Vyombo vya habari na asasi za kiraia

Salma Said akitoa mada katika semina ya mahusiano ya vyombo vya habari na asasi za kiraia katika kuimarisha serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar

Hatua hizo za mashirikiano na vyombo vya habari zilizopelekea kufikia SUK, zilianza Novemba 5, 2009 baada ya Rais wa Zanzibar kwa wakati huo Dk Amani Karume kuwa na mazungumzo ya faragha ya hatimaye kupeana mkono na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad. Hatua hiyo ambaye haikutarajiwa na wengi ilikiwa ni kuzaliwa kwa mashirikiano mapya yaliyokuja kujulikana baadae kuwa ni Maridhiano. Mimi huyaita Maridhiano yanayotokana na herufi ya moja ya ‘T ‘ambayo ni Tusameheane, Tusahau aliopita na Tujenge Zanzibar mpya.
MAHUSIANO KATI YA VYOMBO VYA HABARI, ASASI NYENGINEZO KATIKA KUIMARISHA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA ZANZIBAR

MAKALA ILIYOTOLEWA KATIKA SEMINA

ILOANDALIWA NA TAASISI YA UTAFITI NA ELIMU YA

DEMOKRASIA YA CHUO KIKUU CHA TANZANIA (REDET)

JUNI 29-30 2011

BWAWANI HOTEL, ZANZIBAR

Na Salma Said
Utangulizi

Nimetakiwa nizungumze juu ya Mahusiano Kati ya Vyombo vya Habari, Waandishi, na Asasi Nyenginezo katika ujenzi na uimarishaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) hapa Zanzibar. Mada yangu ni sehemu ya mada kuu ya warsha hi inayoangalia nafasi yetu waandishi wa habari na Assasi za kiraia tunaweza kusaidia kujenga umoja visiwani baada ya miaka mingi ya migongano na chuki.

Mada niliyopewa ni pana lakini nitajaribu kuikunja kwa kuzingatia muda niliopewa bila kuacha kugusa vipengele vyote vinavyohusiana na mada hii, lengo likiwa kutizama kile ambacho waandishi wanaweza kukifanya katika kuchangia kuimarisha SUK na tukijua kuwa wajibu huo ni wa lazima maana waandishi wa habari kama wana taaluma wengine wamo ndani ya jahazi moja na wananchi wengine wa Zanzibar na kwa hakika kwenye safari moja.

Na ndio maana mada hii ikaelekeza juu ya kutizama uhusiano wa vyombo vya habari na waandishi na taasisi nyengine lakini kwanza Serikali yenyewe, kasha asasi zisizo za kiraia, kidini na jinsia kabla ya kuhitimisha kwa kutizama waandishi wa habari na vyombo vya habari kama mhimili wa amani.

Kwa hakika hatua ya kuwa na warsha hii ni muhimu na kusema kweli imechelewa. Tangu kuundwa kwa SUK, inaonekana kuwa viongozi serikalini haiwajaendeleza kubuni kazi ambazo zinaweza kufanywa na waandishi au vyombo vya habari katika ujenzi wa SUK, na ndio maana na shawishika kusema kuwa huu unakuwa ni mkusanyiko wa mwanzo kwa dhamira hiyo.

Mwaka jana serikali ya Zanzibar iliona umuhimu wa kuwashirikisha waandishi na vyombo vya habari katika hatua nne za awali katika kuelekea kuundwa kwa SUK, ambapo hatua zote hizo zilifanikiwa kwa kiwango kikubwa, na ndio moja ya sababu ya kujivunia amani na utulivu hivi sasa bada ya mwongo muongo mmoja na nusu wa siasa za ushindani zilizoambatana. Tunakumbuka siasa za ushindani ziliruhusiwa tena 1992 kufuatia upepo wa mageuzi uliokuwa ukizikumba nchi mbali mbali kwa usshawishi wa nchi za magharibi hasa Marikani baada ya kusambaratika kwa umoja wa nchi za socialist chini ya urusi.

Hatua hizo za mashirikiano na vyombo vya habari zilizopelekea kufikia SUK, zilianza Novemba 5, 2009 baada ya Rais wa Zanzibar kwa wakati huo Dk Amani Karume kuwa na mazungumzo ya faragha ya hatimaye kupeana mkono na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad. Hatua hiyo ambaye haikutarajiwa na wengi ilikiwa ni kuzaliwa kwa mashirikiano mapya yaliyokuja kujulikana baadae kuwa ni Maridhiano.

Hatua ya pili ya ushiriki wa waandishi, na vyombo vya habari ikawa ni wakati wa Hoja Binafsi ya aliyekuwa Kiongozi wa Upinzani katika Baraza la Wawakilishi Abubakar Khamis Bakary juu ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa;
Hatua ya tatu ikawa ni kipindi cha kuelekea Kura ya Maoni; Na
Hatua ya nne ikawa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka jana, 2010. Hatua zote hizo ushiriki wa waandishi na vyombo vya habari ulionekana na viongozi kuwa ni muhimu sana.

Vyombo vya habari na utumishi wa jamii
Kumbukumbu zinaonesha kuwa Zanzibar ilitangulia kuliko nchi zote za Afrika Mashariki katika tasniya ya habari na kwa hivyo kupatikana uzoefu wa miaka mingi wa vyombo vya habari ambavyo hivi sasa tunausema ni muhimili muhimu katika ujenzi wa demokrasia. Kutokana na nafasi hiyo, kuna baadhi ya dhana kuwa vyombo vya habari ni muhimili wa nne (Fourth estate) katika nchi baada ya Serikali (Executive), Bunge au Baraza la wawakilishi kwa Zanzibar (Parliament), na Mahkama (Judiciary).

Uzoefu huo wa vyombo vya habari Zanzibar ulikuwa katika Nyanja zote yaani kama ni za kisiasa, kijamii, kiuchumi na hata za kielimu maana ni Zanzibar peke yake katika miaka ya 1920 1940 ilikuwa na gazeti likiitwa “Mazungumzo ya Waalimu”, mahsusi lilozama katika mambo ya elimu na kuunganisha waalimu wa Visiwa hivi.

Pia maeneo ya uchumi magazeti hayakuwa nyuma kwani Serikali ya wakati huo ilianzisha magazeti kadhaa ambayo yalikuwa kwa mfano na “mtizamo wa kilimo” na pia yale ambayo yalikuwa ni ya kiuchumi na fedha kama vile hapakuwa na uhaba wa magazeti ya kisiasa na yale wa wafanyakazi kuunga mkono harakati za madai ya haki zao.

Lakini ni ukweli kuwa sehemu kubwa ya machapisho ya magazeti ya Zanzibar kutoka ‘Samachar’ kwa maana ya gazeti rasmi la kibiashara la mwanzo kabisa hadi hivi sasa tukiwa na Zanzibar Leo, chombo cha Serikali, yamezama kwenye mambo ya siasa.

Zanzibar sasa inaingia katika muongo wa 7 wa siasa za ushindani tokea kundwa kwa chama cha kwanza cha siasa 1954 kwa jina la Zanzibar Nationalist Party (ZNP), kupitia chaguzi 4 kabla ya Uhuru wa 1963 na Mapinduzi ya 1964 na pia chaguzi nyengine nne baada ya kurudishwa mfumo wa vyama vingi 1992, katika miaka ya 1995, 2000, 2005 na 2010.

Uandishi wa habari Zanzibar imepitia katika vipindi vya ukinzani mkubwa, ubaguzi mkubwa, ukandamizaji mkubwa, utawala wa mabavu, utawala wa vyama vyenye nguvu hadi hivi sasa baada ya kuchoshwa na yote uamuzi umefanya katika Kura ya Maoni ya Julai 31, 2010 kuwa kinachoifaa Zanzibar sio mshindi wa kuchukua kila kitu (winner takes all) bali mfumo wa mgawano wa madaraka.

Kwa sababu hiyo basi tokea awali kabisa waandishi wa Zanzibar hawakuonea haya kujipa jukumu la kutumikia jamii kwa vile ilionekana kuna mwamko mkubwa baina yao kuwa wana kazi hiyo na kiasi cha wingi na nguvu za magazeti yaliokuwepo wakati huo ilidhihirisha dhamira hiyo.

Hapana shaka kwa wakati huu njia kuu ya kutoa na kupokea habari ilikuwa ni kwa magazeti ambapo teknolojia yake illingia mapema na kwa kiasi kikubwa ilikuwa ni rahisi kutumika na kutia tija katika jamii.

Kumbukumbu pia zinaonesha kuwa Jamii ya wazananzibari yenyewe iliwahimu waandishi wa habari kufanya kazi yao kwa kuwa ni wasomaji wazuri, watoa maoni wazuri katika machapisho mbali mbali ya zama hizo ambapo msambao wa elimu ulikuwa si mkubwa na kipato cha kuwa na ziada ya kununua gazeti kilikuwa si kikubwa.

Lakini bado magazeti kwa lugha kadhaa yalikuwa yakitoka na kupata wasomaji na tabaan wanunuzi na kwa maana hiyo mzunguko katika sekta ya uchapishaji ulikuwa ni endelevu katika idadi ndogo mno ya watu kwa wakati huo.

Kwa maneno machache ni kusema kuwa utamaduni wa kuandika habari, na utamaduni wa kusomwa habari lakini zaidi utamaduni wa uhusiano baina ya jamii na vyombo vya habari na waandishi wa habari ni wa muda na ulikuwa katika jamii ya Kizanzibari ambayo ilianza kusoma gazeti mwanzo kabisa kabla ya nchi yoyote katika eneo hili la Afrika Mashariki na kati.

Ustaarabu huu haukuja bure bure bali ulipandwa, ukakuzwa na kuhimizwa kuanzia nyumbani, barazani na kwenye sehemu za elimu kwa sababu kwa kawaida yao Wazanzibari siku zote wamekuwa ni watafuta taarifa na kwa hivyo pia ni wapokeaji na ndio maana kukuwa na ukuruba mkubwa baina ya vyombo vya habari na jamii katika upana wake.

Na hio ndio ikawa sababu ya Zanzibar kuhusishwa na kurekodi maendeleo ya haraka katika miaka ya 1800 mpaka kwenye miaka ya kuelekea nchi kupata uhuru na kufanya mapinduzi na hoja zikitoka kuwa ni baada ya hapo ndio Zanzibar ilianza kudorora, lakini kwa leo hilo haliko katika hoja na kwa hivyo hatutakuwa na nafasi ya kulijadili.

Habari na Serikali

Kama ilivyo katika mazingira mengine yoyote basi pia kwa upande wa Zanzibar palikuwa na taratibu ambazo ziliifanya Serikali kuwa katika ukaribu na vyombo vya habari na pia waandishi wa habari.

Ukuruba huu ulikuwa wa aina mbili. Aina ya kwanza ni ile ya Serikali kuwa na vyombo na taasisi zake wenyewe za kihabari ili kutoa matamko yake lakini pia kuwa na Wizara ambayo kazi yake kuu imekuwa ni kusimamia sekta hiyo kwa ujumla.

Wizara ya Habari ukitoa miaka michache tu ya mwanzo ya Mapinduzi, imekuwa haikosekani katika muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar , ingawa muundo wake hubadilika kila baada ya muda kutokana na mapendekezo ya Rais ambaye kikatiba ndie mwenye mamlaka ya kuunda Wizara za Serikali.

Chini ya Wizara hutolewa miongozo na hupangwa sera ambazo ndizo ambazo zinapaswa kufuatwa na vyombo vya habari na waandishi na hawa wawe ni wale ambao wako Serikalini lakini pia wale ambao wako nje ya mfumo wa Kiserikali kwa maana ya vyombo na waandishi binafsi.

Na huu ndio ukaribu wa pili baina ya Serikali na vyombo vya habari na waandishi. Kwa maneno mengine ni kusema kuwa ni ukweli kwamba Serikali yoyote ile katika hali ya kisasa ya ukuaji wa demokrasia lazima itoe fursa kwa vyombo vya habari binafsi na waandishi binafsi kustawi katika nchi.

Na katika hili Serikali lazima itengeneze mazingira maalum ya uwekezaji na pia utendaji wa kazi za waandishi na ndipo utungaji wa sheria unapokuwa wa lazima kuwepo ndani ya nchi ili kila mwandishi na kila chombo kijue wajibu wake katika nchi.

Kwa maana hiyo Serikali imetunga Sheria kadhaa za kusimamia masuala ya habari ikiwa ni pamoja na Sheria ya Magazeti ya 1989 pamoja na mabadiliko yake yaliofanywa, Sheria ya Utangazaji inayosimamia sekta ya televisheni na radio na pia tuna sheria maalumu iliyounda Idara ya Habari Maelezo.

Katika Sheria zote hizo waandishi wa habari wanaguswa moja kwa moja. Sheria ya Magaezeti ni kuhusiana na uchapishaji, utendaji wao na hata kuingizwa masuala ya uchochezi; wakati sheria ya Utangzaji ni utendaji katika sekta ya eletroniki lakini pia jinsi mawimbi yanavyogaiwa na Sheria ya Idara ya Maelezo ni jinsi chombo hicho kinavyoweza kufanya kazi yake kama mdomo wa Serikali lakini pia kama kiungo baina ya waandishi na Serikali.

Inavyotarajiwa ni kwamba mbele ya Serikali na watendaji wake wote waandishi na vyombo vyote viwe sawa kwa maana vyote vinahitajika vifanye kazi moja yaani ya kuwaarifu wananchi kile ambacho kinatokea ndani ya nchi yao na pia kuchukua maoni ya wananchi juu ya Serikali yao na watendaji wake.

Kwa hivyo ushirikiano ni wa lazima na unaohitajiana, iwe ni vyombo vya habari vya umma au vile vya binafsi kwa sababu vyombo vya habari vina wajibu wa kuhimiza uwazi na uwajibikaji na njia bora ikiwa ni kufuatilia na kuripoti matendo na maamuzi ya Serikali na huku Serikali ikiwa na deni kwa wapiga kura na wananchi wa kukuza utawala bora na kukuza uwazi wa Serikali ili kuepusha au kupunguza utumiaji mbaya wa madaraka, upendeleo na rushwa.

Kusema kweli uhusiano huo si mzuri sana kwa hapa Zanzibar tokea imekuja SUK, lakini sio kusema kwamba ulikuwa mzuri sana kabla ya hapo. Mara nyingi kuna upendeleo wa wazi na uchaguzi wa mwanzo (preference) kwa waandishi wa serikali na vyombo vya umma ukilinganisha vyombo na waandishi binafsi.

Matarajio ya wengi yalikuwa ni kwamba milango ya kupata habari na kuifikia Serikali ingefunguliwa zaidi, lakini sivyo ilivyo na kufikia hata Rais wa Zanzibar kusema wazi kuwa wanasiasa na watendaji wafunguke zaidi, na labda alikuwa pia aseme wawe wazi zaidi kwa vyombo vyote lakini naamini vyombo na waandishi binafsi vina nafasi zaidi ya kuikosoa Serikali hasa katika maizngira ya hapa Zanzibar ambapo vyombo vya umma vinajichunga binafsi (self censorship) zaidi.

Habari na asasi za kiraia

Kama ilivyo katika nchi nyingi zinazoendelea asasi zisizo za kiserikali bado ni jambo geni ambalo limeingia miongo mitatu hivi sasa na kwa hivyo si mambo yaliostawi ingawa yapo na yanaendelea.

Kabla ya kuja kwa asasi hizi kulikuwa zaidi na zile za kikabila na kidini ambazo upana wake wa kazi haukuwa mkubwa na kwa hivyo maeneo chungu nzima hayakuwa yakikabiliwa kama vile kupambana na maradhi, kuondosha umasikini, kupunguza ujinga na hata kuhimiza watu kujua haki zao za kiraia.

Hata baada ya uhuru katika nchi nyingi Serikali ziliogopa nguvu ambazo zinaweza kuwa nazo asasi hizi na huku Serikali ikitaka kuendelea kutawala kila eneo linalogusa raia na kwa hivyo kuchukua muda kuruhusiwa kufanya kazi.

Kwa Zanzibar ni mwaka 1995 ndipo sheria ya kwanza ya usajili wa asasi hizi uliporuhusiwa na kuiondoa ile ya Kikoloni ambayo ni wazi ilikuwa imepitwa na wakati kutokana na mabadiliko mengi yakiwemo ya kiuchumi, kijami na kisiasa na ikieleweka pia kuwa uelewa wa wananchi ulikuwa mpana na mabadiliko ya Katiba ya 1984 yakiruhusu uhuru wa kujiunga na kujikusanya.

Pia Serikali imetayarisha sera inayohusiana na asasi hizi ingawa kuna uchache wa maelekezo juu ya wajibu wao. Hivi karibuni Rais wa Zanzibar Dk. Ali Muhammed Shein alitoa tamko linaelekea upande huo pale aliposema wajibu wa asasi hizo uwe ni kumkomboa mwananchi kutoka umasikini na kuzitaka pia zipunguze wingi wao kwa kuunganisha nguvu zao kwa vile nyingi ya asasi hizo zinafanana katika malengo na majukumu.

Jumuia zisizo za kiserikali zinajikusanya chini ya mwamvuli wa ANGOZA ambayo hadi sasa imekuwa ni kiunganishi kizuri na kimbilio la asasi hizo katika masuala mengi. ANGOZA yenyewe imekuwa na miradi yake kwenye maeneo kadhaa yakiwemo ya demokrasia, kupunguza umasikini na hata kuongeza uwezo wa kiutendaji wa asasi zilizo chini yake.

Ingawa kuna stahiki kuwa na ukuruba mkubwa baina ya asasi hizi zisizo za kiserikali (NGOs) na vyombo vya habari, lakini kwa sasa hali sivyo ilivyo. Uhusiano wa pande hizi mbili tunaweza kusema ni ule wa kimatukio (event based). Waandishi huitwa panapokuwa na semina, warsha au kongamano tu na waandishi pia hawazitafuti asasi isipokuwa kwa mambo hayo.

Kwa kiasi kikubwa waandishi hawafanyi bidii kujua mafanikio na matatizo ya asasi hizo na hivyo kuwakosesha wananchi kujua zinafanya nini na wanawezaje kuzifikia kwa sababu asasi zipo kwa ajili ya kuwafikia wananchi kujaliza pale ambapo Serikali imeshindwa kufanya.

Ni asasi chache zenye watu ambao wana uwezo na ujuzi wa kutumia vyombo vya habari na bado asasi nyingi hazijajitambua kuwa zinapaswa kuwa karibu na vyombo vya habari kwa manufaa ya uwazi lakini pia kujijenga mbele ya jamii.

Ni asasi kubwa kama ANGOZA, Chama cha Waalimu, Jumuia ya Watu Wenye Ulemavu, Kituo cha Sheria, Chama cha Wanasheria na baadhi ya jumuia za watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI ndizo ambazo zimeweza kuvitumia vyombo vya habari vyema na umuulizapo mwandishi yoyote akutajie asasi za kiraia basi ni majina ya hizo ndio yanayokuja haraka mdomoni mwake.

Habari na asasi za kidini

Katika miongo miwili iliyopita Zanzibar imeshuhudia taasisi nyingi za kidini pengine ni kwa ajili ya kujaza pengo ambalo lilikuwepo muda mrefu lakini pia kwa sababu ya mtizamo kuwa maadili ya kdini na ya kijamii yamekuwa yakiporomoka.

Asasi hizi ni pamoja na Jumuia ya Uamsho, Jumuia ya Maimamu, Jumuia ya Misikiti lakini pia kuna UKWEM ambao husimamia malengo ya kiuchumi na elimu na pia jumuia ya waislamu wa kike na nyengine kadhaa wa kadhaa zikiwemo pia za kigeni kama African Muslim Agency.

Asasi nyengine kama Istiqama zimejitosa katika mambo ya kiafya na pia umiliki wa magazeti na hata radio, ingawa ni radio ndizo ambazo zinaonekana zaidi. Lakini pia kuna asasi kadhaa za Kikristo Unguja na Pemba zikiwa na malengo ya aina mbali mbali na kujikita katika sekta mbali mbali pia.

Ingawa jumuia hizi husajiliwa chini ya sheria ile inayosajili asasi zisizo za kiraia zisizo za kidini, lakini usimamizi na miongozo ya asasi hizi za kidini hufanywa zaidi chini ya Sheria ya Mufti ambayo ina wajibu wa kusimamia mambo ya Kiislamu ndani ya Zanzibar.

Nyingi ya jumuia hizi zina wana harakati hodari ambao wamepanua wigo wao kadri miaka inavyokwenda kwa mfano hivi sasa baadhi ya jumuia hizo hazijitengi na masuala ya elimu ya upigaji kura na elimu ya uraia.

Jumuia za Kiislamu mwaka jana zilishiriki kikamilifu katika suala la Kura ya Maoni, zikahimiza upigaji kura wa amani katika Uchaguzi Mkuu na hivi sasa zinajishirikisha kwa nguvu zote katika masuala ya Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nyingi ya jumuia hizi hufanya kazi zake kwa uwazi na hivyo kuwa karibu na vyombo vya habari lakini kwa hakika si kiasi cha kutosha na hivyo kuwanyima wananchi fursa ya kujua wanacho kifanya na maeneo ambayo wameshindwa kufanikiwa ili waweze kuungwa mkono.

Waandishi wengi pengine kwa uelewa wao mdogo hawaziendei asasis hizi kutafuta taarifa kwa kwa kuamini kuwa hazipaswi kuhojiwa kutokana mazoea ya muda mrefu ya Wazanzibari kutohoji vitendo vya viongozi wa dini hasa katika vyuo na misikiti na kada ya maulama ikiwa haifikiki kirahisi.

Lakini pia nyingi wa asasi za kidini zinakosa mbinu bora za kupenya katika vyombo vya habari na kwa hivyo taarifa zinazofika vyombo vya habari ni zile za matukio makubwa tu kiasi ambacho wananchi wengi huachwa gizani juu ya mambo mengine kadhaa yanayotokea ndani ya taasisi hizo na kujenga imani kuwa zinahubiri dini zaidi na sio kuwa na mchango katika jamii kwenye mambo kadhaa.

Habari na jinsia

Suala la jinsia limezungumzwa sana Zanzibar na kwa hakika uelewa wake umekuwa ukiongezeka kila uchao. Na usawa wake pia kuna kila dalili kuwa umekuwa ukihimizwa katika ila kipembe.

Sheria nyingi zinazotungwa hutaka suala hili liwepo. Sheria na maelekezo kadhaa hutamka wazi wazi juu ya umuhimu wa kuwa na upande wa wanawake kulinganisha na wanaume ili kuweka sawa mizania ambayo kwa sababu ya dini na utamaduni wanawake hukosa fursa nyingi jambo ambalo linatokana na uhaba wa elimu lakini pia mtizamo wa Wazanzibari wenyewe.

Hii haina maana hata kidogo kuwa wanawake wa Zanzibar wananyimwa nafasi maana historia inaonyesha kuwa mwanamke Christabela Majaliwa alikuwa Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria huko mwaka 1949 na wanawake wa Zanzibar wakaanza kupiga kura katika mwaka 1961 na huku viriri vya siasa vikipandwa na kushukwa na wanawake kadhaa wa shoka kama Fatma Karume, Asha Makwega, Johari Yussuf Akida na wengine katika muda ambapo wanawake wengi Afrika walikuwa ndio kwanza wako jikoni.

Wanawake wa Zanzibar wameshika nafasi kubwa za uongozi na wengine kujaribu hata kugombea Urais kama Amina Salim Ali na Naila Jidawi lakini bila ya shaka imedhhirika kuwa bado jamii haijawa tayari kwa hilo ingawa idadi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia vitu maalum wamongezeka katika juhudi za kuwaweka wanawake kwenye maeneo ya maamuzi.

Sekta ya Habari ni eneo zuri la kudhihirisha jinsi ambavyo usawa au tuseme mapammbano ya uswa wa jinsia yanavyoendelezwa kwa kuona namna ambavyo wingi na hata ubora wa waandishi wa habari ulivyo hapa Zanzibar, ingawa bado wanawake hawajafikia katika ngazi ya uongozi na baadhi ya radio za Kiislamu zikichagua kutompa nafasi mwanamke kwa sababu za kimaadili.

Lakini bado kuna hitajika kuwa na mashujaa wa mifano ambao kwa sasa sio wengi na kwa hivyo uhusiano wa vyombo vya habari na waandishi na masuala ya jinsia ni wa kuripoti matukio na watu tu na sio kuzungumzia masuala makubwa na msingi yanayogusa sheria na sera na njia bora zaidi za kusonga mbele.

Habari kuhusu masuala ya jinsia zinaandikwa mara kwa mara na hata vipindi kufanywa katika radio, lakini si kwa undani unaohitajika kwa sababu hata hao waandishi wenyewe wengi si weledi wa eneo hilo na kwa hivyo maandishi yao yanalenga kuhesabu idadi ya wanawake bila ya kujali mambo mengine kadhaa yanayozunguka suala hili la jinsia.

Katika kujenga Zanzibar mpya lakini pia hata Serikali kuu inabidi ibadilishe mtizamo wake kwa vile haijaonekana bado kupania katika kujenga usawa sio tu kwa kuchagua na kupandisha vyeo bali kuwasogeza wanawake katika sehemu za maamuzi na kuwapa nguvu za kweli na sio za bandia au kama vile wanafanyiwa ihsani.

Habari na Migawanyiko

Tumeeleza huko mwanzo kuwa waandishi wa Zanzibar wamepata kila aina ya uzoefu katika kuripoti habari katika miongo 8 iliyopita. Tokea siasa ikianza, ikipata kasi, ikileta uhuru, ikileta mapinduzi, ikileta udiketeta, ikileta muungano, ikileta chama kimoja na ikirudisha siasa za ushindani na kunyanyua kiwango cha uhasama na magomvi.

Zanizbar imegawanyika mara kadhaa na tabaan waandishi wake wakagawanyika mara kadhaa. Siasa zimeigawa jamii ya Zanzibar, ukabila umeigawa jamii ya Zanzibar lakini hata matukio kama vile ya biashara ya utumwa na mauaji makubwa wakati wa Mapinduzi yameigawa Zanzibar.

Katika wakati ambapo magazeti yalikuwa mengi katika miaka ya 50 na 60 na siasa za kupigania uhuru zilipokuwa motomoto waandishi waligawika. Lugha za uchochezi zilikuwa zimeenea na kwa kweli ziliwachochea watu kuhasimiana na kugombana na hata kuingia kwenye mapigano.

Baada ya Mapinduzi aina ya uandishi ilikuwa ni ile iliyotukuza (glorify) tukio hilo bila ya kujali watu ambao waliumizwa na tukio hilo kama vile wao wenyewe kuwa ni wahanga lakini pia kupoteza jamaa na mali zao, matukio mengine yakitokea siku siku, majuma na miezi kadhaa baada ya Mapinduzi yenyewe.

Kuwepo kwa vyombo vya Serikali tu kulisaidia kuzuia fursa ya watu kutoa joto lao na kwa hivyo yaliokuwa yakichapishwa na kutangazwa na vyombo vya Serikali hayakusaidia kuponyesha majeraha.

Muda mwengine ambao jamii iliingia mpasuko ni kipindi cha 1992 zilipoingia siasa za vyama vingi hadi 2005 ambapo ni uchaguzi wa mwisho ulipofanyika kwa njia ya mfumo wa mshindi kuchukua kila kitu. Kipindi hicho chuki ya kisiasa ilikuwa juu na kwa kiasi fulani waandishi walikuwa na mchango wao hasi.

Lakini kwa ujumla inaweza kuwa ni sahihi kabisa kusema kwamba hapajawahi kufanyika uchochezi mkubwa uliofikia kiasi cha kupiganisha au watu kuuwana kama ambavyo tumeona na kusikia yaliotokea huko Kenya au Rwanda.

Kunaweza kuwa na sababu nyingi. Mojawapo ni kutokuwepo kwa watu wenye siasa kali, pili kutokuwepo na tatizo na kikabila, tatu ukuruba wa watu na jinsi walivyoingiliana, nne vyama vya siasa kwa kiasi vimejizuia kuchochea watu wao, kuwepo kwa sheria kali ya uchochezi ingawa haijawahi kukunjua makucha yake kikweli kweli na pia inawezekana ni kwa sababu ya msingi mkubwa wa kidini yaani kuwepo na idadi kubwa ya waumini wa kidini na zaidi Waislamu.

Hii haina maana kuwa watu wamekuwa na imani ya mia kwa mia na vyombo vya habari katika suala hili, la. Mara kadhaa vyombo vya habari vya Serikali hasa Radio na Televisheni vimetumiwa kuandaa propaganda chafu yenye kuweza kutishia uchochezi na machafuko ndani ya nchi bila ya Serikali kukemea jambo kama hilo.

Changamoto

Tasnia ya habari duniani inakuwa kwa kasi sana kiasi ambacho sasa inaanza kuwa vigumu kufuatana nayo. Inavyohitajika pia kwamba tasinia hiyo pia iwe kwa kasi inayolingana na hiyo ya dunia ili waandishi wetu wasiwachwe nyuma. Kuingia dijitali kutoka analogi si jambo linalozuilika kama vile kuingia katika njia za kisasa za kupashana habari kama za blogi, twitter na nyenginezo.
Lakini pia kuna changamoto ya ubora wa habari unaoambatana na ukweli kwa sababu ya kupanua wigo wa uelewa wa watu wetu ambao si rahisi kundelea kudanganyika maana wanaweza kuwa na vyanzo vingi vya kuchunguza na kuthibitisha habari.

Pia kuna changamoto ya ushindani baina ya vyombo jambo ambalo wakati mwingi linavila vyombo hivyo ambavyo kwa sehemu kubwa kwa hapa Zanzibar vimekuwa ni vya kijungu meko na hivyo kudhoofisha kiwango cha utoaji habarikwa ukosefu wa vifaa na ubora wa watangazaji na waandishi.

Wengi wanaamini kwamba waandishi wengi Zanzibar wana vyama vyao, ingawa watajaribu kiasi kikubwa kujizuia lakini inapobidi kukipa msaada chama kilicho moyoni mwake atafanya hivyo bila ya kujali maadili ya kazi yake na kwa hilo limechangia katika mahusiano mabaya ya waandishi na vyanzo vya habari.

Kuna changamoto ya uelewa na uwezo mdogo wa waandishi katika masuala mengi ya ki-nchi na kwa hivyo wanakosa uwezo wa kuripoti kama inavyohitajika kama ambavyo inavyokuwa kwa mtu aliyekuwa hakutayishwa sawa sawa. Si kuripoti bajeti, Baraza la Wawakilishi, mfumo wa uendeshaji wa Serikali na hata habari za kiuchunguzi.

Kutokuwepo kwa fursa nyingi za kutangaza na kuandika pia ni tatizo kwa vyombo vya habari na waandishi wa Zanzibar, ambapo watu wengi kalamu zao zinakauka wino na sauti zao zinafanya mgando kwa kukosa fursa hizo na matokeo yake ni baadhi ya vipaji kuvunjika moyo na waandishi kutafuta kazi nyengine za kufanya.

Kuhusiana na Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuna changamoto nyingi ambazo japo zinaweza kukabiliwa lakini pia SUK ina uwezo wa kuziondoa ili kuwepo na ulaini wa kuripoti na hata kuweza kufikia habari zilizojificha ambazo kwa kweli tunaamini ni nyingi tokea kundwa SUK.

Wengi wetu tunaamini kuwa hatujaripoti vya kutosha katika kipindi hiki kwa sababu ya Serikali kubana taarifa zake na hata vikao muhimu kama kile cha semina elekezi ambayo Tanzania Bara kilikuwa wazi kwa waandishi, hapa waandishi hawakunusa kitu zaidi ya kupewa taarifa.

Hali kadhalika kuna changamoto ya kupatikana mawaziri na hata viongozi wakuu. Leo ni miezi 8 tokea kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa waandishi hawajapata fursa kamilifu ya kuzungumza na Rais Shein juu ya uendeshaji wake wa Serikali lakini yeye mwenyewe akiwataka watendaji na mawaziri wake wawe wepesi kwa waandishi.

Lakini inaonekana mwelekeo katika mahusiano kati ya vyombo vya habari na SUK si mbaya, baada ya waziri wa nchi-Ikulu hivi karibuni kutangaza kuwa rais atakuwa akikutana na waandishi wa habari mara moja kila baada ya miezi mitatu ili kuzungumzia maendeleo ya zanzibar. Kwa hakika, kama ahadi hii itaweza kutekelezeka ni hatua ya matumaini.

Kwa ujumla tunaamini vyombo vya habari sio tu vina jukumu lakini pia vina uwezo mkubwa wa kusaidia katika ujenzi wa umoja wa kitaifa, lakini hilo halitawezekana iwapo havitapata ushirikiano mkubwa zaidi kutoka Serikali na taasisi zake na waandishi kuwezeshwa kitaaluma kwa kuwa majukumu yake yamebadilika sasa.

Kwa kijigazeti kimoja kiliopo tena la Serikali na vijiredio vichache ambavyo japo zinajitahidi lakini kwa hakika chembilecho vijana ziko zaidi kiburdani, hatuwezi kutaraji waandishi watatoa mchango mkubwa katika kuhimiza umoja wa kitaifa katika hali ambayo wengi vyombo wanvyoripotia ni vya Tanzania Bara ambako kuna ajenda nyenginezo muhimu zaidi kwao na sio ujenzi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA NA NIPIGIENI MAKOFI
Rejea (Refereces)

Biswa, M (20 May 2007), Developmental Issues in News Media: NGO-Media Interaction, Volume 9, Issue 3, July 2007
Commonwealth Observer Group (October 2000): The elections in Zanzibar, United Republic of Tanzania, 2000
Ally Saleh (2010). Seminar papers- social responsibility and the the role of media in promoting unity and government of national unity (GNU).
International Study Commission on Media, Religion and Culture (2000). A CONSULTATION ON RELIGION AND MEDIA IN AFRICA available at http://web.utk.edu [accessed 28 June 2010]
Sturmer, Martin (1988). The Media History of Tanzania comprises ZANZIBAR PROTECTORATE (1914):
Tanzania Elections (and Zanzibar), 2010. Wikipedia archve. [Online] Available at: http://en.wikipedia.org [Accessed 27 June 2010].

Thomas, Hobbes (1995). The Political Impasse- The Zanzibar elections of October 22, 1995.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s