Penye nia pana njia

 

Na Ally Saleh

Shirika la Umoja la Mataifa la Elimu, Utamaduni na Sayansi la Umoja wa
Mataifa (UNESCO) kwa ufadhili wa taasisi mbali mbali za nje na
ushirikiano wa taasisi ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe
(STCDA) waliandaa kikao cha mafunzo juu ya dhana mpya ya utunzaji wa
miji mikongwe na ya historia kama ya Zanzibar.

Dhana hii mpya imekuja si kwa kuwa zile za zamani hazifanyi kazi au
kwamba kumekuwa na mkwamo wa utendaji, la ila imeletwa ili kutanua
mtizamo wa uhifadhi wa miji kama hiyo na kukazia maneeo mbali mbali
mbali ambayo hapo nyuma yalikuwa yanatizamwa kwa wepesi.

Mipango ya uhifadhi wa miji imekuwa ni muhimu katika miaka ya karibuni
kwa kuwa dunia imeaamka kwamba historia isipotee na sio tu itunzwe
bali iishi kwa miaka mingi ijayo kwa faida ya vizazi vya leo na kesho,
keshokutwa na mtondogoo.

Ndio maana dunia imeunda taasisi maalum ambayo inafanya kaazi hiyo
lakini pia kumekuwa na mipango ya kuona kuwa kila ambacho kinahitaji
kutunzwa basi hakitunzwi kwa maneno tu bali kinatambuliwa na kupewa
hadhi yake na kwa hivyo dunia nzima inahusika katika utunzaji wa kitu
hicho hata kama hakiko katika nchi yake.

Hiyo ndio maana ya kuwa ni urithi wa dunia. Kwa kutunzwa Mji Mkongwe
wa Zanzibar haina maana ni fakhari ya Zanzibar tu bali ni ya
ulimwengu mzima. Kama ambavyo sisi tuna fakhari ya Mji Mkongwe basi
pia aliyepo Brazil ndio maana anakuja kwetu kuangalia, na uhifadhi wa
kitu kilichoko China ni chetu sote na ndio maana sisi tunakwenda
kuangalia Ukuta Mkubwa wa China.

Dhana ya vitu vinavyohifadhiwa ni pana sana. NI miji, majengo, maziwa,
bustani, vihame na wakati mwengine mtu huwezi kuamini hata
inajumuisha sauti na harufu ambazo ni sehemu muhimu sana ya uhifadhi.

Mtu wa kawaida hawezi kuamini ila ukweli ni kuwa kwa mfano ziko harufu
ambazo zinapatikana hapa Zanzibar na pengine zisipatikane kwengine.
Kwa mfano harufu ambayo inapatikana eneo la Malindi kwa muda mrefu
imekuwa ni namna mbili.

Ya kwanza ya vumba na matope ya pwani ambayo inaweza ikamkera sana mtu
asiye Mzanzibari lakini kwa mtu wa Zanziba au aliyekulia maeneo ya
pwani basi harufu hiyo inakubalika kwake na haimkeri hata kidogo na
harufu nyengine kwa muda mrefu ilikuwa ni ile ya karafuu kwa sababu
palikuwa pana kiwanda cha karafuu. Ilikuwa raha ilioje wakati huo.

Sasa dhana mpya iliyoletwa na UNESCO inaitwa Historical Urban
Landscape (HUL) na ndio kwanza mbichi na huku taasisi hiyo ndio
inaieneza sehemu mbali mbali katika madhumuni hayo hayo tuliyo yaeleza
hapo juu.

Dhana hii ina maana ya kujali utunzaji wa mji au hifadhi yoyote kwa
kuangalia historia lakini pia na taswira. Kwa maana ya kuwa utunzaji
wa mji au hifadhi upanuliwe kwa kuwa na mikakati ya utunzaji
inayotizma ushikishwaji kikamilifu wa wadau.

Kwa mfano katika Mji Mkongwe au Mji wa Mawe wa Zanzibar unahitajika
ufanyike uhifadhi ambao unaweza kumilikiwa na wakaazi wote ili
washiriki na kuupenda mji wao kwa kujua una faida kwao na sio kuwa
wawe ni wakaazi tu lakini hawana sauti.

Lakini pia uhifadhi wa mji kama huu, ambao mimi ni mkaazi wake wa
kudumu, unatakiwa pia ushirikishi umma mkubwa zaidi kwa sababu kama ni
Wazanzibari basi pia ni wadau wa mji huo kwa sababu ni wao ndio
wamiliki halisi.

Kwa mfano ikiwa mkaazi mwengine wa Zanzibar asiye wa Mji Mkongwe basi
pia ana wajibu wa kutovunja, kutoharibu rasilmali ya Mji Mkongwe kwa
sababu yeye unamuhusu, sio kwa kuwa Mzanzibari tu, lakini kwa kuingia
na kutoka kila siku.

Na hili la kuingia na kutoka pia ni muhimu. Kwa sababu ni muhimu kujua
kiasi cha watu waingiao na watokao maana wengi hawaoni kuwa kuna
mnasaba na utunzaji wa mji. Kama vile ambavyo pia ni muhimu kujua
idadi ya watu na hata uongezekaji wake kwa vile pia kuna mnasaba na
utunzaji.

Kwa lugha nyengine uingiaji na utokaji unaathiri matumizi ya barabara,
unatikisa nyumba na kuzitia ubovu lakini pia zinatoa moshi ambao
unaathiri pia nyumba na wakaazi hao Mji Mkongwe na kwa hivyo kujua
idadi ya vyombo vya moto vinavyoingia sio tu idadi yao ijulikane
lakini pia kujaribu kudhibiti ukubwa wa magari yaingiayo.

Kwa bahati mbaya Mji Mkongwe una bandari ambayo ni moyo wa Zanzibar na
ambayo ni vigumu kuhamishika na kwa hivyo lazima taasisi inayosimamia
utunzaji wa Mji Mkongwe iwe na mipango ya kina na endelevu na haiwezi
kuna na mpango wowote ambao hautahusisha bandari.

Ila pia hatuwezi kuwa na Mji Mkongwe bila ya kuwa na uhusiano na eneo
lilo karibu nalo. Kwa mfano Mji Mkongwe unaotunzwa hauwezi kuishi
pweke bila ya uhusiano na maeneo inayopakana nayo, kwa vile ni
ujirani ambao hauepukiki.

Mpaka wa Mji Mkongwe ni barabara ya eneo la Darajani na kuzidi kidogo,
lakini kuna uhusiano wa muda mrefu na uhusiano wa moja kwa moja na
eneo la Darajani lenyewe, Vikokotoni na hata Mlandege. Kwa macho ya
kawaida tu kila kitu kilichoko Mji Mkongwe halisi unakiona katika
maeneo hayo.

Mji Mkongwe bila ya maeneo hayo hauwezi kuwa kama ulivyokuwa na kama
utakavyo endelea kuwa kwa sababu hata mahusiano ya mtu na mtu ya
wakaazi wa eneo hilo ni ya karibu sana na tabia zao na utamaduni wao
unafanana.

Ni ukweli pia kwamba utamaduni na mila ni sehemu ya Mji Mkongwe na
mambo hayo ni ya ulazima katika utunzaji wa mji kama tulivyosema kule
juu kuhusu suala la sauti na hata harufu, na kwa hivyo hatuwezi
kutenga maeneo hayo katika uhifadhi.

Katika kuonyesha kuwa Mji Mkongwe hauwezi kuishi peke yake wana warsha
waliamua kwa pamoja kwamba wakati umefika wa kufufua Bustani iliopo
eneo la Kilimani kwa jina la Botanic Garden, ambayo pamoja na kwamba
iko nje ya mji lakini ina uhusiano mkubwa na Mji Mkongwe.

Eneo hilo kwa sasa limevamiwa, limejengwa na kuharibiwa kwa kiasi
kikubwa lakini nia ilikwekwa wazi lifanywe kila litalofanywa lakini
bustani hiyo irudishwe halan, maana inahitajika sana.

Najua kuna sheria mpya ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe, na
kuja kwa mpango huu wa HUL basi lazima STCDA lazima ijipange upya ili
mipango yake iendane na utekelezaji wa dhana hiyo ambayo inasambazwa
kote duniani na Zanzibar haiwezi kubaki nyuma.

Tunaitakia STCDA utekelezaji mwema wa dhana ya HUL na wakijua kuwa
mpango huo utalinda zaidi maslahi ya pande zote yaani wakaazi,
wananchi na taasisi yenyewe lakini pia kwa upande mwengine jamii ya
kimataifa basi ni kheri na Baraka.

Ni muhimu katika hili kupata ushirikiano na Serikali, lakini pia
mgongano wa kisheria ambao upo baina ya STCDA na taasisi nyengine kwa
mfano Baraza la Mji la Zanzibar jambo ambalo lilijitokeza sana katika
warsha hiyo kiasi cha kuonyesha picha mbaya. Kila kitu kinawezakana na
muhimu ni kuwepo nia tu.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s