Wao ndio wazembe wanamsingizia Mungu

Mohammed Aboud Mohammed, Waziri wa Nchi (Afisi ya Makamo wa Pili wa Rais) Zanzibar

SHAGHALABAGHALA inayohusu takwimu za watu katika ajali ya meli ya mv Spice Islander ndiyo hiyohiyo iliyosababisha meli kupelekwa kuzama Bahari Kuu ya Nungwi.

Ni muhimu mapema hivi kulaumu viongozi wenye dhamana kwa kushindwa kutenda maana watu wanamsingizia Mwenyezi Mungu wakati ndiye huyo aliyewapa akili ya kufikiri kabla ya kuamua. Yanayoendelea baada ya meli kuzama, yanatia huzuni.

Tena wakati nazingatia kinachoetajwa ni “mipango ya Mwenyezi Mungu” ningependa kuwaelekeza viongozi hawa warudi na kujiangalia upya wapi walikosea na nani hasa alikosea.

Nayahoji haya leo, siku tano baada ya ajali mbaya kwa historia ya usafiri wa baharini Zanzibar , kwa kuamini – na hata ukipitia wanayoyasema viongozi serikalini, unagundua pasina shaka – chanzo kikuu cha ajali ni udhaifu katika uwajibikaji.

Inasikitisha mpaka sasa, bado viongozi hawa hawaamini ufanisi katika kutelekeza kazi zao. Kumbe wanajua si kitu kuzembea maana siku ya mwisho, hawataulizwa kitu na aliyewateua. Baadhi yetu tunawauliza na tunataka waseme, tena waungame.

Leo, hata kama hakuna kiongozi atakayethubutu kujiuzulu kwa ajali kutokea na kuishia na vifo vya mamia ya ndugu zetu, mfumo wa utumishi wa umma unadhihirisha wazi una matundu mengi.

Mezani hapa nina magazeti mengi ya Jumatatu, likiwemoZanzibar Leo, gazeti la taasisi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ). Takwimu zilizochapishwa kuhusu idadi ya watu waliokutwa hai hazilingani.

Hakuna mlingano katika takwimu za waliokutwa wafu na hakuna pia hicho kwa idadi ya maiti waliokutwa na kuzikwa na serikali baada ya kushindikana kutambuliwa na ndugu zao.

Kidogo hili linavumilika maana naelewa mazingira ya utendaji kazi yetu waandishi wa habari. Muda wa kukamilisha uandaaji wa taarifa na kupeleka gazeti mtamboni au kurushwa redioni na katika televisheni, unatofautiana taasisi moja kwenda nyingine.

Lakini, tena ya msisitizo, hawa wanaotoa taarifa si ni watu haohao walioandaliwa na serikali ilipoamua ghafla kubana mlango wa utoaji taarifa za ajali? Isitoshe, mengine si yameelezwa kwenye mikutano na waandishi?

Nataka kuamini waandishi hawana kosa hapa; isipokuwa hawa viongozi watoaji taarifa. Walikuwa wengi na walioulizwa walishindwa kujibu “Ninajua lakini fulani ndiye mtoa taarifa. Labda nikupe ila unihakikishie utazithibitisha kwa mhusika kabla ya kuchapa.”

Kwa mwandishi makini umemsaidia sana . Ni chanzo cha taarifa na lazima akathibitishe. Najua wapo wavivu wanaojitia ukaidi na matokeo yake ni kuvuruga taarifa.

Nimelitaja katika kadhia hii gazeti hilo maana ni matumaini ya wananchi kupata taarifa sahihi kupitia kwa chombo cha serikali kwa kuwa watendaji wake ndio walioteuliwa kikatiba kutoa taarifa.

Tusisahau vyombo hivi vinaendeshwa kwa kodi za wananchi. Ndipo inapokuja mantiki ya suala hili.

Ni hivyo kwa sababu kubwa: Serikali ndiyo yenye wajibu wa kikatiba kujulisha wananchi kilichotokea na athari zake ikiwemo kuwahimiza wao kutulia wakisubiri taarifa sahihi.

Eti ajali ile ni mipango ya Mwenyezi Mungu. Kiimani katika dini ni sawa kusema hivyo maana akitaka anatenda au kutotenda na anayetabiri itakuwa wakati gani au vipi, huitwa mshirikina. Ushirikina ni dhambi na ameweka adhabu kali.

Ila, hebu tuelimishane kidogo hivi laiti ofisa bandari kuu ya Malindi, mjini Zanzibar , angezuia meli kufungua nanga na kuondoka na akaamuru watu wapungue, angefukuzwa kazi?

Hilo la kwanza. Pili, hivi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Maji na Barabara (ZUMATRA) angemwamuru ofisa aliyepo bandarini wakati meli ikipakia aizuie, angewajibishwa?

Tuseme mkurugenzi hakuwepo bandarini. Kwa utaratibu wa kazi, hakuna wasaidizi wanaoshinda na ikibidi kulala bandarini ili kuchunga kama wenye vyombo wanatii sheria za usafiri?

Tatu, bandarini kuna utitiri wa maofisa, tena wengine wakubwa tu, wa vyombo vya ulinzi na usalama – jeshi la ulinzi, usalama wa taifa, polisi, uhamiaji na wa vikosi vya SMZ. Walikuwa wapi?

Taarifa za walioshuhudia meli ikikaribia kufungua nanga ili iondoke Malindi, zinasema walikuwepo watu waliokuwa wanahangaika kutoka nje ili kuacha safari kwa kuhofia janga na wale waliokuwa wakihangaika kutaka kuingia kwa kuona wanahitaji kusafiri tu.

Wapo waliofanikiwa kutimiza dhamira zao; baadhi wakisabilia tiketi zao ili kujinusuru. Walinusa hatari mbele ya safari.

Nachelea kuwalaumu waliojitosa kulazimisha safiri. Hapa kuna suala jingine kabisa la uzembe wa serikali kuchelewa kutatua shida za watu na kujitia kulia na kumsingizia muumba kunapotokea janga.

Nataka kuamini watoto au familia za wakurugenzi na makamishna serikalini hawapandi meli hizi. Hutumia za mchana au hata ndege. Wanazo hawa kwa sababu wengi wanaishi katika kufisidi mali ya umma zinazowafungamanisha na matajiri walaji.

Wale wema – wasiotumia vibaya madaraka ya umma – huwaingiza ndugu wa mbali kidogo na familia zao kuu katika kutumia vyombo vya aina ya Spice Islander. Hawana nyingi.

Inachekesha kusikia kiongozi anasema wamepeleka helikopta pamoja na timu ya waokoaji eneo la tukio ili kuokoa watu wakati taasisi hizo zina utitiri wa watumishi wake wakishuhudia meli inaingia kutoka Dar es Salaam, ikishusha na kupakia abiria na mizigo zaidi kwa safari ya Wete, Pemba.

Hivi kiongozi kama IGP Said Mwema anaweza kurudia kasi iliyotumika 27 Januari 2001 kupeleka helikopta Micheweni kuswaga waandamanaji? Zinalingana?

Ni mzaha mtu analalamika kutopata msaada kwa zaidi ya saa tatu za kuwasiliana na taasisi hizi za ulinzi na usalama. Meli ilianza kuzama saa 8 usiku lakini watu wanaokolewa saa 1.30 asubuhi au zaidi.

Ndipo ninapoumia Mwenyezi Mungu kusingiziwa ameleta ajali. Kwani alivyopanga mipango si ni pamoja na kuwapa wanadamu akili ya kufikiri na kuamua kwa manufaa ya umma?

Ni vibaya kupeleka kila uzembe wetu kwa muumba na wengine tutaendelea kulalamikia utamaduni huu mchafu. Muumba aachiwe yake, nasi wanadamu tutende aliyotuelekeza yatunufaishe.

Si kweli kwamba alimshushia wahyi ofisa bandari aachie tu meli huku akiiona na kujua waziwazi itapata matatizo kwa kupakia abiria na mizigo zaidi sana ya uwezo wake.

Ni uzembe mtupu wasioukubali wananchi. Kama hawajui matokeo ya uzembe, basi ni majnun (wendawazimu). Hawafai kuongoza watu.

Na wazembe si huwajibika au wanaposita, huwajibishwa pale uzembe wao unapoleta madhara? Wala tusisingizie “muhali” maana na hili huwa kisingizio kingine cha ovyo.

Nimesita mapema kutaja takwimu. Nimeumia sana zilivyovurugwa. Namkariri Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed niliyemsikia Jumapili mchana akisema mpaka hapo, watu 619 walikuwa wamepatikana hai.

Watu 300 kati yao , waliruhusiwa kuchukuliwa na jamaa zao; 319 walisubiri kufanyiwa uchunguzi zaidi wa hali zao. Nachelea kumkariri aliposema watu watano walikuwa wamelazwa hospitali. Idadi itazidi alichotaja kabla.

Afrika Kusini walipata wapi waokoaji makini? Walipata wapi utendaji wenye ufanisi? Au wanapenda zaidi raia zao kuliko walivyo viongozi wengine Afrika?

Labda sisi tu wajinga, makosa yetu ya nyuma hayatufunzi lolote. Hivyo hatujui hata jina kamili na nahodha.

Tutadurusu pamoja haya!

Advertisements

2 responses to “Wao ndio wazembe wanamsingizia Mungu

  1. Asante sana dadangu mimi binafsi inaniuma xana walah ndani kwetu kuna mtu ambae amenusurika kwa kauli yake anatuambia watu wanazidi 1000 waliokuemo leo tunambiwa meli ilibeba watu mia sita hii ni haki walah wapemba sjui tumekosa nini kama unavosema nakumbuka nikiwa mdogo januari 27 ilikua kilio kwa wapemba na helikopta zililetwa kutoka bara kuja pemba kuuwa watu le kwa vile humuwezi kuttuwa kwa silaha ndo munatuuwa kwa meli makusudi jamani tukitakacho haki itendeke ingawa najua hakuna liwalo juu ya hili lakini kuna siku watu watachoka,dasalma angalia najua una uchung zaidi yangu lakini serekali hii bora muda mwengine unyamaze au yafiche

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s