Balozi Idd achia ngazi Kitope

Balozi Seif Ai Iddi (kulia) ambaye ni makamu wa pili wa rais wa zanzibar na mbunge wa jimbo la kitope kaskazini unguja akizungumza na spika wa baraza la wawakilishi Pandu Ameir Kificho katika mkutano wa kwanza wa kuwatambulisha viongozi wapya wa CCM uliofanyika zanzibar baada ya uamuzi wa CCM kutaka kujivua gamba

Na Ally Saleh

Demokrasia ya uwakilishi ni muhimu sana na katika zama hizi
huunganishwa moja kwa moja na suala la maendeleo, amani na utawala
bora. Imekuwa kama mambo haya hayetenganishiki.

Na yeyote yule anataka au kutamani tu kutenganisha basi hafiki mbali
na kama akifika mbali ni kwa ukandamizaji na mwisho wa ukandamizaji ni
umma kuikataa seirkali kwa nguvu zao chache walizonazo.

Kila raia ana haki ya kusema, kudai kile anachoona bora kwake, familia
na jamii yake na pahala pa kusemea ni katika Baraza la Kutunga sheria,
kwa jina lolote liwalo, lakini hapa kwetu ni Baraza la Wawakilishi
(Baraza) na katika picha kubwa ya Tanzania ni Bunge la Jamhuri ya
Muungano (Bunge).

Ni kupitia katika Baraza na au Bunge ndipo sauti hizo za matakwa ya
wananchi zitafikishwa Serikalini, iwe ya Zanzibar au ya Muungano,
kupitia vinywa vya wawakilishi wa wananchi au japo vitendo vyao.

Wao ndio waunganishi wa umma na serikali, na kufanya kazi vyema kwao
ndio kuwa na Serikali imara, na kulegalega kwao ndio kuwa na Serikali
lege lege na isio wajibika kwa wapiga kura. Iwe hapa kwetu Zanzibar,
Tanzania au pengine popote pale.

Ingawa kwa utaratibu wetu wa Zanzibar na Tanzania kila mgombea wa
uwakilishi na ubunge lazima awe ni mwanachama wa chama cha siasa
lakini katika baadhi ya nchi hilo haliko hivyo.

Juhudi zimeshaanzwa kufanywa hapa kwetu kuwa kama kuna uhuru wa mtu
kuteuliwa na chama kuwa mgombea, basi pia uwepo uhuru wa mtu
kujidhamini mwenyewe ili awe mgombea ubunge au uwa kilishi maana hata
yeye lengo ni kutumikia wananchi.

Na mifano ya wagombea huru ipo mingi na mengine ni ya kupigiwa mfano
kama ule wa Meya wa London Ken Livingstone ambaye baada ya kutemwa na
Labour alikuwa mgombea huru na akashinda na kushikilia Umeya wa jiji
hilo kubwa kwa vipindi viwili.

Lakini itoshe kuwa hapa kwetu ni mgombea wa chama na chama kinachukua
sehemu ya jukumu na dhamana ya kwamba mgombea wake akishinda atatumia
muda wake, akili yake na uwezo wake kutumikia jimbo kwa sababu watu wa
jimbo wanampa mamlaka ya kuwatumikia.

Mamlaka kama hayo wamepewa wajumbe 50 wa nafasi za ubunge na
uwakilishi wa majimbo 50 ya Unguja na Pemba na nafasi hizo zimegawika
kwa vyama vikuu viwili vya CUF na CCM. CUF ikishinda viti 22 na CCM
28.

Si haja ya makala hii kuchambua viti hivyo viligawika vipi katika
mwaka wa uchaguzi wa 2010 wala kutizama mgawanyo huo kiutawala
unakwenda vipi kwa sasa
ila madhumuni ya makala hii ni kutizama nafasi ya Mbunge wa Jimbo la
Kitope ambaye pia ni Makamo wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd.

Hii ya 2010 haikuwa mara ya kwanza kwa Balozi Seif Idd ambaye muda
mwingi amekuwa nje ya nchi kushika nafasi hiyo ya Ubunge, na nafasi ya
kwanza naamini baada ya kutoka nje ilikuwa ni kushika nafasi ya Naibu
Katibu Mkuu wa CCM kwa upande wa Zanzibar.

Kuna taarifa za hakika kabisa kipindi cha 2005-2010 Balozi Seif Idd
alifanya kazi nzuri sana jimboni kwake kiasi ambacho hangeweza
kupingika na mtu yoyote katika uchaguzi wa 2010 na kila mtu anajua ni
rahisi kusema kuwa yeye anaweza kuwa ndio Mbunge bora kabisa kati ya
wabunge wote wa Unguja na Pemba.

Lakini baada ya kushinda ubunge mwaka jana, Rais Dk. Ali Muhammed
Shein akamuona anafaa kuwa Makamo wa Pili wa Rais, akimuacha mzoefu wa
miaka 10 Shamsi Vuai Nahodha na wengine wengi ambao angeweza
kuwachagua.

Tunaheshimu uamuzi wa Dk. Shein kwa sababu ni lazima alikuwa na sababu
za msingi kabisa kuacha kuchagua miongoni mwa wawakilishi 28 wa CCM
kumfanya mmoja kuwa Makamo wa Pili wa Rais, lakini akaamua kutumia
nafasi zake 10 za uteuzi.

Ni uteuzi mzuri kwa matokeo yake kama ambavyo tunamuona Balozi Seif
Idd anavyofanya kazi yake, lakini makala hii inaona athari kubwa ya
Balozi Seif Idd kuendelea wakati huo huo kuwa Mbunge wa Jimbo la
Kitope ambako wananchi wana imani nae.

Sijaambiwa wala sijatumwa lakini naona wananchi wa Kitope hawatendewi
haki na Balozi Seif Idd kwa sababu hawawakilishi ipasavyo katika Bunge
kwa kuwa muda mwingi anakuwa katika Baraza la Wawakilishi ambako yeye
ni Mkuu wa Shughuli za Serikali.

Lakini pia ikitokezea kuwa Balozi Seif Idd anakwenda Bungeni basi
gharama kubwa hutumika kumpeleka yeye na msafara wake wa zaidi ya watu
10 kwa cheo chake cha Makamo wa Pili, na naambiwa gharama kama hiyo
huweza kufikia shillingi millioni 60.

Kutumika pesa hizo za walipa kodi nafikiri ni kuwadhulumu walipa kodi
kwa jambo ambalo si lazima. Si lazima kwa sababu hakuna haja ya Balozi
Seif Idd kuendelea kushikilia nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Kitope
ilhali hana nafasi ya kuhudhuria vikao vya Bunge kama inavyostahiki.

Ingekuwa fedha hizo wanazitoa watu wa jimbo lake sawa, lakini fedha
hizo zinatoka katika mfuko mkuu wa Serikali, nadhani Balozi Seif Idd
angemsaidia Rais na Serikali kwa kuiwacha nafasi hiyo na igombewe na
watu wengine na nikiamini kuwa jimbo hilo ni salama kwa CCM kushinda
tena.

Lakini pia nina wasi wasi na heshima ambayo Balozi Seif Idd anaweza
kuipata katika Bunge kama Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, maana
kule Bungeni yeye anaingia kama Mbunge, na Sheria ya Bunge haimtambui
kuwa yeye ni Makamo wa Pili wa Rais.

Inawezekana kabisa akajikuta katika nafasi ngumu na hata kuvunjiwa
heshima, kwa kuwa tumeona hata Waziri Mkuu ambaye ni Mkuu wa Shughuli
za Serikali ya Muungano akipata wakati mgumu, seuze yeye ambaye hana
itifaki yoyote zaidi ya ile ya Ubunge nay a Umakamo wa Pili inaishia
katika mlango wa kuingia ukumbi wa Bunge.

Tayari Zanzibar ina wabunge wa kutoka majimbo, ina wabunge wa viti
maalum wa CUF na CCM na pia ina wabunge ambao ni kutoka Baraza la
Wawakilishi, si lazima tena kuwa na Mbunge wa Jimbo la Kitope kwa sifa
tu kuwa nae pia ni Makamo wa Kwanza wa Rais.

Sidhani kuwepo kwake Bungeni kuna msaada wowote kwa Serikali ya
Zanzibar kwa maana ya kuisemea Zanzibar, maana hataulizwa wala
kutakiwa kutoa kauli kuhusu Zanzibar, na wala hakuna fursa kama hiyo,
na hivyo Serikali ya Zanzibar kumlipia gharama za kwenda Bungeni ni
ufujaji au utumiaji mbaya wa fedha za umma.

Ushauri wangu kwa Balozi Seif Idd ni kuwa wakati umefika wa kufanya
maamuzi kwa maslahi ya watu wa jimbo lake, chama chake, Serikali yetu
na nchi yetu. Kushikilia nafasi hiyo hakusaidii jimbo, chama chake,
Serikali na nchi yetu.

Naamini Balozi Seif Idd sio katika watu wanaodhani kuwa kuendelea
kushika nafasi hiyo kutampa fursa ya pensheni ya mkono wa kulia kama
Makamo wa Pili na ya kushoto kama Mbunge, maana Balozi Seif Idd ni
muungwana na mzalendo wa kweli aliyeweka utumishi wa wananchi kuwa ni
jambo la mbele.

Msaidie Rais, isaidie Serikali na saidia nchi, lakini kubwa ni
kuonyesha mfano utaoingia katika rekodi, si Zanzibar na Afrika bali
duniani.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s