ZNZ haina sheria ya uchimbaji mafuta

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Zanzibar, Omar Yussuf Mzee

ZANZIBAR HAINA SHERIA YA UCHIMBAJI MAFUTA

LICHA ya Zanzibar kutokuwa na sheria ya kuchimba mafuta wala haiwezi kutoa leseni kwa ajili ya kazi hizo, Serikali Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijaizuilia Zanzibar kuchimba mafuta yake.

Sheria iliopo hivi sasa ya kuchimba mafuta ni ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar inataka suala la mafuta liondolewe katika mambo yaliopo katika orodha ya mambo ya Muungano.

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Zanzibar, Omar Yussuf Mzee ameliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi jana wakati akifanya majumuisho na kujibu hoja mbali mbali za bajeti yake katika kikao kinachoendelea huko Chukwani Mjini Unguja.

“Waheshimiwa wajumbe Zanzibar haijazuwiliwa kuchimba mafuta yake lakini tatizo hadi sasa hakuna sheria ya kuchimba mafuta….sheria iliopo ni ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kama tukichimba basi mafuta hayo yatakuwa pamoja na Muungano hayatakuwa peke yetu” alisema Mzee.

Mzee alilazimika kutoa ufafanuzi wa kina katika suala la mafuta na gesi kufuatia wajumbe wengi waliochangia bajeti ya serikali kulalamika kwamba serikali haijaeleza lolote kuhusu suala la mafuta na gesi ambalo tayari limeamuliwa na baraza la wawakilishi kwamba liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano.

Asilimia 70% ya wajumbe wa baraza la wawakilishi waliochangia bajeti ya serikali kwa mwaka 2011-2012 walizungumzia suala la mafuta na kuitaka serikali haraka kuharakisha mipango ya uchimbaji wa nishati hiyo ambayo kwa mujibu wa tafiti mbali mbali zinaonesha kwamba mafuta yapo pamoja na gesi katika mwambao wa visiwa vya Unguja na Pemba.

“Mafuta ni sehemu ya uchumi wa Zanzibar na mambo ya uchumi wa Zanzibar hayamo katika mambo ya Muungano hivyo wawakilishi kutaka suala la mafuta litolewe katika mambo ya Muungano ni sahihi”alisema Waziri Mzee.

Alisema suala la mafuta zipo sehemu ya alama nne zinazoonesha kuwepo kwa mafuta, ambapo tayari yapo makampuni mbali mbali kutoka Uingereza, Urusi na Brazil wameonesha nia hapa nchini kwa ajili ya kazi za uchimbaji mafuta.

Hata hivyo alisema wawekezaji watakaokuja kuchimba mafuta watahitaji kupatiwa leseni za kazi za uchimbaji ambapo hutolewa na jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa sababu Zanzibar haina sheria ya mamlaka ya kuchimba mafuta.

“Waheshimiwa wajumbe tukiamuwa leo tunataka kuchimba mafuta basi tunaweza kufanya hivyo…lakini je tujiulize sheria ya kuchimba mafuta tunayo? Na jee utoaji wa leseni? Alihoji waziri huyo.

Alisema inawezekana kuamuwa kuchimba mafuta sasa kwa kushirikiana na muungano au kusubiri hadi kukamilika kwa taratibu za kuliondowa suala hilo katika orodha ya mambo ya Muungano.

Waziri huyo alisema Zanzibar inataka kuliondowa suala la mafuta katika orodha ya mambo ya muungano ni kulipeleka suala hilo bungeni na huko kufuata taratibu zake kwa kupigiwa kura na wajumbe wa bunge la Jamhuri ya Muungano.

Hata hivyo Mzee alisema suala la kuondoshwa mafuta katika orodha ya mambo ya muungano linahitaji nia njema na kupata baraka kutoka kwa rais Jakaya Kikwete akishirikiana na rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Sheni tu.

“Waheshimiwa wajumbe wenzangu hili ni suala la kuwepo kwa nia njema kwa viongozi wetu mheshimiwa Rais Kikwete na mheshimiwa rais Dk Shein” alisema waziri huyo.

Akizungumzia suala la kujikwamua na uchumi alisema serikali ya Zanzibar imeweka kipaumbele katika sekta ya uwekezaji ikiwemo ya viwanda kama mkombozi na kuongeza ajira kwa wananchi wake.

Alisema hadi sasa mchango wa sekta ya viwanda katika pato la taifa ni mdogo sana hivyo mkazo utawekwa katika kuwekeza viwanda vidogo vidogo ambavyo vitasaidia kuongeza ajira na sekta ya uzalishaji wa vyakula.

Katika kuimarisha dhana ya utawala bora alisema serikali imo katika hatua za kutayarisha sheria ya viongozi kutangaza mali zao ikiwa ni sehemu ya kuimarisha dhana ya utawala bora.

Alisema baadhi ya viongozi waliomo katika baraza la wawakilishi tayari wametangaza mali zao kupitia bunge la jamhuri ya muungano ambalo linao utaratibu kama huo wa kutangaza mali za wajumbe na viongozi wa serikali.

“Mheshimiwa spika mimi tayari nimetangaza mali zangu kule bungeni…..hapa yupo makamo wa pili wa rais balozi Seif Ali Iddi amefanya hivyo pamoja na waziri Haroun na Fatma Fereji na wengine” alisema.

Waziri huyo alisema katika kusimamia maadili ya viongozi waziri mwenye dhamana ya waziri wa nchi afisi ya rais na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Mwinyihaji Makame afanye iwezekavyo apeleke haraka sheria ya kutangaza mali za viongozi ambazo wazoefu wapo wataweza kumsaidia katika suala hilo.

“Kiongozi aliechuma mali kwa nguvu zake hawezi kuongopa kutangaza mali zake mheshimiwa Spika”.alisema Mzee.

Waziri huyo akifafanua bajeti hiyo kwa wajumbe alisema sekta ya viwanda inahitaji kupewa msukumo mkubwa kwa sababu ili nchi iweze kukua uchumi ambapo nchi nyigi duniani zenye viwanda zimefanikiwa kukua uchumi wake kwani kila mwaka hupanda kwa kiasi kikubwa.

Alisema mbali ya viwanda lakini nguvu ielekezwe ndani ya ufugaji uvuvi na kilimo cha mboga mboga kwani hivi sasa mahoteli yaliopo Zanzibar yanaagiza mboga mboga kuto nje ya Zanzibar hivyo alielekeza wananchi kujikita zaidi katika kilimo na mboga mboga.

Wajumbe wa baraza la wawakilishi kwa kauli moja wamepitisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2011-2012.

KARUME NI BABA WA TAIFA LA ZANZIBAR

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema rais wa kwanza wa visiwa vya Zanzibar hayati Abeid Amani Karume anatambuliwa kama ndiye baba wa taifa la Zanzibar kutokana na mchango wake mkubwa wa kuleta ukombozi wa visiwa hivi.

Hayo yalisemwa na waziri wa nchi ofisi ya makamo wa pili wa rais Mohammed Aboud Mohammed wakati akijibu swali aliloulizwa na mwakilishi wa jimbo la Chake Chake (CUF) Omar Ali Shehe aliyetaka kujuwa mwasisi wa taifa la zanzibar hayati Karume kama anatambuliwa kama ni nani.

Aboud alisema historia ya siasa ya visiwa vya zanzibar inamtambuwa hayati Karume kama baba wa taifa wa zanzibar kutokana na mchango wake mkubwa wa harakati za ukombozi wa taifa hili hadi kufikia mapinduzi ya zanzibar ya mwaka 1964.

Aidha alisema ofisi zote za serikali ya mapinduzi ya zanzibar zinatakiwa kuweka picha za kiongozi huyo,na ni kosa kwa ofisi ya serikali ambayo haitakuwa na picha yake.

Alisema eneo la Kisiwandui ofisi kuu ya CCM kwa sasa ni eneo la kihistoria kwa sababu ndiyo pahala ambapo kiongozi huyo aliuwawa kikatili na wapinga maendeleo tarehe 7-4-1972.

Alisema kutokana na serikali kutambuwa mchango wake mkubwa, tarehe 7-4-1972 ni siku ya kumbukumbu ya kitaifa ya kifo chake,ambapo hufanyika shunguli mbali mbali ikiwemo kisomo cha ibada ya hitma.

Alisema wananchi wanaruhusiwa kutembelea eneo hilo hapo kisiwandui kwa ajili ya kuona kaburi lake na baadhi ya maeneo ya kihistoria ambapo maelezo hutolewa na maofisa wahusika katika ofisi hiyo.

Serikali ya jamhuri ya muungano inamtambuwa hayati mwalimu Julius Nyerere kama baba wa taifa na rais wa kwanza wa jamhuri ya muungano wa Tanzania ambapo makamo wake alikuwa hayati Abeid Amani Karume.

ADHABU YA KIFO IPO PALE PALE ZANZIBAR

SERIKALI ya mapinduzi ya zanzibar imesema adhabu ya kifo haijafutwa kwa watu wanaotiwa hatiani na matukio mbali mbali ya uhalifu, waziri wa katiba na sheria Abubakar Khamis Bakary aliliambia baraza la wawakilishi.

Abubakar alisema hayo wakati akijibu swali lililoulizwa na mwakilishi wa jimbo la CHAANI kwa tiketi ya (CCM) Ussi Jecha Simai aliyetaka kujuwa kama adhabu hiyo bado inatekelezwa na mahakama za hapa licha ya wanaharakati kupiga kelele na kutaka kuondoshwa.

Abubakar alisema sheria ya adhabu no.6 ya mwaka 2004 kupitia kifungu cha cha 26 inaruhusu kwa mahakama kutoa adhabu ya kifo kwa baadhi ya makosa.

Alisema mtu yoyote atakayetiwa hatiani kwa kosa ambalo linatoa adhabu ya kifo pale inapoonekana inafaa basi Mahakama haitasita kutoa adhabu hiyo.

Alisisitiza adhabu hiyo haijafutwa kwa sababu sheria inaruhusu kufanya hivyo ingawa alisema inahitaji kupata baraka za rais wa nchi katika utekelezaji wake.

Abubakar ambaye alipata kuwa mwanasheria mkuu wa serikali ya mapinduzi ya zanzibar alisema utekelezaji wa adhabu hiyo sio kwenda kinyume na haki za binaadamu.

Alikiri kuwepo kwa mjadala mkubwa kuhusu kuwepo kwa adhabu hiyo au kufutwa pamoja na uhalali wake duniani kote,ambapo baadhi ya makundi yanataka adhabu hiyo isiondolewe kwa sababu mtu anayefanya kosa hilo lazima na yeye ajuwe kama akipatikana na hatia nae ananyongwa.

Hata hivyo Abubakar alisema kwamba suala hilo halijapatikana ufumbuzi wake wa kudumu ambapo kwa upande wa zanzibar ni wajibu wetu kuielimisha jamii na kupata maoni mbali mbali kwa wananchi pamoja na vyombo husika ikiwemo Tume ya kuchunguza sheria na Afisi ya mwanasheria mkuu.

Serikali baada ya kupata maoni yote hayo hatimaye itaamuwa kama adhabu hiyo kuendelea kuwepo au kufutwa moja kwa moja kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo Abubakar aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba utekelezaji wa adhabu ya kifo ni lazima upate ruhusa ya rais wa nchi.

Alipoulizwa ni watu wangapi walionyongwa hadi sasa alisema kwamba hana kumbukumbu na suala hilo atalijibu baada ya kuangalia kumbukumbu ziliopo katika taasisi husika.

Mahakama kuu ya zanzibar mwezi uliopita ilimtia hatiani na kumuhukumu Juma wa Juma kunyongwa hadi kufa na mahakama kuu ya zanzibar kwa kosa la kumuuwa kwa makusudi mpenzi wake kwa kumpiga nyundo.

SHERIA YA ZSTC

Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imesema inakusudia kutayarisha sheria mpya ambayo itaimarisha na kuainisha kazi za shirika la taifa la biashara (ZSTC) ili kuongeza ufanisi wake katika majukumu ya kuimarisha zao la karafuu.

Hayo yalisemwa na naibu waziri wa biashara,viwanda na masoko Thuwaybah Edington Kissasi wakati akijibu swali lililoulizwa na mwakilishi wa jimbo la TUMBE kwa tiketi ya (CUF) Rufai Said Rufai aliyetaka kujuwa mikakati ya kuimarisha zao la karafuu ambalo limepunguwa uzalishaji wake kwa asilimia 40%.

Kisasi aliitaja mikakati ya kuimarisha shirika hilo ikiwemo kuuanda muundo mpya wa shirika pamoja na kupendekeza wafanyakazi wanaohitajika na aina ya taaluma zao.

Mikakati mengine ni kufanya mapitio ya gharama za uendeshaji wa shirika pamoja na kuandaa sheria ya kuanzishwa kwa mfuko wa maendeleo ya karafuu.

Alisema matayarisho hayo pamoja na mapendekezo mengine lengo lake ni kuleta ufanisi wa na utendaji wa shirika hilo kwa ajili ya kuimarisha zao la karafuu na kulifanya kuwa tegemeo la uchumi wa nchi.

Aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba zao la karafuu bado ni tegemeo zaidi kutokana na bei yake katika soko la dunia kupanda.

Aidha alisema shirika la taifa la biashara ZSTC linakusudia kuimarisha zao la karafuu ikiwemo kutengeneza karafuu katika vifurushi maalumu ambavyo vitauzwa nchi za nje.

Lengo la kufanya hivyo ni kuimarisha soko la karafuu la zanzibar,ambapo karafuu zinazozalishwa visiwani hapa ni zenye ubora wa hali ya juu kutokana na ladha yake kuwa bora.

Naibu waziri alitoa takwimu na kusema uzalishaji wa zao hilo umepunguwa kwa wastani wa tani 2,673 kwa mwaka 2008-2009.

Hata hivyo alisema takwimu hizo zinaonesha kwamba wakulima wanafaidika na malipo ya ununuzi wa karafuu ambayo yanafikia kati ya sh.7,000 Milioni na sh.120,000 Milioni kwa mwaka wa msimu wa 2008-2010.

KERO ZA MUUNGANO KUMALIZWA

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kwamba yapo mafanikio makubwa katika kuzipatia ufumbuzi kero za muungano ikiwemo malalamiko ya wafanyabiashara wa zanzibar kutozwa kodi mara mbili.

Hayo yalisemwa na makamo wa pili wa rais balozi Seif Ali Iddi wakati akiwasilisha makadirio mapato na matumizi ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2011-2012 hapo katika baraza la wawakilishi mjini hapa.

Balozi aliyata baadhi ya mambo ambayo yamepatiwa ufumbuzi wake ikiwemo malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili na taasisi za kutoza kodi ikiwemo mamlaka ya mapato nchini (TRA).

Alisema kero hiyo kwa sasa haipo tena kwani bidhaa zinazoingizwa nchini na kukamilisha taratibu zote za kiforodha kupitia kituo chochote rasmin cha forodha zitahesabiwa kuwa zimeingia ndani ya jamhuri ya muungano wa Tanzania na hazipaswi kulipiwa kodi mara mbili.

Alisema katika kuhakikisha tatizo hilo halijitokezi tena nchini,mamlaka ya mapato nchini (TRA) itachukuwa hatua za kinidhamu kwa watendaji wake ambao watashindwa kutekeleza maagizo hayo halali kwa mujibu wa sheria.

Kero nyengine iliyopatiwa ufumbuzi wake ikiwemo mgawanyo wa mapato yanayotokana na misaada kutoka nje ya nchi,ambapo sasa Zanzibar inapata mafao yake yote kwa mujibu wa sheria.

Balozi alisema Zanzibar sasa inapata asilimia 4.5 misaada ya kibajeti,aidha katika mwaka wa fedha 2009-2010 SMZ imeweza kunufaika na asilimia 4.5 ya mikopo ya kibajeti .

Aidha alisema suala la utekelezaji wa sheria ya haki za binaadamu sasa limepatiwa ufumbuzi wake ambapo tume hiyo imekuwa na ofisi zake hapa Zanzibar ambapo wananchi wamekuwa wakiitumia kwa kuwasilisha malalamiko yao mbali mbali.

Balozi aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba kero zilizobakia za muungano mazungumzo kati ya pande mbili yanaendelea vizuri katika kila sekta huku yakitoa mwelekeo mzuri wa mafanikio.

Alisema lengo ni kuondowa manunguniko kwa wananchi na kila pande ili kuwepo kwa muungano bora imara wenye maslahi ya pande mbili za jamhuri ya muungano.

Akizungumzia suala la ardhi,balozi alisema kwamba visiwa vya Zanzibar kwa sasa vimekumbwa na tatizo kubwa la migogoro ya ardhi ambayo inatokana na watu kuvamia ardhi bila ya kufuata sheria.

Alisema serikali inakabiliwa na changamoto kubwa katika suala la ardhi ikiwemo kuweka utaratibu mzuri wa ugawaji wa ardhi ili kuepuka migogoro na mivutano ambayo haina faida kwa taifa na wananchi kwa ujumla.

Katika kudhibiti migogoro,balozi alisema serikali imo katika maandalizi ya sera ya ardhi ambayo itaweka wazi matumizi ya ardhi na mambo mengine kwa faida ya wananchi kwa ujumla.

Aidha aliwataka viongozi mbali mbali wa kitaifa kuepuka kujiingiza katika migogoro ya ardhi katika maeneo ya majimbo wanayoishi,ikiwemo kujifanya kwamba wao ni madalali wa kuuza ardhi.

Alisema viongozi watakaojishungulisha na migogoro ya ardhi serikali itawachukuliya hatua kali ikiwemo kuwanyanganya ardhi hizo,kwani matatizo hayo yamepunguza imani kwa wananchi mbele ya serikali yao.

Kuhusu Ukimwi,balozi alisema ukimwi ni janga la kitaifa na kuwataka wananchi kuendelea kuchukuwa kila aina ya tahadhari ili kukabiliana na janga hilo ikiwemo kundi la vijana ambalo lipo katika hatari kubwa.

Aliitaja mikakati ya kupunguza ukimwi ikiwemo kushuka kasi ya maambukizi kufikiya asilimia 0.6 ambapo jumla ya watu 7,000 wanaishi na virusi vya ukimwi Zanzibar.

Aliyataja makundi ambayo yapo katika hatari kubwa ya kuambukizi ya ugonjwa huo ikiwemo watu wanaotumia madawa ya kulevya pamoja na kujidunga sindano ambapo maambukizi yake yamefikia asilimia 10.8.

Alivitaja vitendo vya ukahaba vimeongezeka ambapo sasa maambukizi yake yamefikia asilimia 12.3 huku wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsi moja yamefikia asilimia 16.

Alizitaja wilaya zilizoathirika na kasi ya maambukizi ya ukimwi ni mkoa wa mjini mangaribi,wilaya ya kati na Chake Chake pamoja na Micheweni kwa kisiwa cha Pemba.

Alisema mpango wa awamu ya pili ya kupambana na ukimwi umeelekeza nguvu zake zaidi katika kuishirikisha sekta binafsi ambayo nafasi yake kwa jamii ni kubwa.

Mapema Balozi aliipongeza Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa kufanikisha vizuri chaguzi mbali mbali ikiwemo kura ya maoni na uchaguzi mkuu wa mwaka jana ambapo Zanzibar imepata sifa kubwa mbele ya washiriki wa maendeleo.

Aliwapongeza wananchi kwa kushiriki vizuri katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana ambapo amani na utulivu ilidumishwa kwa kiwango cha hali ya juu.

Tangu kuingia kwa mfumo wa vyama vingi na uchaguzi mkuu wa kwanza katika mwaka 1995 Zanzibar imekumbwa na machafuko ya kisiasa katika chaguzi zake kiasi ya kufikiya hatua ya maridhiano ya kisiasa ya maridhiano.

Ofisi ya makamo wa pili wa rais kwa mwaka wa fedha 2011-2012 imeomba kuidhinishwa jumla ya sh.9,129,925,000 kwa matumizi ya kawaida kati ya hizo sh.4,500,000,000 kwa matumizi mengineyo ili kutekeleza majukumu yake vizuri.
mwisho.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s