Msiba mkubwa Zanzibar

Baadhi ya wanajeshi wa kikosi cha jeshi la polisi (FFU) pamoja na wnaharakati wengine wa uokozi wakibeba majeruhi aliyenusurika na kifo katika ajali ya kuzama kwa meli ya Mv Spice Islanders katika ufukwe wa bahari ya Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja

Baadhi ya wanajeshi wa vikosi mbali mbali vya ulinzi wakiwa wamembeba majeruhi Mariam Mohammed Muradi (29) kutoka Tanga, aliyenusurika na kifo katika ajali ya kuzama kwa meli ya Mv Spice Islanders iliyotokea katika ufukwe wa bahari ya Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akiwafariji majeruhi wa tukio la kuzama kwa meli ya Mv Spice Islanders katika ufukwe wa bahari ya Nungwi mkoa wa Kaskazini Unguja.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk Ali Mohamed Shein, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwafariji majeruhu wa tukio la kuzama kwa meli ya Mv Spice Islanders katika ufukwe wa bahari ya Nungwi, mkoa wa Kaskazini Unguja

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, akishauriana jambo na Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, baada ya kuwafariji majeruhi wa tukio la kuzama kwa meli ya Mv Spice Islanders katika hospitali ya Kivunge.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, (wa pili kushoto) Makamo wa kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Mama Mwanamwema Shein, na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja,Pembe Juma wakiwa katika hali ya majonzi walipofika katika kijiji cha Nungwi kuangalia hali halisi ya matukio ya majeruhi katika meli iliyozama ya Spice Islanders

Baadhi ya wanajeshi wa vikosi mbali mbali vya ulinzi wakibeba majeruhi walionusurika na kifo katika ajali ya kuzama kwa Meli ya Mv Spice Islanders katika ufukwe wa bahari ya Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja

Askari wa vikosi nbali mbali vya ulinzi wakibeba majeruhi waliookolewa katika meli iliyozama huko katika Bahari ya Nungwi Mkoa wa kaskazini Unguja wakifikishwa katika ufukwe wa Nungwi

Askari wa vikosi vya ulinzi wakiwa katika doria kuhakikisha usalama unapatikana kwa raia wakati wa upokeaji wa majeruhi waliokolewa katika meli iliyozama ya Mv Spice Islanders ikitokea Unguja kuelekea Pemba

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, akiwafariji majeruhu wa tukio la kuzama kwa meli ya Mv Spice Islanders katika ufukwe wa bahari ya Nungwi mkoa wa Kaskazini Unguja

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, akimfariji Sharif Juma Sharif kutoka Maziwa Ng'ombe kisiwani Pemba akiwa ni katika majeruhi katika ajali ya meli ya Spice Isladers iliyozama katika bahari ya Nungwi mkoa wa Kaskazini Unguja

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, akimfariji Ramadhan Haji, mkaazi wa Saateni Mjini Unguja, majeruhi wa tukio la kuzama kwa meli ya Mv Spice Islanders katika ufukwe wa bahari ya Nungwi, mkoa wa Kaskazini Unguja

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, akimfariji majeruhi wa tukio la kuzama kwa meli ya Mv Spice Islanders katika ufukwe wa bahari ya Nungwi, mkoa wa Kaskazini Unguja, Nasra Muhsin wa Ole Pemba, akiwa amelazwa katika hopitali ya Kivunge, Kaskazini Unguja

Baadhi ya wananchi wakiwa katika viwanja vya Hospitali ya Mnazi Mmoja kusubiri maiti za jamaa zao waliokufa katika ajali ya meli iliyozama ya Mv Spice Islanders huko Nungwi mkoa wa Kaskazini Unguja

Picha zote kwa hisani ya Othman Ramadhan wa Ikulu, Zanzibar

Ajali ya Mv Spice Islander…
Monday, 12 September 2011
  
Kikwete: DNA itumike kutambua marehemu
*Waliokufa sasa wafikia 240
* Sheni kuongoza ibada maalumu
* CCM yaomboleza
NA MWANDISHI MAALUMU, ZANZIBAR
RAIS Jakaya Kikwete, ameagiza sayansi ya vinasaba (DNA), itumike mara moja kusaidia operesheni ya utambuzi wa miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya kuzama kwa meli ya Mv Spice Islander. Ajali hiyo mbaya ya meli ilitokea katika pwani ya Nungwi, Zanzibar usiku wa kuamkia juzi.  Aidha, Kamati ya Taifa ya Ulinzi na Usalama ilikutana jana, Ikulu, Zanzibar chini ya Uenyekiti wa Rais Kikwete, kutathmini hali ilivyo kutokana na ajali hiyo, ambapo watu 192 wamethibitika kufariki dunia. Mbali ya hilo, Rais Kikwete, ametoa shukrani kwa wanakijiji cha Nungwi, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na taasisi zote zilizoshiriki katika kuokoa maisha ya watu waliokumbwa na ajali hiyo.
Hadi juzi usiku, ilithibitishwa kuwa watu 650 walikuwa wameokolewa katika ajali ya meli hiyo iliyokuwa inasafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Pemba kupitia Zanzibar.   Rais Kikwete, jana aliagiza kutumika kwa vinasaba wakati alipotembelea kituo na eneo la maafa cha Nungwi kilichoko kwenye kijiji hicho, ambako karibu watu wote waliookolewa katika ajali hiyo na miili ya waliofariki ilihifadhiwa. Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini, Unguja, Pembe Khamis, alimweleza Rais Kikwete kuwa, habari walizonazo ni kwamba meli hiyo ilianza kuzama saa 6.00 usiku wa Ijumaa, na viongozi wa mkoa huo, walipata habari kuhusu mkasa wa meli hiyo saa 7.00 usiku ambapo uokoaji ulianza mara moja. Khamis alisema kituo hicho cha maafa cha Nungwi kilipokea miili 134 na majeruhi 78, na kwamba utafutaji zaidi ulikuwa ukiendelea.
Akiwashukuru madaktari na wataalamu mbalimbali wa afya na sekta nyingine ambao walishiriki katika uokoaji kuhudumia waliokolewa na kuziweka kwenye hali nzuri maiti zilizoopolewa, Rais Kikwete alikaa kwenye kituo hicho kwa dakika 40. “Nawashukuruni sana kwa kazi kubwa, kwa yote mliyoyafanya na kwa moyo mzuri mliouonyesha. Mimi nimekuja kuungana nanyi kuwashukuru kwa kazi hiyo,” alisema Rais Kikwete.
Kuhusu kasi ndogo ya utambuzi wa maiti, Rais Kikwete alisema kwa jinsi uokoaji unavyokwenda, inawezekana kuwa si miili yote itakayotambuliwa kabla ya kuzikwa, hivyo aliagiza utaalamu wa DNA utumike kuweka kumbukumbu za waliopoteza maisha. “Kila maiti ichukuliwe sampuli ya DNA (vinasaba) na ikitokea kuwa pengine ndugu zake wamechelewa kuja kuitambua, basi akifika hata kama mwili tayari umezikwa waweze kutambua kuwa ndugu yao alipoteza maisha katika ajali ya meli hiyo,” alilisema.
Licha ya mtaalamu wa utambuzi wa magonjwa na uchunguzi wa magonjwa na vyanzo vya kifo, Dk. Ahmad Makata, alisema kuwa walikuwa wanaipiga picha miili yote na kuhifadhi nguo za waliopoteza maisha kama namna ya kuweka kumbukumbu. “Miili ya binadamu hubadilika na kuharibika haraka, kasi kubwa na katika muda mfupi. Miili ile ya ajali ya Mv Bukoba ilibadilika na kuwa myeupe katika kipindi kifupi sana. Hivyo, naagiza tutumie vinasaba katika kuweka kumbukumbu. Si mnao wataalamu wa vinasaba katika timu yenu?” aliuliza.
Rais Kikwete aliongeza: “Tufanye ‘DNA profile’ ya miili yote ambayo haijatambuliwa. Huko mbele, hii itasaidia kuepukana na kuwa na makaburi ya watu wasiotambuliwa kabisa kwa sababu inawezekana kuwa baadhi ya ndugu wa waliopoteza maisha katika ajali hiyo wakachelewa kuitambua kabla ya kuzikwa. “Ukweli kwamba watu wengi wameokolewa kuliko waliopoteza maisha ni matokeo ya juhudi zetu na kazi yenu nzuri. Nakushukuruni sana kwa moyo wenu huo. Nakushukuruni pia kwa kutoa vyombo vyenu vya usafiri kwa ajili ya kusaidia uokoaji na uopoaji wa miili ya ndugu zetu waliopoteza maisha katika ajali hii. “Navishukuru vile vile vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, polisi, jeshi letu na taasisi nyingine za ulinzi na usalama kwa kazi nzuri ya kushughulikia janga hili la taifa letu,” alisema.
Miongoni mwa waliompokea Rais Kikwete kwenye kituo hicho cha maafa ni pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Ulinzi na Usalama, wakiwemo Waziri wa Ulinzi na Kujenga Taifa Hussein Mwinyi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt.
Rais Kikwete ambaye aliwasili mjini Zanzibar juzi jioni kushirikiana na viongozi wa Zanzibar katika msiba huo mkubwa wa kitaifa, alirejea Dar es Salaam jana jioni. Akiwa Zanzibar, Rais Kikwete, ambaye aliongozana na mkewe Mama Salma,  alitembelea viwanja vya Maisara mjini Zanzibar kujionea harakati za kutambua miili iliyoopolewa kutoka baharini. Kwenye viwanja hivyo, Rais Kikwete alilakiwa na Rais Dk. Ali Mohammed Sheni wa Zanzibar, Makamu wawili wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharrif Hamad na Balozi Seif Idd, Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na viongozi wa juu wa SMZ.
Akiwa katika eneo hilo la utambuzi, Rais alishuhudia miili ya watu wazima iliyokuwa imefungwa au kufunikwa na ile ya watoto wadogo ambao sura zao zilikuwa zimeachwa wazi ili kuwa rahisi kuwatambua. Baadaye, Rais Kikwete alitembelea Hospitali ya Mnazi Mmoja, kuwaona na kuwapa pole majeruhi wa ajali hiyo. Tayari serikali ya Muungano imetoa sh. milioni 300 kusaidia katika shughuli ya uokoaji, usafirishaji na kuzika miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo. Aidha, SMZ imetoa sh. milioni 100, kwa shughuli hiyo. Pia, Serikali ya Muungano pia imekubali kuwapokea wapiga mbizi kutoka Afrika Kusini kwa ajili ya kusaidia kufanya tathmini ya ajali hiyo.
IDADI YA WALIOKUFA
Kwa mujibu wa taarifa, watu waliokufa katika ajali sasa wamefikia na kufikia 240 badala ya miili 190 iliyopatikana juzi. Kutokana na vifo hivyo, Mkuu wa Operesheni ya Uokoaji, ambaye pia ni Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Alli Mussa, alisema shughuli za uokoaji zinaendelea vyema na kwamba hadi sasa hawana matumaini ya kupata mtu katika eneo la tukio.
Mussa alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na Kituo cha Televisheni cha TBC 1, na kuongeza kuwa eneo la tukio maji yanatembea kwa kasi kubwa. Alisema miili ya watu ambao hawajaonekana inawezekana kusombwa na maji na kupelekwa maeneo mengine, yakiwemo ya mikoa ya Tanga na Kusini Pemba.
Kamishna huyo alisema, wanaendelea kuwasiliana na viongozi wa mikoa hiyo na jirani kuona kama kuna maiti au majeruhi aliyesombwa na maji na kufikishwa katika maeneo hayo. Alisema wana matumaini makubwa ya kuipata meli hiyo ambayo imezama na kwamba juhudi za kuiokoa zinafanyika.
MELI ILIZIDISHA UZITO
Akizungumza na waandishi wa habari  jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais, Mohammed Aboud alisema meli hiyo ilipakia abiria na kubeba mizigo tofauti na uwezo wake. Alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa waliosajiliwa pekee walionekana kuwa 610, wakati uwezo wa meli hiyo ni abiria 600, huku ikiwa na mizigo ya tani 500 wakati uwezo wake ni kubeba tani 95.
Mmoja wa mabaharia aliyenusurika katika ajali hiyo, alisema meli hiyo ilikuwa imepakia shehena kubwa ya mizigo kuliko uwezo wake, na kwamba mingi ilipangwa vibaya kwa kuegemea upande mmoja. “Nahodha angepatikana angeweza kueleza mwenyewe ukweli, ila tunachofahamu mimi na wenzangu ni kuwa meli ilizidisha sana mzigo, na imekuwa tabia ya meli hizo kurundika mizigo kila inaposafiri, na wamekuwa wakiachiwa tu wakaguzi,” alilalamika baharia huyo.
Alipoulizwa alikuwa akimaanisha nini, alifafanua kuwa: “Utakuta baba na mama wanakata tiketi, lakini wanaingia chomboni na watoto wadogo zaidi ya watatu ambao hawawakatii tiketi, na hivyo kutotambuliwa katika orodha ya wasafiri.” Aidha, alisema kuna baadhi ya wasafiri ambao hawakati tiketi ofisini, bali hukatia ndani ya meli, ambao alidai pia walikuwa wengi.
HALI ZA MAJERUHI
Waziri Aboud alisema hadi jana jioni  kulikuwa na majeruhi watano tu waliobaki hospitali, ambapo baadhi walipata matibabu na kuruhusiwa, huku mmoja kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) mjini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Alisema baadhi ya abiria katika meli hiyo hawajapatikana, ambapo serikali na vikosi vya ulinzi na usalama vinaendelea kuwatafuta. “Kuna badhi ya watu wengine waliokuwemo katika meli hiyo bado hawajapatikana, hivyo serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi tunaendelea kuwatafuta na tukiwapata tutawatangazia,” alisema.
WENGINE HAWAJULIKANI WALIPO
Habari zilizotufikia kutoka Unguja na Pemba zinasema kuwa, baadhi ya watu waliokuwemo katika meli hiyo hawajaonekana. Wakizungumza na Uhuru kwa njia ya simu, baadhi ya wananchi walisema hadi sasa hawajawaona ndugu zao na hawajui kama wamekufa au la.
Saidi Issa Said mkazi wa Kisiwani kwa Binti Abedi, Wete, Pemba, alisema ndugu zake saba ambao walikuwemo katika meli hiyo bado hawajaonekana na hawajui kama wapo hai au wamekufa. Alisema ndugu zake saba, wakiwemo dada zake wawili na watoto wao wanne ambao walipanda meli hiyo kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda Pemba hadi sasa hawajawaona. “Tuna majonzi makubwa, tumepoteza watu saba wa familia moja na hadi sasa hatujawaona, hatujui kama wamekufa au la,” alisema.
Naye Bakari Hamad Omar, kutoka kisiwa cha Kojani mkoa wa Kaskazini Pemba, alisema amepoteza mtoto wake ambaye hadi sasa hajaonekana. Alisema mtoto wake huyo alikuwa anatarajia kufunga ndoa Ijumaa ya wiki hii na alipanda meli hiyo Unguja, akiwa na wenzake 10 ambao sita kati yao wamefariki.
Omari alisema katika kisiwa cha Kojani kilichopo wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba watu wengi wamefariki dunia. Alisema majonzi makubwa yametawala katika kisiwa hicho kutokana na watu wanaoishi kisiwani humo kuwa ndugu wa karibu.
Ali Hamad Bakari wa Kijiji cha Mwane, Mchanga Mdogo, alisema katika ajali hiyo, amepoteza watoto wake watatu, ingawa mkewe amenusurika. Alisema katika kijiji hicho, watu 24 wamefariki dunia kutokana na ajali hiyo, na kwamba hadi sasa watu tisa hawajulikani walipo. “Ni msiba mkubwa, siwezi kuusahau katika maisha yangu, watoto wangu watatu wamekufa… hapa kijijini kwetu watu 24 wamekufa, tuna majonzi makubwa,” alisema.
NAHODHA MSTAAFU AZUNGUMZA
Nahodha mstaafu ambaye amewahi kuendesha meli mbili, ikiwemo ya Mv Bukoba, Ibrahim Bendera, alisema jana kuwa kwa kawaida nahodha hutakiwa kuwa na taarifa muhimu za meli anayoendesha ili kubaini iwapo ina hitilafu.
Bendera ambaye aliwahi kuendesha meli za Mv Liemba na MvBukoba iliyozama Mei 21, 1996 katika Ziwa Victoria mkoani Mwanza, aliyasema hayo wakati akielezea uzoefu wake katika uendeshaji wa meli na tukio la ajali kwa jumla. Alisema mambo mengine anayopaswa kuyafahamu nahodha anapokuwa anaendesha meli ni kujua kitovu cha meli kiko wapi na kuongeza kuwa meli inapoelea inakuwa na nguvu mbili ndani na nje ya meli. Bendera ambaye ana uzoefu mkubwa wa meli alisema, kuna sababu nyingi zinazosababisha meli kuzama ikiwa ni pamoja na mawimbi makubwa na wingi wa mizigo.
Kwa mujibu wa nahodha huyo, ukongwe wa meli hausababishi meli kuzama kutokana na kila baada ya mwaka meli kutakiwa ifanyiwe marekebisho makubwa. Alisema meli hiyo ilitengenezwa mwaka 1963 na ilinunuliwa Tanzania mwaka 2007, ambapo ilisajiliwa Zanzibar na mwenye jukumu la kuikagua ni Mrajisi wa Meli Zanzibar.
“Msiba ni mkubwa, tuangalie uchunguzi wa serikali ufanyike… kwa sasa huwezi kumlaumu mtu kutokana na ajali hiyo mpaka tutakapopata ripoti ya serikali, cha msingi ni kuwa na subira,” alisema. Alisema nahodha aliyekuwa akiendesha meli ya Mv Spice Islander ni mzoefu na alikuwa ni miongoni mwa mainjinia waliojenga meli ya Mv Bukoba.
CCM WAOMBOLEZA
CCM kimetenga siku tatu kwa ajili ya kuungana na Watanzania wengine kuomboleza msiba uliolikumba taifa kutokana na ajali ya kuzama kwa meli na watu zaidi ya 200 kupoteza maisha. Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikani na Uenezi Nape Nauye alisema Chama kimeamua kuungana na serikali kwa kuamua kusitisha kampeni za shamra shamra ama kufanya mikutano ya hadhara kwa siku tatu.
“Tumeamua kuungana na Watanzania katika kuomboleza msiba huu. Hivyo tuna siku tatu za maombolezo ambazo zimetolewa na serikali, na sisi kama Chama tumeamua hatutafanya kampeni aidha za shamra shamra ama mikutano ya hadhara. “Kama tutafanya jambo kwa ajili ya Chama katika siku hizi tatu, basi itakuwa ni vikao vya ndani tu na si kufanya hizo shamra mtaani,” alisema Nape.
TANGA WAHAHA
Mji wa Tanga umezizima tangu kuanza kutangazwa habari za kuzama kwa meli hiyo. Baadhi ya watu walikuwa wakihangaika kuhusu jinsi ya kusafiri ili waweze kwenda kushuhudia na kuwatambua ndugu na jamaa zao. Uhuru imeshuhudia watu wenye asili ya Pemba waliopo mitaa ya Makorora, Kwanjeka, Ngamiani, Mtupie na vijiji vilivyo kando ya bahari ya Hindi wakifanya mikutano ya mchana na usiku kutafakari, ambapo pia wamekuwa wakichangishana fedha.
“Hapa tupo kwa ajili ya kuchangishana fedha ili tuweze kumuwezesha Adam Amin, ambaye mdogo wake aitwaye Safia Amini alikuwa miongoni mwa abiria waliokuwa ndani ya meli hiyo alikuwa anakwenda shule baada ya kumaliza likizo,” alisema Rashidi Ali.
Mbali ya wakazi wa Tanga, pia kuna magari mengi yatokayo mji wa Mombasa kupitia mpaka wa Horohoro ambayo yamekuwa yakiwafikisha jijini hapa abiria kwa ajili ya kusafiri kwenda Zanzibar kupitia Dar es salaam. Wingi wa abiria wenye nia ya kwenda  Zanzibar kushuhudia jamaa zao kupitia Dar es Salaam, umesababisha mabasi yanayosafiri kati ya Tanga hadi Dar es Salaam kujaa na hivyo kuwepo kwa msongamano wa abiria katika kituo kikuu cha mabasi mjini hapa.
Waliiomba SMZ kupeleka meli yoyote mjini Tanga itakayofanya kazi ya kuwasafirisha watu ambao wanahaha kutafuta usafiri wa kwenda kuwashuhudia ndugu zao waliopata maafa. “Unajua hapa kuna mambo mawili wapo ambao tayari wamefahamishwa kuwa jamaa zao wameshakufa hivyo hawa wanahangaika kwenda kwenye matanga Pemba, lakini wapo ambao jamaa zao wameokolewa na wapo Hospitali ya Mnazi Mmoja, Unguja hawa na wana nia ya kwenda kuwajulia hali majeruhi,” alisema Mohamed Juma
Walisema mkoa wa Tanga unaongoza kwa Tanzania Bara kuwa na wenyeji wengi wa visiwa vya Unguja na Pemba, ambao wengi kati yao wamefiwa na jamaa zao waliokuwa wakisafiri na meli hiyo. Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kitaifa wa Taasisi ya Kiislamu ya Istiqama, Sheikh Seif Ally ametoa salamu za rambirambi kwa wafiwa waliokufa katika ajali ya Meli ya Mv Spice pamoja na SMZ.
SHENI KUONGOZA IBADA MAALUMU
Wakati huo huo, Dk. Sheni leo anatarajiwa kuwaongoza wananchi katika ibada maalumu ya kuwaombea waliofariki na kujeruhiwa kutokana na ajali hiyo. Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana, ibada hiyo itafanyika saa 10.00 alasiri kwenye viwanja vya Maisara na kuhudhuriwa na wananchi mbalimbali wa Zanzibar. Mbali na hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Aboud, alisema serikali imeunda kamati ya uchunguzi kuhusiana na ajali hiyo.
Aidha, alisema hadi jana ni majeruhi watano tu kati ya zaidi ya 300, ndiyo waliokuwa wamesalia hospitali wakipatiwa matibabu. Waziri Aboud alisema miili ya watu 154 ilitambuliwa na ndugu na jamaa wakati 39 ilizikwa na serikali. Nayo Benki ya NBC Zanzibar, imeanzisha akaunti maalumu itakayotumika kukusanya michango kutoka kwa watu wenye nia ya kusaidia waathirika wa ajali hiyo.
CHANZO: UHURU

Advertisements

6 responses to “Msiba mkubwa Zanzibar

  1. The pain is not on the time of missing our dears. The pain is really start when we live without them and with their presence in our mind. May ALLAH bless those who lost their loved ones..

  2. Poleni kwa w0te ambao wametokewa na hili tukio… lakini ni msiba wetu wote watanzania! POleni woteee!

  3. pole sana ndungu zetu wa zanziber kwa msiba huu mkubwa ila tunawaombea kwa mungu awape moyo wa ujasiri katika kipindi hiki cha msaba na mungu alaze roho za marehemu mahali pema peponi amini.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s