Joka hili haliondoki hadi lipazwe

Moja ya vituo vya kusambazia huduma ya mafuta hapa Zanzibar, huduma ambayo imeadimika kwa kiasi kikubwa na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi

Ally Saleh

Kwa wiki mbili nzima nchi ilikuwa rehani. Ilikuwa katika mikono na
huruma ya makampuni makubwa ya mafuta nchini Tanzania ambayo kwa lugha
ya kejeli kidogo tunaweza kusema hata mkononi hayajai.

Na mara nyingi Mswahili akisema kitu hakijai hata mkononi ana maana
kuwa kitu si muhimu, hakina nguvu au hakiwezi kuzima wala kuwasha, na
Mswahili akiamini hivyo basi ndio ameamini hivyo na taabu kumshawishi
vyenginevyo.

Lakini kwa hizo wiki mbili tumeona jinsi ambavyo kumbe makampuni hayo
machache ya mafuta si makampuni yasojaa mkononi wala si makampuni
ambayo hayazimi wala hawawashi na kwa kweli kumbe yana nguvu kupita
ziada.

Nguvu hizo zimetokana na ukweli kuwa nguvu zao zinatokana na eneo
walilolishikilia ambalo ni nishati ya mafuta na likiwa ni eneo ambalo
linaendesha nchi hii kwa kila dakika ya pumzi zake, bila mafuta yawe
ya petrol au dizeli au mafuta maalum ya ndege basi nchi itaganda.

Na kwa hakika nchi iliganda sana. Haikuganda tu kwa sababu magari
yalikuwa hayaendi na kurudi, na wala sio tu kwa sababu umeme
ulizimika, na wala tu si kwa sababu huduma zilizorota lakini kwa
sababu Serikali yenyewe ilitekwa ikiwa ni zaidi ya nchi kuwa katika
rehani.

Kwa bahati hayo yakitokea Bunge la Jamhuri ya Muungao likiwa katika
kikao lakini bado makampuni haya ya mafuta yakathubutu kukaidi amri
ziliotolewa na taasisi ya EWURA, ambayo ziada ya nguvu zake ni kutoa
leseni za makampuni hayo.

Lakini makampuni hayo yakawa na nguvu na jeuri ya kukataa mapendekezo
ya EWURA na kwa hivyo Serikali, na moja ya makampuni hayo ni lile na
British Petroleum ambalo Serikali ya Tanzania inashikilia hisa ndani
humo.

Pia tukio hilo lilitokea ikiwa ni siku chache baada ya kufanyika kikao
cha Jukwaa la Wahariri ambalo moja ya azimio lake kubwa baada ya
kukutana Arusha ni kupigia kelele suala zima la nishati yaani iwe ya
umeme na ile ya petroli kwa kuamini kuwa nishati ndio damu ya nchi,
bila damu hiyo nchi kama mwili haiwezi kuwa na uhai.

Kwa fikra zangu si rahisi kukubali kuwa tukio kama hilo ni la kirahisi
tu ( one off issue), lakini naamini kuwa ni tukio lilopangwa na
makampuni hayo ambayo sasa yanaanza kuwa kama joka kubwa ambalo
linakuwa na nguvu na nguvu hizo haziwezi kuondoka bila ya kupazwa.

Tukio hilo limetushituakuwa sasa tuna mkusanyiko wa kisekta ambao una
nguvu kubwa na kwamba mikusanyiko kama hiyo inaweza kufanya
tusiyoyatarajia ambayo kwa sasa tunasikia kwa wengine tu huko, lakini
tukumbuke ule mchezo wa watoto wa nyoka naapite, na sasa nyoka yumo
mwetu ndani.

Hapa nakumbuka maneno ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ulinzi,
Usalama na Mambo ya Nje Hassan Zungu aliposema kitendo cha wafanya
biashara ya mafuta kuficha na kukataa kuuza mafuta kitaifa ni hatari
kwa usalama wa nchi.

Usalama wa nchi si tu wa mipakani lakini hata katikati ya nchi kwa
sababu kulikuwa na nafasi kubwa ukosefu wa mafuta wa wiki mbili, kwa
maana watu walikosa kufanya kazi na kwa hivyo njaa iliwazonga,
ingeweza kuzusha fujo za kijamii kama zile ambazo tumeziona Uingereza
hivi karibuni.

Tuondoke na mawazo kuwa Tanzania itaendelea kuwa kisiwa cha amani kama
ambavyo Uingereza pia ilikuwa ikiamini, lakini wakati huo huo
tukitenda matendo ya kuwakosesha watu uhai na kazi zao, tukitaraji
kila siku watabeba bango la amani, la iko siku watalibwaga.

Tukitoa makapuni ya mafuta tujue kuna makampuni ya umeme, uagiziaji,
mawasiliano, usafiri, usafirishaji na mengi mengine ambayo yanagusa
moja kwa moja huduma za kila siku za umma katika upana wa nchi..

Na katika zama hizi za biashara huru ambapo Serikali haina chochote
katika eneo hilo, ni wazi kuwa Serikali iko uchi, na uchi wenyewe ni
mbele ya wanafamilia na hilo limedhihirishwa na makampuni ya mafuta.

Makampuni ya mafuta yametoa mwanya au yametoa dalili kwa makampuni
katika sekta nyengine kuwa yanaweza kuiweka rehaini serikali basi pia
tujue kunaweza kuyapa moyo makampuni mengine katika sekta nyengine
kujaribu pia kufanya hivyo.

Kwa maana ikiwa makampuni hayo waliiteka nchi kwa wiki mbili, na iwapo
hatua za kweli za kuzuia hali hiyo isitokee tena basi tujue kuwa
kitendo kile ni hakika kitarudiwa tena, na kikija tena kitakuja na
vitimbi zaidi maana kuna msemo usemao anarithi huzidi.

Tunaweza tukapata watoto watundu wengine katika mawasiliano. Tunaamka
makampuni ya mawasiliano yanasema yanakata huduma za simu mpaka hiki
kiwe vile na hiki kiwe vipi. Yanakataa kukutana na Serikali, yanasema
lao ndio lao, na nchi kwa wiki mbili haina mawasiliano.

Fikiria picha hiyo vizuri na usiamini haiwezi kutokea kwa sababu mbona
imeweza kutokea kwa makampuni ya mafuta? Na mbona BP walishiriki jee
TTCL nayo haiwezi kuwemo katika mgomo kama huo kwa ushirikiano na
wenzao wa sekta moja?

Katika kile cha hatua hiyo Wabunge walikuwa wakali na wakapendekeza
mambo mengi ya hatua za nguvu nguvu zichukuliwe kama Polisi kusimamia
uuzaji, Jeshi kusimamia usambazaji lakini la kujiuliza jee vitendo
hivyo vingekuwa na mashiko ya kisheria?
Jee kama hatua hizo zingechukuliwa za kuyatoa na kuyauza mafuta kwa
nguvu kungekuwa na athari gani za muda mrefu na muda mfupi kiserikali
na kinchi? Tusingekuwa na lebo ya nchi ambayo inakosa utawala wa
sheria, isiyostahamilia biashara huru na mengi ambayo yakishiliwa na
nchi za Magharibi yanakuwa na athari kubwa.

Hapa ndipo ambapo hoja yangu ya suluhu sasa itakapojikita ili kuweza
kuzuia matokeo kama yale yasitokee tena pamoja na kuendelea kuheshimu
kuwepo na uhuru wa biashara na ikiwa ni pamoja na suala la bei kwa
mujibu wa soko.
Hii inailazimisha Serikali ikae vyema na kutizama upya mambo mengi juu
ya huduma zinazotolewa na makampuni ya sekta mbali mbali katika macho
ya taifa kwa kutizama athari zinazoweza kutokana na migomo kama hii.

Turudi kupunguza makampuni yasiwe na nguvu za kibiashara ( cartels);
turudi tutizame upya mamlaka ya Serikali katika uratatibu wa sekta kwa
sekta; tutizama suala la athari kwa binaadamu katika biashara zote
kubwa; turudi nyuma kutizama upya juu ya ubora wa sera zetu katika
zama hizi za biashara huru na ushindani; nafasi mpya ambayo Serikali
inaweza kuwa nayo kwa hali ambao imeweza kujitokeza na pia ni namna
gani taasisi za usimamizi (regulatory bodies) zinavyoweza kusimama kwa
uhuru kuzigomba kampuni kama hizi.

Lakini pia sijui hili litatizamwa vipi ambapo imekuwa ikisemwa jeuri
kubwa ya makampuni ya mafuta tuliyoiona kunatokana na kuwa kuna
wanasiasa ambao wana hisa katika kampuni kama hayo. Hili pia
linatazamiwa liwekewe muelekeo maana haliwezi kuwa na khatma nzuri.

Kwa jumla ninachotaka kusema ni kuwa kila njia itumiwe ili kukusanya
mafunzo yote yaliopatikana katika sakata ya mafuta ili nchi hii isiwe
tena katika kitambo cha rehani cha wiki mbili.

Tutizame vipi Uingereza ilipokuwa rehani kwa siku tatu nini
kimetokezea, na watu husema inafaa kuchukua hadhari kabla ya athari.

Advertisements

One response to “Joka hili haliondoki hadi lipazwe

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s