Kisa cha nchi mbili katika bahari moja

Bait el Ajaib ni moja ya majengo yenye kutoa sura ya Kisiwa cha Zanzibar liliopo Mji Mkongwe

Barazani kwa Ahmed Rajab
HAYA ni masimulizi ya nchi mbili: Zanzibar na Mauritius. Zote ni mchanganyiko wa visiwa vilivyo katika Bahari ya Hindi. Zote zina wakazi wapatao milioni moja na laki mbili. Zote zina watu wa mchanganyiko wa makabila. Zote zikitawaliwa na Waingereza. Zote zinapendwa na watalii wa kimataifa.Wakati nchi hizo mbili zilipopata uhuru- Zanzibar mwaka 1963 na Mauritius mwaka 1968 zote zikitegemea mauzo ya zao moja tu (sukari ikisafirishwa na Mauritius na Zanzibar ikijinata kwa karafuu zake.)


Hii leo ukiyalinganisha maendeleo ya nchi hizo mbili utaona kwamba Mauritius imeipita sana Zanzibar. Mauritius ni nchi iliyoendelea yenye uchumi wa wastani, si wa kati na kati bali wa juu, ilhali wananchi wengi wa Zanzibar ni hohehahe hahehohe wanaishi kwa kasoro ya dola moja tu ya Marekani kwa siku. Wengi, mjini na mashamba, wanamudu mlo mmoja tu kwa siku.

Katika mfungo huu uliopita wa Ramadhani nilishangazwa sana kusikia kwamba kuna watu katika sehemu za mashamba ambao wamekuwa wakilia kwa ughali wa mhogo, seuzi wa vyakula vingine.Hali hiyo ya ukosefu wa lishe bora itaziathiri vibaya hasa afya na akili za watoto wetu.
Tukiwaangalia wenzetu kwenye Bahari ya Hindi tunabakia tukizimezea mate hali za maisha yao wananchi wa Mauritius. Nathubutu kusema kwamba maisha yao ni ya hali ya juu kwa sababu kinyume na nchi nyingi za Kiafrika, Mauritius haikuwa na machafuko na machafuzi kama ya mapinduzi — si ya kiraia si ya kijeshi — na ilijiepusha na mfumo wa udikteta wa chama kimoja cha kisiasa.
Yote hayo yamechangia kuwafanya wananchi wa Mauritius hii leo wawe wanaishi maisha aali yaliyo bora ukilinganisha na yale ya wananchi wa Zanzibar. Wananchi hao pia wana matumaini mema kwamba mustakbali wao utakuwa mwema. Wananchi hao wameweza kuwa na hali hizo kwa sababu Mauritius imekuwa na uhuru wa kuzidhibiti kwa ukamilifu sera zake za kiuchumi na kijamii na majaaliwa yake kwa jumla.
Kwa ufupi, Mauritius inaweza kujipangia mambo yake yenyewe kwa ushirikiano wa wananchi wake wa itikadi tofauti za kisiasa.Mauritius imesimama imara yenyewe; haikuwa kama Zanzibar iliyohaulisha madaraka yake muhimu kwenye Serikali ya Muungano baada ya Muungano huo kuundwa kutokana na njama za shirika la ujasusi la Marekani la CIA mwezi Aprili mwaka 1964.
Miaka mitano kutoka sasa yaani kufikia mwaka 2016 Mauritius itakuwa ni kisiwa chenye uchumi usiotoza ushuru. Hivi sasa Mauritius ina Jumla ya Pato la Taifa la dola za Marekani 7,000 kwa kila mtu na kima hicho kinatazamiwa kupanda na kufikia dola za Marekani 8,500 kwa kila mtu kufikia mwaka huo wa 2016.
Zanzibar, kwa upande wake, miaka 47 baada ya kuungana na Tanganyika, ina Jumla ya Pato la Taifa la dola za Marekani 360 kwa kila mtu na ni Mungu tu ajuaye mustakbali wake utakuwaje miaka mitano kutoka sasa kwa vile hatuna takwimu za kiuchumi zilizo sahihi na zenye kuaminika.
Tusisahau pia kwamba mwaka 1964 Zanzibar ilikuwa imeendelea kuipita Mauritius na ilikuwa ya pili baada ya Afrika ya Kusini katika eneo hili letu. Mwenye kuutaka ushahidi wa haya na aende akaangalie ripoti za serikali za nchi hizo mbili za wakati huo au ende kwenye Banki Kuu ya Dunia akaangalie takwimu za wakati huo zilikuwaje.Swali linalozuka ni kwa nini basi Zanzibar ikawa iko nyuma sasa na Mauritius ikawa imeendelea ilivyoendelea na kupata sifa ya kuwa pepo ya utalii wa visiwa na kivutio cha wawekezaji?
Nadhani kuna sababu kuu mbili. Bila ya shaka sababu ya kwanza inayonijia haraka kichwani ni machafuko ya kisiasa yaliyokuwa yameivaa Zanzibar tangu mwaka 1957 hadi mwaka 2010 ilipoundwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Udhaifu huo wa hali ya kisiasa baadhi ya nyakati ulisababisha umwagaji wa damu na ulisababisha pia kuvunjika kwa taasisi muhimu za dola kama vile Utumishi wa Serikali, Mahakama na kuparaganyika kwa mfumo wa elimu uliokuwa umeendelea pamoja na kuoza kwa huduma za afya.Isitoshe pakazuka hali zilizokuwa na uhasama na zilizowazuia Wazanzibari wasiweze kuwekeza na kushiriki katika maendeleo ya nchi yao.
Mambo nchini Mauritius yalikuwa tofauti kabisa. Nimeyaeleza haya kwa marefu na mapana kwenye sahafu zilizopita na kama nilivyosema serikali mbalimbali zilizotawala nchi hiyo tangu ilipopata uhuru mwaka 1968, zikiwa pamoja na serikali za chama cha Kikomunistu, hazikuzichezea au kuzigeuzageuza taasisi za dola. Wala Mauritius haikuitangua au kuibatilisha katiba yake ya wakati wa uhuru.
Kadhia za nchi hizi mbili inaonyesha bayana tofauti iliyopo kati ya nchi yenye madaraka makamilifu na uwezo wa kujiamulia mambo yake yenyewe bila ya haja ya ushauri au ridhaa ya dola ya kigeni na ile ambayo haina madaraka na uwezo huo.Wazanzibari wanahitaji kusoma kutoka historia ya nchi yao na kutoka historia ya visiwa vingine duniani vilivyoendelea kupita sehemu za mwambao au za mabara zilizo karibu navyo.
Wanapaswa waangalie jinsi visiwa hivyo vilivyo na amani, usalama, utulivu na hali thabiti za kisiasa. Yote hayo ni muhimu kwa mandeleo ya kiuchumi ya nchi yoyote ile.Jambo jingine muhimu linaloifanya nchi iendelee kiuchumi au kijamii ni mfumo wake wa elimu. Mfumo wa elimu wa Zanzibar ambao ulikuwa wa kupigiwa mfano ulifujwa ijapokuwa kweli kulikuwa na nia njema ya kuutanua mfumo huo na kuhakikisha kwamba watoto wengi zaidi wanakwenda skuli na kupatiwa elimu ya kisasa.
Nchini Mauritius hali ilikuwa tofauti. Mfumo wake wa elimu haukufujwa bali uliendelezwa kufika hadi kwamba sasa watoto wanaohitimu na kufaulu mitihani ya masomo ya sekondari wanakubaliwa moja kwa moja kuingia kwenye taasisi za kigeni za elimu ya juu. Tukija kwetu tunaona kwamba vyeti vinavyotolewa na taasisi za elimu ya juu za Zanzibar havitambuliwi hivyo duniani.
Kwa jumla, tunaona kwamba ni muhimu kuzihifadhi taasisi tulizo nazo na kama kuna haja ya kuzibadili basi mabadiliko yasifanywe kwa papara na yawe yanafanywa na watu wenye elimu inayohitajika, uzoefu na ujuzi na kamwe yasiachiwe watu wasiotambua athari za hatua zao.
Lau Zanzibar itaendelea na kupata mafanikio sawa na ya Mauritius basi haitokuwa na ufukara uliozagaa. Hii leo wananchi wa Mauritius wanaishi uzuri, wana elimu nzuri, wana huduma nzuri za afya, watu wake wasio na ajira hawafiki idadi ya asilimia 60 na zaidi kama ilivyo Zanzibar.
Si hayo tu bali uchumi wa Mauritius unastawi kwa kasi na huwasikii wananchi wake wakilalamika kuwa bei za vyakula ni za kuruka sana au kwamba hawamudu milo mitatu kwa siku. Ndiyo maana wachambuzi wa mambo ya kiuchumi na wataalamu wengine wanasema kwamba Mauritius ni mfano mwema wa maendeleo kuigwa na nchi nyingine za Kiafrika.
Zanzibar inaweza kuwa na fursa nzuri sana kuishinda Mauritius kuwa kitovu cha biashara na huduma katika eneo hili la Afrika. Mafanikio ya Zanzibar lakini yatategemea pakubwa juu ya jinsi zitavyoondoshwa tofauti zilizopo kati ya Tanganyika na Zanzibar zikiwa nchi mbili tofauti kila moja ikiwa na ajenda yake.
Endapo hali ya mambo itaselea kuwa kama ilivyo basi hatutokuwa na budi ila kujilaumu wenyewe kwa hali tunayojikuta nayo. Tukisema kweli katika miaka iliyopita viongozi Wakizanzibari waliokuwa wakiiwakilisha Zanzibar katika Muungano hawakutekeleza kazi zao sawasawa.
Ni muhimu kwamba katika siku zijazo Wazanzibari wanaopewa dhamana ya kuiwakilisha Zanzibar katika huu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wawe wanahakikisha kwamba wanaitetea Ajenda ya Zanzibar na wala si sera za kisiasa za kichama au zao binafsi.
Makala hii imechapishwa na Gazeti la Raia Mwema

Advertisements

2 responses to “Kisa cha nchi mbili katika bahari moja

 1. Mimi namuunga mkono mwandishi wa makala hii,lakini nataka niwe tofauti kidogo katika baadhi ya mambo.Hivi ni mpaka lini wazanzibari tutaendelea kuwa watumwa wa historia? badala ya kupiga hatua kuanzia hapa tulipo tunatumia muda mwingi kusifia tuu tulikotoka… kabla ya mapinduzi tulikua hivi..tulikua vile!, mpaka lini? Wengine wanakwenda mbali zaidi kuhamishia matatizo yetu kwenye muungano.Mimi napenda kuuliza maswali yafuatayo:
  1) Hivi ZNZ kushindwa kujitosheleza kwa chakula au hata mbogamboga na kuitegemea bara wakati wizara ya kilimo iko chini ya SMZ ni tatizo la muungano?
  2) Kufanya selection ya wanafunzi wa form2 kisiasa na hatimae kushindwa kufanya vyema mtihani ya form4 ni tatizo la muungano?

  3) SMZ kuajiri wafanyakazi wengi na wasio na sifa na kutumia sehemu kubwa ya pato lake kwa mishahara ni tatizo la muungano?
  4) Kuwaachia UWAMSHO waharamishe kazi za mahoteli na hivyo kuwaacha wageni wanufaike na ajira hizo na kuwaacha wenyeji wakin’gaa ng’aa macho na kulalamika ni tatizo la muungano?
  5) SMZ kushindwa kukata viwanja na kuwaacha watu wajenge ovyo ovyo hili kweli ni tatizo la muungano

  3) Kuedelea kuajiri wafanyakazi wengi na wasio na sifa ktk.SMZ na kutumia sehemu kubwa ya mapato ya SMZ kwa mishahara ni tatizo la muungano

 2. Eh..nimesahau! na kuwapa watu vibali vya kuongeza floor katika nyumba za mji mkongwe kwa kutumia matofali ya saruji ili yale majengo yaporomoke vizazi vijavyo wasiyakute..hili pia ni tatizo la muungano?

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s