Zanzibar yawakaribisha diaspora

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Mwinyihaji Makame Mwadini

ZANZIBAR YAKARIBISHA DIASPORA

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefunguwa milango wazi kwa Wazanzibar waliopo nje ya nchi kuja nchini na kushirikiana na wananchi katika ujenzi wa nchi na kuleta maendeleo zaidi kufuatia kuwepo kwa mazingira mazuri ya kisiasa ya amani na utulivu nchini.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Mwinyihaji Makame Mwadini wakati akiwasilisha makadirio mapato na matumizi ya bajeti hiyo kwa mwaka wa fedha 2011-2012 hapo katika baraza la wawakilishi.

Dk Mwinyihaji alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambuwa mchango mkubwa wa wananchi hao katika kusaidia na kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo imeanzisha idara ya kuratibu maendeleo ya wazanzibari walipo nje inayojulikana kwa jina la Diaspora.

Alisema Idara ya Ushirikiano wa kimataifa na uratibu wa shughuli za Wazanzibari waliopo nchi za nje (DIASPORA) tayari imeandaliwa mipango ya kuwashirikisha wataalamu mbali mbali katika mikutano ya kikanda ikiwemo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mjadala wa soko la sarafu.

Aidha Idara hiyo pia imeanza utaratibu wa kukutana na wazanzibari walionje ya nchi ikiwemo Uingereza na kuwataka kuwa tayari kushirikiana na serikali ya Zanzibar kwa kutoa michango yao baada ya kuandaliwa kwa mpango na sera inayowashirikisha na serikali yao.

Dk Mwinyihaji alisema mazingira ya kisiasa yaliopo sasa ni mazuri,ambapo Zanzibar ipo chini ya mfumo wa Serikali ya umoja wa kitaifa iliyowashiriikisha wanan chi wote kufanya kazi.

Aliwaambiya wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba serikali tayari imeanza kufanya mawasiliano na wazanzibari waliopo nje kuja na kushirikiana na wananchi kwa ajili ya ujenzi wa nchi.

Alisema mafanikio hayo yameanza kuzaa matunda ambapo wizara ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa kwa kushirikiana na umoja wa wazanzibari waliopo Uingereza kufanya mkutano mkubwa ambao ulikuwa na lengo la kuwakutanisha na kutambuwa Mchango wa Watanzania walio nje ya nchi.

“Mkutano ule ulikuwa na manufaa makubwa ambapo ulihudhuriwa na waziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa Bernard Membe…..watendaji wetu kutoka SMZ walihudhuria na mambo mengi yalizungumzwa kwa faida ya Zanzibar ikiwemo kuitangaza Zanzibar”alisema Mwinyihaji.

Alisema tangu kufanyika kwa mkutano huo yamekuwepo mafanikio makubwa kwa baadhi ya wananchi wazanzibari waliopo nje kuonesha nia ya kuja nchini na wengine kusaidia shunguli mbali mbali za ujenzi wa taifa.

Mwinyihaji aliliambiya baraza la wawakilishi kwamba Zanzibar inashirikishwa kikamilifu katika mikutano mbali mbali ya kimataifa na kanda ikiwemo taasisi za kimataifa.

Kwa mfano Mwinyihaji alisema kwamba Zanzibar itanufaika kwa kiasi kikubwa kufuatia kuanzishwa kwa eneo huru la biashara la utatu COMESA pamoja na Jumuiya ya Afrika ya mashariki pamoja na SADC.

Alisema eneo la soko hilo ni muhimu sana likiwa na nchi wanachama zipatazo 26 likiwa na idadi ya watu Milioni 600 na wastani wa pato la taifa linalofikiya dola za kimarekani Trilioni moja.

Mwinyihaji alisema kuanzishwa kwa soko huru la utatu utakuza biashara na kuongeza uwekezaji katika viwanda na kukuza miundo mbinu katika nchi wanachama wa jamhuri ya muungano wa Tanzania.

“Mheshimiwa hili eneo la biashara la utatu ni muhimu sana tukilitumia vizuri basi yapo manufaa makubwa ya kuimarika kiuchumi na biashara” alisema waziri huyo.

Aidha aliwaambiya wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba Zanzibar inashiriki kikamilifu katika vikao vyote vya jumuiya ya Afrika ya mashariki,ambapo watendaji wake wamekuwa wakishiriki katika mikutano ya matayarisho la baraza la mawaziri na wakuu wa nchi.

Mwinyihaji aliliomba baraza la wawakilishi kuidhinisha jumla ya sh.33,127,.2 Milioni ambapo kati ya hizo jumla ya sh.29,386.2 kwa ajili ya kazi za kawaida na jumla ya sh.1,930.0 kwa kazi za maendeleo katika mwaka 2011-2012.

ZIARA ZA MAALIM SEIF ZIMELETA TIJA

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wameipitisha bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ambayo iliwasilishwa juzi Barazani hapo na waziri wa Wizara hiyo Fatma Abdul-habib Ferej huku akitetea ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais nje ya nchi kwamba zilikuwa na maslahi na faida kubwa kwa maendeleo ya nchi.

Bajeti hiyo ilipitishwa baada ya wajumbe wote wa baraza hilo kuridhishwa na ufafanuzi wa hoja na masuali yao waliyouliza wakati wakijadili ambapo alitaja ziara za Makamu wa Kwanza faida zake ni nyingi ikiwemo ile ziara ya nchi za Mashariki ya Kati alipokutana na wafanyabishara na wawekezaji ambao baadhi yao wameonyesha nia ya kushirikiana na Zanzibar katika uwekezaji kufungua mahusiano kati ya Zanzibar na nchi hizo.

Katika ziara ya nchi za kiarabu ikiwemo Oman Waziri huyo alisema Makamu wa kwanza katika ziara yake hiyo imefungua milango kwa kurejesha mahusiano mema kwa kuwa Zanzibar na Oman ni marafiki na ndugu wa muda mrefu ambapo katika mazungumzo hayo yameweza kurejesha upya safari zake kati ya Oman na Zanzibar, mazungumzo ya kuanzisha shirika jipya la ndege la Zanzibar na msaada wa uchimbaji mafuta.

Wakati wakichangia hutuba ya bajeti ya ofisi ya makamu wa kwanza wa rais baadhi ya wawakilishi walitaka kujua mafanikio yaliopatikana katika ziara za makamu wa kwanza wa rais kwa kuwa kitabu cha hutuba hakijaeleza mafanikio yoyote yaliopatikana katika ziara hizo.

Aidha waziri huyo alisema mbali ya faida hizo, pia yalifanyika mazungumzo ya kuomba msaada wa ujenzi wa Bandari mpya na kudumisha uhusiano mwema baina ya Zanzibar na nchi za eneo hilo.

Akizungumzia suala la madawa ya kulevya ambalo limechukua muda mrefu kujadiliwa na wajumbe na kuitaka serikali kujikita katika suala hilo kwa kuweka mkazo mahsusi kwa lengo la kuwanusuru vijana Waziri huyo alisema anakubaliana na maoni ya wajumbe na kuahidi kwmaba serikali itaendelea na juhudi zake na kupambana na tatizo hilo kwa kushirikiana na vyombo husika na wananchi.

Kuhusu maambukizi ya vizuri ya ukimwi Ferej alisema Zanzibar kwa akiasi fulani imefanikiwa kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi na kueleza huku akijibu hoja za wajumbe ambao wamehji mfuko huo kutengewa fedha nyingi alisema ni kutokana na umuhimu wa kazi hiyo kubwa na kupambana na ukimwi.

Alisema Ofisi ya makamu wa kwanza wa rais ipo kwenye mikakati ya kuangalia mapungufu ya sheria ili kuweza kuzuia uingiaji wa dawa hizo nchini ambazo zimekuwa zikiathiri vijana wengi na hatimae kupata maambukizi ya vizuri vya ukimwi.

Kuhusu uharibifu wa maliasili zisizorekebishwa alilifahamisha baraza hilo kuwa Ofisi yake ipo hatua za mwisho kuweka kanunui ambazo zitasaidia kuzilinda na kuzififadhi kwa manufaa ya vizazi vilivypo na vijavyo.

Alisema Zanzibar inakabiliwa na changamoto ya tabia nchi, ikiwemo mashamba kuingia maji ya bahari, maji kuingia chumvi na hata baadhi ya maeneo kumengwa na bahari na kubainisha kuwa ofisi inaandaa mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Wakichangia bajeti ya Ofisi hiyo wajumbe hao wajumbe wa Baraza hilo waliomba nyumba za Sober House ambazo zimekuwa zikiwahifadhi vijana walioacha matumizi ya dawa za kulevya kujengwa mbali ya nyuma za makaazi ya watu.

Aidha alizungumzia suala zima la sekta ya utalii ambapo alisema zinapaswa kuwa na mikakati ya madhubuyi ya kupunguza kasi ya maambukizi ya ukimwi, pamoja na kuongeza kasi ya mapambano hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar imekuwa na uingiaji na utokaji mkubwa wa watu kutoka sehemu mbali mbali.

DK CHEIN KUONGEA KILA MWEZI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein ataanza kuwasiliana na waananchi kupitia vyombo vya habari kila baada ya miezi mitatu imeelezwa.

Hayo yameelezwa waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, wakati akisoma bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2011/2012 ndani ukumbi wa Baraza la wawakilishi uliopo Chukwani Mjini Zanzibar.

Alisema Utaratibu huo una dhamira ya kukuza mawasiliano kati ya wananchi na serikali yao na waandishi wa habari watatakiwa kuuliza maswali mbali mbali yatakayotolewa ufafanuzi ili wananchi wapate kujua masuala yanayoendelea katika serikali yao.

Lengo la kutekelezwa kwa mpango huo moja ni kuwasiliana na wananchi moja kwa moja lakini pia kuweka twaasira nzuri baina ya Rais na wananchi wake na washirika wengine wa maendeleo ambao wanaisaidia Zanzibar katika masuala mbali mbali.

Alisema katika mazungumzo hayo na vyombo vya habari yatalenga zaidi masuala yanayohusu Zanzibar na maendeleo yake kwa kuwaelezea wananchi yale yalioahidiwa na serikali kuyatekeleza katika awamu hii ya saba.

Waziri huyo alisema kuwa utaratibu huo utapoanza kutumika utaweza kukuza mawasiliano ya umma kama kiungo kati ya rais na wananchi wake ambapo wizara hiyo imeamua kuutumia baada ya kuimarisha taasisi ya mawasiliano Ikulu.

Hatua ya serikali kuanzisha utaratibu wa rais kuzungumza na vyombo vya habari umeitikiwa kwa furaha na wajumbe wa baraza la wawakilishi wkatai wakichangia bajeti hiyo ambapo wamesema ni hatua nzuri ambayo itatoa fursa ya wananchi kufahamu yanayofanyika kwa serikali yao.

Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu alisema wananchi wengi wamekuwa na malalamiko juu ya serikali yao kutokana na ukimya wa taarifa juu ya mambo muhimu yanayotendea ndani ya serikali yakiwemo yake ya mafanikio.

Alisema katika kipindi kifupi cha serikali ya umoja wa kitaifa kmekuwepo na mafanikio makubwa ambayo wananchi walipaswa kuyafahamu lakini kutokana na kutokuwepo taarifa sahihi kwa wananchi imesababisha wananchi hao kulalamikia sana serikali yao jambo ambalo alisema linapaswa kuwekwa wazi ili wajue nini serikali yao inawafanyia kwa lengo la kukuza demokrasia na maendeleo ya nchi yao.

“Ni utaratibu mzuri ulioanzishwa kwamba mheshimiwa rais atakuwa na mazungumzo na waandishi wa habari kila baada ya miezi mitatu….yapo mambo mengi ambayo amefanyika tokea kuanza mfumo mya wa serikali ya umoja wa kitaifa lakini wananchi haafahamu kwa kuwa hayaelezwi sasa kwa utaratibu huu itasaidia kupunguza malalamiko ya wananchi” alisema Jussa.

WAZANZIBARI WATANO NI MABALOZI

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kwamba ni Wazanzibar watano tu ambao wana hadhi ya kuwa mabalozi kamili wanayoiwakisha Tanzania nje ya nchi.

Waziri wa nchi ofisi ya makamo wa pili wa rais Mohamed Aboud Mohamed aliliambiya baraza la wawakilishi. Kati ya Wazanzibari hao wawili tayari wamestaafu kazi akiwemo aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Italia balozi Ali Karume.

Aboud alisema hayo wakati alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na mwakilishi wa jimbo la Kiwani (CUF) Hijja Hassan Hijja aliyetaka kujuwa ni wazanzibari wangapi ambao ni mabalozi kamili wanayoiwakilisha Tanzania nje ya nchi na vigezo gani vinavyotumika katika kuwachaguwa.

Akifafanua zaidi Aboud aliwataja mabalozi hao kuwa ni Balozi Mohamed Mwinyi Mzale ambaye anaiwakilisha Tanzania huko Sweden, balozi Ali Shauri anayeiwakilisha Tanzania Misri,balozi Omar Ramadhan Mapuri aliyeko China pamoja na Ali Karume aliyekuwa Italia na Hussein Said Khatib huko Oman ambao tayari wamestaafu kazi.

Alifafanua na kusema kwamba vigezo vya mtu kuwa balozi kamili anayeiwakilisha Tanzania ni kufuata ngazi mbali mbali ambazo zipo katika wizara ya mambo ya nchi za nje ikiwemo vyeo na elimu.

Aidha alisema uamuzi wa kuteuliwa kuwa balozi unatokana na rais wa nchi ambapo akiamuwa kumteuwa mtu kuwa balozi basi anakuwa balozi na kumtangaza.

Aboud alisema Zanzibar haina sifa kuwa na ofisi kamili za ubalozi wa nchi za nje ziliopo Tanzania ambapo kwa mujibu wa sheria za kibalozi,makao makuu ya nchi ndiyo huwepo ofisi za kibalozi.

Kwa sasa Zanzibar zipo ofisi ndogo za ubalozi wa nchi za nje ikiwemo ubalozi wa China.India pamoja na ubalozi wa Misri,Oman pamoja na Msumbiji na nchi za Skandinavia. Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa ni miongoni mwa mambo yaliomo katika orodha ya mambo ya muungano ya asili.

FEDHA ZA WAJASIRIRIAMALI TAYARI

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema tangu kuanzishwa kwa mfuko wa kusaidia wajasiriamali unaojulikana kwa jina la AK pamoja na JK jumla ya sh.1,463,640,000 zimetumika kwa ajili ya kuwakopesha wajasiriamali mbali mbali Unguja na Pemba.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji wananchi Kiuchumi na Ushirika Haroun Ali Suleiman wakati akijibu swali aliloulizwa na mwakilishi wa jimbo la Matemwe (CCM) Abdi Mosi Kombo aliyetaka kujuwa wananchi wa kipato cha chini wamefaidika vipi na mifuko hiyo.

Haroun alisema jumla ya sh.Bilioni mbili zimebakia zikiwa zinawasubiri wajasiriamali kwa ajili ya kukopeshwa na kuanza kufanya miradi mbali mbali ya maendeleo na kukuza uchumi.

‘Mheshimiwa spika mfuko wa JK na AK kwa sasa upo katika harakati za kuwapatia elimu ya ujasiriamali wananchi mbali mbali kwa ajili ya kupiga hatua kubwa za kiuchumi’alisema Haroun.

Aidha alisema mipango imo mbioni kuona kwamba unaanzishwa mfuko wa AS ambao ni wa rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi dk.Ali Mohamed Sheni.

‘Mheshimiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi Serikali ipo katika hatua za mwisho kuanzisha mfuko wa AS ambao ni wa rais wa Zanzibar dk.Ali Mohamed Sheni’alisema Haroun.

Alisema suala la kuwapatia elimu ni muhimu sana kwa wajasiriamali ambao watapewa mikopo hiyo ni ili kuweza kujuwa kama wakipata fedha hizo watazitumia kwa njia gani.

Alikiri mikopo iliyopita ambayo walipewa wajasiriamali mbali mbali Unguja na Pemba marejesho yake yalikuwa na matatizo hali ambayo ilipelekea benki kusitisha utoaji wa mikopo hiyo.

Haroun aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba wananchi katika majimbo ya uchaguzi wakae mkao wa kula kwa ajili ya kuibuwa miradi mbali mbali ambayo wataifanyia kazi wakati watakapopewa fedha hizo.
Alisema lengo la serikali ya mapinduzi ya Zanzibar lengo lake kubwa ni kuona kwamba wananchi wake wakiwemo wajasiriamali wanajikomboa na umasikini wa kipato.

ZIARA ZA SHEIN ZALETA MATUNDA

Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imesema kwamba ziara zilizofanywa na rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Sheni zimeanza kuleta matunda ikiwemo ile ya Uturuki.

Hayo yalisemwa na waziri wa nchi ofisi ya rais na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Dk Mwinyihaji Makame wakati akiwasilisha makadirio mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2011-2012.

Dk Mwinyihaji alisema rais Shein alifanya ziara ya kiserikali nchini Uturuki mwaliko wa mwenyeji wake rais wa Uturuki Abdull Gul ambapo nchi hiyo imeahidi kuisaidia Zanzibar katika sekta mbali mbali ikiwemo utalii, uwekezaji pamoja na sekta ya afya.

Alisema katika sekta ya afya, Uturuki kupitia wataalamu wake wanatazamiwa kufanya ziara kuja Zanzibar na kuangalia maeneo ya kuisaidia Zanzibar.

Aidha alisema Uturuki itaipatia Zanzibar nafasi za masomo kwa vijana mbali mbali wa Zanzibar katika sekta ya afya, ikiwemo kuipatia madawa,madaktari pamoja na wataalamu wa maradhi ya moyo.

Katika sekta ya utalii, serikali ya Uturuki imeonesha kuisaidia Zanzibar katika maendeleo ya sekta ya utalii na kuifanya sekta hiyo kusaidia kuingiza mapato ya nchi.

Katika mikakati hiyo, Uturuki inakusudia kuimarisha Chuo cha Utalii kiliopo Maruhubi kwa ajili ya kukipa nyenzo mbali mbali ili kuweza kutoa mafunzo zaidi kwa wanafunzi wanaosoma hapo.

Aidha alisema mazungumzo yameanza kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na serikali ya Uturuki kuanzisha safari za shirika la ndege moja kwa moja kuja Zanzibar.

Hatua hiyo Mwinyihaji alisema kwamba itasaidia sana kuinuwa sekta ya utalii kwani Zanzibar itakuwa ikipokea watalii moja kwa moja kutoka nchi mbali mbali za bara la Ulaya na Asia na hivyo kufanikiwa kulifia soko la Asia.

Katika hatua hizo hizo za kuimarisha sekta ya utalii, Uturuki imekubali kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la kihistoria la Beit-el-Jaib liliopo eneo la mji mkongwe kwa ajili ya kuimarisha haiba yake ambayo ni moja ya kivutio kikubwa cha sekta ya utalii na historia.

Katika sekta ya elimu, Mwinyihaji alisema kwamba Uturuki imeonesha nia nzuri ya kuipiga jeki sekta ya elimu ambapo mashirikiano yameanzishwa kati ya Chuo kikuu cha Zanzibar SUZA pamoja na Vyuo vikuu vya Istambul na Ankara Uturuki.

Katika sekta ya kilimo, serikali ya Uturuki imekubali kukisaidia na kukipa uwezo Chuo cha Kilimo kilipo Kizimbani kwa ajili ya kuimarisha huduma za wanafunzi.

Alisema Chuo hicho kitapewa uwezo wa kufanya tafiti mbali mbali za kitaalamu ambazo zitasaidia kuwafanya wakulima kupiga hatua kubwa ya kuzalisha mazao mengi.

“Mheshimiwa kwa ujumla ziara ya rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Sheni nchini Uturuki imekuwa na mafanikio makubwa katika sekta mbali mbali kwa maslahi ya wananchi wa visiwa hivi” alisema.

Advertisements

5 responses to “Zanzibar yawakaribisha diaspora

 1. Ni vyema Salma unavyotupa habari za Baraza la Wawakilishi, lakini ingelikuwa vyema zaidi kama ungelizitenganisha kwa ajili ya ufahamu na mijadala pia. Kwani zikiwa zimechanganywa hivi, msomaji anakosa hamu ya kusoma mambo mengi kwa wakati mmoja na pia inakuwa vigumu kuchangia. Kwa mfano, stori kuhusu Wazanzibari walio kwenye nafasi za ubalozi imemalizia kwa kusema kuwa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ni katika mambo ya asili ya Muungano. Huu si ukweli. Ukweli ni kuwa Mambo ya Nje tu ndilo lililomo katika orodha ya mambo 11 ya asili ya Muungano. Ushirikiano wa Kimataifa halijawahi kuwa jambo la Muungano hadi sasa, ingawa wizara ya Mambo ya Nje imechanganywa kinyemela na Ushirikiano wa Kimataifa.

 2. baada ya wananchi kuanza kupayuka kutoona cho chote kilofanyika baada ya miezi saba naona kunataharak ,hivyo watazungumza wakati wa budget tuu miezi iliyobaki wale kuku naona wametoa too little too late tunaona zaidi ni maneno kuliko vitendo , uhalifu uomezidi usalama hakuna watu wanaingia nchini bila ya mpango ajira walizoahidiwa vijana hamna naona mawaziri bado wapo honeymoon yapo mengi yanaweza kurekebishwa , leo tunamsikia abubakar khamis anatuhalalishia muungano na unajua zimetumika hadaa kongomano ilikuwa tosha kusema wazanzibari wanaburuzwa la leo lifanywe leo wawakilishi na wabunge wajue hawana time ya kulala mahkama iwe huru tunajua wengi wa wabunge na wawakilishi wamepita kwa mazingaombwe sio chaguo la watu kuanzia rais bila ya kuwa true representive wa watu hakuna kitachofanyika tusihalalishe haramu kutegemea kheri

  • Na hao wawakilishi wengine kazi yao ku entertain waigizaji wa Bongo movies wakati wanawake wanaowazalisha wanashindwa kuwatunza na watoto ila pesa za kustarehesha waigizaji wanazo.

 3. Nimefarijika Mh Mwinyi kwa kutukaribisha wazanzibari tulioko nje kuja kuekeza zanzibar,kwanza tungeiyomba serikali sisi wazanzbari tuliko nje tumepoteza uzanzibari wetu kwa kupatia uraia huku njee,sasa basi kuna vikwazo sasa hivi vimetukabili kama umiliki wa ardhi,sisi ni wazaliwa wa zanzibar tunataka kurudi nyumbani kuwekeza na kuishi kabisa,lakini sasa hivi hatuwezi kumilikishwa ardhi kwa sababu hatuna vipande vya ukaazi,sasa tunaomba serikali badala ya kutumia vipande vya ukaazi pia tutumie hata vyeti vye vya kuzaliwa ili tuweze kumili ardhi.

  Suala jengine katika sector ya afya,tunaomba serikali ipe kipao mbele sana zaidi kwa sababu tatizo kubwa sisi linalotukabili zanzbar huduma hii,na kama hakuna huduma ya uhakika na madawa tutashindwa kuja kuwekeza na pia kuwashawishi watu wengine mataifa mengine kuja kuwekeza.

  Suala la Ushuru,limekuwa usumbufu sana,sisi wazanzibari tuliko njee tunataka kulete bidhaa mbali mbali za kibiashara lakini imekuwa kero na TRA kwa kutusumbua na kutukomoa katika kodi,halii ndio inyodhoofisha uchumi wa zanzibar,tunawaomba viongozi mujitahidi hili suala muliondoe katika orodha ya muunganono ya forodha,TRA iyondoke zanzibar,ikiwa kweli munataka tujenge nchi.

  Elimu nayo ndio muhimu zaidi,tuna familia zetu tunataka kuja nazo huko nyumbani,tunawaomba vingozi hili suala pia mulipe kipaombele,kwanza natoa shukurani sana kwa serikali ya umoja wa kitaifa kutoa ushiriano wenu kwa pamoja kwa kuunda wizara ya zanzibar ya mikopo ya wanafunzi,tunaomba pia mutuondolee hili suala la NECTA na badala ya tuwe na baraza letu la mitihani NECZA ili kuepuka tatizo la watoto wetu kufelishwa,niliwahi kuongea na mwalimu mmoja kutoka tanganyika anasomesha zanzibar,ananiambia kuwa zanzibar watoto wanasoma sana ukitofautisha na tanganyika lakini anashangazwa sana kuona tunafail,kwa hio hii ndio ishara tosha kuwa wanafelishwa watoto wetu.

  Jengine tunaomba serikali ijenge maghala ya kisasa,ma shopping makubwa ili iwe kivutio kwa wafanya biashara na wawekezaji wengine,kuna wawekezaji huhitaji ma factory tu moja kwa moja,au mashopping na kuwekeza biashara zao.

  Tunaomba serikali iyongee na serikali ya japan,china kuwekeza zanzibar katika sector za bishara kwa mfano ma company ya toyota,PC world,n.k. waje kuweka vituo vyao zanzibar ili kukuza uchumi na kutanua kibiashara.

 4. ASALAM ALAYKUM!

  Mie mmoja ambaye ninaunga mkono hilo la kuwakarifu Muhajirina au Waliondoka na kuishi nje kurudi nyumbani lakini suala langu kubwa tumeandaa Mpango gani? Nini tunachotaka kuchangiwa? Hawa watu wengi wao wana Passporti za kigeni sasa wakija tunawachukulia vipi?

  Programu za Muhajirina zimepata mafanikio mengi Afrika khasa khasa Somali, Kenya, Uganda na hata Zanzibar ingawa Zanzibar haielewi kinacholetwa ni kiasi gani na hawa walio Hajir na vipi kinatumika.

  Ninachoamini kinachohitajika kufanyika kwa sasa nikuandaa Strategy kisha tukaisambaza kwenye MTANDAO, baada ya hapo tukaitisha Mkutano/Kongamano la Uwazi kwenye miezi ya June-July kuwaalika hawa wenzetu.

  Pakuanzia ni pale ambapo niliwahi kuomba kupitia ZANZINET kuandaa Data Base ambayo tutajijua, kwa ufupi Jina, Umri, Qualification , nchi unayoishi, Uraia, baada ya hapo katika kuichambua hiyo Data Base tutaona nini tunachoweza kukifanya.

  Area ya Health kama tutaipata kwa mfano, tuna Madaktari wangapi Muhajirina tuseme 50 kati ya hao Madaktari wa watoto wangapi? Mifupa wangapi? Watoto wangapi? Moyo wangapi Sukari wangapi? n.k. Kisha kati ya hao waliostaafu ni wangapi? Wangapi katika kipindi cha miaka 5 ijayo nao watastaafu, baada ya hapo hawa watu baada kuwa na anuwani zao tutakuwa na Desk la Health, Environment, Energy, Education etc. Watu wakila Desk watatakiwa wawasiliane na individulas kwanza kutaka kupata opinion zao na kueleza kuwa nini utakuwa mchango wao? Taarifa zitazokusanywa ndio itayopelekea mazungumzo ya katika Kongamano.

  Sio Muhajirina wote bado wanahisia na wanataka kuja au kusaidia, hilo lieleweke fika wala tusijidanganye, muhimu ni kuwafahamu wale wenye hisia na sio tu wao nini watakachokifanya kwa mahali amabapo wana Usuli nako, lakini na jee Zanzibar itawafanyia nini? Haya ni mambo yalio muhimu kutekelezwa kwanza.

  Muhajirina ni watu waliondoka Zanzibar kwasababau mbalimbali, muhimu kuwapokea wala sio kuwahoji, kwani tutapokosea tu, itakuwa lengo zima limekwenda Arijojo.

  Ndivyo Nionavyo

  Mzee Shari

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s