Balozi wa Misri aangwa

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Balozi wa Misri, Wael Adel Nasr, aliyefika ofisini kwake Ikulu Dar es Salaam leo Agost 22, kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake nchini. Kushoto ni Msaidizi wa Balozi huyo Amr Mahmoud.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL AKUTANA NA BALOZI WA MISRI NCHINI TANZANIA WAEL ADEL NASR, IKULU JIJINI DAR ES SALAAM: AGOSTI 22, 2011

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo Jumatatu Agosti 22, 2011 amekutana na Balozi wa Misri nchini Tanzania Wael Adel Nasr ambaye amefika ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam kumuaga kufuatia kupangiwa kazi nyingine, ikiwa ni baada ya kukaa nchini kwa miaka minne.

Balozi Nasr ambaye sasa anahamia kitengo cha nchi za Afrika Mashariki na Kati kama mwakilishi wa Misri alimwambia Makamu wa Rais Dkt. Bilal kuwa kuwepo kwake Tanzania kumemfunza mengi na kubwa ni kuwa Tanzania ni nchi ya amani na upendo hali iliyomfanya kuishi bila kujiona mgeni katika kipindi chote alichokuwepo nchini.

Balozi huyo aliongeza kuwa, hali inayoshabihiana katika utamaduni na maisha sambamba na mahusiano ya kihistoria baina ya nchi hizi mbili ni miongoni mwa sifa nyingine ambazo zimeyafanya maisha yake nchini Tanzania kuwa mazuri, hali inayomlazimu kutamka kuwa anaondoka Tanzania kimwili lakini moyo wake upo hapa Tanzania.

Akizungumzia mapinduzi yaliyofanyika nchini mwake, Balozi Nasr amefafanua kuwa, mapinduzi hayo yatabadili kwa kiasi kikubwa sera ya Mambo ya nchi za Nje ya Misri ambapo sasa nchi hiyo itarejesha sera inayotazama mahusiano ya karibu katika kuleta ukombozi na utanuzi wa demokrasia katika Afrika, kama ilivyokuwa wakati wa harakati za kupigania uhuru wa nchi za Afrika.

“Kama unakumbuka ndege ya kwanza kutua Tanganyika ilitoka Misri tena ilitua saa mbili baada ya Tanganyika kutangazwa huru. Hii inaonyesha kuwa ndege ile ilianza safari ya kuja Dar es Salaam saa kama nne kabla ya kutangazwa uhuru wa Tanganyika na hili ni moja ya mambo tunayoyakumbuka sana katika mahusiano yetu na Tanzania,” alisema Balozi Nasr.

Kwa upande wake Makamu wa Rais Dkt. Bilal alimwambia Balozi Nasr kuwa anashukuru kwa maelezo mazuri aliyoyatoa juu ya Tanzania na kwamba anatambua mchango wa Misri katika maendeleo ya Afrika na akasisitiza kuwa ni wakati sasa Afrika kujitegemea kwa kuongeza mashirikiano katika kukuza uchumi wa wananchi wa bara hili.

Dkt. Bilal alisema, mashirikiano ya kiuchumi katika COMESA, SADC na EAC ni mfano wa muhimu na kwamba jitihada maridhawa zinatakiwa kufanywa ili mashirikiano hayo yakue ikiwemo kuanzisha mapya baina ya nchi na nchi. “Hakuna sababu ya kulalama kuhusu sababu ya Tanzania kutokuwa mjumbe wa COMESA, bado Misri inaweza kufanya makubaliano na Tanzania, na kisha kuweza kufanya mambo mengi pamoja baina ya nchi hizi mbili,” alisema na kuongeza;

“Natambua kuwa yapo mazungumzo yanayoendelea katika jumuiya zetu za SADC, EAC na COMESA juu ya kutanua wigo wa ushirikiano kiuchumi, lakini mazungumzo haya si lazima yasubiliwe sana. Inawezekana nchi moja moja zikawa na maafikiano juu ya kutanua mahusiano ya kiuchumi jambo ambalo linaweza kufanyika kwa Tanzania na Misri na Tanzania haina hofu yoyote ya kushirikiana kiuchumi na Misri,” alimalizia.

Imetolewa na: Boniphace Makene

Mwandishi wa Habari wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Jumatatu Agosti 22, 2011

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s