Mswaada wa mafao warejeshwa.

Waziri anayeshughulikia fedha, uchumi na mipango ya maendeleo ya Zanzibar, Omar Yussuf Mzee

Mswaada wa mafao ya wakubwa warejeshwa serikalini

Mswaada uliotayarishwa kwa ajili ya kutengeza sheria mpya ya maslahi na mafao ya viongozi wa kisiasa baada ya kustaafu pamoja na mambo mengine umeondoshwa katika shunguli za orodha ya baraza la wawakilishi kutokana na wawakilishi kuukataa.

Mswada huo umeondolewa baada ya kubainika kuwepo kwa kasoro mbali mbali ikiwemo tafsiri ya maneno. Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho alikiri kuondolewa kwa Mswaada huo ingawa hakutoa ufafanuzi zaidi wa sababu zake.

Aidha Katibu wa Baraza la Wawakilishi Ibrahim Mzee Ibrahim naye kwa upande wake alikiri kuondolewa kwa mswaada huo katika orodha ya shunguli za baraza la wawakilishi ambapo kikawaida shughuli zote za baraza zinazofanyika huandikwa katika utaratibu maalumu.

‘Ni kweli mswaada wa sheria ya maslahi na mafao ya viongozi wa kitaifa umeondolewa katika orodha ya shunguli za Baraza la Wawakilishi’ alisema kwa ufupi bila ya ufafanuzi wa ziada kwa mwandishi wa habari hizi.

Mwenyekiti wa kamati ya viongozi wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma alisema Mswaada huo wamekubaliana urejeshwe Serikali ili ufanyiwe marekebisho mbali mbali muhimu kwani kuna kasoro ambazo zinahitaji kufanyiwa marekebisho kabla ya kuwasilishwa katika kikao cha baraza la wawakilishi ili kutoa fursa ya wajumbe kuujadili na kuupitisha.

‘Tumekubaliana mswaada huo urudi tena Serikali katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwa ajili ya ufafanuzi wa ziada…zipo tafsiri ya maneno mbali mbali ambazo zinahitaji ufafanuzi lakini utakaporejeshwa utafanyiwa kazi na wataalamu baadae ndio utawasilishwa barazani na sisi kama wajumbe tutaweza kuujadili’ alisema Hamza.

Mswaada huo ulikuwa uwasilishwe katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Mwinyihaji Makame Mwadini alitarajiwa kuuwasilisha barazani hapo.

Baadhi ya vipengele vilivyotajwa katika mswaada huo ikiwemo kuwashirikisha kulipwa mafao wajane wa viongozi wa Serikali,watoto wao,wahudumu pamoja na Spika na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi jambo ambalo linaelezwa kuwa ni gharama zisizo za lazima zinazojibebesha serikali wakati serikali ina mambo muhimu ya kufanya katika kuwaletea maendeleo wananchi wake na kuimarisha sekta mbali mbali za huduma za kijamii.

Vipengele hivyo kinachomhusu mtu ataeshika nafasi ya rais wa Zanzibar atalipwa kama inavyomstahikia na endapo atafariki kizuka wake atastahiki kulipwa na mamlaka husika pencheni ya kila mwezi inayokuwa sawa na mshahara wa rais aliye madarakani.

Kipengele kidogo cha (3) cha kifungu cha 10 cha sheria hiyo kimeeleza kuwa endapo rais mstaafu atafariki dunia watoto wake walio chini ya umri wa miaka 18 watastahiki kulipwa pencheni ya kila mwezi iliyo sawa na kima cha chini cha mshahara wa mtumishi wa umma.

Spika wa Baraza la Wakilishi, Pandu Ameir kificho, alisema wajumbe wengi wameona ni bora kuwekwa vipaumbele kwenye masuala ya uchumi na  mambo yanaohusu jamii kuondoa umaskini. “Suala hili lingali linaleta mgawanyiko kidogo kwenye jamii, ndiyo maana wajumbe wakaona ni vyema kuliweka kando kwanza na kwenda kulitafakari upya kwa maslahi ya taifa,” alisema Kificho na kuongeza:“Muswada huo umeondolewa kutokana na kuwapo kasoro nyingi na hata upande wa tafsiri yake katika vifungu vingi havifahamiki.”

Katika muswada huo ulikuwa unampa rais uwezo kupokea mshahara wake wote baada ya kustaafu na pindi anapofariki, mkewe angepokea pencheni kama mshahara wa rais aliyopo madarakani.Kwa upande wa makamu wa rais, kama akifariki mkewe angepokea kwa muda wa miaka mitatu mshahara sawa na aliokuwa akipokea mume wake akiwa madarakani.Pia, spika akistaafu angelipwa kiinua mgongo kwa asilimia 50 mshahara wake aliokuwa akilipwa akiwa madarakani. Kuondolewa kwa mswada huo ni kuzima hasira za wananchi kutokana na kudai kuwa Serikali inatoa kipaumbele kwa viongozi, ilhali wananchi wanaendelea kuwa maskini wa kutupwa.

mwisho.

Sheria mpya kuwabana wasiorejesha mikopo

Zaidi ya shingili bilioni 7 sehemu ya fedha zilizotolewa na elimu ya juu Zanzibar na kukopeshwa kwa wanafunzi mbali mbali kwa ajili ya masomo bado hazijarejeshwa na kusababisha waombaji wapya kukosa.

Waziri wa Elimu Zanzibar, Ramadhan Abdalla Shaaban alisema hayo wakati alipozungumza na gazeti la Habari Leo kuhusu hali ya mikopo na kusema kwamba miongoni waliopewa mikopo hiyo tayari wameajiriwa katika utumishi wa serikali.

Alisema fedha hizo sh.Bilioni 7.8 kwa njia moja au nyengine zimesababisha mwaka huu baadhi ya wanafunzi na waajiriwa wengine wa Serikali walioomba vyuo vya nje ya nchi kukosa fursa hiyo.

Shaaban alisema bodi haijakaa kimya na inaendelea kufuatilia suala hilo iliwemo kuwafuata watumishi walioajiriwa serikalini ambao walichukuwa mikopo hiyo. ‘Bodi bado haijazisamehe fedha hizo nyingi za serikali….imeanza kufuatilia kwa kutumia nasaha kuona zinarejeshwa na kutumiwa kwa matumizi mengine;alisema Shaaban.

Waziri alifahamisha na kusema kwamba tayari bodi imeanza kutumia sheria mpya namba 3 ya mwaka 2011 ya kuanzishwa kwa bodi ya mikopo ya elimu ya juu kuanzia mwezi wa july na kufuta sheria nambar 6 ya mwaka 2001.

Sheria hiyo mpya miongoni mwa majukumu yake ni kuhakikisha kwamba madeni yote ya zamani yaliyopo mikononi mwa wanafunzi yanafuatiliwa na kurejeshwa.

mwisho.

SMZ inatafuta meli ya abiria kwenda Pemba.

Serikaliya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inatafuta usafiri wa uhakika wa meli kwa ajili ya kutoa huduma za abiria katika kisiwa cha Pemba.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundo Mbinu; Issa Haji Ussi wakati akijibu swali aliloulizwa na Mwakilishi wa viti maalumu CCM Shadya Mohamed Suleiman aliyetaka kujuwa lini Serikali itawapatia wananchi wa Pemba uhakika wa meli.

Ussi alisema alisema Serikali inafahamu tatizo la usafiri linalowakabili wananchi wa Pemba zaidi baada ya ajali ya MV.Spice Islande iliyotokea mwezi uliopita.

‘Serikali inafahamu tatizo la usafiri linalowakabili wananchi wa Pemba…..tunalishungulikia suala hilo ikiwemo kufanya mazungumzo na taasisi mbali mbali zinazotoa huduma za meli za kimataifa.’alisema Ussi.

Alisema tatizo la usafiri wa meli kwenda katika kisiwa cha Pemba umejitokeza hivi karibuni baada ya meli ya MV.Serengeti kusitisha safari zake kutokana na matatizo ya hitilafu mbali mbali.

Ussi alisema meli hiyo imezuiliwa kusafiri kwenda Pemba baada ya kujitokeza kwa hitilafu mbali mbali ambazo zinatakiwa kufanyiwa marekebisho yake kabla ya kutoa huduma za usafiri wa abiria.

‘Tumewataka kufanya marekebisho ya matengenezo mbali mbali katika meli hiyo kabla ya kutoa huduma za usafiri kwa abiria…’alisema.

mwisho.

Mahabusu kuachana na makarandika.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itafanya mazungumzo na jeshi la Polisi kuona kwamba mahabusu wanaofikishwa mahakamani wanapata usafiri mzuri wa mabasi na sio makarandinga ambayo hutumika hivi sasa kuwabeba.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Mwinyihaji Makame Mwadini wakati akijibu swali la Mwakilishi Shadya Mohamed Suleiman wa viti maalumu CCM aliyetaka kujuwa lini Serikali itaanzisha huduma za usafiri wa mabasi kwa mahabusu wanaofikishwa mahakamani kama vile Tanzania Bara.

Mwinyihaji alikiri na kusema kumekuwepo na mabadiliko makubwa ya utoaji wa huduma za usafiri kwa wafungwa na mahabusu wanaofikishwa katika mahakamani huko Tanzania Bara ikiwemo kutumia mabasi.

Alisema kwa upande wa Zanzibar utaratibu wa kupeleka mahabusu katika mahakama upo chini ya Jeshi la Polisi,lakini suala hilo litafanyiwa kazi.

‘Tutauangalia utaratibu huo na kuona kama unatufaa basi tutautumia kwa sababu lengo la serikali ni kutoa huduma nzuri kwa mahabusu na wafungwa katika magereza yake’alisema Mwinyihaji.

Alisema kutoa huduma nzuri kwa wafungwa na mahabusu ikiwemo kuwapatia usafiri mzuri wakati wa kwenda mahakamani ni sehemu ya utekelezaji mzuri wa utawala bora na kuheshimu haki za binaadamu.

Kwa mfano alisema hivi sasa huduma katika magereza ya Zanzibar zimeimarishwa ikiwemo wafungwa na mahabusu kupata chakula kizuri na sehemu nzuri ya malaazi.

Habari zote na Khatib Suleiman

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s