Busara itumike kwenye karafuu

Wananchi wa Micheweni wakiwa nje ya skuli ya Micheweni wakiwa wamesimama na watoto wadogo wakiuza biashara ya juice nje ya skuli hiyo

 

Na Ally Saleh

Katika tukio la mwanzo ambalo Serikali ya Umoja wa Kitaifa ililifanya
katika ngazi ya kitaifa na kutaka kuonyesha uwezo wake lilikuwa ni
hili suala la uchumaji wa karafuu hasa Kisiwani Pemba.

Hii ilikuwa kwa hakika ndio kampeni ya mwanzo ya kitaifa na ambayo
viongozi wote wa ngazi za juu walijielekeza nalo ili kuhakikisha kuwa
lengo la kuzipata tani 20,000 zilizokisiwa zote zinapatikana.

Kupatikana kwa kiasi hicho cha mzigo wa karafuu mwaka huu likafanywa
ni jambo la kitaifa na hatua muhimu sana kiuchumi kwa Zanzibar juu ya
ukweli kuwa bado karafuu ni zao muhimu sana kwa Zanzibar pamoja na
kusinizia sinzia kwake.

Hiyo pia ni pamoja na maelezo kuwa sekta kiongozi kwa sasa ni ile ya
utalii, ambayo kwa asilimia 95, kwa makisio yangu hutegemea utalii wa
nje ambao hujaa kila aina ya mashaka na kuharibika kwake ni suala la
kufumba na kufumbua.

Kwa mfano mdogo tu ni matukio mfulululizo ya uchomaji wa baa hapa
Zanzibar au tamko la Serikali wakati wa mwezi wa Ramadhan kuwa
ataekamatwa anakula mchana atafungwa ni sababu tosha ya watalii
kukimbia kituo cha utalii, ingawa pia kuna uhuru na haki ya nchi
kulinda utamaduni wake.

Umuhimu wa kulipata zao lote la karafuu mwaka huu, umetokana na
maelezo kuwa miaka sasa Zanzibar imekuwa ikigawana na Kenya karafuu
zake wenyewe na kwa wakati mwengine Kenya kuonekana ni mzalishaji
zaidi hata kuliko Zanzibar kwa kiasi cha karafuu kinachouzwa nje.

Hapa nazungumzia suala la magendo ambalo Zanzibar imejaribu hata
kulitia katika vipaumbele vya Tanzania kwenye mikutano ya Jumuia ya
Afrika Mashariki ili Zanzibar ilindwe, lakini bila ya mafanikio.

Waziri wa Biashara Nassor Mazrui katika hatua ya kuonyesha nia na
mkazo wa Serikali akatangaza kuongezwa kwa bei ya zao hilo katika
kiwango ambacho hakijawahi kuonekana kabla ili kuwa chachu na
ushawishi wa wananchi kuuza karafuu zao ndani yaani kwa Shirika la
Biashara ZSTC.

Pia kukatangazwa mazingira kadhaa ya kurahisha na kujenga uaminifu
baina ya wananchi na ZSTC na Serikali yenyewe kwa njia ya kutoa
uhakika kuwa wananchi hawatakopwa karafuu zao kama ambavyo imewahi
kutokea huko nyuma kwa ukosefu wa fedha za manunuzi.

Makamo wa Kwanza wa Rais Seif Shariff Hamad, kama alivyo mkaazi au
mzawa yoyote wa Pemba, yeye mwenyewe aliwahi kuwa mchumaji wa karafuu,
ndio aliiengia dimbani kuhimiza uchumaji wa zao hili akitilia mkazo
jinsi litavyosaidia katika uchumi wa nchi ambao kwa sasa una tatizo la
kukosa kutawanyika ( diversification).

Katika lile la kupigana na magendo ya karafuu Maalim Seif alisema
Serikali itabana kila pembe, kila diko na kila njia ili karafuu
zisiuzwe nje kwa njia ya magendo na kunena pia hataonewa mtu na wala
hatastahamiliwa mtu kwa sababu ya cheo chake ikiwa atahusika na
magendo.

Kisha katika jambo lisilo la kawaida katika dhana hii ya uchumaji wa
karafuu, basi Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Muhammed Shein akatangaza
uzinduzi wa uchumaji huko Pemba katika kile nilichokisema mwanzo
kusudi la kuonyesha kuwa hii ni kampeni ya kitafia na suala la
kipaumbele kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa SUK.

Ikawa sherehe kubwa, bila ya shaka na fedha nyingi zikatumika na
msisitizo wake yeye pia ukawepo katika suala la magendo na akisema
wazi wazi kuwa magendo ni adui wa uchumi wa Zanzibar na anaefanya
magendo haitakii mema nchi yake.

Lakini sasa pamoja na yote hayo ya wakubwa bado suala a magendo ya
karafuu ni tatizo au pia suala la watu kujitokeza kuuza karafuu zao
zote walizovuna ni tatizo kubwa huko kisiwani Pemba.

Tayari kuna matukio ya kujaribu kusafirisha karafuu kwa njia isio
halali na mtu angepaswa kujiuliza watu hawa wanaofanya hivyo wanataka
nini zaidi ilhali karafuu zimeongezwa bei?

Pili, watu hao wanataka nini zaidi ilhali pamoja na bei nzuri lakini
pia faida ya karafuu ikirudishwa ndani ya nchi ndio kupatikana elimu
bora kwa mwanae, afya bora kwake, barabara zao kwa wote, maji safi kwa
kila mtu na maendeleo kadhaa wa kadhaa?

Tatu, inakuwaje mtu anajitia katika magendo ya karafuu ilhali
uwezekano wa kupoteza maisha yake ni mkubwa au uwezekano wa kukamatwa
na kufungwa na kupoteza utumishi wake kwa familia yake na hivyo kuitia
katika mateso, kwa nini anafanya hivyo?

Nne, ni kwa sababu gani za msingi watu ambao wanauwezo wa kupata kiasi
kikubwa cha fedha waingie katika tombola ya kukosa kabisa kwa kujaribu
kuingia kwenye magendo na kuhatarisha mali zao kuzama au kufilisiwa na
kubaki katika umaskini kwa kukosa fedha za Serikali na zile ambazo
walizitarajia kuzipata kwa kuuza magendo huko Kenya?

Hivi sasa kuna maneno kuwa watu kadhaa wanabakisha karafuu zao
majumbani na Serikali imekuwa ikizifuata ama kulazimisha kuwa
wazipeleke kwenye mauzo na kama kuhifadhiwa basi zihifadhiwe na ZSTC,
mtu aweza kujiuliza kwa nini ifikie kiasi hicho, na jee sheria
inatumika sawa sawa na haki inazingatiwa?

Imewahi kusemwa na hata kurudiwa mara kadhaa kuwa karafuu kwa Unguja
na Pemba karafuu sio tu uchumi bali ni siasa, na sio tu ni siasa na
uchumi bali pia ni maisha na utamaduni. Na kwa hivyo zinaweza kuwa
fitna na uchonganishi mkubwa na hasama ndani ya jamii.

Ni fikra ya makala hii kuwa bado elimu ya kutoshwa haijafanywa na bado
kabisa uhamishaji wenye uzalendo wa kutukuka haujafanywa kuhusiana na
zao hilo na mnasaba wake katika nchi na mtandao wake kwa kila mtu.

Inawezekana mambo ya jumla jumla yamefanywa na kuamini kuwa elimu na
uhamasishaji umefanywa lakini mambo yanayoendelea kutokea yanatitilia
shaka uwepo wa ukweli kama huo.

Lakini pia utoaji wa matamshi kadhaa ya kuzuia, kutisha au kumtia
mkwara wa uuzaji wa karafuu au kuhifadhi karafuu majumbani, kuwe ni
maneno ya sikio moja kupitia sikio nyengine iwapo busara pia
haikutumika.

Maana popote pale nguvu tupu hazijawahi kuwa suluhisho la muda mrefu
la jambo lolote lile bila ya pia kutumika rai. Na rai ni kulifuatilia
tatizo katika msingi wake na kumuonyesha kila mtu uhusiano uliopo wa
karafuu na pumzi zake yeye mwenyewe za kila siku, lakini pia
kumsisitizia jambo hilo juu ya mwanawe na ndugu yake na kila ahli
wake.

Ni kumjengea uzalendo na mapenzi ya nchi yake ili aache kuifisidi na
kidhulumu na akijua pia kuwa mapenzi yake kwa nchi yake ndio kipimo
cha juu cha uzalendo wake kwa sababu haishi yeye kama Juma, Nasoro au
Machano bali yeye ni sehemu ya mnyoror ambao kipingili kimoja
kikimeguka basi uhai wake pia unaweza kuwa mashakani.

Katika karafuu hata kama tumefanya nini huko nyuma ni wazi kuwa elimu,
elimu, elimu bado inahitajika.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s