Hutuba ya Dk Salim

Waziri Mkuu Mstaafu Dk Salim Ahmed Salim akihutubia mkutano wa uzinduzi rasmi wa Taasisi ya Utafiti na Sera za Umma (ZIRPP) leo 16 Juni 2010, uzinduzi uliofanyika Hoteli ya Bwawani Zanzibar na kuhudhuriwa na watu mbali mbali ambapo Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo.

HOTUBA YA DR SALIM AHMED SALIM KATIKA UZINDUZI RASMI WA TAASISI YA UTAFITI NA SERA ZA UMMA (ZIRPP), JUMAMOSI TAREHE 16 JUNI 2010, HOTELI YA BWAWANI, ZANZIBAR.

Mheshimiwa Dk. Ali Mohammed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;

Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais;

Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi;

Waheshimiwa Mawaziri;

Mheshimiwa Mkuu Wa Mkoa wa Mjini Magharibi

Mstahiki Meya

Bibi Maryam Hamdani, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa ZIRPP;

Viongozi, Wageni Waalikwa; Mabibi na Mabwana;

Kwanza kabisa, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwenye wingi wa Rehma kwa kutuwezesha kufika hapa leo katika hafla hii muhimu ya uzinduzi rasmi wa Taasisi yetu ijuulikanayo kwa jina la “Zanzibar Institute for Research and Public Policy” (ZIRRP) tukiwa sote katika afya njema.

Pia, napenda kutumia fursa hii kuungana na viongozi wa taasisi walionitangulia, kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwako wewe Mheshimiwa Rais na kwa viongozi wote na wageni waalikwa kwa kukubali mwaliko wa kuja kujumuika nasi katika kusherehekea uzinduzi wa taasisi yetu.

Uzinduzi huu rasmi wa taasisi ya ZIRRP unafanyika kwenye wakati muhimu katika historia ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Wakati ambao wazanzibari kwa sauti ya pamoja wameweza kukubaliana na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo ina jukumu la kuongoza mchakato wa kuimarisha mahusiano na maelewano baina ya wazanzibari wote.

Kuwepo kwa Serikali hii ya Umoja wa Kitaifa kumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kujenga mazingira ya kipekee ya kisiasa, yenye kuwawezesha Wazanzibari bila ya kujali tofauti zao kuhusiana, kushirikiana na kuelewana zaidi. Hili ni jambo ambalo Wazanzibari wengi pamoja na ndugu zetu wa Tanzania bara na bara letu la Afrika kwa ujumla walikuwa na shauku kubwa kuliona.

Ni wazi kuwa matunda ya mazingira hayo ya kisiasa tayari yameanza kuonekana. Kwa muda mfupi tu ambao tumekuwa na Serikali hii ya Umoja wa Kitaifa tumeweza kuona ile hali ya chuki na uhasama iliyokuwa imeshamiri hapo kabla, imeondoka ama imepungua kwa kiasi kikubwa. Hali hii imejenga matumaini makubwa miongoni mwa Wazanzibari pamoja na wale wote wenye nia njema na kuitakia mema Zanzibar. Matumaini ambayo yanahitaji ushiriki wetu sote katika kutekeleza malengo yake.

Lakini, Serikali ya Umoja wa Kitaifa sio mwisho wa safari bali ndio mwanzo. Ni mwanzo wa safari ya kuwawezesha Wazanzibari kwa umoja wetu, kuweza kukaa pamoja, kuangalia na kubuni namna ambavyo wananchi kwa ukamilifu, wanaweza kupambana na changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Wakati tunatambua wajibu wa serikali katika kujenga misingi na miundombinu ya kuwaletea wananchi wake maendeleo, ni muhimu pia kutambua kwamba hii si dhamana ya serikali pekee. Serikali ina jukumu lake. Lakini serikali kama serikali ya wananchi ni lazima isaidiwe ipate ushirikiano na mchango wa wananchi wenyewe.

Serikali haina uwezo na wala haitakuwa na uwezo wa kutoa ufumbuzi wa kila jambo. Si serikali ya Mapinduzi Zanzibar, si serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, si serikali yoyote ya kiafrika na wala si serikali za mataifa mengine yakiwemo yale makubwa yenye kuweza kutatua matatizo yote ya wananchi wake bila ya ushiriki wa wananchi wenyewe.

Hivyo basi, ni wazi kuwa ili matumaini ya Wazanzibari yatimizwe, Serikali ya Umoja wa Kitaifa inahitaji sana ushirikiano wa wananchi kwa kupitia wananchi, mmoja mmoja au katika jumuia au katika umajumui wao.

Ndugu mgeni rasmi, mabibi na mabwana;

Wakati taasisi ya ZIRRP inazinduliwa, tunapaswa kutambua kuwa taasisi hii pamoja na taasisi nyengine za kiraia zina dhamana kubwa. Mbili muhimu katika hizo ni kusaidia serikali na kusaidia wananchi kujiletea maendeleo na ufanisi maishani mwao siku za mbele.

Taasisi zetu za kiraia, hasa taasisi za utafiti kama ZIRRP, kwa kushirikiana na serikali yetu zina jukumu la kutafiti, kubuni, kushauri na kutekeleza mikakati na miradi mbalimbali ya kisera ambayo italenga katika kuboresha uchumi na kuleta maendeleo ya watu.

Ni wajibu wa Taasisi za kiraia kushiriki katika juhudi mbalimbali za kukabiliana na changamoto zinazoikabili Zanzibar. Changamoto hizi ni pamoja na zile za Elimu, kupambana na umasikini, kupunguza ukosefu wa ajira, janga na athari za madawa ya kulevya, kuporomoka kwa maadili ya jamii yetu n.k.

Miongoni mwa changamoto nzito zinazokabili nchi zetu za Afrika ni suala la hali na mustakbali wa vijana wetu.

Kizazi cha vijana wa leo ni kikubwa sana kupita vyote katika historia ya dunia. Takriban nusu ya idadi ya watu duniani (karibu bilioni 3) ni vijana walio chini ya umri wa miaka 25. Takriban vijana 238 milioni ulimwenguni, sawa na asilimia 22.5, wanaishi katika hali ya umasikini uliokithiri – yaani wenye kipato cha chini ya $1 kwa siku. Karibu asilimia 85 ya vijana hao wanatoka katika nchi zinazoendelea.

Bara la Afrika ndilo lenye kundi kubwa la vijana linalozidi kuongezeka kwa wingi ulimwenguni. Inakisiwa kwamba takribani asilimia 70 ya watu wa Afrika ni vijana wenye umri wa miaka 30 na kushuka chini. Zaidi ya asilimia 20 ya idadi yake ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 24.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kazi Ulimwenguni (ILO), asilimia 36 ya watu wenye umri wa kufanya kazi ni vijana; na watatu kati ya watano wasiokuwa na ajira ni vijana.

Ni muhimu kutambua kuwa Zanzibar, kama zilivyo nchi zingine barani Afrika, inakabiliwa na tatizo kubwa kuhusiana na jinsi gani ya kushughulikia changamoto za vijana. Changamoto hizo ni pamoja na vijana waliomaliza shule pamoja na vyuo vikuu lakini wamekosa ajira au shughuli za kujiendeleza; vijana wanaoshindwa kumaliza shule; vijana waliokosa misingi bora kimaadili; vijana waliokata tama na pia vijana wenye kuamini kuwa wanaweza lakini wanakumbana na vizingiti mbalimbali vinavyowakatisha tamaa.

Ndugu mgeni rasmi, mabibi na mabwana;

Vijana ni rasilimali kubwa ya taifa. Ndiyo sehemu ya viongozi na watendanji wakuu wa leo na wa kesho.

Jinsi gani ya kuienzi, kuimarisha na kuitumia ipasavyo nguvu hii ni changamoto kubwa sio kwa Zanzibar tu, wala sio kwa Tanzania, bali Afrika kwa ujumla.

Katika upeo huo ni muhimu sana kuhakikisha kuwa vijana wanawezeshwa katika suala zima la uongozi wa mataifa yetu chini ya misingi ya demokrasia na utawala bora.

Taasisi kama hii yetu na taasisi nyingine za kiraia zinapaswa kuzingatia jinsi gani ya kutoa mchango thabiti ili kuliwezesha taifa kukabili changamoto hizi na nyinginezo kwa kusaidia serikali na jamii kwa jumla.

Mheshimiwa Rais, mabibi na mabwana

Taasisi hii ni changa, ina majukumu mengi, inahitaji nyenzo. Kwa bahati njema kuna Wazanzibari wengi, ndani na nje ya nchi, ambao wamejidhihirisha kuchangia katika kufanikisha malengo yake.

Miongoni mwao ni wazanzibari wenye taaluma mbalimbali na umahiri katika fani zao. Lakini hapohapo naomba kutoa mwito kwa jamii ya wazanzibari na watanzania kwa jumla waipe ushirikiano na kila msaada taasisi hii ili kufanikisha malengo yake.

Ndugu mgeni rasmi

Kwa upande wake taasisi ina jukumu la kuhakikisha inapata, inaenzi na kutumia vyema michango na ushiriki wa Wazanzibari wote, walio ndani ya nchi na wale walio nje, pamoja na wengine wote walio ndani ya Tanzania na nje ya Tanzania, ambao wana nia njema na Zanzibar, katika kujiwezesha na kutekeleza malengo na majukumu yake.

Baada ya kusema hayo, sasa nakuomba kwa heshima na taadhima, Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kutupa nasaha zako na kutuzindulia rasmi taasisi yetu.

Karibu ndugu mgeni rasmi.

Omar Ilyas
Tanzanianjema Advisory LTD
Dar Es Salaam, Tanzania

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s