Serikali isicheze na bei ya mkate

Mwandishi wa habari wa BBC; Sheikh Ally Saleh Abdallah (Alberto)

Na Ally Saleh

Waswahili wana msemo wao iwapo kuna jambo ambalo waliamini kuwa ni baya au uovu lilikuwa litokee lakini kikavunjika. Huwa wana sema Mwenyeenzi Mungu amepitisha kheri yake. Na Mswahili humtegemea sana Mungu kuwa ndio nguzo yake.Naamini wengi wa Waswahili wa Zanzibar waliinua mikono juu kushukuru kuwa kwa sababu moja au nyengine, Muswada uliokuwa ujadiliwe na pengine baadae kupitishwa, uliondolewa katika Baraza la Wawakilishwi kwa kurudishwa Serikalini.

Wengi wa watu mitaani walikuwa wakilalamika kuwa Muswada huo haukuwa zingatifu kwa wakati na umma kwa sababu nyingi na kwamba kuondoshwa kwake Barazani kumeleta faraja kwa watu wa kawaida ambao maisha yanazidi kubana kwao.

Muswada huo ukipania kuongeza marupurupu ya kustaafu viongozi wa kisiasa basi ni wiki iliyopita tu chakula kikuu cha Mzanzibari, ambacho karibu kila siku hula mara mbili, yaani boflo, kimepanda bei.

Wakati Serikali ikipeleka Muswada kunenepesha mafurushi ya ustaafu ya viongozi hao ambao wametafsiriwa katika Muswada huo kuwa ni Rais, Makamo wa Rais, Mwanasheria Mkuu, Maspika, Mawaziri na Manaibu, mkate wa boflo umepanda kutoka shs 150 hadi shs 200.

Bila ya shaka tafsiri ya kupeleka Muswada huu Mahakamni ni kuonyesha kuwa Serikali haijui kinachotokea mtaani, na kama inajua basi si zingatifu. Kuongezeka kwa kitanzi cha boflo katika baadhi ya nchi moja nikikumbuka ni Sudan kulimuondosha Rais Jaffar Numeir.

Ila kwa Zanzibar hilo lisingetokea hata siku moja baada watu wake ni wataratibu, watiifu kiasi ambacho wachache kama sisi ambao huwa tunasema tunaonekana kuwa ni wakorofi na kuna wakati hata tulibandikwa jina la wachochezi.

Lakini ni haki gani aliyonayo kiongozi wa kisiasa kumwita mtu mkorofi au mchochezi kwa kudai kuwa si haki kabisa kupanga kuongeza marupurupu ya viongozi hao ilhali wananchi waliowaweka madarakani wanasota na kudhikika?

Kuongezeka kwa bei ya boflo kwa mtu mwenye familia ya watu 7 ambao ni ya wastani hapa Zanzibar ina maana ni ongezeko la zaidi ya shs 20,000 kwa mwezi ambazo hazijaongezeka katika kipato chake kwa njia moja au nyengine.

Kama Serikali ina wachumi imara itajua ni kiasi gani nakisi ya kipato cha watu kinachodidimia kwa kuhesabu shs 20,000 kwa kaya moja na kisha izidishe kwa kaya zote za Zanzibar na kisha ifanye hesabu hiyo kwa mwaka.

Lakini sidhani kama wapangaji wa haya wanafikiria yote hayo. Ni kama ile hadithi ya Mfalme wa Ufaransa aliyeshangaa kwa nini watu wanaandamana kwa kukosa boflo na akasema kwa nini basi wasile keki.

Nilisema hapo awali kuwa bei ya boflo ilitosha kumuondosha Numeir madarakani kwa sababu wananchi wake walikereka seuze sasa na kuongezewa vunge la marupurupu ya wakubwa wetu ilhali nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi ikawa ni nyimbo ya kisiasa ya mafanikio yajayo ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kumbe, kwa macho yangu sasa naona ni chambo. Hata kabla ya nyongeza hiyo haijalipwa kwa wafanyakazi, pengine kama nakumbuka uzuri italipwa mwezi huu, ndoana ikachapuzwa kwa Muswada huu.

Muswada umeenda mbali zaidi kwa kuongeza tafsiri ya viongozi wa kisiasa kujumuisha pia Washauri wa Rais ambao hivi karibuni waliteuliwa kwa mkururo. Lakini pia baadhi ya washauri hao wanashikilia nafasi nyengine mbali mbali ambazo kwa wakati huu zinawapatia kipato kikubwa na hata pia waliapata viinua mgongo vyao kwa kazi zao za huko nyuma na pia kwa maana hiyo wanakula pensheni zao kama kawaida.

Muswada una vifungu vinavyoelezea juu ya marupurupu ya mwanasiasa kulipwa kwa mjane wake iwapo atafariki lakini pia kulipwa kwa watoto wake wakiwa ni warithi wake halali.

Huyu kizuka mbali ya kitita cha kustaafu ataendelea kupata pensheni ya kila mwezi. Kwa Rais hakuna suala la muda na kwa maana hiyo kizuka wake atalipwa uhai wake wote lakini kwa Makamo wa Rais wajane wamewekewa muda wa miaka mitatu

Ila Kifungu cha 26 kimenitisha kidogo kwa sababu kinajenga mazingira magumu ambayo kuachwa wazi yanaweza kuleta hali ya kujipendelea kwa Rais aliye madarakani au pia kutumika vibaya. Kifungu kinasema Rais aliye madarakani ataweza kuweka utaratibu wa malipo ya mafao kwa kizuka wa Kiongozi wa Kisiasa.

Kuna kipengele cha watoto wa Rais kulipwa pensheni ya kila mwezi hadi watapotimia miaka 18 na kwa mtoto wa kile iwapo ataolewa kabla ya umri huo, jambo amblo naliona ni la kibaguzi kwa nchi ambayo inajenga usawa wa raia wake na watoto wa Makamo wa Rais pia watastahili pensheni hiyo.

Halafu kwenye mpangilio wa Jadweli ndiko ambako hesabu hasa mtu unaziona za marupurupu ya viongozi hao wa kisiasa yangekuwa iwapo Muswada ungepita au pengine utapopelekwa tena iwapo hakuna watu watalalamika juu ya mkubwa wake.

Mfano Rais kulipwa kiinua mgongo kwa kiasi cha asilimia 50 ya mshahara wake, posho la kumaliza muda , pensheni ya kila mwezi kwa asilimia 80 ya posho la matunzo analolipwa Rais aliye madarakani, nyumba ya makaazi na msururu mwengine mrefu.

Na haya pia hufanyiwa Makamo wa Rais na Spika kwa mujibu wa kiwango chao kwa kuoneyesha tofuati ya daraja zao ambazo pia kisiasa ziko wazi.

Sasa haya yakipita tujue kuwa Zanzibar ina wastaafu wengi kabisa na Sheria ikapendekeza kuwa waliowahi kuwa Mawaziri Viongozi nao wahesabiwe kuwa na hadhi ya Makamo wa Rais, naam na wao wataula kwa staili mpya kabisa ya vyeo ambavyo hawakuvitumikia lakini wanavyofananishwa navyo.

Nilisema pale mwanzo kuwa baadhi ya watu walishukuru kuwa Muswada huo umeondoshwa Barazani lakini sote tunajua kuwa Muswada huo utarudi tena kwa hoja kuwa kuwepo kwa sheria ya viinua mgongo na pensheni za viongozi ni jambo la lazima, na hilo tunalikiri.

Lakini jambo ambalo halitasemwa ni kwa nini marupurupu hayo ni makubwa sana, yanahusisha wigo mpana sana na kwa hivyo yanameza sehemu kubwa ya mapato ya nchi? Sijajaribu kupanga hesabu itavyokuwa lakini naamini kwa msururu wa viongozi tulionao basi bajeti ya kuwalipa viongozi wa kisiasa kwa mwaka itakuwa kubwa kiasi mabega ya taifa yataelemewa.

Ila najua kama kawaida ya Wazanzibari hili litapita. Wachache tutaosema, wachache tutaolalamika na wachache tutaotoa sauti na kuandika, lakini hakuna ataesikia na kuona athari kubwa ya kuwa na msururu wa viongozi wanaolipwa mafao makubwa kwa ukosefu wa dawa, ukosefu wa madeski maskulini mwetu.

Na maisha ya Mzanzibari yatasonga mbele kwa bei ya boflo, petroli, vyakula kuongezeka na akisononeka yeye na watoto wake kimya kimya. Na kesho wakati wa kampeni utafika na atakwenda kupiga kura. Mungu iweke Zanzibar na watu wake watiifu.

source: mwananchi

Advertisements

One response to “Serikali isicheze na bei ya mkate

  1. Bi Salma musijali sana, kama mkate ni ghali basi tutakuombeni na kwa muda huu kwanza mule KEKI hadi hapo bei ya mkate itakaposhuka.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s