Mapinduzi ya kilimo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wa awamu ya sita, Dk Amani Abeid Karume akivuna mpunga katika msimu wa mavuno huko katika shamba la mpunga la serikali Cheju.

Mpango wa kuleta mapinduzi ya kilimo muafaka!

Kalamu – 27 Julai 2011

NIMEFARIJIKA sana kusikia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa (SUK) inaamini mapinduzi kwenye sekta ya kilimo.

Nimevutwa na mkakati wake wa kusaidia wakulima hasa wa mazao ya chakula, ikiwemo mpunga ambao chakula chake – wali – ndio chakula kikuu cha watu wa Zanzibar .

Kwa miaka mingi, wakulima wa Zanzibar wamekuwa wakishiriki shughuli za kilimo wakiwa wakiwa. Ingawa serikali kila wakati huahidi kusaidia pembejeo, mbegu bora, zana na utaalamu, ahadi hizo zinabakia maneno.

Serikali ilifundisha vijana wengi fani mbalimbali za kilimo, lakini kwa miaka mingi ilishindwa kuwawezesha na hivyo kushindwa kuwafikia wakulima mashambani.

Ule mkazo uliokuwepo hadi mwishoni mwa miaka ya 1980, wakati serikali ilipotekeleza Mpango wa Taifa wa Kuzalisha Chakula cha kutosha (MTAKULA), mabwana shamba waliishia ofisini na siyo mashambani waliko wakulima wanaohitaji msaada.

Wale waliogharamiwa na serikali katika kozi mbalimbali za kilimo waliishia kuendeleza mashamba ya mfano tu. Kutosaidiwa kwao kuliwavunja moyo na wengi wakakimbilia sekta binafsi. Baadhi yao walitafuta kazi Bara na wachache wakaenda nje ughaibuni.

Matokeo ya wimbi la wataalamu wa kilimo kubadilisha kazi na kutowezeshwa kutumikia wakulima, ni kushuka sana kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara Zanzibar .

Uzalishaji wa mpunga uliokuwa ukifadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ulififia baada ya wafadhili kutoka Ulaya kujitoa kuisaidia SMZ kutokana na shutuma za serikali kuharibu uchaguzi mkuu wa mwaka 1995.

FAO ilikuwa ikifadhili uzalishaji wa mbegu za mpunga wa umwagiliaji; Uholanzi ikisaidia sekta ya usimamizi na hifadhi ya mimea, na Finland ikisaidia uendelezaji wa misitu.

Japan ikisaidia kilimo cha mpunga unaotegemea mvua hasa katika Bonde la Cheju .

Wakati hadi miaka ya mwisho 1980 Zanzibar ikimudu kuzalisha angalau asilimia 30 ya mahitaji yake ya mchele, utegemezi wa zao hilo uliongezeka kwa kiwango kikubwa mpaka kipindi hiki.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa kwa sasa kuna upungufu wa tani 64,000 za mchele kwa mwaka katika mahitaji halisi ya tani 80,000. Maana yake, ni tani 16,000 tu za mchele zinazalishwa Zanzibar .

Ili kuondokana na takwimu hizi zinazotafsirika kwa asilimia 15 tu ya mchele unaozalishwa ndani ya nchi, serikali mpya (SUK) imekuja na mpango wa kuongeza uzalishaji wa mchele ili kupunguza utegemezi wa mchele unaoagizwa kutoka nje.

Waziri wa Kilimo na Maliasili, Mansour Yussuf Himid aliliambia Baraza la Wawakilishi alipokuwa akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara hiyo wiki iliyopita kwamba wanakusudia kuinua kiwango cha uzalishaji hadi kufikia asilimia 65 ya mahitaji ifikapo mwaka 2015. Muafaka!

Anasema serikali itafidia nusu ya gharama za pembejeo (mbolea na madawa) na zana za kilimo ikiwemo matrekta. Ina maana pale trekta linapokodishwa kwa Sh. 100,000 serikali imeahidi kutoa Sh. 50,000 kumsaidia mkulima.

Pia itasimamia kwa nguvu ukomeshaji wa wizi wa mazao ya mashambani, tatizo linalokua kwa kasi kubwa Zanzibar . Wakulima wa mazao ya nafaka wamekuwa wakilalamikia tatizo hili kwamba linashusha morali yao .

Mazao ya nafaka yamekuwa yakitegemewa sana kama chakula mbadala ya wali na ndio mazao tegemeo kwa futari wakati wa mgungo wa Ramadhani utakaoanza mapema wiki ijayo.

Msiba wa Mwakiteleko

Niseme kweli, sikupata nguvu kujikita kulijadili hili. Kwa siku nne sasa, akili yangu imeguswa mno na ugonjwa na hatimaye msiba wa mwandishi Daniel (Danny) Mwakiteleko.

Tukio hilo lililotokana na ajali ya gari aliyopata usiku wa Jumanne, Julai 19, wakati akitoka kazini kwake Sinza kurudi Tabata Chang’ombe, limegusa sana wanahabari na washirika wake.

Danny, kijana mwenyeji wa kijiji cha Mwakaleli, Rungwe, mkoani Mbeya, ni mmoja wa waandishi mahiri niliopata kufanya nao kazi kampuni ya Business Times Limited (BTL), mtaa wa Lugoda, eneo la Gerezani, Dar es Salaam .

Alikuwa hodari wa kazi, mchangamfu, mshirika mzuri, mtulivu wa akili na mtu ambaye alikuwa rafiki kwa kila mtu. Akipenda sana wale waliokuwa karibu naye katika kazi.

Anayemfahamu vizuri Danny, atathibitisha hapa kuwa si kwamba namsifu kwa sababu ya kumsifia tu kwa vile hatunaye tena. Hakika, alikuwa mtu mwema sana .

Danny alikuwa mmoja wa memba wa kikosi kabambe cha waandishi waandamizi tuliokuwa mfano wa timu imara ya BTL tukitambua wajibu wetu kitaaluma kwa taifa.

Alinikuta tayari gazeti la Majira alipofika yeye na Jesse Kwayu mwaka 1997. Haikuchukua muda mrefu, wakajitokeza kuwa ni waandishi wakubwa kwa maana ya uhodari wa kazi na vile walivyofanikiwa kutoa mchango uliotakiwa wakati ule.

Danny alijaaliwa kipawa cha kuzungumza kila kitu huku akitabasamu. Nasema kila kitu hata kile ambacho kwa wengine kilisababisha uchungu. Akijulikana sana kwa utamaduni wa kutaniana na kila mtu.

Alichukulia kila kitu kwamba ni cha kawaida na kama ni tatizo, basi laweza tu kutatuka. Ni hapa alipokuwa tayari kutoa mchango wake ili kupatikana ufumbuzi wa tatizo.

Alikuwa mmoja wa wahariri waliokuwa tukipanga na kuamua nini cha kukaa mbele gazetini, nini cha kufichwa ndani na katika nafasi nduchu, na nini cha kusubiri kesho.

Danny alikuwa mjuzi wa kutoa vichwa vya habari. Kwa sifa hii, alimkaribia Masoud Sanani katika wale waandishi waliounda “kikosi kabambe cha wanahabari” ndani ya BTL.

Wengine nawakumbuka Jacqueline Liana (Naibu Mhariri Mtendaji, Uhuru), Danny Mwaijega (Mhariri, Mwananchi Jumapili), Joseph Kulangwa (Mhariri Mkuu, HabariLeo) chini ya aliyekuwa Mhariri Mkuu wetu, Theophil Makunga ambaye sasa ni Mhariri Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL).

Acha Makunga ambaye kwa nafasi yake hakuwa na muda sana wa kutoka na waandishi waliokuwa Majira, tuliobaki pamoja na Danny, tuliwahi kupanga kuanzisha gazeti letu kwa kuweka akiba japo kiasi kidogo cha fedha kila mwezi. Ndoto ile haikufanya kazi.

Danny, aliyezikwa jana kijijini kwao, atakumbukwa kama mwanataaluma mahiri aliyetutoka kabla ya kutimizwa kwa ile dhamira ya taaluma ya habari – kuwa na jamii iliyo sawa kiuchumi. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake pema – AMIN.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s