Wahariri watekeleze walichoazimia

Wahariri wa vyombo vya habari vya Tanzania Bara na Zanzibar walipotembelea kiwanda cha uzalishaji wa bia za Serengeti huko Moshi

Na Ally Saleh,

Kwa siku mbili Wahariri mbali mbali wa vyombo vya habari walikutana mjini Arusha katika kile kilichoitwa mkutano wa kujitzama upya na dhana kuu ya mkutano huo ikipewa jina la Uandishi wa Dhamana ( Responsible Journalism.)

Waandishi hao waliwezeshwa kukutana na Kampuni ya Serengeti Breweries na kwa hakika huo ulikuwa ni mkutano mkubwa wa pili wa Jukwaa la Wahariri tokea kuundwa kwake mwaka jana.

Kama lilivyo jina lake Jukwaa la Wahariri liliundwa ili kutoa fursa ya watendaji hawa wa vyombo vya habari walio katika ngazi muhimu ya maamuzi kupata uwanja wa kujitathmini na kutathmini kazi zao kwa undani zaidi.

Mkutano huo, kama ambayo Jukwaa la Wahariri limejijengea kufanyika kila mara, ni fursa nzuri ya kujikosoa na kujirudisha katika mstari lakini pia kujenga uhusiano mzuri baina yao na kwa kweli mawazo kadhaa ya msingi yalitolewa.

Na kwenye hili la kujikosoa kwa hakika lilifanyika. Hatuna haja katika makala hii kuzungumzia mambo yote yaliotokea uchawini, lakini napenda msomaji wangu aamini kuwa Wahariri hawakuoneana haya katika hili maana mficha uchi hazai na matarajio yalikuwa ni kuwekana sawa ili baada ya Arusha kadri itavyowezekana watu wazaliwe upya.

Lakini pia Jukwaa la Wahariri lina lengo la kusaidia kuwaongoza watendaji hawa juu ya mambo muhimu ya kitaifa na kuyasemea kwa sauti moja kadri inavyowezekana kwa maana ya kuwa waunganishwe katika baadhi ya mambo.

Jukwaa la Wahariri pia lina madhumuni ya kuhakikisha kuwa linalinda viwango vya tasnia hiyo ili sio tu isichujuliwe lakini pia isivamiwe na watu wasiopikwa sawa sawa na matokeo yake kuitoa fani hiyo katika malengo yake makuu ya asili ya kuelimisha, kutoa habari na kuburudisha.

Ila pia katika zama hizi majukumu ya vyombo vya habari yameongezeka na inaeleweka sasa pia majukumu yake zaidi ya hayo ya asili basi pia ni kuwawezesha wasikilizaji au wasomaji kufanya maamuzi lakini pia kuongoza ajenda katika jamii.

Mwelekeo wa mkutano huo wa Jukwaa la Wahariri ulitandikwa na Jaji Mstaafu Mark Bomani, Mwenyekiti wa Serengeti Breweries, lakini pia mjumbe muhimu katika upande wa maadili katika Baraza la Habari la Tanzania (MCT).

Bomani alikumbusha kilio cha wananchi cha kuwa na matarajio makubwa ya wananchi kutaka waandishi wa habari wawaongoze katika masuala ya kitafia kama vile kupiga vita umasikini, rushwa na kuihoji Serikali katika mambo mbali mbali.

Mkutano huo ulikuwa na mada kadhaa zilizolenga kutoa uchokozi katika maeneo mbali mbali na kwa hakika mada zilitolewa kwa ufundi mkubwa kiasi ambacho zilikuwa ni chachu ya mijadala mikali ndani ya ukumbi kwa siku zote mbili.

Wahariri baada ya mkutano huo waliondoka na makubaliano muhimu ambayo kila mmoja wao amekubali kuyatekeleza lakini pia kuyasimamia katika taasisi zao za kazi na pia kushusha maamuzi hayo kwa watu walio chini yao.

Makuabaliano hayo yapo katika kile kilichoitwa Azimio la Kwanza la Jukwaa la Wahariri –Arusha ambalo wengi wameelezea ni moja katika mambo muhimu kutokea nchini Tanzania kwenye tasnia vyombo vya habari ambayo ingawa ina umri mdogo tokea fursa ya ushindani ilipotokea, lakini imekuwa kwa kasi kubwa.

Hivi sasa idadi ya magazeti ya wiki na ya kila siku ni kubwa, vituo vya radio ni vingi nchi nzima na vituo vya televisheni vinastawi kila siku. Lakini pia vyombo vya mawasiliano vya kisasa kama blogi zimekuwa zikipata nguvu kila siku na kuchukua idadi kubwa ya wasomaji.

Ndani ya Azimio hilo waandishi wameona umuhimu wa kusitisha mashambulizi baina yao yanayotokana na kutumiwa ama na wanasiasa, wafanya biashara au watu wenye maslahi yanayogongana .

Pia waandishi wameona haja ya kuwa wao wawe mstari wa mbele kuongoza hoja mbali mbali zenye umuhimu wa kitaifa na kadri inavyozekena iongoze pia kutandika ajenda za taifa kadri pia itavyowezekana kwa mujibu wa wakati.

Kwa mfano waandishi wameona kuwa lazima walisimamie kidete suala la uhaba wa umeme nchini ambapo haielekei kabisa Tanzania Bara ikiwa inaelekea katika miaka 50 ya uhuru inashindwa hata kuwa na umeme unaotosha robo ya mahitaji ya nchi.

Wahariri wameona ipo haja ya kuibeba ajenda hii kwa kila hali ili kwa miaka michache ijayo lazima Tanzania iwe na umeme usipungua megawati 10,000 lakini hasa kiwango kizuri ni megawati 15,000 ili nchi iweze kuwekeza kikweli katika viwanda na kilimo.

Pia wameona haja ya Wahariri kulisukuma taifa katika uhuru wa kiuchumi Tanzania ikisonga mbele katika kupita kipindi cha miaka 50 huku bado kipato kikiwa cha chini lakini pia rushwa na umasikini ukisokota umma wa wananchi wa nchi hii ambao ni wakulima.

Kuhusu fani yao, Wahariri wamesema wanataka kuondokana na dhana kuwa kazi ya uandishi ni ya walioshindwa katika masomo na kwa hivyo kuvitaka vyuo vya kati kusimamia fani hiyo kwa makini zaidi kwa kutizama upya mitaala yake na pia kutizama upya juu ya namna ya kutoa ajira za fani hiyo kwenye vyombo.

Suala la vivazi vya waandishi lilijadiliwa kwa umuhimu wake na Wahariri kutoka na azimio kwamba hilo lisisitizwe sana hasa miongoni mwa waandishi wanaochipukia ambao walisema hufika hata kuvaa vivazi vya aibu na kwa hivyo kujishusha wao wenyewe na fani kwa ujumla.

Lugha lilikuwa ni jambo jengine muhimu na walioelekezwa kidole zaidi ni radio ambazo zilielezwa haizchukui bidii kubwa katika eneo hili kiasi ambavho Kiswahili kinaonewa sana kwa kuvuliwa nguo na sababu ikiwa ni kwenda na wakati au lugha ya vijana.

Lakini pia azimio lilitoa indhari juu ya matumizi ya makosa ya lugha katika magazeti na radio na ikakubaliwa kwamba kila mara yatolewe maelekezo ya matumizi sahihi ya misemo na maneno na hata masuala kama ya serufi.

Wahariri walikemea sana juu ya tabia ya vituo vya radio kuyasoma magazeti yote kwa undani katika vipindi vyao vya asubuhi kiasi cha kuwatoa hamu wasomaji kununua magazeti na kwa hivyo kuchangia katika kushudha mauzo ya magazeti hapa nchini.

Wahariri walikubaliana kwamba kuna haja ya kujenga mshikamano baina yao na kwamba kujikusanya chini ya Jukwaa la Wahariri kusichukuliwe kwa wepesi bali ni fursa adhimu ambayo inaweza kujenga nguvu ya pamoja.

Na ndipo pia waandishi wakaazimia kuwa kadri itavyowezekana basi ni vyema iwapo waandishi wataweza kujiuunga pamoja na kujitengezea nguvu za umiliki wa chombo cha habari kwa kuwa wao ndio wanaoujua undani wa fani hiyo na sio wafanya biashara au wanasiasa wanaoingia kwenye tasnia hiyo kwa malengo ya kujijenga kisiasa au vyenginevyo.

Sasa Jukwaa la Wahariri likiwa linaanza kuingia katika mwaka wake wa pili ni kwa chombo hicho muhimu kushika wajibu wake sawa kwa kusimamia maadili, nidhamu, uwezo wa vyombo lakini pia kuongoza kwenye masuala yenye umuhimu wa kitaifa na kama walivyosema kusimamia maslahi ya taifa bila ya kumuonea haya mtu yoyote na aliye nafasi yoyote.

Naamini vyombo vya habari vya Tanzania vimejijngea tayari uwezo huo, sasa kilichobaki kama Azimio la Kwanza lilivyosema ni kusaidia kujenga uzalendo. Na ujenzi huu wa uzalendo ndio utapopata wananchi ambao wataunga mkono kazi za waandishi wa habari, maana ndipo kutakuwa na umma utaojua vyombo vya habari vipo kwa ajili yao na kwa ajili ya umma na kwa hivyo kila mmoja wetu.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s