Ubabe ndio unaowaponza akina Qadhafi

Na Ahmed Rajab

MAJUZI hivi jijini Nairobi rafiki yangu mmoja alinisimulia mkasa alioushuhudia siku moja alipokuwa nyumbani kwa Mzee Jomo Kenyatta huko Gatundu katika Mkoa wa Kati wa Kenya. Aliniambia kwamba akiwa kwenye mlango wa sebule ya Gatundu, alimsikia Kenyatta akiwaambia hivi baadhi ya mawaziri wake (ambao majina yao ninayahifadhi): ‘Ondokeni hapa karibu nami nendeni mketi kule. Mkiketi hapa nikaja kuhamaki naweza kuwapiga. Na mkiketi huko mkumbuke kwamba kamba yangu ni ndefu na naweza kuirusha nikawaburuta.’
Sahibu yangu aliniambia kwamba aliwaona mawaziri hao ghafla wakinywea; wakaondoka ‘kama kuku waliotiwa maji’ na wakenda kukaa mbali na Kenyatta. Siwacheki wala siwalaumu kwa kufanya hivyo. Jomo Kenyatta alikuwa pandikizi la mtu aliyekuwa na sauti ya unga, sauti ya mtu aliyeshiba. Akifungua mdomo ilikuwa lazima umsikilize kwa haiba ya sauti yake.
Kusema kweli, sijapatapo kusikia kama Kenyatta akiwachapa mawaziri wake. Hata hivyo, namjuwa Rais mmoja wa zamani, Jerry Rawlings wa Ghana, aliyekuwa na tabia ya kuwaingilia mwilini mawaziri wake. Safari moja alifika hadi ya kumtandika makonde Makamu wake wa Rais.
Lakini, hicho kisa cha Jomo Kenyatta alichokishuhudia rafiki yangu pamoja na ubabe wa JJ Rawlings ni kama vioo vilivyoonyesha jinsi tawala za Kiafrika zilivyokuwa baada ya wakoloni kutimuliwa barani Afrika. Visa kama hivyo viliashiria ujio wa udikteta na kushamiri kwake Barani Afrika.
Baada ya kuvikalia viti vya utawala viongozi wengi wa nchi za Kiafrika walianza kujisahau. Baadhi yao walijiona— na wakiamini hasa — kwamba wao ni ‘mababa’ wa mataifa yao. Wengine wakiamini kwamba hakuna mwingine nchini mwenye uwezo wa kushika madaraka ya urais; na hivyo wakajitangaza kuwa ni marais wa maisha; mfano ni Hastings Kamuzu Banda wa Malawi. Jean-Bedel Bokassa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati hakutosheka na Jamhuri aliyokuwa akiiongoza. Aliibadili na kuifanya iwe tawala ya Kifalme na yeye mwenyewe akajitangaza kuwa ndiye Mfalme.
Wengine, na hawa ndio wengi, hawajajitangaza hivyo; lakini walihakikisha kwamba wataendelea kutawala mpaka mwisho wa uhai wao. Kati yao ni Omar Bongo wa Gabon, Hosni Mubarak wa Misri, Zein al Abidin Ben Ali wa Tunisia na Muammar Qadhafi wa Libya. Karibu na kwetu Daniel arap Moi wa Kenya alijaribu lakini akashindwa. Kuna dalili kwamba Yoweri Museveni anazifuata nyayo hizo, ingawa yeye mwenyewe atayakana hayo.
Tukiiangaza miaka 50 iliyopita ya historia ya Afrika tutaona kwamba nchi nyingi barani humo zilidhalilishwa na udikteta; hasa katika enzi za mfumo ulioruhusu kuwapo chama kimoja tu cha kisiasa na kukifanya chama hicho kiwe ndicho adhimu katika siasa za nchi na mazingira mengine. Nchi zilizokuwa na mfumo aina hiyo hazikuwa na serikali zilizokuwa zikichaguliwa na wananchi wao katika chaguzi huru na za haki.
Nchi iliyofurutu ada kushinda zote kwa hayo Barani Afrika ilikuwa Libya chini ya Muammar Qadhafi. Libya haikuwa hata na chama kimoja cha kisiasa. Nchi ikiongozwa kwa mazingaombwe ya mtu mmoja. Kwa muda wa miaka 47 tangu Qadhafi na wenzake waliokuwa jeshini walipoupindua utawala wa Mfalme Idris, nchi hiyo imekuwa ikiendeshwa kwa mabavu na kwa njia za kiajabuajabu zisizo za kawaida.
Hivyo si jambo la kushangaza kuyashuhudia yanayotokea leo nchini humo, yaani huu mpambano wa kijeshi baina ya wapinzani wa Qadhafi na wale wenye kumuunga mkono. Pia si ajabu kuona ulingano kati ya yaliyojiri Tunisia na Misri na yanayojiri sasa Libya, Yemen, Syria na hata nchini Bahrain. Mote humo wananchi wanahisi kwamba wanatawaliwa bila ya ridhaa zao; mara nyingine kwa nguvu na mara nyingine kwa vitisho vya aina mbalimbali. Lengo lilikuwa moja tu: kuwahifadhi madarakani viongozi wa nchi hizo pamoja na aila zao, marafiki zao na washirika wao wa kisiasa.
Mfumo wa utawala wa aina hiyo, ambao ni muovu, hauwezi kudumu milele. Kwa vile ni mfumo wa ukorofi wenye kugandamiza watu hatima yake huwa ni kubomolewa na hao wenye kugandamizwa. Hutokea siku wenye kugandamizwa wakauvua unyonge wao na wakatumia kila njia hata ikiwa pamoja na kuzisabilia nafsi zao na kuyatolea mhanga maisha yao, ili haki zao zipatikane na kuyaondosha madhila yanayowasononesha mijini mwao, vijijini mwao na kwenye vitongoji vyao.
Baada ya kupigana kwa muda wa miezi sita wakitumia kila aina ya silaha za kisasa, wapinzani wa Qadhafi hivi sasa wanaishikilia sehemu ya zaidi ya asilimia tisini ya ardhi ya Libya. Si hayo tu bali Qadhafi, ambaye katika miaka ya karibuni alijibandika cheo cha ‘mfalme wa Wafalme Wakiafrika’ hivi sasa anasakwa. Aliyejidai jana kuwa jabari leo anawindwa kama hayawani aliye hatari.
Hamna shaka yoyote kwamba wapinzani wa Qadhafi wasingaliweza kupata ushindi wa haraka walioupata lau si kwa msaada wa madola ya Magharibi. Madola hayo yalijiingiza katika mzozo wa ndani ya nchi baina ya mapande mawili ya Walibya na yakawaunga mkono wapinzani wa serikali ya Libya kwa kisingizio cha kwamba majeshi ya Qadhafi yalikuwa yakiwaua wananchi wao na kwamba yakiandaa mauaji zaidi ya halaiki.
Hatua hiyo ya nchi za Magharibi imeanzisha mtindo mbaya na unaoweza kuleta madhara hasa kwa Bara la Afrika. Umoja wa Mkataba wa Kijeshi wa NATO, ambao uliundwa kwa dhamira ya kulihami Bara la Ulaya na nchi za Amerika ya Kaskazini, hivi sasa umeyatanua mamlaka yake nje ya Bara la Ulaya na kuyatumia kwingineko.
Tangu ulipoanza mzozo huu, Qadhafi amekuwa akishikilia ya kuwa huo uasi dhidi ya utawala wake ulichochewa na watu kutoka nje. Kwa hilo hakukosea. Pia amekuwa akishikilia ya kwamba lengo lao ni kubinafsishisha na kupora mali asili ya Libya. Kwa hilo pia huenda akawa hakukosea.
Aidha, Qadhafi amekuwa akishikilia ya kuwa miongoni mwa waliokuwa wakimuasi walikuwa wafuasi wa mtandao wa al-Qa’eda. Kwa hilo, bila ya shaka hajakosea. Ninasema hivi kwa sababu nyingi. Ya kwanza, ni kwamba ngome ya Qadhafi ya Bab al-Aziziya ilipotekwa wiki iliyopita walioiteka walikuwa ni wanamgambo Wakiberber kutoka milima ya Kusini-Magharibi mwa Tripoli. Hilo si la kutia hofu wala kushangaza. La kushangaza ni kwamba wapiganaji hao waliongozwa na kijana mwenye umri wa miaka 45 anayeitwa Abdelhakim Belhaj.
Wanamgambo hao wa Belhaj walipatiwa mafunzo ya siri ya kijeshi kwa muda wa miezi miwili na Vikosi Maalum vya Marekani. Na walipoiteka ngome ya Bab al-Aziziya Belhaj alikuwa akijigamba kwa namna walivyoiteka ngome hiyo na jinsi wanajeshi wa Qadhafi walivyokuwa wakikimbia kama panya. Belhaj ni mfuasi wa al-Qa’eda na aliwahi kuwako Afghanistan, Pakistan na Iraq ambako akishikiriana na yule katili Abu Musab al-Zarqawi.
Muhimu kwa mada yetu ni kwamba yeye alikuwa muasisi wa lile kundi la wapiganaji Wakiislamu wa Libya liitwalo Libyan Islamic Fighting Group (LIFG); kundi ambalo lilikuwa na kambi za mafunzo ya kijeshi nchini Afghanistan. CIA, lile shirika la Ujasusi la Marekani, lilikuwa likimjuwa Belhaj; na mwaka 2003 Wamarekani walimtia mbaroni huko Malaysia na halafu wakamhamisha na kumpeleka kwenye gereza la siri nchini Thailand ambako aliteswa.
Mwaka mmoja baadaye Wamarekani wakamgeuza zawadi na wakamtunukia Qadhafi. Belhaj aliselelea jela hadi mwezi Machi mwaka jana ambapo baada ya kutubu aliachiwa huru pamoja na magaidi wenzake wapatao 200. Na mwezi Februari mwaka huu akajiunga na waasi dhidi ya Qadhafi. Naye si mfuasi wa al-Qa’eda pekee aliye katika uongozi wa kijeshi wa waasi. Wapo wengine pia.
Inasemekana kwamba kundi hili la kina Belhaj ndilo lililomuua kamanda wa jeshi la waasi Jenerali Abdelfattah Younis mwezi Julai. Walimuua kwa sababu Younis ndiye aliyekuwa akiongoza mashambulio ya majeshi ya Qadhafi dhidi ya wapiganaji hao Wakiislamu huko Cyrenaica kutoka mwaka 1990 had 1995.
Vyombo vya usalama vya nchi za Magharibi vinaamini kwamba ikiwa Qadhafi hatotekwa au kuuliwa basi anaweza kuendelea kupigana kwa muda wa miezi kadhaa ijayo na ndiyo maana sasa vimeamua kwamba ni kheri Qadhafi auliwe ili mambo yamalizike.
Lakini mambo hayatomalizika kwa sababu hawa wapiganaji wenye mrengo wa al-Qa’eda watafanya juu chini wapambane na madola ya Magharibi; kwani hawatokubali kuiachia Libya iendelee kuchezewa na madola hayo.
La kuhuzunisha katika sakata hii nzima ya Libya ni kwamba yote haya yasingalimfika Qadhafi lau angeliziacha ndaro zake, hanjam zake, ubabe wake; na zaidi lau asingelikuwa akiwaminya wananchi wenzake na kuzifuja, tena kwa israfu kubwa, fedha za nchi hiyo. Angeliwasikiliza wenzake na akaufungua mfumo wa kisiasa, pengine kama asingeliendelea kuwa kiongozi angekuwa angalau na ushawishi mkubwa katika Libya mpya.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s