya “armed forces” akasema kuwa, ni majeshi yenye silaha za kivita zikiwemo bunduki, mizinga, vifaru, makombora na ndege za kivita, na yaliyoundwa kwa ajili ya kupigana vita na nchi/askari adui.

Akasema, toka Kanisa limetoa taarifa hiyo Waislamu wamekuwa wakihoji nini maana ya kuwa na tume hiyo, je, ina maana kanisa lina jeshi lake la kivita na kazi yake nini? Linataka kupambana na askari/watu gani adui? Au tume hii inafanya kazi ndani ya JWTZ na kazi yake nini?

Hata hivyo akasema kuwa toka mwaka 1990 mpaka sasa serikali haijaweza kutoa majibu.

Ni katika hali hiyo ikaulizwa kwa nini askari wengi wa Bara wanapelekwa Zanzibar, ni kwa nini wakati wa uchaguzi ambapo Zanzibar ilikuwa kama imevamiwa kijeshi, askari wengi walimiminwa kutoka Bara na hao ndio wanatuhumiwa kufanya mauwaji ya kutisha, kupiga watu ovyo na kubaka?

Katika kuhoji maswali hayo, mtoa mada akataka serikali na Wazanzibari kurejea taarifa hiyo ya Tume ya Majeshi ya Kivita ya Kanisa Katoliki na kuhoji isije ikawa kwamba kilichokuwa kikifanya kazi na kuwauwa Wazanzibari ni ile Tume ya Majeshi ya Kivita ya Kanisa.

Akihimiza jukumu la Serikali ya Mapinduzi (SMZ) katika kuwalinda Wazanzibari, Sheikh Ilunga aliwakumbusha viongozi wa SMZ kutambua kuwa wanadhima kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na wataulizwa kesho Akhera kama watafanya ajizi na kuacha Mfumo Kristo uendelee kuleta fitna, farka, mauwaji na idhilali kwa Waislamu Zanzibar.

Kama ilivyokuwa kwa kongamano la Pemba, Ilunga akakumbusha tena jinsi Zanzibar ilivyoporwa nguvu zake za kiuchumi, kisiasa, nguvu kazi na maadili yake mema ya Kiislamu.

Akikumbusha jinsi muasisi wa Mfumo Kristo alivyokuwa na chuki dhidi ya Waislamu wa Zanzibar, Sheikh Ilunga aliwataka Wazanzibari kusoma kitabu cha Harith Ghasani ambapo pamoja na mambo mengine anaeleza chuki ya Nyerere na mbinu alizotumia kuifisidi Zanzibar.

Akitoa mfano aligusia ile kauli ya Nyerere aliposema kuwa angetamani kuvivurumisha visiwa vya Zanzibar na kuvitosa mbali baharini.

Akifafanua kauli hiyo kama ilivyonukuliwa na waandishi wengi wa vitabu Ilunga alisema kuwa kilichomfanya Nyerere aichukie Zanzibar ni mambo makubwa mawili.

Akayataja kuwa ni Uislamu na uchumi uliokuwa madhubuti wa Zanzibar.

Ni kutokana na chuki hiyo mkakati maalum ukawekwa ambapo hivi sasa Zanzibar imepoteza nguvu yake ya kiuchumi na maadili ya Kiislamu nayo yanaishia.

Kwa kugusia Ilunga alikumbusha jinsi Zanzibar ilivyokuwa tegemeo la bidhaa muhimu kwa watu wa Bara, Uganda, Kenya, Zambia, Malawi, Zaire, Burundi na Rwanda ambapo wafanyabiashara walikuwa wakifurika Zanzibar kufunga mali.

Ambapo tafsiri ya hilo ni kuwa mzunguko wa fedha ulikuwa mkubwa mno, watu wakiwa na pesa.

Kwa upande mwingine, vijana wa Kizanzibar walikuwa wasambazaji wakubwa wa bidhaa mbalimbali kuanzia nguo na vifaa vya elektroniki wakafikia kufungua maduka makubwa ya jumla huko Bra.

Akasema, hii ni kwa sababu bandari ya Zanzibar ilikuwa ikifanya kazi vizuri meli zikipanga foleni kushusha bidhaa.

Nini kimetokea mpaka hali hiyo ikawa leo imebaki hadithi, ndipo ikakumbushwa kuwa hiyo ni kazi ya Mfumo Kristo ambao Wazanzibari pamoja na serikali yao wanatakiwa kuufahamu, kuukataa na kuhakikisha wanakata kitanzi walichotiwa kinachowafanya kuwa watwana wa Mfumo huo.

Katika jumla ya mambo aliyosisitiza Ilunga ni kwa Wazanzibari kuona neema iliyokuja na maridhiano.

Akawataka kuwaunga mkono viongozi wa serikali ya umoja wa kitaifa na kuhakikisha kuwa hawarejeshwi tena katika shimo la moto ambalo walikuwa wakikaribia kutoswa na Mfumo Kristo.

Aliwakumbusha kuwa miafaka iliyotangulia ilifeli kwa sababu ilikuwa imedhibitiwa na Mfumo Kristo ambao hauwatakii salama Wazanzibari.

Akasema, Rais Mstaafu Amani Abeid Karume na Maalim Seif wamefanikiwa kuleta maridhiano kwa sababu waliupiga chenga mfumo huo tahamaki ukistuka Wazanzibari washapatana.

Wakati huo huo, kile kisa cha “Mbwa Immigration” Vs mauwaji ya Waislamu Mwembechai kimekumbushwa ili kuwakumbusha Waislamu waijue hadhi yao katika nchi hii.

Wasije kujitia nao kusherehekea miaka 50 ya uhuru wakati “mbwa” anathaminiwa zaidi kuliko wao.

Akikumbusha kisa hicho Ilunga amesema kuwa baada ya mauwaji ya Mwembechai Waislamu waliomba serikali ifanye uchunguzi- maarufu Inquest (PI) kama sheria inavyotaka, lakini serikali ikagoma.

Akasema, hata zile taasisi za kiraia, vyombo vya habari, wanasheria na wale walio katika taasisi za kutetea haki za binadamu, hakuna hata mmoja aliyefunua mdomo kutaka sheria ifuatwe PI ifanyike.

Haukupita muda akauliwa mbwa kule Sumbawanga kwa hukumu ya mahakama.

Kuuliwa kwa mbwa huyo mashuhuri Immigration kulizua zogo kubwa katika vyombo vya habari, wanasheria, taasisi za uma zikaja juu na uchunguzi ukafanyika ambapo ilionekana kuwa hakimu alikosea kuamuru mbwa auliwe.

“Fikiria kisa hiki cha mbwa na Waislamu Mwembechai, ndio utajua hadhi ya Muislamu Tanzania.”

Alisema Sheikh Ilunga akionesha mahali Mfumo Kristo ulipowafikisha Waislamu.

Akahitimisha kwa kusema kuwa Jumapili Oktoba 16, Waislamu wanakutana Diamond Jubilee kuzungumzia namna ya kuondokana na idhilali hii. (An nuur Oktoba 14, 2011)

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s