Mwekezaji etelekeza kiwanda

SPIKA wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho akisisitiza jambo na Wajumbe wa Baraza, Fatma Abdulhabib Ferej na Zahra Ali Hamad ambao wote ni mawaziri wakiwa nje ya Ukumbi baada ya kuhairishwa kwa kikao cha baraza hilo,

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekiri na kusema kwamba muwekezaji aliyepewa kiwanda cha sukari kiliopo Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja amekitelekeza kwa kushindwa kuzalisha sukari kama ilivyokusudiwa.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Viwanda Biashara na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui wakati akijibu swali aliloulizwa na Mwakilishi wa viti maalumu; Panya Ali Abdalla aliyetaka kujuwa lini muwekezaji huyo atazalisha sukari na kama ameshindwa kwa nini harudishi mashamba hayo serikalini yakatumiwa kwa ajili ya kilimo kwa wananchi.

Akifafanua zaidi Mazrui alisema tangu kiwanda hicho kuchukuliwa kwa muwekezaji zaidi ya miaka mitano sasa bado hajazalisha sukari kwa ajili ya matumizi ya soko la ndani na nje.

Alisema alichofanya muwekezaji huyo,ni kuzalisha sukari guru pamoja na spiriti tu kinyume na malengo yaliyokusudiwa na kufikiwa kati ya muwekezaji na serikali.

Hata hivyo Mazrui aliwataka wananchi kumpa muda zaidi muwekezaji huyo kuendelea na shunguli zake huku akifanya juhudi za kuweza kuzalisha sukari hiyo.

Aidha alisema serikali imeunda kamati tatu kuchunguza kuhusu hali ya kiwanda hicho na muwekezaji huyo ili kujuwa hatma yake.

Alisema kwa mujibu wa mikataba iliyofikiwa kati ya muwekezaji huyo na mamlaka ya vitega uchumi lazima yaheshimiwa na hakuna sababu za kuvunja mkataba kwa sasa.

Aidha Mazrui alikemea vitendo vya hujuma vinavyofanywa na wananchi wanaoishi jirani na kiwanda hicho cha sukari na kusema kwamba vinaweza kuisababishia serikali hasara kubwa.

‘Nawaomba wananchi wawe na subra wakati suala hilo likifanyiwa kazi….hakuna sababu yakufanya hujuma kama hizo zinazofanywa na baadhi ya watu kuchoma moto mashamba ya miwa’alisema Mazrui.

Kiwanda cha sukrai kilijengwa na msaada mkubwa na wataalamu kutoka China katika mwaka 1971,ambapo kilikuwa kikizalisha tani za sukari 6,000 kwa mahitaji ya ndani na nje katika soko la Afrika ya Mashariki.

Pia kilikuwa kikizalisha Pombe kali pamoja na sabuni za manukato zilizopata umaarufu mkubwa katika soko la ndani na nje.

mwisho.

Doria za ukanda wa bahari kuu zimesaidia

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema imeanzisha doria katika ukanda wa eneo la bahari kuu kwa ajili ya kupambana na vitendo vya uharamia ikiwemo uvuvi haramu unaofanywa na meli kubwa za kigeni.

Hayo yalisemwa na waziri wa uvuvi na mifugo, Said Ali Mbarouk wakati akijibu swali aliloulizwa na mwakilishi wa viti maalumu wanawake kutoka kusini Unguja CCM, Asha Abdi Haji aliyetaka kujuwa juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kupambana na uvuvi haramu ikiwemo doria.

Mbarouk alisema mara utakapomalizika ujenzi wa jengo la Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu Serikali itanunuwa kifaa ambacho kitawekwa kwa ajili ya kuratibu na kuangalia vyombo vyote vinavyojishungulisha na uvuvi haramu.

‘Tayari tupo katika hatua za mwisho za kununuwa chombo cha aina hiyo ambacho kitawekwa kwa ajili ya kuratibu shunguli za uvuvi haramu’alisema Mbarouk.

Aidha alitaja mikakati inayochukuliwa kwa sasa katika kukabiliana na uvuvi haramu ikiwemo idara ya Uvuvi kushirikiana na vyombo vya ulinzi ikiwemo KMKM kufanya doria za mara kwa mara.

‘Kwa sasa huwa tunafanya doria za mara kwa mara katika ukanda wa bahari kuu kwa kushirikiana na Polisi pamoja na KMKM…..ndiyo maana uvuvi haramu uliokuwa ukifanywa na meli za kigeni kwa sasa umepunguwa sana’alisema.

Alisema juhudi hizo kwa kiasi kikubwa zimesaidia kulinda Maliasili za Baharini ikiwemo Matumbawe pamoja na Samaki ambao walikuwa wakitoweka kwa kiwango kikubwa.

Aidha Mbarouk alisema hivi sasa Zanzibar imepata sifa kubwa ulimwenguni kwa kulinda matumbawe ya baharini pamoja na mikakati ya kutenga maeneo ya hifadhi ambapo Uvuvi haramu umedhibitiwa kwa sasa.

mwisho.

Serikali kufikisha huduma za miundo mbinu.

Serikali imesema itapeleka huduma za miundo mbinu ya maji na umeme sehemu za makaazi mapya ikiwemo Tunguu ambayo yamepimwa kwa ajili ya makaazi ya wananchi.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Ardhi,Makaazi Haji Mwadini Makame wakati akijibu swali aliloulizwa na mwakilishi wa jimbo la KOANI CCM Mussa Ali Haji aliyetaka kujuwa kwa nini Serikali inatoa viwanja katika maeneo ambayo bado haijafika miundo mbinu ya huduma muhimu za maji safi na salama.

Mwadini alikiri kuwepo kwa tatizo hilo katika maeneo ambayo yamepimwa na wizara kama miji mipya,lakini hadi sasa hakuna huduma muhimu za maji safi na umeme.

‘Mheshimiwa nakubaliana na mwakilishi kwamba yapo maeneo ambayo tumeyapima kwa ajili ya makaazi mapya ya wananchi ikiwemo Tunguu….lakini hadi sasa bado huduma muhimu hazijafika ikiwemo umeme na maji’alisema Mwadini.

Hata hivyo Mwadini alisema Serikali ya Awamu ya saba itaendelea na jukumu lake la kuona huduma hizo zinawafika wananchi bila ya matatizo.

Alisema kwa mfano huduma za maji safi zinaendelea kusambazwa kupitia katika miradi mbali mbali inayofadhiliwa na wafadhili ikiwemo Serikali ya Japan.

Aidha huduma za nishati ya umeme,kazi hiyo inaendelea kuona vijiji vinapata umeme kwa ajili ya kuleta maendeleo kupitia mradi wa umeme vijijini.

mwisho.

BADEA kujenga barabara za maeneo ya kilimo.

Waziri wa Mawasiliano na miundo mbinu Hamad Masoud amesema barabara ya Jendele hadi Cheju itajengwa kwa kiwango cha lami ikiwa ni mkopo kutoka kwa Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika BADEA.

Hamad alisema hayo wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu juhudi za ujenzi wa barabara zinazokwenda katika miradi ya kilimo cha mpunga Unguja.

Alisema kimsingi uongozi wa Benki hiyo umekubali kutoa mkopo kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo ambayo itapita eneo la Cheju kwenda Unguja Ukuu Kaibona

‘Tupo katika hatua za mwisho za makubaliano ya kuanza kwa ujenzi wa barabara ya Jendele hadi Unguja Ukuu….tunatazamiya kuanza kazi za uchambuzi wa maombi ya wakandarasi ‘alisema Hamad.

Alisema jumla ya mambo ya wakandarasi watano yamewasilishwa maombi yao katika wizara yake kwa ajili ya hatua za mwisho za kumpa mkandarasi mmoja tayari kwa ajili ya kuanza kazi za ujenzi wa barabara hiyo.

Hamad alisema Serikali ya Mapinduzi ya awamu ya saba imejizatiti kuona kwamba barabara zote zinazokwenda vijijini zinajengwa kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafiri wa wakulima.

MWISHO.

wawakilishi wa CCM waanza kampeni za ubunge..

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka katika chama cha Mapinduzi wameanza kufanya kampeni kali za kumpata Mjumbe mmoja ambaye ataliwakilisha Baraza katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho aliwaambiya wajumbe kutoka katika chama cha Mapinduzi na kusema kazi za uchaguzi wa hatua za awali zitaanza ili kupata majina ya wajumbe watatu watakaopigiwa kura na wajumbe wote wa baraza la wawakilishi na hatimaye kupata jina mmoja.

‘Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi shunguli za leo zimemalizika kwa maswali na majibu…..baada ya hapo wajumbe wa CCM tukutane ili tufanye uchaguzi wa hatua za awali za mchujo ili kupata majina matatu yatakayopigiwa kura’alisema.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi watafanya uchaguzi kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Mwakilishi Mussa Khamis Silima kutoka CCM aliyefariki dunia miezi miwili iliyopita baada ya kupata ajali ya gari huko Dodoma.

Baraza la Wawakilishi linatoa wajumbe watano ambao huingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,ambapo wajumbe watatu ni kutoka CCM na wawili kutoka CUF.

Mwakilishi wa jimbo la MKWAJUNI kwa tiketi ya CCM Mbarouk Wadi Mussa aliliambiya gazeti hili kwamba ameingia katika kinyanganyiro hicho kuwania nafasi ya kuliwakilisha Baraza la Wawakilishi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

‘Nimeamuwa kujitosa katika kinyanganyiro cha kuwania nafasi ya uwakilishi katika nafasi ya Ubunge….nimeanza kampeni kwa wajumbe wote wa CCM pamoja na wa CUF ili wanichaguwe’alisema Mbarouk.

Mwakilishi mwengine aliyeamuwa kujitosa katika kinyanganyiro hicho ni Hamza Hassan Juma,mwakilishi wa jimbo la KWAMTIPURA kwa tiketi ya CCM ambaye alisema ameanza kampeni kwa wajumbe wote.

‘Unajuwa uchaguzi huu lazima upate baraka ya kura kutoka kwa vyama vyote vya siasa katika hatua za mwisho ili uwe Mwakilishi katika Bunge’alisema Hamza.

Habari zote na Khatib Suleiman

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s