Majibu ya ICU ni yangu

Waziri wa Afya Zanzibar, Juma Duni Haji

WAZIRI wa Afya Juma Duni Haji amesema kwa mujibu wa kanuni za Baraza la Wawakilishi yeye kama waziri wa wizara hiyo, ndiye anayepaswa kulieleza Baraza hilo taarifa za wizara kwa niaba ya serikali.

Waziri Duni alisema kutokana na hali hiyo haiwezekani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi asimame ndani ya Baraza hilo kuelezea tatizo linaloikabili wodi ya wagonjwa mahututi (ICU), katika hospitali ya Mnazimmoja.

“Kwa kanuni hizi, mimi kama waziri wa Afya ndiye mwenye mamlaka ya kuelezea matatizo ya ICU ya Mnazimmoja kwa niaba ya serikali”,alisema waziri huyo baada ya kuchambua vifungu kadhaa vya kanuni za Baraza hilo.

Waziri Duni alieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi alipokuwa akifanya majumuisho na kujibu masuali na na kutoa ufafanuzi wa hoja mbali mbali za wajumbe wa Baraza hilo, baada ya kuchangia hotuba ya bajeti ya makadirio na matumizi ya wizara hiyo.

Kauli hiyo ya waziri huyo, imekuja kufuatia baadhi ya wajumbe wa Baraza hilo kupendekeza Makamu wa Pili wa Rais asimame Barazani atoe msimamo wa serikali juu ya tatizo yanayoiandama wodi ya wagonjwa mahatuti (ICU) katika hospitali ya Mnazimmoja.

Waziri huyo alikiri kuwepo kwa matatizo makubwa katika wodi hiyo na kusema kwamba wajumbe wa Baraza hilo na kueleza kutoshangazwa kwa wajumbe wa Baraza hilo kueleza kwa hamasa na uchungu.

“ICU hairidhishi ni kweli kuna matatizo, iko katika hali mbaya, matatizo yaliyopo ni mapungufu makubwa kwenye hospitali hiyo ya rufaa, serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha inaifanyia matengenezo ICU”, alisema waziri Duni.

Alisema China imekubali kusaidia matengenezo ya chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali hiyo, lakini endapo misaada huo utachelewa ndani kipindi cha miezi sita, serikali itahakikisha inaijenga wodi hiyo hiyo kwa kutumia fedha zake.

“Endapo hadi miezi sita ijayo China itakuwa haijatusaidia kutujengea kama ilivyoahidi, serikali itaka pua na kuunga wajihi, itatoa fedha zake kuijenga ICU”,alisema Duni.

Akizungumzia suala la hospitali ya Mnazimmoja, waziri Duni alisema unapoizungumzia hospitali hiyo ni sawa na kuilinganisha na taasisi huku ikiwa na vitengo kadhaa ambapo ili uendeshaji wake uende kwa uhakika zinahitajika shilingi bilioni 2.8.

Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyokatika Umoja wa Kitaifa imedhamiria kwa dhati kushughulikia matatizo ya afya, ambapo kwa msingi huo imekuwa ikijitahidi kuongeza bajeti ya sekta hiyo kila hali inaporuhusu.

Aidha katika majumuisho hayo waziri huyo alizungumzia matumizi ya fedha za msamaha, ambapo alisema fedha hizo zimekuwa zikitumika kwa ununuzi wa vifaa mbali mbali vya ikiwemo CT Scan ambapo tangu inunuliwe mamia ya watu wameshachunguzwa na kiasi cha wagonjwa 104 wamefanyiwa operesheni.

Akizungumzia juu ya wajawazito wanaofanyiwa upasuaji kutakiwa kulipa shilingi 40,000, alisema tatizo hilo linafanyiwa utafiti ili kupata uhakika mzazi anayehitaji operesheni anahitaji kiasi gani na kuacha kuwalipisha wajawazito.

Kuhusu makusanyo ya hospitali hiyo alisema wamekubaliana na wizara ya Fedha kuandaa mikakati itakayohakikisha fedha wananazochangishwa wananchi zote zinaingia katika mfuko wa serikali.

Alisema baada ya fedha hizo kuingia kwenye mfuko huo zitarejeshwa kusaidia matumizi katika utoaji wa huduma, huku tayari wahasibu wanane wakiwa wameshaandaliwa kwenda kukusanya fedha hizo, ambapo pia fedha hizo itafanyiwa ukaguzi.

Wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya Afya baadhi ya wajumbe wa baraza la wawakilish wametishia kuzuwia shillingi katika bajeti ya wizara ya afya kama hawatopewa maelezo ya kutosha kuhusu kwa nini Serikali imeshindwa kuimarisha huduma za kitengo cha wagonjwa mahututi ICU.

Mwakilishi wa jimbo la Mpendae (CCM) Mohamed Said Mohamed alisema hajaridhishwa na juhudi za Serikali katika kulipatia ufumbuzi tatizo la kitengo cha wagonjwa mahututi ICU.

“Jamani tumeweka rehani afya za wananchi wetu….kitendo cha Serikali kushindwa kukipatia vifaa vya kisasa kitengo cha wodi ya wagonjwa mahututi kinatia aibu sana na kinaonesha kwamba hatupo makini katika kuzingatia afya zao”alisema.

Alisema hivi sasa wananchi wengi wanaogopa kupeleka wagonjwa wao katika hospitali ya Mnazi mmoja kwa sababu haina vifaa vya kutosha na badala yake watu wengi sasa wanakwenda Muhimbili na hospitali nyengine za Tanzania Bara.

Alitishia na kusema atazuwia shilingi katika bajeti ya wizara ya afya kama hatopewa maelezo ya kutosha ya kuridhisha kuhusu juhudiza Serikali katika kukabiliana na tatzo la kitengo cha ICU.

Mwakilishi wa jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Ayoub Hashim kilio chake kilikuwa kitengo cha ICU na kusema ni kipindi cha miaka mitatu sasa hali ya kitengo hicho ni mbaya.

“Mimi kilio changu kwa wizara ya afya ni kitengo cha ICU kipo katika hali mbaya na hakistahiki kwa kweli kwani ukipelekwa pale ndiyo safari ya kifo imewadia”alisema Ayoub.

Mwakilishi wa jimbo la Kwahani (CCM) Ali Salum Haji alisema huduma katika hospitali za Mnazi mmoja ni mbaya sana kiasi ya kuwavunja moyo wananchi wengi.

‘Mheshimiwa spika hospitali ya Mnazi mmoja ndiyo kimbilio la wanyonge….mtu mwenye pesa yake ikiwemo wakubwa hawendi pale kutibiwa kwa sababu wanajuwa huduma zake pale duni’alisema mwakilishi huyo.

Mwakilishi wa jimbo la Mtambwe (CUF) Salim Abdalla Hamad amekasirishwa na tabia ya baadhi ya madaktari kulazimisha kupewa fedha za matibabu hata kabla ya mgonjwa kupatiwa huduma za dharura ikiwemo wagonjwa wanaopata ajali huku wakiwa katika hali mbaya.

Alitoa mfano wa hivi karibuni alikuwa na mgonjwa aliyepata ajali ya gari,lakini mara baada ya kufikishwa hapo katika hospitali ya Mnazi mmoja,madaktari walidai kupewa fedha za matibabu hata kabla ya kumkaguwa na kumpatia matibabu.

‘Mheshimiwa spika jamaa wa mgonjwa yule walilazimika kuweka rehani simu yao ili mgonjwa yule apatiwe matibabu ya dharura…..jamani hivi madaktari wetu hawana ubinaadamu’aliuliza Hamad.

Naye Mwakilishi wa nafasi za wanawake (CCM), Panya Ali Abdallah aliitaka wizara ya afya kufanya utafiti kuhusu kuongezeka kwa tatizo la akinamama wajawazito kufanyiwa upasuaji wakati wanapotaka kujifunguwa katika hospitali mbali mbali za Zanzibar.

Panya alisema ameingiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu kuwepo kwa upasuaji kwa akinamama wanaotaka kujifunguwa na kusema utafiti unahitajika kufanywa ili kukabiliana na tatizo hilo.

‘Mheshimiwa naibu spika tufanye utafiti katika suala hili…kwa nini hivi sasa kuna wimbi kubwa la akinamama wanaotaka kujifunguwa kufanyiwa upasuaji…wasiwasi wangu mkubwa isije ikawa huu ni mradi wa madaktari’alisema Panya.

Aidha mwakilishi huyo alitaka kuimarishwa kwa hudumza wa wakunga wa jadi ikiwemo kupatiwa vitambulisho maalumu katika utoaji wa huduma zao.

Aliwapongeza wakunga wa jadi na kusema wanafanya kazi kubwa za kuhudumia akinamama wajawazito na ndiyo maana hivi sasa limekuwepo wimbi kubwa la akinamama kujifunguwa majumbani kwa wakunga wa jadi

Kabla ya waziri huyo kutoa ufafanuzi huo, Naibu wake Dk. Sira Ubwa Mamboya alisema Zanzibar ina madaktari wazuri ambao wamefikia viwango vya kimataifa na kutambuliwa na shirika la Afya duniani (WHO).

Baada ya majumuisho hao wajumbe wa Baraza hilo, waliridhia na kupitisha makadirio ya makusanyo na matumizi ya wizara hiyo.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s