Ofisi ya uchaguzi Pemba haina hadhi

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Khatib Mwinchande

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema jengo la ofisi ya Tume ya uchaguzi liliopo Chake Chake Pemba halina hadhi ya kuwa ofisi yenye jukumu kubwa la kusimamia shunguli nyeti kama za uchaguzi mkuu.Kaimu Waziri wa Nchi ofisi ya makamo wa pili wa Rais, Ali Juma Shamhuna aliyasema hayo wakati akijibu swali la Mwakilishi Shadya Mohamed Suleiman (CCM) aliyetaka kujuwa lini ofisi mpya ya Tume ya Uchaguzi itajengwa huko kisiwani Pemba.

´Nakiri ofisi ya Tume ya uchaguzi iliopo sasa hapo Chake Chake jengo lake halina hadhi ya kuwa ofisi ya uchaguzi…..napenda kuwaarifu wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba tumepata kiwanja cha kujenga ofisi mpya hapo Mfikiwa Chake Chake´. alisema Shamhuna.

Alisema kazi za ujenzi wa ofisi hiyo zitaanza mara baada ya serikali kuu kuingiza fedha katika kasma ya Tume ya uchaguzi.

Shamhuna alisema eneo la Mfikiwa ni zuri na lenye usalama wa hali ya juu na kuwatoa wasiwasi wajumbe wa baraza la wawakilishi kuhusu ofisi hiyo ambayo inatarajiwa kujengwa katika eneo hilo.

Baadhi ya wajumbe wa baraza la wawakilishi walidai kwamba ofisi mpya itakayojengwa huko Mfikiwa ipo mbali sana na mji kiasi ya kuwapa usumbufu wananchi pamoja na wanasiasa.

Akijibu hilo la kuwepo mbali ofisi mpya Shamhuna alisema eneo hilo katika kipindi kifupi litakuwa mji wenye mahitaji mbali mbali muhimu kwani upo katika njia inayokwenda katika uwanja wa ndege wa Karume Pemba sehemu ambayo imechangamka katika harakati mbali mbali.

Uwanja wa ndege wa Zanzibar kupanuliwa jengo.

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume uliopo Unguja utafanyiwa ukarabati mkubwa ukiwemo upanuzi wa jengo la abiria,naibu waziri wa mawasiliano na miundo mbinu Issa Haji Ussi aliwaambiya wajumbe wa baraza la wawakilishi.

Ussi alikuwa akijibu swali lililoulizwa na Mwakilishi wa nafasi za wanawake kutoka (CCM) Mwanaidi Kassim Mussa aliyetaka kujuwa kwa nini baadhi ya huduma katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Abeid Amani Karume Zanzibar hazipo imara ikiwemo za kibenki ya za afya.

Ussi alisema kwamba juhudi za kuimarisha huduma hizo kwa sasa zinaendelea huku akitoa mfano kama ujenzi wa jengo la kisasa kujumuisha mambo yote muhimu ikiwemo taasisi za kifedha za kibenki.

‘Tumekusudia ujenzi wa kisasa wa upanuzi wa jengo la uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume kuwa na hadhi ya kimataifa……tunataka kuona huduma za kibenki na afya ikiwemo hospitali zinapatikana’alisema Ussi.

Benki ya Exim kutoka China imeipatia Zanzibar mkopo wenye masharti nafuu kwa ajili ya kazi za ujenzi wa jengo la abiria litakalokuwa na hadhi ya kimataifa. Alisema mikakati hiyo imeandaliwa na mamlaka ya viwanja vya ndege vya Zanzibar kwa ajili ya kutoa huduma katika muelekeo wa kimataifa.

Kwa mfano alisema Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume kwa sasa umekuwa ukipokea zaidi ya watalii Laki moja kwa mwaka, hatua ambayo inatakiwa kwenda sambamba na uimarishaji wa huduma hizo ili wageni watakaoingia Zanzibar waweze kupata mazingira mazuri na huduma muhimu katika uwanja huo.

Uvamizi wa vyanzo vya maji.

WATU watakaojenga karibu na vianzi vya maji hawatolipwa fidia na ni marufuku kufanya hivyo serikali imesema katika kikao cha baraza la wawakilishi kufuatia maswlai na majibu ya baadhi ya wajumbe wa baraza hilo.

Waziri wa Ardhi, Makaazi Maji na Nishati, Ali Juma Shamuhuna alisema hayo wakati akijibu swali aliloulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Ayoub Hashim aliyetaka kujuwa hatua gani zinazochukuliwa kwa watu wanaojenga katika vyanzo vya maji ambao mbali ya kuharibu mazingira lakini pia huvamia maeneo vianzio hivyo vya maji.

Shamuhuna alisema hivi sasa kumekuwepo na kasi kubwa ya ujenzi wa nyumba katika vyanzo vya maji kiasi ya kuhatarisha maisha ya wananchi wanaotumiya maji ambayo huchanganyika na uchafu ikiwemo vinyesi na kuhatarisha afya za wananchi wengi.

‘Kasi ya ujenzi wa nyumba katika vianzio vya maji ni kubwa sana kwa sasa…wananchi wanajenga karibu sana na vyanzo vya maji ambapo ipo hatari kubwa wananchi kupata maradhi kutokana na maji hayo kuharibiwa kwani inapotokea maradhi ya miripuko ndio hali huwa mbaya zaidi’ alisema Shamuhuna.

Alizitaja baadhi ya vyanzo vya maji ambavyo vipo katika hatari kubwa ya kuharibiwa ikiwemo Bububu na Mwanyanya ambapo wananchi wamevamia vyanzo licha ya kuondoshwa mara kadhaa lakini wamerudi tena na kuendelea kuishi huku wengine ndio kwanza wakianza kujenga nyumba zao katika maeneo hayo.

Aidha alisema kasi ya ujenzi wa makaazi ya nyumba za watu ni moja ya sababu kubwa inayochangia kuwepo kwa ujenzi holela ikiwemo katika vyanzo vya maji jambo ambalo limekuwa likipigiwa kelele sana na mamlaka zinazohusika ikiwemo mamlaka ya maji na idara ya mazingira kwa kuwa ni sehemu hatarishi kwa wananchi kuishi.

Mswada wa madawa ya kulevya..

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetakiwa kujenga Vituo maalumu kwa ajili ya kuwatibu vijana ambao wameathirika na matumizi ya madawa ya kulevya; Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa kamati ya Katiba na Utawala Bora Ali Abdalla Ali wakati akiwasilisha maoni ya kamati hiyo katika mswada wa kurekebisha baadhi ya sheria na kuweka masharti bora ndani yake.

Abdalla alisema hivi sasa yamekuwepo mafanikio makubwa kwa baadhi ya taasisi kuwachukuwa na kuwapatia tiba vijana kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya. ‘Tumepata taarifa kwamba wapo zaidi ya vijana 200 sasa wameachana na matumizi ya madawa ya kulevya kutokana na juhudi za baadhi ya taasisi kuwahifadhi vijana hao kwa kuwatibu na kuwapatia ushauri nasaha’alisema.

Alisema juhudi hizo ni lazima ziungwe mkono na Serikali kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wimbi la vijana wanaoyumia madawa ya kulevya linapunguwa. Mapema Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Othman Masoud Othman imesema serikali imedhamiria kupambana na vitendo vya usafirishaji wa fedha haramu pamoja na madawa ya kulevya ambayo kasi yake ni kubwa.

Othman aliwaambiya wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba Mswaada huo kwa ujumla una mambo matatu ikiwemo kudhibiti madawa ya kulevya na marekebisho yake ya sheria nambari 9 ya mwaka 2009, makosa ya jinai sheria nambari 7 ya mwaka 2004 pamoja na usafirishaji wa fedha haramu ya nambari 10 ya mwaka 2009.

Alisema Zanzibar imeamuwa kuja na mswada wake na kutotumia ule wa Jamhuri ya Muungano uliowasilishwa bungeni. Alifafanua zaidi na kusema katika marekebisho ya mswada huo kwa upande wa madawa ya kulevya utaruhusu kuundwa kwa Tume ya kuratibu madawa ya kulevya ambayo itakuwa chini ya Ofisi ya Makamo wa kwanza wa rais.

Awali katika sheria iliyopita tume hiyo ilikuwa chini ya ofisi ya Waziri Kiongozi kabla ya kubadilika kwa muundo na mfumo wa Serikali ya Mapinduzi ambapo nafasi hiyo kwa sasa haipo tena. Alisema mswada wa madawa ya kulevya umefanyiwa marekebisho mara kadhaa kwa lengo la kuweka masharti sambamba na sheria ya usafirishaji wa fedha haramu ambayo biashara hiyo inahusishwa na madawa ya kulevya.

‘Tumefanya marekebisho ya sheria zetu ili zende sambamba na sheria ziliopo katika jumuya ya nchi za SADC katika mapambano ya madawa ya kulevya na fedha haramu’ alisema Othman.

Habari hizi ni kwa hisani ya Khatib Suleiman

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s