Maulid Hamad Maulid afariki dunia

Mwandishi wa Habari wa ITV na Radio One, Maulid Hamad Maulid amefariki dunia leo asubuhi akisumbuliwa na kifua kikuu lakini pia Maulid alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya moyo kwa muda mrefu ambapo aliwahi kufanyiwa upasuaji nchini India Mwenyeenzi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi AMIN

Maulid hakupenda kuokota habari akairusha
Na Amir Mhando; Tarehe: 21st October 2011
JUMANNE majira ya saa nne asubuhi, napokea simu kutoka kwa Suleiman akiwa Zanzibar, alinijulisha kuwa mwandishi mahiri wa habari, Maulid Hamad Maulid amefariki dunia. Nilishtuka kwa kiasi kikubwa, lakini kwa vile binadamu sote njia yetu ni moja nikajipa moyo wa kijasiri kwa kusema Inna Lillahi aina ilaihi rrajiun. Kwa Waislamu unapopata taarifa ya msiba kitu cha kwanza tunafundishwa kutoa maneno hayo yakiwa na maana kwamba yeye ametangulia na hakika sisi ni wa Mungu na kwake tutarejea. Nilimuuliza Suleimani ambaye ameoa sehemu moja na Maulid ambaye alinipa taarifa za msiba kwamba utaratibu wa maziko washaeleza? Akanijibu bado, kwani ndiyo muda huo alikuwa amefariki hivyo atakapopata taarifa zaidi atanijulisha.Nilikuwa nafahamu suala la kuumwa kwa Maulid, lakini haikuwa kiasi cha kuweza kuhatarisha uhai wake, nilijisemea tena moyoni hakika sisi duniani tunapita na huwezi kujua lini kifo kitakutokea.

Hivi hali niliyomuona pale hospitalini Mnazi Mmoja ilikuwa mbaya na ugonjwa ule ndiyo umemuondoa kaka yangu Maulid? Narudisha mawazo yangu hadi Septemba 9 mwaka huu, ambapo nilisafiri kwenda Unguja kumjulia hali Maulid aliyekuwa amelazwa hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Zanzibar.

Nakumbuka nilifika jioni wakati muda wa kuona wagonjwa ukiwa umeshapita, nikiwa nimeambatana na mwandishi Juma Mohammed anayefanya kazi Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) upande wa televisheni.

Ni kweli muda ulikuwa umeshamalizika wa kuona wagonjwa, lakini tulijaribu kuwasihi wauguzi pale wakatukubalia kwa mbinde kwenda kuonana na Maulid, lakini kwa sharti tusiingie wote badala yake aingie mmoja tu.

Kwa vile Juma alikuwa anaishi Zanzibar, alinipa nafasi ya kwanza mimi ambaye nilisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kumjulia hali, hivyo niingie kwenda kumuona na bahati nzuri, nilipofika kitandani kwake akanieleza alikuwa anahitaji kwenda msalani, hivyo tutoke nje.

Alisimama mwenyewe, huku nimemshika mkono kwa vile alinieleza alikuwa na uchovu wa kulala kwa muda mrefu na dawa zilikuwa zinamchosha kupita kiasi, akaingia mwenyewe msalani na alipotoka nikarudi naye mpaka kitandani kwake.

“Nakushukuru sana mdogo wangu kwa kuja, wewe kweli ni mtu wangu, naumwa lakini tangu asubuhi leo najikia vizuri sana,” nakumbuka sana kauli hiyo alinieleza Maulid.

Nilizungumza naye kwa dakika zisizopungua 30, nikampigia simu Juma naye akaingia wodini kuja kumuona Maulid, ambapo kwanza alilaumiwa kwa nini haji kumuona rafiki yake hospitalini, lakini ukweli ni kuwa Juma hakuwa na taarifa za kuumwa kwake.

Alimueleza kwamba hakuwa akifahamu kama amelazwa na kama si mimi kumpigia simu anisubiri bandarini asingeweza kufika kwani simu ya Maulid ilikuwa haipatikani. Nikamuacha Juma akiwa na Maulid, mimi nikatoka nje nikawa nazungumza na mke wa Maulid, Jamillah Nassor ambaye nafahamiana naye vizuri tuna ukaribu wa kifamilia, ambao kwa kiasi kikubwa ulichangiwa na Maulid.

Mkewe alinieleza kwa kirefu kuhusu kuugua kwa mumewe, ambaye nafahamu ana tatizo la moyo kwa muda mrefu, lakini kilichokuwa kikimsumbua wakati huo si moyo na kwamba aligundulika kuwa na tatizo la kifua.

Basi baada ya Juma kutoka wodini tukaagana na ndugu mbalimbali waliokuwa nje hospitalini hapo, nami nikawaeleza ningefika kesho asubuhi kuwajulia hali.

Usiku wa siku hiyo ndipo lilipotokea tukio la kuzama meli ya mv Spice Islanders eneo la Nungwi, ambapo nilipanga niondoke mchana kurejea Dar es Salaam, lakini kutokana na tukio hilo nikasema itabidi niwahi maana huenda kungekuwa na tatizo la usafiri.

Hivyo asubuhi nikaenda hospitali kumuaga Maulid, kwa imani kwamba nitarudi siku nyingine kuonana naye, kumbe ilikuwa siku ya mwisho kwangu kukutana na kaka yangu, ilikuwa siku ambayo niliagana naye na hatutaonana tena duniani. Inauma sana.

Nakumbuka wakati nilipoingia wodini kitu cha kwanza baada ya kusalimiana naye, aliniuliza kama nimepata taarifa ya kuzama kwa meli?

Nilimjibu nimepata kisha nikajaribu kumdanganya kwamba hakuna madhara makubwa ili asije akapata hofu kubwa, lakini kuna watu wengine ambao niliwakuta pale kitandani kwake tayari walishamueleza mengi kuhusu ajali hiyo, hivyo mimi nilionekana sikuwa najua lolote na zaidi ni mnafiki.

Sikupenda afahamu kuhusiana na habari ile, kwani niliamini ingemfikirisha mambo mengi sana, lakini juhudi zangu zilikwama, alianza kufikiria mambo mengi sana, nikawaeleza waliokuwa pale kitandani kwake ambao sikuwa nawafahamu sana kwamba wasimjulishe zaidi kuhusiana na ajali hiyo.

Walinielewa na wao wakakiri kwamba walifanya kosa kumjulisha kulingana na hali yake. Baada ya hapo niliagana na Maulid, nikamwambia nitakuwa nawasiliana naye kadri hali itakavyokuwa.

Nikatoka wodini nikiwa na imani kwamba mgonjwa yupo fiti, nikaanza safari ya kurejea Dar es Salaam. Siku mbili baadaye Maulid akaruhusiwa kutoka hospitali akawa nyumbani kwake Jang’ombe, Zanzibar na nikawa nawasiliana naye mara kwa mara kuhusu afya yake, ingawa hakupona kiasi cha kufanya kazi, lakini ilikuwa ikitia matumaini.

Kwa hiyo taarifa za kufa kwake baada ya kuzipata asubuhi ya Jumanne wiki hii, nikaanza kuwajulisha baadhi ya wadau ambao wanamfahamu vyema Maulid, lakini kwanza niliwajulisha wale tuliokuwa naye Maulid Kisiwani Pemba mwaka 2009 katika suala la uandikishaji wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.

Namfahamu Maulid tangu mwaka 2003, lakini navuta hisia kuhusiana na tukio lililotokea wakati nilipoenda kwenye uandikishaji wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, Pemba mwaka juzi. Nalikumbuka daraja moja zuri, ambalo zege iliyojengewa inaonekana ya kizamani, ingawa pia si miaka mingi linaonesha kwamba lilikarabatiwa.

Kwa ufupi ni daraja imara na lipo sawasawa. Hili ni daraja la Piki lililopo kijiji cha Piki kinachopatikana kwenye shehia ya Piki wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Hapo ndio eneo ambalo watu wasiojulikana walitaka kulilipua daraja hili kwa mabomu, ambapo baadhi ya wananchi wasio wazalendo walitaka kufanya hujuma hiyo kwa sababu wamekataliwa kuandikishwa kwenye daftari la wapiga kura.

Wakati baadhi ya wananchi wa maeneo ya Tanzania Bara wanalilia barabara ya lami na wengine madaraja, wakazi wa Pemba (wachache) wao walifanya vitendo vya kihuni kuhujumu madaraja ambayo ni kiungo muhimu kuunganisha Wilaya mbalimbali kisiwani Pemba.

“Hebu njoo nikupige picha kwenye daraja la Piki, siku moja utaikumbuka,” naikumbuka kauli ya Maulid, ambapo waandishi wengine tuliokuwa tukifuatilia uandikishaji huo tukapiga picha kila mmoja kwa wakati wake na mpigaji alikuwa Maulid ambaye mpaka mauti yanamkuta alikuwa akifanyia kazi vituo vya ITV na Radio One.

Waandishi hao walikuwa Juma Mohammed ambaye wakati huo alikuwa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, Deodatus Balile wakati huo akiwa gazeti la Rai, Bakari Mkondo wa gazeti la Mzalendo, Rose Athumani wa Daily News na mimi.

Wakati huo matukio yasiyo ya kiungwana yalikuwa yakijitokeza sana Pemba, kulikuwa kunafanyika hujuma mbalimbali, ambapo tulishirikiana kwa karibu sana na Maulid katika kufuatilia matukio hayo.

Mambo ya baadhi ya watu kumwagiwa tindikali au nyumba zao kumwagiwa mafuta ya petroli na kuchomwa moto au kupigwa mabomu ya kienyeji, yalikuwa yakijitokeza sana. Baadhi ya watu waliopata kukumbwa na athari hizo mwaka huo alikuwa Sheha wa Shehia ya Msuka Magharibi, Amina Khatib Ally ambaye alipigwa na mabomu nyumbani kwake na watu wasiojulikana.

Pia Sheha wa Shehia ya Kinyasini Raia Amour Othman, ambaye pia naye alikumbwa na horuba la kufanyiwa hujuma. Sheha mwingine aliyeonja joto ya jiwe alikuwa wa Mihogoni, Salim Said Salim, ambao wote walipatwa na matatizo ya kupigwa mabomu nyumba zao.

Nilikuwa natafakari namna tulivyokuwa tukishirikiana sana na Maulid kikazi, lakini sasa ni marehemu. Sikuwa nimeamini kwa kiasi kikubwa, hivyo Jumanne nilisafiri kwenda Unguja kushiriki maziko na niseme nilipata uchungu zaidi wakati jeneza lililombeba marehemu lilipokuwa likitolewa kwa kaka yangu Dau Hamad Maulid kupelekwa msikitikini kuswaliwa.

Marehemu aliswaliwa msitiki wa Noor Mohammed uliopo eneo la Mombasa kwa Mchina, ambapo wanamichezo mbalimbali akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho walishiriki.

Baadaye msafara ukaelekea kijiji cha Bumbwini mkoa wa Kaskazini Unguja kwa maziko yaliyofanyika saa tano asubuhi, ambayo yalihitimisha safari ya maisha yake Maulid hapa duniani.

Kwangu mimi jambo ninaloweza kulizungumzia kuhusiana na Maulid ni kuwa hakupenda kuokota habari, hata aelezwe na nani lazima atataka ahoji na upande wa pili, tena alipenda zaidi habari zile za kiuchunguzi.

Ushahidi ni zile habari zilizohusu masuala hayo ya vurugu za Pemba, habari za migogoro ya ardhi Unguja iliyomfanya agombane na baadhi ya maofisa wakubwa serikalini.

Lakini hata katika mambo ya michezo, Maulid alipokuwa msemaji wa Chama cha Soka Zanzibar ( ZFA) hakuwa muoga kusema jambo aliloona linamkera na ushahidi ni wakati wa kuelekea uchaguzi wa chama hicho alikuwa wazi na kuwataka baadhi ya viongozi wake pembeni.

Maulid atakumbukwa kwa msimamo wake wakati akiiongoza Taifa Jang’ombe akiwa Rais wa timu hiyo, kwa kweli aliipandisha chati na aliwahi kuandaa maandamano ya mashabiki kutaka kwenda kumuona Waziri aliyekuwa na dhamana ya michezo wakipinga kupokwa pointi.

Tukio hilo lilimfanya akabiliane na vyombo vya dola na haikuwa ajabu kukamatwa na kuswekwa rumande. Maulid ambaye ameacha mjane na watoto wanane, alipenda kusimamia ukweli na hakupenda kumung’unya maneno ndiyo maana wengi walimlilia kwani si kwa kusema kinafiki, bali tumepoteza mtu muhimu sana.

Maulid amekwenda, sote tutafuata, jambo la msingi ni kuhakikisha yale aliyoyasimamia kwa dhati yanaendelezwa ikiwemo waandishi wa habari za michezo Zanzibar kuwa na nguvu yao kwa maana ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (Taswa) Zanzibar.

Buriani Maulid, nenda kapumzike kwa amani daima nitakukumbuka kwa yote uliyofanya kwa ajili yangu na Taifa kwa ujumla.

CHANZO: HABARI LEO
Buriani Maulid Hamad Maulid


Na Juma Mohammed; 21st October 2011

 

MAULID Hamad Maulid hatunaye tena duniani, amefariki akiwa na umri wa miaka 59 na kuzikwa kijijini kwao Bumbwini Misufini, Wilaya ya Kaskazini B Mkoa wa Kaskazini Unguja Jumatano wiki hii.

Waumini wa dini ya Kiislamu walimswalia Maulid katika msikiti wa Noor Muhammad uliopo Mombasa kwa Mchina saa 3:30 asubuhi na kuhudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, Naibu Spika wa Baraza, Ali Abdallah Ali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Ali Mwinyikai ambapo msafara ukaelekea Bumbwini Mkoa Kaskazini Unguja, ambako alizikwa saa tano asubuhi.

Tasnia ya habari imeondokewa na mmoja wa Makamanda wake mahiri na makini sana, ni pengo kubwa pia katika ulimwengu wa soka na litaonekana kwa muda mrefu.

Kwa dhati ya moyo wangu nakiri kuwa sehemu kubwa ya mafanikio yangu katika tasnia ya uandishi wa habari hapa nilipofikia yamechangiwa na Maulid ambaye alikuwa mwenye msaada mkubwa kwangu wakati ule nikianza kazi nikiwa kijana mdogo sana mwenye umri wa miaka 22.

Nilijifunza mengi na yenye manufaa kwake, hakuwa mchoyo na kwa ujumla Maulid amekuwa mmoja wa waandishi mahiri hapa nchini, nimemfahamu vyema kwa umakini na uandishi wake uliozingatia weledi na misingi ya utu huku akitanguliza mbele uzalendo kwa nchi yake.

Maulid aliwahi kufanya kazi katika Shirika la Habari Tanzania(PST) lililokuwa likimilikiwa na The Guardian Ltd kabla ya kuhamia ITV na Radio One, aliandika habari za uchunguzi na hususan zile za wananchi wa kawaida ambao sauti zao zilikuwa hazisikiki.

Maulid alikuwa ni mtu wa watu, nakumbuka nilipokuwa nikiandika habari za michezo wakati ule katika gazeti la Bingwa lililokuwa likimilikiwa na Habari Corporation Ltd alinisaidia sana si tu katika kupata vyanzo vya habari, lakini kunielekeza njia bora na sahihi ya uandishi wa michezo.

Kwa hakika kifo chake ni pigo kwa uongozi wa sasa wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa), kwani Maulid ni miongoni mwa waanzilishi wa Taswa-Zanzibar akiwa Kaimu Makamu Mwenyekiti.

Maulid amefariki wakati ambapo ushauri wake bado ulikuwa ukihitajika katika kukuza Taswa- Zanzibar ambacho kwa muda mfupi sana tumeona kazi nzuri iliyoanzwa kufanywa na chama hicho.

Maulid wakati wa uhai wake amepata kuwa msemaji wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kabla ya kujiweka pembeni wakati wa uchaguzi uliofanyika mwaka jana.

Ni mwandishi wa habari na mwanamichezo ambaye kamwe jamii ya wanamichezo na hususan waandishi wa habari hawataweza kumsahau mpiganaji huyu ambaye muda wote alikuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya dhuluma, rushwa, ukiukwaji wa haki na mtetezi wa wanyonge.

Kwangu mimi Maulid mbali ya kuwa mwandishi mwenzangu, kaka yangu, lakini alikuwa ni mlezi wangu ambaye muda wote aliniongoza vyema katika ulimwengu huu ambao naweza kusema sasa ni uwanja wa fujo.

Tukiwa katika timu ya Taifa ya Jang’ombe maarufu “Wakombozi wa Ng’ambo” Maulid akiwa Rais wa timu hiyo, mimi Katibu Mwenezi wake, timu yetu ilipata mafanikio makubwa katika ligi kuu ya soka Zanzibar, ingawa hatukuweza kutwaa ubingwa.

Mengi tuliyafanya wakati ule kuendeleza soka si katika Taifa ya Jang’ombe, lakini tuliweza kuhamasisha mashabiki wa soka kupenda timu zao za nyumbani na kila mtu alikuwa akiipenda timu yetu na timu nyingine kama Malindi, Miembeni, Kwaboko na nyinginezo.

Kwa bahati mbaya sana, Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar(ZFA) kwa wakati ule walikuwa hawaipendi timu yetu hatukuwa tukijuwa ni kwa sababu zipi, lakini Maulid alikuwa akitupa moyo muda wote kuwa tuendelee na kuijenga timu na tutetea haki yetu hadi dakika ya mwisho.

Moja kati ya kumbukumbu ya karibu ni pale Halmashauri ya timu ya Taifa ya Jang’ombe ilipoamua kuingiza timu yetu barabarani kufanya maandamano ya amani ambayo baadaye yalitawanywa na Polisi tukidai kupewa ushindi wa pointi tatu katika mechi ya ligi kuu Zanzibar.

Naweza kusema ni timu ya kwanza ya mpira wa miguu kuandamana barabarani kwenda kwa Waziri mwenye dhamana ya michezo kudai haki ya ushindi tuliokuwa tumepokwa na ZFA, lakini hatukuweza kufika ofisini kwa Waziri wakati ule Haroun Ali Suleiman pale Shangani.

Wanachama na mashabiki wetu wakiwamo baadhi ya viongozi na Maulid akiwa Rais wa timu alitiwa mbaroni na Polisi ambao pia walikuwa ni mahasimu wetu kisoka katika Ligi Kuu, mara nyingi tulikuwa tukiwafunga kitendo ambacho walikuwa hawakifurahii hata kidogo.

Ukiacha tukio hilo, nakumbuka pia ngoma zetu za uhamasishaji zilichukuliwa na Polisi na kuhifadhiwa Kituo Kikuu cha Mkoa wa Mjini Mwembe Madema kwa sababu zisizo kuwa za msingi, tunamshukuru sana aliyekuwa Kamanda wa Polisi Wilaya ya Mjini, Mzee Nurdin na Kamanda mstaafu George Kizuguto kuturejeshea ngoma zetu.

Maulid, akiwa Rais wa timu, alitoa wazo la kufufua michezo ya kienyeji ya hapa Zanzibar ambayo tulikuwa tukifanya kila mwaka, mchezo wa bao, kufukuza kuku, kula maandazi, kukuna
nazi, nage, mchezo wa ng’ombe, kuvuta kamba, kutembea katika magunia na mingine mingi.

Maulid ametangulia mbele ya haki, maana kila nafsi itaonja umauti, lakini mambo yake tutayakumbuka daima. *Mwandishi wa makala haya ni Mhariri Mkuu wa Shirika la
Utangazaji Zanzibar (ZBC) upande wa televisheni.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s