Gaddafi ahifadhiwa jokofuni

Marehemu Muammar Gaddafi

LICHA ya makamanda wa kijeshi jijini hapa kukataa kuufanyia uchunguzi mwili wa Muammar Gaddafi licha ya malalamiko kuhusu jinsi kiongozi huyo alivyouawa, hivi sasa wamebanwa kuchunguza mazingira ya kifo hicho.Kiongozi wa muda, Mustafa Abdel Jajil, alisema jana kwamba uchunguzi unaendelea kujua mazingira ya mauaji ya Gaddafi baada ya kukamatwa kwake, akiwa ametapakaa damu akiwa hai, Alhamisi iliyopita jijini Sirte, baada ya serikali nyingi duniani na vikundi vya haki za binadamu kuhoji.

Lakini uongozi wa kijeshi jijini hapa, ambako mwili wa Gaddafi umehifadhiwa katika jokofu la kuhifadhia mboga sokoni na kuwekwa hadharani kwa mara nyingine jana kwa mamia ya watu kuutazama, ulisisitiza kuwa uchunguzi huo utafanywa bila kuchunguza mwili.

“Hakutakuwa na uchunguzi wa mwili leo, wala siku nyingine yoyote,” Msemaji wa Baraza la Kijeshi la Misrata, Fathi al-Bashaagha, aliiambia AFP. “Hakuna atakayeupasua mwili wake.”

Kauli yake ilithibitishwa na wakuu wengine wawili wa kijeshi. Bashaagha alisema kamanda mpya wa utawala wa kijeshi katika Jiji hili, Abdelhakim Belhaj, alitarajiwa kuwasili hapa baadaye jana kuuangalia mwili huo wa mtu aliyeiongoza Libya kwa miaka 42.

Lakini alisema hakukuwa na mipango ya Mkuu wa Baraza la Muda la Utawala (NTC), Abdel Jalil kuzuru hapa. “Abdel Jalil hakuja jana na haji leo, na kwa sasa haitarajiwi kama atakuja.” Kiongozi huyo wa muda alikuwa Benghazi jana akizuru baadhi ya majeruhi waliotokana na mapigano ya miezi minane yaliyomng’oa Gaddafi. “Ndiyo,” alijibu alipoulizwa kama mazingira ya kifo cha Gaddafi yanachunguzwa.

Lakini hakutaka kusikiliza maswali zaidi. Hata hivyo, swali linabaki juu ya jinsi Gaddafi alipokutana na mauti yake baada ya wapiganaji wa NTC kumtoa ndani ya kalvati ambako alijificha kutokana na mashambulio ya angani ya majeshi ya Nato dhidi ya msafara wake akijaribu kutoroka, baada ya Sirte kutekwa. Picha za simu za mkononi zilimwonesha akiwa hai.

Picha hizo zilimwonesha uso wake ukiwa umefunikwa nusu na damu, akivutwa kupelekwa kwenye gari na kundi la watu wenye hasira na kutupwa kwenye boneti. Waliokuwa mbele yake wanaonekana wakimsukuma na kumsukasuka, wakimvuta nywele na kumpiga. Wakati fulani anaonekana akijaribu kuzungumza.

Sehemu nyingine anaonekana akishushwa kwenye gari, akiwa bado hai, na kuoneshwa kwa umati unaopiga kelele, kabla hajatoweka huku mlio wa risasi ukisikika.

Viongozi wa NTC wanakana kuwa alipigwa risasi kichwani alipokamatwa “katika majibizano ya risasi” kati ya wafuasi wake na wapiganaji wa utawala mpya mara baada ya kukamatwa. “Umekuwapo uvumi ukienea tangu mauaji ya Gaddafi, baada ya picha zilizooneshwa, ukidai kwamba wanamapinduzi walimwua,” ofisa mwandamizi wa NTC alisema.

“Hakuna maagizo yaliyotolewa kumwua Gaddafi, na hatuamini kuwa wanamapinduzi wetu walimwua kwa makusudi.”

Lakini kwenye picha za video zinazozunguka kwenye intaneti, anaonekana kijana mpiganaji kutoka Benghazi akidai kumpiga risasi Gaddafi mara mbili baada ya kumkamata – mara moja chini ya mkono na mara moja kichwani. Alisema alikufa nusu saa baadaye. Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, alisema “jinsi kifo chake kilivyotokea inaacha maswali mengi,” na kuhitaji uchunguzi wa kina.

“Picha tulizoona kwenye televisheni, zinaonesha kwamba alichukuliwa mateka akiwa majeruhi na kisha baadaye, akiwa tayari mateka, maisha yake yakaporwa.”

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani, Mark Toner, alisema NTC “tayari inashughulikia kujua hasa kiini na mazingira ya kifo cha Gaddafi na dhahiri tunawataka kufanya hivyo kwa uwazi huku tukisubiri ya baadaye.” Toner alirudia mwito wa Marekani kwa NTC kuwatendea utu wafungwa. Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa (UN), Navi Pillay, naye alitaka ufanyike uchunguzi wa kina.

“Kwa suala la kifo cha Gaddafi juzi, mazingira bado hayaeleweki,” Msemaji wake Rupert Colville, alisema. “Lazima kufanyike aina fulani ya uchunguzi kutokana na tulichokiona jana (juzi).”

Claudio Cordone, Mkurugenzi Mwandamizi wa Taasisi ya haki za binadamu ya Amnesty International, alisema Gaddafi “aliuawa baada ya kukamatwa, hiyo itafanya kuwapo mazingira ya uhalifu wa kivita na waliohusika lazima wafikishwe mbele za haki.” Alisema, “NTC inapaswa kutumia viwango sawa kwa wote, kutumia haki hata kwa wale waliokataa kuitumia kwa wenzao.” Mjane wa Gaddafi, Safia, ambaye alikimbilia Algeria, Agosti, ameitaka UN kuchunguza mazingira ya kifo cha mumewe, televisheni ya Syria, Arrai, imesema.

CHANZO: HABARI LEO

One response to “Gaddafi ahifadhiwa jokofuni

 1. Inalilah waina lilah rajiu’un.
  kwa kweli ni kitendo ja ukatili wa hali ya juu sana,
  ndiyo alikuwa na mapungufu yake kama binadamu tulivyo kwani
  mkamilifu ni mungu pekee. lakini akustahili adhabu hiyo aliyo ipata
  kwakuwa walimchokoza hao walio leta chokochoko za kutaka kuichafua libya
  na kupandikiza chuki kwa wananchi wa libya matokeo yake ni hayo , vifo
  vya watu wengi wasio na hatia. lakini mkumbuke kuwa bila hao wenye chokochoko leo libya isinge kuwa hapo ilipo sasa
  Na wachukia sana wanao shangilia kifo cha gaddaf. M’ mungu akulaze mahali pema peponi amein.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s