Gaddafi auawa

Hatimae Kanali Muammar Gaddafi ameuawa

MAKAMANDA wa Serikali ya Mpito nchini wamedai kumkamata Kanali Muammar Gaddafi, na kumjeruhi na kusababisha kifo chake kutokana na majeraha aliyopata. Taarifa hizo zilikuja jana baada ya vikosi vya Serikali hiyo kudai kudhibiti Jiji la Sirte, mahali alikozaliwa Gaddafi, baada ya wiki kadhaa za mapigano makali.

Kanali Gaddafi inasemekana alijeruhiwa katika purukushani na akapoteza damu nyingi kutokana na majeraha miguuni kulikosababisha apoteze maisha wakati akikimbizwa hospitalini Misrata kwa gari la wagonjwa.

Hata hivyo, awali hakukuwa na uthibitisho wa uhakika wa taarifa hizo. Kanali huyo aling’olewa Agosti baada ya kukaa madarakani kwa miaka 42. Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) inamsaka. “Amekamatwa. Amejeruhiwa miguu,” Ofisa wa Baraza la Taifa la Mpito (NTC), Abdel Majid aliiambia Reuters jana.

“Amechukuliwa na gari la wagonjwa,” aliongeza. AFP ilimkariri ofisa mwingine wa NTC, Mohamed Leith, akisema Kanali Gaddafi alikamatwa Sirte na “alijeruhiwa vibaya” lakini bado alikuwa anapumua. Kama taarifa za kukamatwa kwa kiongozi huyo zitakuwa za kweli, basi Mohammed al-Bibi ndiye atakuwa shujaa. Huku akionesha bastola ya rangi ya dhahabu aliyodai ilikuwa ikimilikiwa na Gaddafi, alibebwa juu kwa juu na wapiganaji wenzake waliokuwa wakishangilia.

“Allah akbar(Mungu mkubwa),” waliimba huku wakifyatua risasi angani. Mohammed, ambaye ni mpiganaji mwenye umri wa miaka ya 20, aliyekuwa amevalia kofia ya wachezaji wa mpira wa magongo wa New York Yankees, alisema alimkuta Gaddafi akiwa amejificha shimoni ardhini.

Aliiambia BBC kwamba kiongozi huyo wa zamani alimwambia kwa upole: “Usiniue”. Wapiganaji wa waasi wanasema Kanali Gaddafi alichukuliwa kwa gari la wagonjwa kupelekwa Misrata. Kama ndivyo, basi Jiji la Sirte litakuwa limeangukia mikononi mwao na sasa kudhihirisha mapinduzi ya uhakika ya Libya – hatua ambayo itaashiria kumalizika kwa mapigano na mchakato wa kisiasa kuanza.

Mwanajeshi aliyedai kumkamata Gaddafi aliiambia BBC kwamba Kanali huyo alipiga kelele za: “Usifyatue risasi.” Habari jijini hapa zinasema ingawa kukamatwa huko hakukuwa kumethibitishwa bado, meli na magari yalisikika yakipiga honi jijini hapa huku bunduki zikihanikiza kwa sherehe.

Mapema makamanda wa NTC walioko hapa, umbali wa kilometa 360 Mashariki mwa Tripoli – walisema Jiji limekombolewa. “Hakuna vikosi vya Gaddafi popote,” Kanali Yunus al-Abdali aliiambia Reuters. “Hivi sasa tunawakimbiza wapiganaji wake ambao wanajaribu kutoroka.” Hakukuwa na uthibitisho wowote kutoka NTC.

Lakini wapiganaji jijini hapa walionekana kushangilia huku wakifyatua risasi angani na kuimba Mungu mkubwa. Vikosi vya serikali ya muda vimekuwa vikikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wadunguaji jijini hapa huku wengine wakitumia mizinga mizito wakati wa mapambano hayo. Maelfu ya raia wamekimbia.

NTC pia ilipata madhara makubwa katika mji wa Bani Walid ulioko Kusini Mashariki mwa Tripoli, katika wiki za karibuni. Jumatatu NTC ilisema ilishakamata asilimia 90 ya mji huo ikiwa ni pamoja na eneo la katikati. “Alipigwa pia kichwani,” ofisa wa NTC, Abdel Majid Mlegta aliiambia Reuters. “Kulikuwa na mapigano makali dhidi ya kikundi chake na alipoteza maisha.”

Mlegta aliiambia Reuters kwamba Gaddafi ambaye alikuwa katika umri wa miaka 60, alikamatwa na kujeruhiwa miguu jana wakati akijaribu kukimbia akiwa katika msafara ambao ndegevita za majeshi ya NATO ziliushambulia. Mpiganaji wa waasi alisema Gaddafi alikutwa amejificha katika shimo ardhini na kuwambia
waliomkamata: “Msifyatue risasi, msifyatue risasi.”

Gaddafi ambaye alikuwa anasakwa na ICC kwa mashitaka ya kuamuru mauaji ya raia aliangushwa na vikosi vya waasi Agosti 23. Gaddafi aliiongoza Libya tangu mwaka 1969 baada ya kuangusha utawala wa kifalme uliokuwapo katika mapinduzi ambayo hayakumwaga damu. Akiwa madarakani mwaka 1977 alitangaza Jamhuri ya Libya kuwa ya kidemokrasia (jamahriya) na kuondoka madarakani miaka miwili baadaye, ingawa aliendelea kuwa na nguvu kisiasa.
Alianzisha na kufuata sera za kupinga ukoloni na sera ya mambo ya nje ya Umajumui wa Afrika huku Marekani na nchi za Ulaya zikilalamika kuwa anafadhili ugaidi.

Kabla ya tukio la jana, Gaddafi aliyekuwa ameapa kufia nchini mwake, alishaiondoa familia yake na kuipeleka uhamishoni na yeye kubaki akishirikiana na vikosi vyake shupavu kupambana na waasi waliokuwa na nguvu ya ziada ya Nato. Mlolongo wa matukio jana Saa 9.32 alasiri: Kuna shamrashamra mitaani Tripoli huku ripoti zikizagaa juu ya kukamatwa na uwezekano wa kuuawa Gaddafi.

Serikali ya Mpito iliwaita waandishi wa habari zaidi ya saa moja iliyopita kwa ajili ya mkutano muhimu, lakini bado halijatolewa tangazo rasmi. Saa 9.16 alasiri: Mpiganaji anaiambia AP kwamba alikuwapo wakati Gaddafi anapigwa kwa bunduki yenye mtutu wa milimeta tisa sehemu za chini ya mwili.

Akiwa amesimama mbele ya lori huku akipongezwa na wenzake, anasema alimpiga kiongozi huyo kwa kiatu – tusi kubwa kwa ulimwengu wa Kiarabu – anakionesha kiatu chake juu kwa
msisitizo. Saa 9.04 alasiri: Jijini Sirte, wapiganaji waliopigana kwa miezi kadhaa kuikamata nchi kutoka vikosi vya Gaddafi wanakumbatiana barabarani huku wakiimba. “Vita vimemalizika.”

Saa 8.54 mchana: Msemaji wa Serikali ya Mpito anasema Gaddafi amekamatwa na yawezekana ameuawa. Waziri wa Habari, Mahmoud Shammam, anasema anatarajia Waziri Mkuu kutoa tangazo katika saa moja ijayo au zaidi.

CHANZO: HABARI LEO

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s