Mifuko ya plastiki ni marufuku

ZANZIBAR imo hatarini kukabiliwa na janga kubwa la uharibifu wa mazingira ya bahari iwapo kasi ya uingizaji mifuko ya plastiki itaendelea, serikali ilionya jana.Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar , Fatma Abdul-Habib Fereji aliwaambia wanandhishi wa habari mjini hapa kuwa ingawa serikali imepiga marufuku miufuko hiyo, bado inaingia visiwani humo kupitia njia za panya.

Alisema mifuko hiyo ina madhara makubwa inapoishia baharini ambako inaweza kuathiri samaki na mazalio yao pamoja na viumbe wengine ikiwa ni pamoja na matumbawe, mwani na mikoko.

Juu ya madhara ya mifuko ya plastiki inayoishia baharini visiwani Zanzibar , Waziri Fatma alisema inahatarisha afya ya binadamu kwa kula samaki wanaoathirika kwa kemikali zitokanazo na mifuko wanapoimeza.

Alisema uharibifu wa mazingira unaosababishwa na mifuko inayoishia baharini pia unavuruga mwenendo wa uchumi wa wananchi, ambao maisha yao yanategemea shughuli ya uvuvi.

“Asilimia 20 ya wakazi wa Zanzibar wanaishi kwa kutegemnea sekta ya uvuvi, jambo lolote linalosababisha uharibifu wa mazingira ni hatari kwa uchumi wao na taifa kwa jumla,” alisema Fatma.

Alisema udhibiti wa uingizaji na matumizi ya mifuko ya plastiki, unahitaji ushiriki wa jamii, wakiwemo viongozi wa dini ni ikiwa ni kuwaepusha wananchi na madhara kama vile ya maradhi ya kansa.

“Mifuko ya plastiki inapochomwa bila vifaa maalum inatoa moshi wenye sumu ambayo inaweza kusababisha maradhi kama kansa kwa binadamu,” alionya.

Alisema wanaoathirika na uchomaji wa mifuko ya plastiki kuwa ni pamoja na wananchi wanaovuta moshi unaotokana na takataka zinazochomwa katika majaa yasiyorasmi katika makazi ya watu, zikiwa zimechanganyika na mifuko ya plastiki.

Akitoa mfano wa madhara ya mifuko hiyo kwa wakazi wa California , Waziri Fatma alisema wanaathirika kwa kutumia samaki wanaopatikana kwenye bahari ya Pacific ambao kwa mujibu wa utafiti wanameza wastani wa tani 24,000 za plastiki kila mwaka.

Kuhusu hgatua za kudhibiti uingizaji wa mifuko hiyo visiwani Zanzibar, Fatma alisema ofisi yake kwa kushirikiana na Idara ya Polisi, Mkurugenzi wa Mashtaka na KMKM, vimekamilisha kazi ya kuangalia upya sheria ili kuiongezea makali ili kuzuia uingizaji, matumizi na utupaji wa mifuko ya plastiki.

Alisema ingawa utekelezaji wake ni mdogo, amri ya kupiga marufuku uingizaji na matumizi ya mifuko hiyo Zanzibar , haijaondolewa na kuonya kwamba uwepo wa mifuko hiyo mjini Zanzibar umeongezeka zaidi wakati huu mfungo wa Mwezi wa Ramadhani unaoendelea.

Alisema wakati serikali inaendelea kuboresha sheria ya kupambana na tatizo hilo , juhudi ya kutoa elimu kwa umaa inaendelea katika maeneo mbali mbali, na kuwataka viongozi kushiriki katika kufanikisha zoezi hilo .

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s