Vyombo vya habari na serikali

Ally Saleh akitoa mada katika semina ya siku mbili kwa waandishi wa habari

Kwa kuwa kila tabaka lilitafuta nusura yake nao Waafrika wakaingia kilingeni kuchapicha magazeti na mtu wa kwanza akawa Mtoro Rehani Kingo hapo 1948 na Afrika Kwetu na kufuatiwa na magazeti ya Agope, Kipanga na Mwiba katika msururu wa mengi.Katika miaka ya 50 kukaja megnine mengi lakini baadhi yao yalikuwa ni Adal Insaf, Agozi, Sauti ya Jogoo, Umma, Vanguard, The Worker ambapo wakati huo mengi hayakuweza.
MADA: WAJIBU WA VYOMBO VYA HABARI NA WAANDISHI WA
HABARI KATIKA KUIMARISHA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA

MADA KUU: NAFASI YA VYOMBO VYA HABARI KATIKA KUIMARISHA
SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA ZANZIBAR

WAANDALIZI: TAASISI YA UTAFITI NA ELIMU KWA DEMOKRASIA
TANZANIA (REDET)

UKUMBI :

TAREHE:

MTOA MADA: ALLY SALEH

Utangulizi

Na Ally Saleh

Dhana ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa sio ngeni Zanzibar kwa sababu iliitokeza kwa mara ya kwanza mara baada ya Uchaguzi wa 1963 ambao ulikuwa na lengo la kutafuta chama ambacho kitaunda Serikali ya Uhuru. Lakini vyama wakati huo vilishindwa kuafikiana.
Ilikuwa ni baada ya kutotokea chama ambacho kilipata ushindi wa moja kwa moja katika uchaguzi huo ambao ulikuwa ni wa 4 chini ya Utawala wa Kiingereza na hivyo Afro Shirazi Party (ASP) kuwa na nafasi sawa na Zanzibar Nationalist Party (ZNP) lakini huku chama cha Zanzibar and Pemba Peoples Party (ZPPP) kikiwa na karata ya turufu.
ASP haikuwa tayari kujaliza viti vya ZPPP ili ipate wingi wa viti na kuunda Serikali kwa kutofautiana kimtizamo na huku pia ZPPP wakiwa wazito kufanya ubia na ASP kwa sababu moja wapo ya uhasimu wa ndani ikikumbukwa kuwa ZPPP ilikuwa ni pande lilogawika kutokana na ASP.
Matokeo ya mgando huo ikawa ni ZNP kupewa viti vya ZPPP na kuunda Serikali huku kukiwa na kilio cha ASP kwamba mfumo wa uchaguzi ulilalia kuisaidia ZNP ambayo ilipata viti vingi kwa kura kidogo za wananchi. Uhuru ukatolewa Disemba 10,1963 na ZNP-ZPPP wakaunda Serikali na ndio ikawa sababu ya kuja Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
Pili fursa ya uwezekano wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni baada ya Mapinduzi hayo ambayo lengo lake ni kumaliza dhulma na upendeleo, lakini kinyume chake yakageuka kuwa baguzi na kandamizi na kuwatenga wananchi wote isipokuwa wale waliokuwa ASP na kidogo Umma Party kwa madhumuni ya kistratejia tu na kidogo kidogo Umma Party ikapigwa kumbo na wananchi wa vyama vyengine vyote hawakuambua kitu.
Fursa nyengine ikajitokeza baada ya Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi wa 1995, baada ya mfumo huo kurudishwa 1992, kutokana na mapendekezo ya Tume ya Jaji Francis Nyalali, ambapo CCM chini ya mgombezi Dk. Salmin Amour ilishinda kwa tofauti ya kura asilimia 0.4 dhidi ya Maalim Seif Shariff Hamad wa CUF na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere akashauri kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini wazo likapigwa teke.
Matokeo ya kulikataa wazo hilo ni chaguzi zenye utata za 2000 na 2005 na kuzalisha ukandamizaji mkubwa wa haki za kiraia, mauaji, uhasama, ukimbizi na kukwama kwa maendeleo katika Visiwa ambavyo siku zote vimekuwa vinataka sababu ndogo tu ya kuripuka kisiasa kwa maumbile ya watu wake kuwa na siasa katika damu zao.
Wakati hayo yakiendelea waandishi wa habari wamekuwa wakisokotwa humo ndani. Wakivutwa kila upande, wakishawishiwa kila upande na kwa hivyo mizania yao kupotea kwa baadhi ya muda na kwa baadhi ya wakati wakivutwa na hisia zao za kisiasa zaidi.
Lakini sio kwamba fani ya habari imekuwa dhaifu wala sio kama haina mashiko katika jamii ila ukweli ni kuwa waandishi wa habari wa Zanzibar wamekuwa ni makini na wachunga maadili ukitoa nyakati chache za kuteleza na hiyo inatokana na historia refu ya kuanzishwa kwake na majaribu na ndio maana pamoja na kuteleza waandishi wa habari wa Zanzibar hawakuwahi kufikia kuwa ni chanzo cha migogoro kama ambayo imeonekana Kenya na Rwanda na ndio maana pamoja na uhasama wote wa kisiasa wa Zanzibar mchango wa waandishi hauwezi kutajwa kuwa umesaidia sana kuchochea.

Historia ya Vyombo vya Habari Zanzibar
Zanzibar imekuwa na historia tajiri sana ya vyombo vya habari sio tu kwa sababu ilitangulia nchi zote za Afrika Mashariki na Kati, lakini pia kwa sababu ya kuwa na utamaduni wa kusoma na uthubutu wa waandishi wake.
Kutokana na Zanzibar kuwa na uhusiano wa kale na nchi mbali mbali kama vile kuwa na mwakilishi wake Ahmed Bin Nu’man, wananchi wa visiwa hivi walianza kusoma mapema magazeti kutoka Jimbo la Masachusettes nayo ni kama vile Salem Gazette (1827-1880) na rEssex Register (1820-1840).
Huwezi kuizungumzia historia ya vyombo vya habari vya Zanzibar bila ya kumtaja Mfalme wa Pili wa Zanzibar Seyyid Barghash bin Said kwa hatua yake ya kuamua kuleta mtambo wa kwanza wa uchapishaji hapo 1875 hapa Zanzibar mtambo ambao ndio ukawa chachu ya fani hiyo kukolea.
Chapisho la mwanzo liloingia katika rekodi ni lile la Msimulizi (1888) ambalo lilikuwa ni la watu waliotoka utumwani na ambao walitamani kuweka njia ya mawasiliano na sehemu zao za asili kama vile Congo, Malawi na Tanganyika ambako ndiko walikotoka na wengi wakiamu kulowea Zanzibar ama kwa kukombolewa au baada ya kumalizika utumwa. Chapicho hili lilikuwa chini ya kanisa UMCA na kuhaririwa na Swithun Ulumana. Ukurasa wa pili wa toleo hilo la mwanzo Oktoba 1888 ulikuwa na maoni haya ya Mhariri:
“ Killa miezi miwili tumepewa ruhusa ya kukusanya habari za hapa Unguja, ndio za Mkunazini na Mbweni na Kiungani, na kupata pia habari za pande za Boonde na za Nyassa na za Newala na miji ya kule, na kuzipigia chapa hapa Kiungani na kuzifanya kuwa kitabu kidogo, killa miezi miwili kitabu kipya, na kuchanganya nazo habari za kazi za Upelekwa mgine, kama habari za ndugu zetu kule Mwita ao pangine kwa kadiri kutakavyojaliwa kuzipata, na kutia pia habari yoyote itakayowapendeza mskikie. Na kitabu hiki kitakachopigwa chapa killa miezi miwili kitawaletea habari zetu mpya na za ndugu zetu za pande zote. Killa miezi miwili habari ngine. Tena kwa kuwa kitabu hiki kama kitatusimulia habari za ndugu zetu killa mahali.”
Serikali ikafanya umakusudi wa kuwa na machapisho yake wenyewe ili kuwasiliana na umma na ndipo machapisho mawili yakaanzishwa kwa madhumuni hayo na ndipo ikatoa magazeti ambalo lilianzishwa February 1892 kwa ajili ya kutumikia Zanzibar na Afrika Mashariki na likapewa jina la The Gazette of Zanzibar and the East African. Magazeti mengine yaliokuwa chini ya Serikali yalianzishwa mwaka 1918 na yalikuwa ni pamja na Mkulima ; Produce Market Report, Quaterly Market Report na Monthly Trade Information
Katika historia ya magazeti ya Zanzibar mwaka 1902 hautasauhaulika kwani ndipo gazeti la kwanza rasmi na la binafsi lilipoanzishwa na lilikuwa kwa jina la Samachar na lilichapishwa kwa lugha ya Gujerati na ambapo lilikuwa na kurasa 30 na inaeleweka lilikufa 1968. Lilofuatia baada ya hapo ni lile liloitwa jina la Ruta kuigiza jina la Shirika la Habari la Kiingereza Reuters na ambalo lilanzishwa wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza 1914-1918 na Mhariri wake akiwa Khalili Ali Khalil.
Gazeti lilopata umaarufu sana kwa wakati wake na kusomwa kwa wingi lilikuwa ni lile la Mazungumzo ya Waalimu ambalo sio tu lilienga sekta maalum lakini lilikuwa na utamu mkubwa wa lugha ya Kiswahili na makala nyingi za kupanua akili.
Rekodi zinaonyesha kuwa gazeti la kwanza la kila siku lilikuwa ni lile la The Zanzibar Voice liloanzishwa 1922 na kuchapishwa kwa Gujerati na Kiingereza na lilikuwa likichapishwa nakala 400 hadi 700. Gazeti la kwanza lilochapishwa kwa lugha ya Kiarabu likawa ni Al Falaq hapo 1929 lakini pia likawa linatolewa kwa lugha ya Kiingereza.
Serikali ikarudi tena ulingoni 1939 kuanzisha magazeti yake na mara hii ikiwa ni chini ya Idara ya Habari na ambapo magazeti hayo yalikuwa ni ya kila siku, kila wiki na kila mwezi na yalikuwa na majina yanayofanana na utoaji wake kama hivi: Daily News Bulletin, Habari za Wiki na Monthly Newsletter.
Mwaka huo huo wa 1939 likaja gaeti la Ali Khalil la The Zanzibari was na likajikita eneo
La kijamii na kutoa hadi nmakala 1,000 na Ahmed Kharusi ilipofika 1941 akatoa gazeti la
Kiswahjili Mwongozi na Jumuia ya Kiislamu hapo 1945 ikaja na gazeti kwa jina la Zanzibar
Times.
Kwa kuwa kila tabaka lilitafuta nusura yake nao Waafrika wakaingia kilingeni kuchapicha
magazeti na mtu wa kwanza akawa Mtoro Rehani Kingo hapo 1948 na Afrika Kwetu na
kufuatiwa na magazeti ya Agope, Kipanga na Mwiba katika msururu wa mengi.
Katika miaka ya 50 kukaja megnine mengi lakini baadhi yao yalikuwa ni Adal Insaf,
Agozi, Sauti ya Jogoo, Umma, Vanguard, The Worker ambapo wakati huo mengi hayakuweza
kuficha misimamo yao ya kisiasa katika wakati ambapo harakati za kupigania uhuru zikiwa ndio
zinaanza.
Shirika la mwanzo na pekee la habari la Zanzibar lilikuwa ni ZANEWS liloanzishwa mwaka
1963 na Chama cha Kwanza cha Waandishi wa Habari Zanzibar kilikuwa ni AZJO kiloanzishwa pia mwaka 1963 hadi chama chengine kilipopata uhai kwa jila la JAZ hapo 1989 miaka 10 tokea ilpotajwa chini ya Sheria ya Magazeti ya 1989.
Baada ya Mapinduzi ya 1964 ambayo yalisitisha utawala wa Kikatiba magazeti yaliyokuja kaunzishwa yalikuwa na milki ya Serikali nayo ni pamoja na Kweupe (1964), Ukweli Ukidhihiri (1970) na nakala ya Kiingereza ikaitwa When Truth Prevails na baadae kugeuka kuwa Nuru (199) na mwisho kama ilivyo hivi sasa Zanzibar Leo.
Kwenye magazeti binafsi tunakumbuka Jukwaa (1995) na baadae kuja Dira (2002) tambalo likapigwa marufuku na Serikali baada ya kuchapishwa kwa mwaka mmoja tu na kasha likaja Asumini la Muhammed Sif Khatib na pia tukashuhudia gaeti jengine kwa jina la Zanzibar leo ambalo lilianzishwa asubuhi ilipofika mchana likafa hili ni Zanzibar Daima.
Kwenye vyombo vyengine Radio Zanzibar ilikuwa ya mwanzo kuanzishwa 1951 na Televisheni ikanzishwa 1973 lakini radio binafasi ziliopo hivi sasa zimeanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 2,000 na maarufu kati ya hizo ni Coconut, Hits, Zenj na Chuchu na zikiwepo pia za Kiislamu kama Annur, Istiqama na radio ya Kikristo Maria.
Zanzibar ina sheria mbili zinazogusa vyombo vya habari moja kwa moja nazo ni ya Utangazaji ya 1997 pamoja na mabadiliko yake na ile ya Magazeti na Machapisho ya 1989 lakini pia ina sera kamilifu ya Vyombo vya Habari ambayo ilipitishwa hapo 2008.
Uhusiano Vyombo vya Habari na Jamii
Kwa muda wote vyombo vya habari hapa Zanzibar vimekuwa karibu sana na jamii. Jamii siku zote pia ndio imekuwa na sauti katika uchapishaji na usambazaji wa magazeti ambao kwa sehemu kubwa ndio ambao ulikuwa njia kubwa zaidi ya kupata na kupashana habari.
Sababu za uhusiano mzuri baina ya jamii na vyombo vya habari vya binafsi na hata vya umma ni nyingi. Na nyingi katika hizo zina mizizi mirefu na ndio maana katika umri wa vyombo vya habari vya Zanzibar pamoja na wingi wake lakini bado kumekuwa na kesi kidogo sana za watu kukashifiwa na kufungua kesi katika Mahakama.
Tunaweza kusema sababu ya kwanza ni kuwa kwa mdua mrefu magazeti hapa Zanzibar yalikuwa ama ni miliki ya familia au mtu binafasi ambapo tumetangulia kuona majina maarufu kama ya Khali, Kharusi, Rehani lakini hata kina Abdula Amour walifikia kuwa na magazeti na mtu mmoja mmoja wakiwa ni wamiliki wake.
Pili, magazeti ya Zanzibar yamekuwa mara nyingi yakijikita katika kufuata sera na maadili yake na ya jamii na kwa hivyo hadi hivi leo gazeti likichapishwa Zanzibar ni ambalo linaweza kusomeka ndani ya nyumba na mtu wa kila rika na kwa hivyo linapendeza na kukubalika.
Tatu, ni kwamba ukuruba na uhusiano wa watu ndani ya jamii ambayo imekuzwa zaidi katika maadili ya Kiislamu, unazuia mikinzano mikubwa ya kijamii iwe ya kisiasa, kirasilmali na kiuchumi na kwa hivyo katika mioyo ya wachapishaji siku zote kuna neno kiasi, ambalo ni mtu kujua ukomo wa jambo na kujali kutomuumiza mwengine.
Hata wakati wa kipindi cha mivutano mikubwa ya kisiasa katika miaka ya 50 na 60 na pia kujirudia katika miaka ya 90 na 2000 kulikuwa na kiasi fulani cha aina ya uchapishaji. Na jinsi makala za kukashifiana na kuvunja staha ya jamii zilivyokuwa chache watu walioshi moja ya nyakati hizo watakuwa wanazikumbuka.
Lakini pia watu kama hao watakuwa pia wanakumbuka jinsi ambavyo waandishi waliovuka mipaka walivyotupiwa jicho baya na jamii na ikawa ni rahisi kwa magazeti yao kutokudumu kwa kutoweza kukubalika na jamii ambayo wanaitumikia.
Mfano wa sasa wa vyombo vya habari vya eletroniki ni wa kati na kati kuhusiana na mahusiano na jamii. Wakati vyombo hivi vimeongeza kasi ya upatikanaji wa habari ndani ya umma, lakini suala la mahusiano limekuwa na mtihani wake kwa kiasi fulani kwa sababu mbili.
Ya kwanza ni ya vipindi vyake ambavyo wakati mwingine vinakwaza usikilizaji na utazamaji kwa vile vinaonyesha picha za matusi au mazungumzo ya matusi na wakati mwengine wakati wa mchana ambao pia kuna wasikilizaji wa umri mdogo na hivyo kuharibu hali ya hewa ndani ya jamii.
Sababu ya pili ya kutia mushkeli wa uhusiano baina ya vyombo hivyo na umma ni matumizi ya lugha. Wengi wa watangazaji hawa si watu walioshiba lugha ya Kiswahili sawa sawa na hivyo kuwakirihi baadhi ya wasilizaji kwa upotofu wa lugha ilahli kisingizio mara nyingi huwa ni lugha inayokwenda na vijana na wakati na hilo sio lazima iwe ni kweli kwa sababu kila kipindi kina wasikilizaji wake ambao ni walengwa, lakini mambo ya msingi ya lugha lazima yabakie kama yalivyo.
Kwa ujumla vyombo vya habari vya Zanzibar kwa muda mwingi vimekuwa karibu na watu kwa kuandika yanayowahusu na kuwakereketa na kuweza pia kufikika na watu na hivyo kuwa kiungo kizuri baina ya wananchi na watawala. Hapana tofuati kubwa katika hili baina ya vyombo vya binafsi na vya serikali isipokuwa kwa kiasi fulani kuna mipaka ambayo vyombo vya serikali haviwezi kuivuka hata vikijaribu kuwa karibu na jamii kiasi gani na mifano ya vipindi vyake vilivyozimwa ni pamoja na Tuambie na Jicho la TVZ.
Vyombo vya habari na mgogoro wa 1992-2009
Mgogoro ni mchakato. Hauripuki tu kama mgogoro lakini kwanza huanza kama tukio, kisha kutofahamiana, kisha mzozo, uhasama na baadae kuwa mgogoro. Kwa maana nyengine mgogoro ni matokeo ya ukinzani wa muda mrefu ambao ama haujpatiwa suluhu au suluhu yake hairidhishi pande husika na hatua inayofuatata baaada ya mgogoro ni vita.
Kipindi cha mgogoro wa Zanzibar baina ya 1992-2009 ni matokeo ya muda mrefu. Ni tokea kuanza kwa siasa za ushindani hapa Zanzibar katika miaka ya 50 lakini wengine wanauweka mgogoro huo wa 1992-2009 pia unatokana na matokeo ya kijamii-kiuchumi yaliozaa biashara ya utumwa na baadae biashara ya mashamba makubwa na mwisho kabisa tatizo la ardhi hapa Zanzibar.
Lakini ni vyema pia tukakubali kuwa kipindi cha 1964-1984 kilikuwa pia ni kipindi cha mtihani amabacho kimechangia katika kukuza mgogoro uliokuja kuibuka kwa ghamidha 1992-2009 pale ilipokuja kupatikana sababu ya kurudishwa mfumo wa vyama vingi au ushindani wa kisiasa.
Miaka ya 50 na 60 vyama vilikinzana kisiasa na kwa hivyo ukabila na madhila ya historia kama vile utumwa, suala la ardhi likawa ni chachu ya kugawanya watu ambao pia waligawika zaidi mapande pale wengine wakiona wana haki zaidi ya kuitawala nchi kuliko wengine na wengine wakitaka uhuru uzuiliwe hadi mazingira yawe mazuri zaidi.
Yote haya yalijenga hasama kubwa ambayo kwanza ilijitokeza katika mapigano ya Juni 1961 ambapo watu 63 walifariki lakini pia kuja kwa mapinduzi ya 1964 kwa kuonyesha kuwa walio wengi hawakuridhika na kutolewa Uhuru wa Disemba 10, 1963 ambao Disemba 16, 1964 uliipa Zanzibar kiti katika Umoja wa Mataifa.
Ila Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ambayo yalikuwa na lengo la kuondosha dhuluma, chuki na ubaguzi na kulimaliza suala la tatizo la ardhi, yenyewe yakawa ni tatizo kubwa kwa kuwepo dhuluma, ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu pamoja na mauaji ya watu maarufu wakiwemo mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Pia Mapinduzi yakatengeneza mazingira ya mgogoro kuja kuibuka mbele kutokana na muda mrefu kukataa kuruhusu uhuru wa kujieleza, uhuru wa kujikusanya na hata uhuru wa kujiuunga na hata baada ya kuzaliwa katiba ya Zanzibar ya 1985, na kuhakikisha Haki za Binaadamu, bado baadhi ya mambo haya yakawa magumu katika uhalisia.
Kwa hivyo viliporudishwa vyama vingi 1992 basi Wazanzibari wakaingia katika zama hizo mpya wakiwa na vipakacha, vibahasha na vifurushi vyao walivyotoka navyo huko nyuma, iwe kabla au baada ya Mapinduzi kwa sababu Mapinduzi yalishindwa kuleta suluhu ya jamii na kwa hivyo siasa zikafanywa kama kwamba ni zile zile za miaka ya 50 na 60 na ndipo CCM ikawa ASP na CUF ikafanywa kuwa ni ZNP na ZPPP pamoja na mambo yakakorogeka.
Ikawa ni hasama kubwa kuanzia uchaguzi wa 1995, 2000 na 2005 kama ilivyotokea katika chaguzi za 1961 mara mbili na 1963 na kama ilivyotokea mapambano Juni 1961 basi pia kukawa na mapambano Januari 26-27, 2001 na watu zaidi ya 30 kuuawa na wengine zaidi ya 4,000 kuwa wakimbizi nchi Kenya na hata Somalia.
Naafasi ya waandishi na vyombo vya habari katika kipindi hicho ilikuwa ni ngumu sana. Wengi wakiwa ni vijana hawakujua yaliotokea huko nyuma na kwa hivyo wakajikuta wakitiwa kati na wanasiasa lakini pia wananchi wa umri mkubwa ambao walikuwa na wakiwatia vijiti vya masikio waandishi hawa na kuwajaza sumu za kiitikadi na kwa hivyo kujeng kada ya waandishi wa jazba.
Ulikuwa ni wakati ambao kila mwandishi alijiona lazima achague upande, na waliokataa kufanya hivyo wakawa hawaeleweki kwenye macho ya jamii. Wale waliokuwa katika vyombo vya umma wakawa na mtihani zaidi kwa sababu walilazimika kuwa upande wa chama kinachotawala na Serikali hata iwapo haikuwa ridhaa yao.
Kwa hakika waandishi walitiwa kati katika wakati ambapo kauli za kalbi kasi zilikuwa zikitoka kila upande na kufikia Wapinzani kususia kufanya kazi na Serikali lakini Serikali yenyewe ikiwakamata wapinzania kama mafungu ya panzi kubanbikizwa kesi kadhaa lakini pia ikiwemo kesi ya uhaini iliyovishwa wanachama 18 wa CUF. Mwandishi wa makala hii ni mmoja ya wananchi yaliyomkuta hayo.
Waandishi wa habari na Maridhiano ya 2009
Maridhiano kwa maana ya makubaliano basi yale ya Novemba 5, 2009 baada ya kupeana mkono Rais wa Zanzibar Amani Karume na hasimu wake mkuu wa kisiasa hadi wakati huo, Seif Shariff Hamad wa CUF, hayakuwa ya kwanza katika siasa za nguvu na magomvi za Zanzibar.
Muwafaka wa Kwanza yalikuwa ni yale ya 1999 ambayo yalifikiwa baada ya uingiliaji kati wa Jumuia ya Madola baada ya uchaguzi wa utata wa 1995 na Muwafaka wa Pili ukawa ni ule wa 2001 baada ya utata mwengine katika uchaguzi wa 2000 ambapo CCM ilichukua tena ushindi dhidi ya CUF.
Uchaguzi wa 2005 ukawa wa utata pia na Upinzani ukakataa matokeo kitendo ambacho kilifanya uendeshaji wa Serikali usiwe wa umakini sana kwa kukosa mchagno wa Upinzani na kusababisha Rais Jakaya Kikwete kuliambia Bunge la Tanzania kuwa utawala wake utapania kuumaliza mgogoro huo ambao unatia doa jeusi Tanzania.
Mazungumzo baina ya CUF na CCM ya miezi 14 hayakusaidia kuliondoa doa hilo, baada ya pamoja na vyama kukubaliana katika meza ya mazungumzo, lakini CCM ikaamua kuwa lazima suala hilo liamuliwe na wananchi katika hali ambayo Zanzibar wakati huo haikuwa na sheria inayohusu Kura ya Maoni wala sheria ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Ndipo Januari 2010 Kiongozi wa Upinzania katika Baraza la Wawakilishi Abubakar Khamis Bakary alipopeleka Hoja Binafsi katika Baraza hilo ili kuweka misingi ya kumaliza mgogoro wa kisiasa ambao ulikuwa mgumu zaidi baada ya Azimio la Butiama ambalo lilisababisha ukimya wa miaka miwili baada ya kumalizika mazungumzo ya CUF na CCM ya Bagamoyo.
Kwa kuwa nia ya kisiasa ilikwisha tandikwa kwa kukutana Maalim na Karume Nove 5, 2009 na kuja kile lilichoitwa Maridhiano, basi hoja hiyo ikapita kama kisu kwenye siagi na nia ya kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya kupigwa Kura ya Maoni ikawekwa.
Waandishi wa habari na vyombo vya habari vilifanya kazi kubwa wakati wa kipindi cha Januari 2010 hadi Julai 2010 wakati ndipo upishi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ulipokuwa chunguni. Baada ya Hoja Binafsi ya Abubakar Khamis Bakary kulikuwa na upitashaji wa Sheria ya Kura ya Maoni mwezi wa Machi ambapo ilifuatiwa na Mabadiliko ya 10 ya Katiba mwezi Agosti.
Waandishi walishiriki katika kuelimisha suala la Kura ya Maoni hasa ilivyokuwa hapakuwa na jukwaa rasmi la kufanya kampeni zaidi ya kazi iliyokuwa ikifanywa na Tume ya Watu Sita iliyokuwa ikiongozwa na Mh. Ali Mzee Ali. Kwa hakika Tume hii ilipata upinzani wa wazi kwa sababu iliaminika kuwa kulikuwa hakuna makubaliano ndani ya kambi ya CCM kinyume na kauli ya pamoja na ndani ya kambi ya CUF.
Makala kadhaa za radio, televisheni na magazeti ziliandaliwa; taarifa kadhaa kushawishi upigaji wa NDIO zilitolewa lakini pia matangazo ya aina kwa aina yalipita katika vyombo vya habari kushindana na kampeni ya siri na chini kwa chini iliyokuwa ikifanywa na waliokuwa wakipinga Maridhiano hayo.
Bahati mbaya sana kwamba wale waliokuwa na mawazo ya HAPANA katika kampeni hiyo hawakuwa na uwezo wa kujitokeza wazi na kwa hivyo maoni yao hayakusikika na kwa hili waandishi wanalaumika kwa kutotoa usawa, ingawa hata wangetaka kufanya hivyo ilikuwa ni vigumu.
Matokeo ya Kura ya Maoni kupitishwa kwa Kura za NDIO 66.2 na zile za HAPANA 33.8 yalithibitisha kazi kubwa iliyofanywa na vyombo vya habari lakini kazi kubwa ikafanywa na wana kada hiyo wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010 ambapo waandishi walijuizuia kabisa kuripoti kwa chuki, dhamira mbaya au upendeleo na matokeo yake ni kuwa na uchaguzi ambao kwa mara ya kwanza hata mwandishi wa habari mmoja hakukamatwa au kudhulumiwa kwa aina yoyote ile.
Hata wanasiasa walipoteleza, jambo ambalo lilikuwa ni nadra waandishi walijizuia kutoa habari za kejeli, kudharau sera za chama kimoja dhidi ya chengine na vyombo vya umma vikiibuka na alam nzuri katika kutoa nafasi kwa vyama, isipokuwa CCM iliendelea kupata fursa kwa sababu ya kuwa chama kilicho madarakani.
Waandishi na taarifa za SUK
Wananchi wengi waliweka matarajio makubwa wakati ilipokuwa ikiundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa vile vyama viwili vilivyokuwa vikivutana kwa miongo miwili na katika chaguzi tatu sasa vitakuwa pamoja kwa maslahi na maendeleo ya wananchi. Fikra mbili zilikuwa zikikinzana sasa zitafanya kazi na kufikiri pamoja.
Wananchi na waandishi wa habari wakatiwa moyo pia na kauli ya Rais wa Zanzibar Dk Ali Muhammed Shein katika hotuba yake ya kuzindua Baraza la Wawakilishi iliyoahidi uwazi na kushirikiana na vyombo vya habari na dhana ikawa kuanza kwa zama mpya za uwazi na kuhoji vitendo vya rushwa, ubabaishaji na kutokuwajibika ndani ya Serikali.
Kwa kiasi kikubwa waandishi wameendelea kuchombeza dhana ya umoja wa kitaifa kwa kuripoti matukio mbali mbali ya Serikali hiyo na hata kukubali kuipa muda Serikali hiyo ijipange kabla ya kuanza kuwa wadadisi zaidi juu ya utendaji wake.
Kinachoonekana hadi sasa ni kuwa hakuna kilichobadilika katika suala zima la utoaji na upatikanaji wa habari ambapo kwanza Serikali yenyewe haijachukua hatua ya makusudi kuimarisha vyombo vyake vya Televisheni, Radio na Idara ya Maelezo viwe imara ki-nguvu kazi na vifaa ili vitoe habari zake.
Pili, hapana mabadiliko yoyote juu ya mfumo wa utoaji habari kwa vyombo habari binafsi ambavyo siku zote vinawekwa nyuma au kuwa ni raia wa daraja la pili katika suala la kuwafikia Wanasiasa au Watendaji isipokuwa panapokuwa na ajenda maalum ambayo hiyo waandishi binafsi watatafutwa.
Tatu, Wizara kwa Wizara pamoja na kuwa na Maafisa Habari lakini hali ya upatikanaji wa taarifa haijabadilika kabisa kiasi ambacho Serikali inakalia taarifa zake nyingi na kuonekana kuwa haijafanya wajibu wake wakati ingeweza kujieleza kwa ubora zaidi na kuridhisha wananchi kinyume na inavyoonekana sasa watu wamekata tama nayo.
Suala la Serikali kukosa Msemaji Mkuu linaathiri sana mtiririko au uharaka au uhakika wa kupatikana habari kwa sababu sio rahisi kwa mwandishi kila mara kumfika Katibu Mkuu wa Wizara ambae au Waziri na hivyo habari nyingi hufa njiani bila ya kuwafikia wananchi au kukosa ufafanuzi baada ya kuingia mitaani kama uvumi.
Waandishi hawakuzuilika hata hivyo kuripoti habari hasi za SUK kama vile suala la ukodishwaji wa eneo la Starehe kwa ujenzi wa Hoteli ya Kempinsky; uamuzi wa Rais wa Zanzibar kuteua Majaji wa Mahakama Kuu ikidaiwa ni kinyume na utaratibu; ukodishwaji wa ukumbi wa disco wa Hoteli ya Bwawani kwa bei ndogo ya millioni 15,000,000 kwa mwezi wakati palikuwepo na mdau wa shs 35,000,000 kwa mwezi; ubadhirifu uliofanywa na Manispaa; ubabe unaofanywa na Manispaa kwenye eneo la biashara la Darajani pamoja na kudharau amri ya Mahakama na matukio mengi mengine.
Kwa hivyo katika kipindi cha tokea kuja Serikali ya Umoja wa Kitaifa waandishi wamefanya wajibu wao sawa sawa kwa kutangaza mafanikio ya SUK lakini pia hawakusita kuikosoa SUK kwenye maeneo ambayo imeonyesha udhaifu hasa kwenye utawala bora na uwajibikiaji

Waandishi na kujenga imani ya maridhiano
Katika eneo hili hapana shaka washiriki wake ni wengi. Ni pande nyingi ambazo kuja kwake pamoja ndiko kutaleta mafanikio na kama sivyo itakuwa ni bwabwaja ile ile ya kila siku na muda wa SUK utakwisha lakini hakuna kikubwa kitachokuwa kimeripotiwa zaidi ya habari za juu juu tu, ambazo mara nyingi si habari kitu zaidi ya kuarifu.
Pande zinazotakiwa kuwa pamoja ni kama ifuatavyo:
1. Serikali
2. Vyama vya Siasa
3. Vyombo vya Habari
4. Taasisi za Kijamii
5. Wananchi
Mkusanyiko wa pande hizi mbili ndiko kutakakosaidia kujenga imani ya Maridhiano na Serikali ya Maridhiano kuwa endelevu. Kuna mifano mingi ya Serikali za Maridhiano kuendeshwa kwa msukosuko na kuvunjika mapema au kama zimedumu si kwa mwisho mwema baina ya washirika wake.
Ingawa Zanzibar inajivuna kuwa muundo wa SUK yake ni wake peke yake kwa kuwa kwengineko serikali hizo zimeundwa baada ya watu kuingiana maungoni lakini ni ukweli pia kuwa na hapa hilo lilitokea ingawa tu makubaliano hayo yalitiwa katika Katiba kabla ya Uchaguzi Mkuu na kwa hivyo hapakuwa na hiari tena bali kutekeleza.
Lakini suala la kujenga imani ni la mchakato na dhamira. Dhamira ya nafsi na dhamira ya kisiasa ina umhimu mkubwa sana na mchakato huu lazima uwe mchakato mtakatifu kwa maana ya ule ambao watu wote wanauamini na wako tayari kuanza mwanzo na kuufikisha tamati yake.
Waandishi wa habari wana kuwa kati kati ya Serikali na Vyama vya Siasa kwa upande mmoja na kwa upande mwengine Taasisi za Kijamii na Wananchi kwa upande mwengine. Nafasi yao hii ya kutafsiri na kurudisha mchakato katika mstari kwa upande mmoja lakini kwa upande wa pili kukumbusha na kuhimiza dhamira binafasi na za kisiasa za wale wote wenye nafasi za maamuzi lakini hata wafuasi.
Kila wapatapo fursa itakuwa ni vyema kwa madhumuni haya waandishi kumkumbusha kila mtu kuwa nchi imo ndani ya kipindi cha Maridhiano na kila tofauti itakeazeapo itazamwe kama changamoto inayohitaji suluhu na sio ugomvi unaotarajiwa kuchochewa na kuleta mgawanyiko kwanza kwenye Serikali, kisha kushuka kwenye vyama na tabaa kuishia kwa raia.
Waandishi wajizuie kuchagua vyama na wajipange katika kuona wanahimiza ajenda za kitaifa ambapo Zanzibar inazo nyingi kama vile ilivyo na tunu nyingi za kitaifa kwa kujua kuwa miongo 7 ya siasa za uhasama umeipotezea Zanzibar mengi na si rahisi kuyapata yote yaliopotea bila ya kurudisha masikilizano na kufanya kazi kwa pamoja ijapo kupingana kwa kiitikadi.

Changamoto zinazowakabili waandishi
Changamoto zinazowakabili waandishi wa habari ni nyingi ambazo baadhi zimo ndani ya eneo la lakini nyengine ziko nje na kwa hivyo namna ya kukabiliana nazo na kuzipatia ufumbuzi itakuwa ni tofauti kabisa. Changamoto hizo ni kama ifuatavyo:
1. Kutoyaelewa Maridhiano kwa undani
2. Kutoielewa Katiba kikamilifu na maelekezo ya SUK
3. Kutotengenezwa “enzi mpya ya habari” katika kipindi cha SUK
4. Serikali kuendelea “kujificha kwenye gamba” katika utoaji habari
5. Kutoimarika utamaduni wa “kupenyezewa habari” kwa waandishi
6. Kutokuwepo na vyombo imara zaidi vya habari
7. Kukosekana chapicho la gazeti la Zanzibar
8. Kukosa uwezo wa uchambuzi na sera za Serikali
9. Kukosekana utaratibu wa Serikali kujua maoni ya wananchi
10. Kutokuwepo na taasisi imara zaidi za kijamii
Kwa fikra za makala hii si vyema kutumaini kuwa Maridhiano au Serikali ya Kitaifa itaimarika kwa kuwa tu kuna nia ya kisiasa au kwa kuwa tu tunataka iwepo na idumu. La ni muhimu SUK itiliwe maji, igwaziwe; itolewe magugu ili kutaraji maua mema, Tusipofanya hivyo haitafika mbali na wajibu wa waandishi wa habari katika hili ni mkubwa.
Lakini ikiwa mpaka leo miezi 9 tokea kuja kwa SUK waandishi wanapapasa tu jee hapo kuna mwendo? Ikiwa mpaka leo miezi 9 baada ya SUK Rais Dk. Shein hajaalika au kutoa fursa kwa waandishi wa habari kuzungumza nao kupata habari kwa pamoja juu ya maendeleo ya Serikali yake pana safari hapo?
Ikiwa mpaka leo miezi 9 baada ya SUK tangu kuwatumia waandishi katika Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu lakini haijawa na utaratibu wowote wa kuwawezesha waandishi kujua kwa undani juu ya Maridhiano na SUK yenyewe, jee patakuwa na mwendo hapo?
Ikiwa hakuna Upinzani rasmi ndani ya Baraza la Wawakilishi na nguvu inahitajika muhimili wa 4 ufanye wajibu wake, lakini hawajengewa uwezo wa kujua namna ya kuihoji Serikali, jee pana safari hapo?
Naamini nimechokoza waandishi wenzangu kiasi cha kutosha na natumai tutachangamka katika kujadili mada hii na kupata njia bora zaidi zetu sisi kuweza kusaidia kuhimiza na kukuza Maridhiano na SUK baada wajibu wa waandishi wa habari ingawa ni wananchi kama wengine lakini ni mkubwa zaidi kwa sababu ya taaluma na nafasi yao.
END NOTES
Abdul – Raheem, T., (ed), 1996, Pan-African Politics, Economy and Social Change in the Twenty-First Centuary; Kampala: Pluto Press.
Mpangala, G, Conflicts and Peace Building in the Great Lakes Region -www.grandlacs.net
Nyerere, J. K., 1966, Freedom and Unity. London.
Othman, H. (ed), 2000, Reflections On Leadership In Africa: Forty Years AfterIndependence. VUB University Press Brussels, and Institute of Development Studies
Saleh, Ally, “Political parties and the media in Zanzibar: Experience and impact”, a paper presented on Feb 25, 2010 Katika Semina iliyofanyika Pemba na kuandaliwa na Media Council in Tanzania
Shivji, I. G., (ed), 1991, State and Constitutionalism: An African Debate onDemocracy, Harare, SAPES Books.
Mtiririko mzima wa Wafalme wa Zanzibar baada ya Said bin Sultan ni kama ifautavyo:
Majid Al Busaid 1856-1870; Barghash Bin Said 1870-1888; Khalifa Bin Said 1888-1890; Ali Bin Said 1888-
1890; Ali Bin Said 1890-1893; Hamid Bin Thuwein 1893-1896; Khalid Bin Barghash 1896-1896; Humoud
Bin Muhammed 1896-1902; Ali Bin Humoud 1902-1911; Khalifa Bin Haroub 1911-1960; Abdullah Bin
Khalifa 1960-1963 and Jamshid 1963 -1964.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s