Haya ni matunda na SUK

Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari aliyesimama ni Waziri wa Biashara Ahmed Nassor Mazrui na kulia yake ni Katibu wake Dk Islam Seif

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad amesema kupandishwa kwa bei za karafuu na ongezeko la mishahara kwa asilimia 25 ni moja ya mafanikio yaliopatikana baada ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa (SUK).

Kauli ya Maalim Seif imekuja siku chache baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoa taarifa kwamba mafanikio hayo yanatokana na ilani ya chama hicho.

Maalim Seif alisema hayo jana leo wakati akijibu maswali na majibu ya waandishi wa habari katika ukumbi wa baraza la wawakilishi la zamani liliopo Maisara Mjini Zanzibar.

Alisema hata katika mkutano ulioitishwa na chama cha wananchi (CUF) viwanja vya Kibandamaiti wiki iliyopita, alisema lengo lake ni kuwaonyesha wananchi mafanikio yanayoendelea kupatikana chini ya uongozi wa serikali ya umoja wa kitaifa bila ya kujali sera hizo zinatokana na chama gani.

“Kwa sasa nimeelekeza juhudi zaidi katika utendaji wa kuiwezesha serikali ya umoja kitaifa kufikia matarajio ya wananchi kuondokana na ugumu wa maisha, na hilo nililisema kule katika mkutano kwamba haya ni mafanikio ya serikali yetu” alisema Maalim Seif.

Akitaja mafanikio hayo ni pamoja na kupanda kwa bei ya karafuu kwa asilimia 100 na kupanda kwa kima cha chini cha mishahara ya watumishi serikalini kwa asilimia 25.

“Mimi nafanyakazi ya kuonyesha mafanikio ya serikali ya umoja wa kitaifa, sio chama, na ndio nilisema kwamba kwa nyakati tofauti mimi na mgembea mwenzangu Dk Shein tuliahidi kwamba tukiingia madarakani tutatimiza ahadi zetu suala la mishahara na kupandisha bei za zao la karafuu … sasa kama wengine wanachukulia hili kisiasa, siwezi kuwajibia,” alisema Maalim Seif.

Katika mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Kibandamaiti, Maalim Seif alisema sera zinazotumika kwa sasa chini ya serikali ya umoja wa kitaifa ni za vyama viwili vya CUF na CCM na kuwataka wananchi kuunga mkono juhudi za serikali katika kufanikisha suala hilo.

Maalim Seif alisema mara kadhaa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka jana, aliahidi kuwa iwapo atashinda ataongeza bei ya karafuu na kupandisha kima cha chini cha mshahara, suala ambalo hata Dk Ali Mohamed Shein pia aliahidi.

Mkutano wa waandishi wa habari na Maalim Seif pia ulihudhuria na Waziri wa Biashara na Viwanda, Nassor Ahmed Mazrui, ambaye wiki iliyopita alitangaza ongezeko la bei ya karafu kwa asilimia 100.

Kwa kiwango hicho, wakulima kuanzia sasa watalipwa shilingi 10,000 kwa kilo moja ya karafuu ya daraja la kwanza, shilingi 9,500 kwa kilo ya daraja la pili na shilingi 9,000 kwa kilo ya daraja la tatu.

Awali bei za karafuu wakulima walikuwa wakiuza kwa shilingi 3,000 hadi shilingi 5,000 kwa kilo jambo ambalo lilikuwa likichangia wananchi wengi hasa kisiwani Pemba kuuza karafuu zao kwa magendo na kuikosesha fedha nyingi serikali.

Aidha Maalim Seif amelitaka shirika la ZSTC kuwachunguza watendaji wake ambao si waaminifu wanaoweza kudhulumu wakulima wa karafuu wakati wa mauzo.

Maalim Seif Alisema shirika ni vyema kudhibiti mtindo wa baadhi ya watendaji wake wenye tabia ya kufanya ubadhirifu wakati wanapopima kwa kuwapunguzi kiwango cha ubora wa karafuu au kutoa malipo hafifu.

“Serikali imefanya maamuzi ili kumuona mkulima wa karafuu anafaidika na zao hilo kupata asilimia 80 ya bei ya dunia” alisema Maalim.Pia watendaji wa Shirika la ZSTC wametakiwa kujua kwamba karafuu hizo wananunua kwa kiwango kutoka kwa mkulima na kuepusha udanganyifu katika ununuzi wa zao hilo kwa hali yoyote.

“Wakulima walikosa motisha miaka ya nyuma ambapo serikali ikinunua karafuu kwa kuangalia bei ya soko la dunia hivyo mkulima aliona akiwa na mabungo anaweza kupata fedha zaidi kuliko karafuu”, aliongeza Maalim Seif.

Hata hivyo aliwaomba wananchi kuhakisha kwamba karafuu ya Zanzibar inauzwa Zanzibar ili kuhakikisha kuwa wananchi wanafaidika kwani kwa kiasi kikubwa wanaosafirisha karafuu kwa njia ya magendo ni wananchi wenyewe.

“Tumeamua kwa dhati kabisa kutoa kipaumbele kwa suala la kuhamasisha uma kujiepusha na kuuza karafuu nchi jirani na badala yake kuuza hapa nchini”.alisema Maalim Seif.

Alisema shirika la ZSTC limejiandaa kulipa fedha taslim kwa wakulima na hakuna atakepeleka karafuu kwa njia ya mkopo na kuwashajihisha kuacha kuweka karafuu nyumbani badala yake wazipeleke akiba ya karafuu katika shirika la ZSTC kwa kujiepusha na hasara inayoweza kuwatokea na kamwe karafuu zake hazitapotea.

Makamu huyo wa wanza alisema kuna shutma za baadhi ya wananchi na hata viongozi wanasafirisha karafuu kwa njia ya magendo ambapo kamwe serikali hautavumilia kwani ni kitendo hicho cha kisaliti kinachofanywa na watendaji wa serikali kwa kushirikiana na wakulima.

Alisema kulikuwa na shutuma baadhi ya vyombo vya kusafirishia karafuu vikiskotiwa kwa vyombo vya ulinzi na hata baadhi ya wengine kutumia magari ya kusafirishia wagonjwa katika kutekeleza ubadhirifu huo.

Malim Seif alisema kwa msimu huu mdogo serikali inakadiria kupata zaidi ya tani elfu tatu za karafuu lakini lengo ni kupata zaidi na pia kuliimarisha zaidi kwa kuwasaidia wakulima.
Maalim Seif alitoa wito kwa wananchi wanatoa taarifa kwa watendaji na wakulima wasio waaminifu ambao wanatumia kuuza karafuu kimagendo.

“Serikali imejizatiti katika suala la kudhibiti magendo na tunawaomba wananchi watoe mashirikiano makubwa na serikali yao, wakimuona mtu anafanya vitendo vya kuuza magendo watoe taarifa hata kama Makamu wa kwanza wa rais anaboti yake anasafirisha basi watoe taarifa” alisema Maalim Seif.

Akizungumzia suala hilo Waziri Mazrui alisema iwapo mtu atatoa taarifa kwa wahusika atazawadiwa magunia mawili kati ya magunia kumi yaliokamatwa hivyo wananchi watoe ushirikiano makubwa ili lengo hili lifanikiwe na serikali iweze kupata mapato kutokana na zao hilo.

Alisema katika nchi za Afrika ni nchi tatu zinazotoa karafuu zikiwemo Madagaska inatoatoa tani 12. Zanzibar inatoa tani 3 na Comoro inatoa tani 600.

Mazrui alisema kutokana na ubora wa karafuu ya Zanzibar uliyonayo katika soko la dunia serikali imekusudia kuekeza zaidi katika zao la karafuu kwani mwaka uliopita Zanzibar ilipata zaidi ya asilimia 67 ya pesa za kigeni.

“Tukiuza karafuu tunapata fedha za kigeni hasara ya kupeleka nje ya nchi ni kukoa fedha za kigeni” alisema Mazrui.

Serikali imetenga kiasi cha Dola milioni 11 za kimarekani ili shirika la ZSTC kuanza kununua karafuu za wakulima ambapo aliwaahidi wananchi na wakulima kwamba hakutakuwa na mkopo kila mkulima atalipwa fedha zake taslim atakapopeleka karafuu zake katika shirika.

Alisema atakuwa karibu na wakulima wa karafu kwa ajili kuwatatulia matatizo yao ya zao hilo ikiwa ni pamoja na kuwapatia miche ya mikarafuu lengo likiwa ni kuwahamasisha wakulima.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s