Hatuna watendaji wenye huruma?

Dk Otto Lymo akiwa ni miongoni mwa madaktari waliokuwa wakitoa huduma za afya katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ambapo mamia ya wananchi walilazimika kupewa huduma ya haraka ili kuokoa maisha yao

Na Ally Saleh

Naam, siku ndio hiyo na tarehe ndio hiyo. Sijui kama ni kumbukumbu au
itakuwa ni doa katika historia ya Zanzibar. Ni siku, kwa vyovyote vile
haitaweza kusahaulika kwa Wazanzibari.

Kwa kupoteza watu 200 nina hakika kwa muda watu wengi wataogopa
kusafiri lakini kawaida ya binaadamu ameumbwa kusahau na haja na
matarajio yake humfanya afanye asilolipenda, na kwa hivyo kesho na
keshokutwa watu wataendelea kusafiri kama kawaida.

Hasa nasema hawa wasafiri wanaokwenda na kurudi Pemba, ambao kwa hapa
kwetu inaonyesha kwa muda mrefu, hatujui kwa kudharauliwa, kwa
kutowajali au kwa urahisi wa mambo tu, vyombo vyao huwa ndio hivyo
hivyo vya Allah atatufikisha.

Ajali ni kubwa na ndani ya ajali kuna mambo mengi. Tuwache yale ya
kuwa ni matakwa ya Mwenyenzi Mungu na kwa hivyo tukio ndio tukio na
hatuna haja ya kulidadisi, la, ipo haja ya kulidadisi tena kwa undani
sana.

Haja ya kudadisi ni kubwa zaidi kwa sababu kwa maumbile ya nchi yetu
ya Zanzibar tukiwa ni visiwa hatuwezi kabisa kukwepa kuendelea na
usafiri wa bahari na kwa hivyo ni lazima tujue uwepo wake na usalama
wake.

Tuna haja ya kudadisi kwa sababu si mara ya kwanza, si ya pili wala si
ya tatu, ila ha
hapana shaka yoyote hii ni kubwa zaidi. Watu husema kuwa ukipigao ndio
ukufunza lakini sisi tumepigwa mara nyingi na hatuonekani kuwa
tumefunzika

Na funzo gani tulilokuwa tukilitarajia, labda ni hili. Maana kuzama
vyombo vya baharini na kupoteza raia ni jambo ambalo limeshatokea mara
kadhaa ikiwemo meli ya MV Fatihi kuzama mbele ya uso wa Zanzibar
katika eneo la bandari na kupoteza maisha ya watu 6.

Hapana shaka yoyote ile kwamba Serikali itajitetea kwa nguvu zote kuwa
haihusiki kabisa na tukio hili. Na sababu zitakuwa ni nyingi tu, na
kwa kuwa ina kauli basi itabaki kuwa kweli Serikali haina makosa.

Itasemwa tumetandika misingi ya sera, tumeweka sheria, tumeweka
taratibu, tumeunda vyombo simamizi vya usafiri na usalama, tumeweka
maafisa wa ufuatiliaji. Tena kama Serikali ilikuwa ifanye nini?

Na kweli sera zipo, taratibu zipo, vyombo vipi, na maafisa wapo…lakini
mbona bado tunakufa baharini? Mbona bado vyombo hasa vinavyokwenda
Pemba ni vibovu kupita kiasi au kama wasemavyo vijana kupita maelezo?

Na pia Serikali itaruka Kimanga ikisema kuwa imejitoa katika masuala
ya kuendesha biashara moja kwa moja na sekta hii imeiachia eneo la
wafanya biashara binafsi lakini Serikali hiyo kwa mambo inayoyataka
imeyashika na kuganda nayo kama ruba kwa mfano zao la karafuu.

Lakini wafanyabiashara nao hawajajikita kama ilivyostahili katika
biashara ya vyombo vinavyokwenda Pemba. Ni wazi kwa maumbile ya sisi
Wapemba ni watu ambao tunapenda kusafiri na mizigo sana, na kwa hivyo
meli inayowafaa Wapemba ni ile yenye uwezo kama huo.

Uwekezaji katika sekta hii kwa muundo wa boti za kasi si msaada mkubwa
kwa wasafiri wa baina ya Unguja na Pemba, na ndio maana tokea kundoka
kwa meli kama Afrika, Jamhuri na baadae Mapinduzi na baadhi yake hapo
kati kati, wasafiri wa Pemba wamekuwa wakipata taabu.

Ingawa si halali na pia mapema mno kutolea uamuzi tukio hili la kuzama
kwa MV Spice, kwa maana ya uzima wake, usalama wake na kadhalika
lakini ni wazi kwa macho ya kila mtu kuwa meli hiyo ilijaza kupita
kiasi.

Kama watu waliozama ni 200 na waliopona ni 620 hao ni 820 na kwa hivyo
tayari imeshapita kiwango ilichopangiwa cha kuchukua abiria 600 na
huku ikielezwa kuwa ilikuwa na kiasi kikubwa cha mzigo ukitokea Dar es
salaam.

Lakini pia hatujui au niseme hapana uhakika kuwa watu waliokufa ndio
hao 200 maana bado kuna malalamiko wakati naandika makala hii kuwa
baadhi ya familia bado hawajawaona jamaa zao kwa maana hawako katika
orodha ya waliokufa wala waliopona.

Bila ya shaka suala la dharura na uokozi bado ni mtihani na kama
tungekuwa tumejitayarisha nina hakika maisha mengi zaidi yangeokolewa
na leo tungezungumza udogo wa madhara.

Na katika hili pamoja na yote lakini tukiri kuwa uwepo wa vifaa vingi
au vyenye uwezo vya uokozi katika meli ya MV Spice kumesaidia sana
kupunguza hasara za maisha kwa sababu ni baada ya kujisaidia katika
vifaa hivyo ndipo wakafikiwa na waokozi.

Pongezi maalum inafaa zitolewe kwa makampuni ya usafiri ya ya Sea
Express na Azam Marine ambao baina ya wameokowa zaidi ya abiria 400 na
pia mahoteli kadhaa katika eneo la Nungwi na watu binafsi waliofika
katika eneo hilo na kuokoa maisha thamini ya wananchi.

Baadhi ya waokozi hao walihatarisha maisha yao kwa ajili ya kuwaokoa
watu, na huu ni ushujaa na uzalendo.

Inafaa pia tujipongeze kwenye maeneo ya matayarisho mbali mbali
yaliofanywa katika hali ya dharura na kupatikana sehemu za kuwekea
maiti, huduma mbali mbali na pia utulivu wa wananchi ambao unapaswa
kupongezwa kupita kiasi.

Wakati tunajua kuwa Serikali itaunda tume huru kuchunguza tukio hili
lakini ni wazi pia baadae pia Serikali itaunda tume nyengine juu ya
namna ya nafasi yake iweje katika uwekezaji kwenye sekta hii, ambayo
kuiwachia upande wa binafsi peke yake, haikhalis kwa Zanzibar.

Kwa fikra yangu kuna haja ya kuwa na kikao cha dharura cha Baraza la
Wawakilishi kujadili suala hili na kama kuna wajibu wa kufanya basi
ufanywe katika hali hiyo ya dharura, kigongwe chuma bado kingali moto.

Ingawa Waswahili husema yaliopita si ndwele tugange yajayo lakini
tunaamini tume itayoundwa au zitazoundwa lazima ziwe na hadidu rejea
za kina ili suala hili kweli lifikiwe mwisho na wananchi waamini kuwa
Serikali iko pamoja nao katika msiba huu lakini pia kuepusha misiba
mengine tena.

Tunataka kuona utaratibu makini zaidi wa kukagua vyombo, lakini
utaratibu enelevu zaidi wa kukagua usafirishaji wa watu kwa mujibu wa
viwango ambavyo kila chombo kimepangiwa na utaratibu wa lazima wa kila
chombo kufanyiwa matengenezo kwa kila muda ambao unahitajika.

Tunajua kuwa katika biashara hii ya usafirishaji kuna tamaa sana ya
fedha kama ulivyo uwezekano mkubwa wa rushwa, lakini upo uwezekano
mkubwa wa kuwa na watendaji waadilifu zaidi na wazalendo zaidi ambao
bado wapo nchi hii, basi hao ndio wapewe nafasi.

Maana utendaji ni wito na wito una huruma. Jee tuheshaishiwa na watu
wenye huruma na wananchi wenzao au na nchi yao? Siamini, siamini
kabisa. Ninachoamini ni kuwa bado wapo Wazanzibari waadilifu, iwapo
Serikali itanyanyua macho yake kutizama mbali na nje ya duara lilozoea
kupewa madaraka na kwa hivyo limelevywa na kwa hivyo ndio hasara hizi
na majanga ya kitaifa.

MWANANCHI

One response to “Hatuna watendaji wenye huruma?

  1. tume itakayoundwa au ambayo imeundwa basi angalao iwe na wataalamu wa mambo ya bahari na utaalam wa navigation na usafiri sio tu iundwe tume

Leave a comment