Buriani Mwakilishi wa Uzini

 
Mwakilishi wa Jimbo la Uzini (CCM) Mussa Khamis Silima, amefariki leo. Kifo chake kimetokana na ajali ya Gari juzi alipokuwa anakwenda Dodoma katika Bunge. Mkewe ambaye alikuwa pamoja katika ajali hiyo alikufa na kuzikwa leo. Mussa alikuwa pia Mbunge kutoka baraza la wawakilishi.

 
Mwakilishi wa Jimbo la Uzini (CCM) Mussa Khamis Silima (58) ambaye alifariki dunia juzi katika hospitali ya Muhimbi wodi ya Mifupa amezikwa leo adhuhuri huko kijijini kwake Kiboje Mkoa wa Kusini Unguja.

 
Mussa alifariki dunia baada ya kupata ajali iliyotokea huko Nzuguni karibu na mji wa Dodoma ambapo  mkewe Mwanakheri  Talib yeye  alifariki dunia hapo hapo baada za kupata ajali ya gari.

Hadi anakumbana na mauti hayo,Mussa alikuwa pia Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano anayeliwakilisha Baraza la Wawakilishi, ambapo alikuwepo Dodoma kuhudhuria kikao cha  Bunge kinachoendelea huko.

Mwili wa marehemu uliwasili Zanzibar jioni juzi kwa ndege ya kukodi ambapo ulisindikizwa na Spika wa baraza la wawakilishi; Pandu Ameir Kificho pamoja na Mbunge viti maalumu Kaskazini Pemba Mauwa Daftari Abeid.

Mara baada ya kuwasili mwili huo ulipelekwa katika jengo la Baraza la Wawakilishi kwa kuombewa dua na kutoa nafasi kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wananchi kwa ujumla kutoa salamu zao za mwisho wa marehemu.

Katika jengo la baraza la wawakilishi mawaziri na wajumbe wa baraza la wawakilishi pamoja na wananchi kwa ujumla walihudhuria na ibada ya dua iliongozwa na Kaimu Kadhi Mkuu pamoja na Katibu wa Mufti; Sheikh Fadhil Suleiman Soraga.

Mnadhimu Mkuu wa shunguli za baraza la wawakilishi ambaye ni Waziri wa Nchi Afisi ya Makamo wa Pili wa Rais; Mohammed Aboud mohammed alimuelezea marehemu kama kiongozi hodari aliyekuwa akiweka mbele maslahi ya taifa pamoja na wananchi wa jimbo lake kutetea hoja mbali mbali za maendeleo.

‘Tumempoteza kiongozi hodari mtulivu aliyeweka mbele maslahi ya taifa na wananchi wake wa jimbo la Uzini’ alisema Aboud.

Aidha naibu katibu mkuu wa chama cha mapinduzi Vuai Ali Vuai alisema chama cha mapinduzi kwa ujumla kimempoteza kada wake aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kupambana na vyama vya siasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

‘Tumepoteza kada imara wa chama cha mapinduzi ambaye alikuwa mpiganaji hodari na shupavu mwenye uwezo wa kupambana na wapinzani ambapo katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana aliibuka na ushindi mkubwa katika jimbo la Uzini’ alisema Vuai.

Hadi anafariki dunia Mussa anashikiliya cheo cha naibu katibu mkuu wa jumuiya ya wazazi ambayo ni moja ya taasisi tatu za chama cha Mapinduzi.

Pia alikuwa mjumbe wa kamati ya siasa ya chama cha mapinduzi katika jimbo la Uzini wilaya ya kati huku akiwa mjumbe wa kamati maalumu ya halmashauri kuu ya CCM Zanzibar.

Marehemu aliibuka na ushindi katika jimbo la Uzini baada ya kushinda katika hatua za awali za kura za maoni dhidi ya mpinzani wake Tafana Kassim Mzee ambaye alikuwa mwakilishi wa jimbo hilo kwa vipindi vitatu.

Mbunge afariki dunia: vilio, simanzi nzito bungeni 

Tuesday, 23 August 2011 20:33
Waandishi Wetu
 
VILIO na simanzi vilitawala bungeni jana mara baada ya Spika, Anne Makinda kutangaza kifo cha Mbunge, Mussa Khamis Silima, (Baraza la Wawakilishi – CCM, ambaye alikuwa amelazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), baada ya kupata ajali juzi nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma.
 
Spika Makinda aliwatangazia wabunge kuhusu tukio hilo la kuhuzunisha akisema, Silima alifariki jana mchana hivyo kutumia kanuni ya 149 kuahirisha Bunge hadi leo saa 3:00 asubuhi.
 
“Waheshimiwa Wabunge, jana asubuhi niliwatangazia kuwa, Mheshimiwa Silima alipata ajali na mkewe aitwaye Mwanaheri, kwa bahati mbaya mkewe akafariki dunia kutokana na ajali hiyo. Silima na dereva wake waliumia wakapelekwa Muhimbili kwa matibabu zaidi na leo asubuhi niliongea naye akasema anaendelea vizuri,” alisema Makinda na kuongeza:
 
“Lakini, nasikitika kuwaambia kuwa muda mfupi uliopita nilipata taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kwamba Mheshimiwa Silima amefariki dunia. Kwa maana hiyo, kwa kutumia Kanuni ya 149 naahirisha kikao cha Bunge hadi kesho asubuhi.”

Nje ya ukumbi wa Bunge, wabunge walikuwa wamekusanyika katika vikundi mazungumzo makubwa yakiwa juu ya msiba huo.

Spika kuongoza ujumbe wa watu 60

Jana, jioni Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alitoa ratiba ya mazishi ya mbunge huyo na kusema Bunge litawakilishwa na ujumbe wa watu 60 watakaoongozwa na Spika Makinda.
Joel alisema katika ujumbe huo, watakuwamo wenyeviti wote wa kamati, wajumbe wa Tume ya Bunge, wajumbe kutoka Kamati ya Nishati na Madini ambayo marehemu alikuwa ni mjumbe wake na kwamba mazishi hayo yanatarajiwa kufanyika leo saa 7:00 mchana.

Alisema ujumbe huo unatarajiwa kuondoka leo saa 4:00 kwa ndege kuelekea Zanzibar kwa ajili ya mazishi hayo.

Watoto wa marehemu wazungumza

Akizungumzia msiba huo, mtoto wa kwanza wa marehemu, Thani Mussa Hamis alisema hakuonana na baba yake hadi mauti yalipomkuta ingawa alizungumza naye kwa simu na kumtaka amletee vitu kadhaa.

“Sikupata muda wa kuzungumza naye, lakini asubuhi ya saa 12 leo (jana) nilizungumza naye kwa simu na alinieleza kuwa hali yake ni nzuri huku akinitaka nimletee vitu vyake kadhaa (hakuvitaja) nilivitafuta na nilipovipata nikaja navyo hospitalini lakini hata hivyo, nilikuta hali yake ikiwa imebadilika.”

“Sikujua ilikuwa kimetokea nini kwani nilipofika na kutaka kumuona baba walinitaka nisubiri kwanza na nilipokuwa nasubiri niliwaona madaktari wakiwa wanahangaika huku na kule na mara alikuwa akilalamika kukosa hewa hivyo wakamvalisha mipira ya hewa na kumhamishia chumba cha wagonjwa mahututi,’’ alisema.

Thani alisema baada ya muda daktari alitoka na kumweleza kuwa amefariki. “Inauma sana… juzi nililia sana kwa ajili ya kifo cha mama yangu, leo tena baba pia nalia lakini hakuna namna ni mipango ya Mungu hivyo tumuombee ampumzishe kwa amani huko alipo,’’ alisema Thani

Mtoto wa nne wa marehemu, Mussa Hamis Suleiman alisema kifo hicho kimewaacha katika masikitiko makubwa kwa kuwa walikuwa wanamtegemea kwa ushauri na mambo mengine. Marehemu ameacha watoto watano, wawili wa kike na wengine wa kiume.

Wabunge wamlilia
Baadhi ya wabunge walizungumzia kifo hicho cha ghafla wakisema watakosa hekima na busara zake katika masuala mbalimbali ya uendeshaji wa Bunge, huku Kamati ya Nishati na Madini ambako alikuwa mjumbe wakisema kuwa “Tumepoteza mzazi katika kamati yetu.”
 
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, January Makamba alisema Silima alikuwa mtu aliyewaunganisha wabunge hata pale palipotokea tofauti za mawazo na kusigana miongoni mwao. “Alikuwa mpatanishi, mara nyingi mimi nilikuwa nampa nafasi ya mwisho wakati wa kuchangia maana hakuwa na utamaduni wa kuzungumza sana na mara zote nilipompa nafasi alitoa kauli ya hitimisho ambayo ilikuwa mwafaka kwa wabunge wote,” alisema January na kuongeza:
 
“Yeye na Mheshimiwa Mariam Kisangi tuliwaona kama wazazi wetu, yeye (Silima) tulimwita baba wa kamati na Kisangi tunamwita mama wa Kamati kwa maana kwamba ni watu wazima kiumri kuliko wengi wetu kwenye kamati yetu lakini pia walitushauri mambo mengi.”

Kauli ya January aliungwa mkono na Kisangi pamoja na Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage ambao walisema kwa nyakati tofauti kwamba mbunge huyo alikuwa mpatanishi. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema Baraza la Wawakilishi, Bunge na Watanzania kwa ujumla wamepoteza mzalendo ambaye alikuwa muhimu sana kwa taifa.

“Alikuwa hana bias (upande), ulikuwa ukipata ushauri wake unauchukua asilimia 100 kwa sababu hakuwa na ushabiki wa aina yoyote, kwa msimamo wake wa wazi na umri wake, amekuwa msaada sana kwa chama chetu (CCM), kwa wabunge wa Zanzibar lakini pia kwa Bunge letu,” alisema Lukuvi.
 
Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed alisema wananchi wa Uzini alikokuwa Mwakilishi wamepata pigo kubwa na amewaachia wabunge wa Zanzibar pengo kubwa. “Ni msiba mkubwa, naweza kusema Mheshimiwa Silima alikuwa na uhusiano mwema na kila mmoja wetu, busara zake zilitufaa sana na alikuwa mtu wa watu, kweli tumepata pigo kubwa lakini hiyo ndiyo njia yetu sote,” alisema Hamad.  

Mbunge wa Busanda (CCM) Lolencia Bukwimba alisema atamkumbuka kama kiongozi mwema:  “Mara nyingi pia nilimwona akiwa kiunganishi cha wabunge wa Zanzibar, wengi walikuwa wakimfuata kuzungumza naye,” alisema Bukwimba.

Ajali ilivyotokea

Silima na mkewe, Mwanaheri walipata ajali juzi katika eneo la Nzuguni nje kidogo ya Mji wa Dodoma walipokuwa wakirejea kutoka Zanzibar ambako walikwenda kuhudhuria msiba wa kaka wa mkewe. Mwili wa Mwanaheri ulisafirishwa kwenda Zanzibar na kuzikwa juzi, huku Silima na dereva wake, Chizali Sembonga walisafirishwa kwa ndege ya kukodi kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam ambako walilazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa ajili ya matibabu. Dereva huyo anaelezwa kwamba anaendelea vyema na amelazwa katika wodi maalumu Mwaisela.

Historia yake

Hadi alipofariki dunia, Silima alikuwa Mbunge akiwakilisha Baraza la Wawakilishi, Mwakilishi wa Jimbo la Uzini na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM (Tanzania Visiwani), nafasi alizozipata mwaka jana. Alisoma katika Shule ya Msingi Mkwajuni Zanzibar (1961- 1968) na baadaye kujiunga na elimu ya sekondari katika Shule ya Uzini (1969 – 1970) kabla ya kuhamia katika Shule ya Sekondari ya Karume ambako alisoma 1971 – 1972.

Baadaye Silima alipata mafunzo ya ualimu wa ngazi ya stashahada katika Chuo cha Ualimu cha Nkurumah (1981- 1983) na baadaye kufundisha katika shule mbalimbali visiwani Zanzibar akiwa mwalimu wa kawaida (1973 – 1988) na baadaye mkuu katika shule mbalimbali (1988 – 1996). Kabla ya kuingia kwenye siasa, Silima aliwahi kufanya kazi katika Ofisi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (2001 – 2010), Mratibu wa Masuala ya Wanafunzi katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (1996 – 2001).

Bunge kuendelea

Kuhusu ratiba ya Bunge, Joel alisema ratiba itabaki kama ilivyo lakini akaongeza kwamba semina ya wabunge kuhusu Muswada wa Sheria ya Kuundwa kwa Katiba mpya ambayo ilikuwa ifanyike Jumamosi, haitafanyika kwani Bunge litaahirishwa Ijumaa jioni kwa hotuba ya Waziri Mkuu. Kwa mujibu wa ratiba hiyo, leo mjadala wa hotuba ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji itaendelea na kumalizika jioni wakati keshokutwa Alhamisi itawasilishwa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Fedha na Uchumi ambayo itahitimishwa Ijumaa mchana kabla ya Waziri Mkuu kuahirisha Bunge jioni.

Habari hii imeandikwa na Neville Meena, Dodoma na Boniface Meena, Festo Polea na Aidan Mhando, Dar.
 
 
MWANANCHI
 
 
Mke wa Mbunge afariki
 
Monday, 22 August 2011 21:46
Habel Chidawali,Dodoma

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana lilisimama kwa dakika moja kumkumbuka mke wa Mbunge mwenzao aliyefariki juzi kwa ajali ya  gari. Spika Anne Makinda, alilitangazia Bunge kuwa mke wa Mbunge Mussa Khamisi Silima (Baraza la Wawakilishi-CCM) alifariki juzi katika eneo la Nzuguni, nje kidogo ya mji wa Dodoma.

“Waheshimiwa wabunge, kwa masikitiko makubwa naomba kuwataarifu kuwa jana Agosti 21 saa mbili kasorobo, katika eneo la Nzuguni, mheshiwa Mussa Silima akiwa na msafara na familia yake, walipata ajali na mke wa mbunge huyo, alifariki papo hapo. Kwa hiyo naomba tusimame kwa dakima moja kumkumbuka,”alisema Makinda.

Alimtaja marehemu kuwa ni Mwanaheri Twalib, na kwamba mwili wake ulisafirishwa jana kwa ndege iliyombeba pia mbunge na dereva wake Dar es Salaam kwa  matibabu.

Makinda alisema, mbunge huyo alikuwa akitokea Zanzibar ambako walikwenda kumzika kaka wa marehemu mke wake.Spika alisema ofisi ya Bunge imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa kuhusu ajali hiyo na kwamba tayari Bunge lilishawateua wabunge nane kwa ajili ya kuwakilisha kwenye mazishi.

Mwananchi lilifika hospitalini jana na kuzungumza na mbunge huyo ambaye alikuwa amelazwa katika wodi ya wagonjwa wa daraja la kwanza.”Nimekwishapoa ndugu zangu, kweli nilikuwa na hali mbaya lakini vipimo vimeonyesha kuwa mguu wangu wa kulia umefyatuka katika nyonga na hivyo nina maumivu makali sana, lakini mke wangu naye nimeambiwa kuwa anendelea vizuri,”alisema Silima kabla hajajua kuwa mke wake alikuwa tayari amefariki.

Mbunge huyo pia alikuwa akilalamika kuwa kifua kilikuwa kinambana zaidi na hasa sehemu ya upande wa kulia ambako hata hivyo, alisema ilikuwa ni tofauti na vile alivyopelekwa juzi usiku hospitalini.

Akizungumzia mazingira ya ajali hiyo alisema “tulikuwa kwenye gari ndogo na mbele yetu kulikuwa na gari kubwa, lakini dereva wangu alipotaka kulipita  gari hilo halikuonyesha ishara kuwa kulikuwa na gari jingine mbele.”‘

Alisema walipotaka kulipita gari hilo, ghafla waliona gari lingine mbele yao huku nyuma kukiwa na gari lingine na walipojaribu kujisalimisha walibanwa katika pande zote na kusababisha ajali hiyo.Wabunge wengi akiwemo Spika wa bunge jana walikwenda hospitalini  kumjulia hali lakini kuliwekwa msisitizo wa kutomwambia juu ya kifo cha mke wake.
MWANANCHI

 
Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s