Dira yetu ni kilimo bora


MAPINDUZI ya kilimo ndio mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya saba yenye nia ya kutekeleza kwa vitendo dhamira ya kuwakomboa wakulima wa Zanzibar kutoka kilimo duni kisichokuwa na tija na uzalishaji na kuwawekea fursa ya kuwawezesha kupata tija na kuwa na uhakika wa chakula na lishe.

Uongozi wa Wizara ya Kilimo na Maliasili iliyasema hayo katika kikao maalum na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein katika muendelezo wa kukutana na Wizara zote za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuangalia mpango kazi wa Wizara na uhusiano wa MKUZA na Dira ya 2020.

Ukieleza mikakati iliyojiwekea Wizara hiyo ikiwemo ile ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2011/2012,ukiongozwa na Kaimu wa Waziri, Mhe. Ramadhani Abdalla Shaaban ulieleza kuwa mwelekeo huo ndio malengo ya Dira ya 2020, maelekezo ya Ilani ya uchaguzi ya CCM 2010- 2015, Mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini (MKUZA II), na Mapango wa Mageuzi ya Sekta ya Kilimo (ATI).

Uongozi huo ulieleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2011/2012 Wizara itatekeleza dhamira ya Mapinduzi ya Kilimo itakayopelekea kutoa mchango zaidi katika kukuza uchumi wa taifa sambamba na kupunguza umasikini ambapo miongoni mwa mikakati iliyowekwa ni kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji maji na kuhamasisha uvunaji wa maji ya mvua ili yatumike.

Uongozi huo pia ulieleza lengo lake la kuimarisha miundombinu ya masoko ya kilimo, kuongeza thamani ya bidhaa za kilimo na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha vijijini na kuimarisha huduma za wakulima na wafugaji na uwezo kwa wakulima juu ya usarifu wa mazao.

Aidha, uongozi ulieleza lengo lake la kutoa huduma za kilimo cha matrekta na huduma za pembejeo kwa wakulima zikiwemo mbolea, dawa ya magugu na mbegu bora pamoja na kutoa huduma za utibabuw a mimea, karantini na ukaguzi wa mazao.

Kwa upande wa kuliimarisha zao la karafuu Wizara ilieleza lengo lake la kuotesha miche 500,000 ya mikarafuu pamoja na kutoa elimu kwa wakulima.

Aidha, Wizara ilieleza lengo lake la kuendeleza misitu ya jamii na kushajiisha matumizi ya gesi ya kupikia, kuzalisha miche ya misitu na kuvuna mazao yake na uendelezaji wa hifadhi za misitu pamoja na kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na makaa kwa kutumia nishati mbadala.

Pamoja na hayo uongozi huo wa Wizara ulieleza lengo la kujitoshelelza kwa chakula na kujenga uwezo wa kuwa na akiba ya chakula, kuongeza tafiti za mazao ya kilimo na maliasili pamoja na kujenga miundombinu ya vituo vya utafiti na uwezo wa wataalamu.

Uongozi pia, ulieleza lengo lake la kukiimarisha chuo chake cha Kilimo kilichopo Kizimbani kwa kutoa wataalamu wa kilimo na kuwajengea uwezo waalimu na utoaji wa huduma za elimu kwa wakulima kupitia mabwana na mabibisamba, skuli za wakulima, Maafisa wa Wilaya na chuo cha Kizimbani.

Pia, uongozi huo ulieleza mchakato wa mradi unaoendelea wa ‘Feed the future’ ulio chini ya serikali ya Marekani ambao unahusisha zaidi suala la kilimo cha umwagiliaji maji, kuimarisha mazao na usarifu wa mazao, sera na utafiti ambao katika Tanzania imeyahusisha maeneo matatu ikiwemo Zanzibar.

Wakati huo huo Dk. Shein alifanya mkutano na uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ukiongozwa na Waziri wake Mhe.Said Ali Mbarouk ambayo ilieleza Mpango Kazi wake kwa mwaka 2011/2012 ikiwa ni pamoja na kueleza matumaini ya wananchi wa Zanzibar kwa kuanzishwa wka Wizara hiyo mpya ambayo itasaidia sekta ya mifugo na uvuvi.

Wizara ilieleza kuwa katika mwaka wake huu wa fedha imekusudia kuanzisha Baraza la Utafiti wa Mifugo ambapo tayari imeshafanya mazungumzo na taasisi ya COSTECH ambayo imeahidi kutoa mafunzo juu ya kutayarisha mapendekezo ya tafiti.

Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa katika kuiimarisha sekta ya uvuvi tayari Wizara imeshafanya mazungumzo na wawekezaji mbali mbali kwa lengo la kuekeza katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu.

Wizara pia, imeeleza lengo lake la kuimarisha huduma za ugani ili iwafikie walengwa wote katika sekta ya mifugo na uvuvi na kukuza huduma za uzalishaji wa mifugo.

Pia, Wizara ilieleza lengo lake la kufanya mapitio ya sera, sheria, kanuni, mipango na mikakati endelevu ya uvuvi na uzalishaji wa mifugo kwa ajili ya manufaa ya wananchi bila ya kuathiri mazingira.

Sambamba na hayo, Wizara ilieleza azma yake ya kudhibiti uvuvi haramu na kuimarisha ulinzi wa rasilimali kwa kuweka doria ikishirikiana na wananchi ikiwa na lengo pia, la kuongeza uzalishaji wa samaki.

Kwa upande wake Dk. Shein alitoa pongezi kwa watendaji hao wa Wizara waliofanya vikao hivyo kwa nyakati tofauti na kueleza kuwa anamatumaini makubwa ya kupata mafanikio katika uendeshaji Wizara hizo sambamba na kufikia malengo na mikakati hiyo waliyojiwekea.

Aidha, alieleza umuhimu wa kuwa na uhakika wa chakula cha kutosha sanjari na elimu kwa wananchi juu ya lishe bora pamoja na kueleza azma ya serikali katika kuziendeleza sekta za uvuvi, mifugo, kilimo na maliasi ili ziweze kueleta faida kwa nchi na wananchi wake.

Rajab Mkasaba

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s