Serikali ilikataa uwazi, Wawakilishi wairudisha chuoni

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho anatazamwa sana na wananchi wanaofuatilia vikao vya baraza na wakati wa kujadili masuala mbali mbali ya serikali ambapo kwa sasa baraza hilo limekuwa ni kivutio kikubwa kwa wananchi ambao wanafuatilia vikao kutokana na uhuru wa kujadili na kupitisha masuala mbali mbali ya serikali huku wawakilishi wakitazamwa na wananchi waliowapigia kura majimboni mwao

Serikali ilikataa uwazi, Wawakilishi wairudisha chuoni

Kalamu ya Jabir Idrissa

KAMPENI ya kuilinda karafuu ya Zanzibar iliyoanzishwa na Rais Dk. Ali Mohamed Shein, inalenga kupambana na ufisadi – uovu unaotafuna uchumi wa taifa lolote duniani liwe tajiri kiuchumi, linalokua au taifa maskini kama Tanzania.Ufisadi unapoiandama nchi masikini kama Zanzibar – sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – athari zake huwa kubwa zaidi maana vitendo vya kifisadi huumiza zaidi wananchi wenye maisha duni.

Ufisadi unasababisha serikali kuwa legelege. Ikiwa legelege maana yake ina viongozi wasiokuwa imara au madhubuti katika kutekeleza yanayowanufaisha wananchi. Aghlabu hushindwa kutekeleza hata yale wanayoyaamua katika vikao halali vya kiutendaji.

Serikali ya aina hiyo hushindwa kukusanya kodi ipasavyo. Ukusanyaji wa kodi – chanzo kikuu cha mapato ya serikali yanayoipa uwezo wa kutekeleza mipango yake ya kuhudumia watu – huwa duni maana baadhi ya viongozi wamefungamana kimahusiano na wakwepa kodi, hasahasa wale wenye biashara kubwa.

Kadhalika, viongozi hao wa serikali legelege hukosa msimamo unaozingatia maslahi ya wananchi walio wengi na hawaoni tatizo kusabilia raslimali za umma kizembe kwa matajiri au makampuni ya kimataifa yanayoingia nchini kwa jina zuri la “uwekezaji.”

Serikali itafanya maamuzi ya kugawa mali hizi na zile, na katika kufanya hivyo, itahalalisha yote hayo kwa kutunga au na kurekebisha sheria na kuibua misamiati mingi isiyo na maana sana kwa ulinzi wa mali hizo.

Utasikia “tumekodisha hichi, kile tumeuza hisa zake, na pale tumepabinafsisha ili kuingiza teknolojia mpya na kuleta uzalishaji wenye tija.”

Anayetamka hayo atasema bila soni, “Wala ndugu wananchi msiwe na wasiwasi, hatukuuza ( mali ) kama inavyoelezwa na wapinzani wetu. Tumekodisha tu na tumeangalia maslahi ya wananchi.”

Aliyeko nje ya serikali, au hata wewe uliyeko ndani bali huridhishwi na mwenendo huo wa mali za umma kusabiliwa kizembe namna hiyo kwa wanaoitwa wawekezaji, unashangaa tu kusikia serikali imekodisha ardhi au jengo lake kwa miaka 99.

Mtizamo kama huo ulinisukuma miezi kadhaa hapo nyuma, kumchambua Dk. Shein baada ya kusikia matamshi yake yaliyonitia uchungu alipokuwa amewasili nchini kutoka ziara ya ng’ambo.

Dk. Shein alisema serikali haiwezi kuhojiwa chochote kwa kuuza mali yake… mali ya serikali ni mali ya serikali ambayo serikali inayo haki ya kuiuza kwa mtu yeyote au kuikodisha. “Nani huyo anayetuhoji,” alitamka.

Akathubutu kusema wananchi wanaoona hawakuridhika na uamuzi huo wa serikali, basi waende mahakamani lakini “hizo kesi zao tutashinda.”

Wakati huo kulikuwa na mjadala mkali wananchi wakihoji uamuzi wa serikali wa kukodisha kwa mwekezaji jengo la Mambomsiige, liliopo Forodhani, karibu kabisa na Bandari ya Malindi, kwa muda wa miaka 99.

Dk. Shein ambaye aliteuliwa kwa mara ya kwanza kuongoza wizara iliyopewa jukumu la kushajiisha misingi ya utawala bora katika serikali mwaka 2000, aliimarisha kile kilichokuwa kimesemwa na waziri wake aliyeko Ikulu, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini.

Waziri huyo alilieleza Baraza la Wawakilishi kuwa jengo hilo limekodishwa kwa nia nzuri ya serikali iliyolenga katika kuongeza miradi ya uwekezaji ambayo husaidia kuimarisha uchumi wa nchi.

Nikajiuliza na kumuuliza Dk Shein kupitia safu hii kama kweli amedhamiria kulinda mali ya umma kama vile alivyosema wakati akila kiapo cha kutumikia Wazanzibari katika nafasi nzito ya urais Novemba mwaka jana.

Niliungana na wananchi kupinga ukodishaji wa jengo hilo uliosababisha kuhamishwa kwa ofisi za taasisi za serikali na kuwekwa kwenye majengo yasiyokuwa imara hivyo.

Wanaharakati wa Mji Mkongwe walichukua hatua makini ya kuwasilisha malalamiko yao kwa Mamlaka ya Uendelezaji wa Mji Mkongwe wakisema wananchi hawakushirikishwa katika uamuzi wa serikali kinyume na taratibu zinazoelekeza kuwa wananchi wana haki ya kuulizwa kuhusu mradi unaoombwa.

Serikali haikusikiliza kilio chao wala cha mtu yeyote kati ya waliopinga. Ilishikilia msimamo wake na kuruhusu mwekezaji aanze utekelezaji wa mradi uliokusudiwa.

Kauli ya serikali ni kwamba mwekezaji aliyekodishwa jengo hilo ni Zamani Kempinski, waliokuwa wakiendesha hoteli ya kitalii iliyoko ukanda wa mashariki mwa kisiwa cha Unguja pamoja na iliyokuwa Hoteli ya Kilimanjaro, mbele ya lango la Bandari ya Dar es Salaam.

Sijafanikiwa kupata uhakika wa fununu mpya kuwa wawekezaji hao wamefuta mradi huo kutokana na shinikizo mbalimbali.

Leo, nafurahi kusikia jengo hili ni moja ya maeneo kadhaa yaliyoundiwa kamati teule na Baraza la Wawakilishi ili kuchunguzwa uhalali wa kukodishwa au kuuzwa kwake kwa watu binafsi.

Uamuzi huo ni tamati ya mijadala mizito iliyokaribia kupasua serikali kutokana na hofu zilizoelezwa na wawakilishi wakati wa mkutano wa bajeti.

Mkutano huo uliopitisha makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2011/12, ulimalizika wiki mbili zilizopita.

Kulingana na taarifa ya Spika Pandu Ameir Kificho, iliyotolewa hivi karibuni kupitia kwa Mkuu wa Utawala wa Baraza, Mdungi Makame Mdungi, ukodishaji au uuzaji wa mali za serikali haukuzingatia maslahi ya taifa.

Kamati hiyo inajumuisha wawakilishi kutoka CCM na CUF, vyama pekee vyenye wawakilishi katika baraza. Wajumbe wake ambao watakapokutana ndipo watachagua mwenyekiti wao, ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT-CCM), Asha Bakari Makame.

Asha, aliyeingia barazani kwa tiketi ya Viti Maalum, aliwahi kuwa waziri wa muda mrefu katika serikali Zanzibar ; anajulikana alivyo miongoni mwa wanawake shupavu walioingia katika siasa nchini.

Wengine ni Hamza Hassan Juma, mwakilishi wa Kwamtipura (CCM) na waziri wa zamani katika Ofisi ya Waziri Kiongozi, serikali ya awamu ya tano chini ya Amani Abeid Karume.

Wajumbe wengine ni Hija Hassan Hija (Kiwani, CUF), Mbarouk Wadi Mussa (Mkwajuni, CCM) na Omar Ali Shehe, mwakilishi wa Chake Chake kupitia CUF na ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi ya Baraza.

Kamati itafanya uchunguzi ulioagizwa kwa kushirikiana na mwanasheria wa baraza, Yahya Khamis Hamad, na Othman Ali Haji ambaye pia ni mtumishi wa baraza la wawakilishi.

Maeneo mengine yatakayochunguzwa na kamati hiyo ni uuzaji wa kiwanja cha Shirika la Utalii Zanzibar (ZTC) kinachoshikana na jengo la kihistoria la makao makuu ya shirika hilo , mtaa wa Livingstone, cha Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano eneo la Maruhubi.

Mengine ni kisiwa cha kitalii cha Changuu kinachotajwa kukodishwa kwa miaka 30 kwa malipo ya dola 3,500 tu wakati kabla, kikiingizia Shirika la Utalii dola 8,000 kwa mwezi kutokana na shughuli za kitalii ikiwemo kutembelewa na watalii.

Hapo, Spika ameruhusu kuondosha shaka iliyotanda vichwani mwa wawakilishi, kwa niaba ya wananchi. Siku zote shaka ikizidi, imani mbaya hushamiri.

Makala hii imechapishwa katika Gazeti la Mwanahalisi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s