Maoni kuhusu bajeti ya SMZ

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakifuatilia moja ya vikao vya baraza hilo vinavyoendelea mjini hapa akiwemo Mwakilishi wa Jimbo la Donge (CCM) Ali Juma Shamhuna anayeonekana hapo mbele

BAJETI ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyowasilishwa juzi na Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee imekosolewa na baadhi ya wananchi na wanasiasa mbali mbali kwa kushindwa kukidhi haja kutokana na serikali kutopunguza gharama za maisha kwa kuzingatia hali ya wananchi wa kawaida kuwa ngumu na kushindwa kuweka wazi kima cha mishahara ya wafanyakazi huku wadau kulalamikia kutoshirikishwa katika uandaaji wa bajeti hiyo.

Shirikisho la Vyama Huru Vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) imeilaumu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutowashirikisha katika suala zima la kuongezwa kwa mishahara kwa watumishi wa umma licha ya kuiomba serikali kara kadhaa kufanya huku shirikisho hilo likiitaka serikali kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu ongezeko la kiasi gani cha mishahara kwa watumishi wa serikali ili waweze kujuwa kwani hiyo ni moja ya haki yao ya msingi.

Katibu wa Shirikisho hilo, Khamis Mwinyi Suleiman ameyasema hayo wakati akitoa maoni yake juu ya bajeti iliyowasilishwa juzi Waziri wa Fedha. Uchumi na Mipango ya Mendeleo, Omar Yussuf Mzee katika kikao cha baraza la wawakilishi ambapo alisema mfumo wa uundaji na utayarishaji wa bajeti ya serikali ya Zanzibar una matatizo kwa sababu makundi mengi hayashirikishwi Katika uandaji wa bajeti hiyo na wamekuwa wakilalamikia utaratibu huo mwaka hadi mwaka..

katibu huyo alisema katika sheria kifungu namba 10 ya mwaka 1986 imeweka kamati za uongozi katika kila idara pamoja na kamati za uongozi katika kila wizara za serikali ya mapinduzi ya Zanzibar, lakini tatizo kubwa wizara haziwashirikishi katika uandaaji na hivyo mara zote bajeti za serikali huwa na mapungufu makubwa hasa katika suala zima la mishahara ambalo wananchi wengi wanalitegemea.

“Shirikisho letu halikushirikishwa katika uandaaji wa bajeti hii hasa katika suala la maslahi kwa wafanyakazi na kama tunavyojua wanafanyakazi wetu kwa muda mrefu kilio chao kikubwa ni mishahara kutaka kuongezewa, bajeti imetaja kuongezwa kwa kiwangi cha mishahara lakini kwa nini kuwepo na usiri mimi ndhani suala hilo liwekwe payana ni kiwango gani cha ziada kitakachoongezwa ili wafanyakazi wenyewe wajue na hiyo ni haki yao ya msingi wao kujua” alisema katibu huyo.

Aidha Mwinyi alisema amesikitishwa katika matayarisho ya bajeti hiyo ambapo ahadi za rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein imepuuzwa ambapo alisisitiza kushirikishwa kwa shirikisho la vyama huru vya wafanyakazi katika kujadili maslahi ya wafanyakazi lakini matokeo yake bajeti imeandaliwa hata bila ya wao kuchukuliwa maoni yao wakati shirikisho linamawasiliano ya moja kwa moja na wafanyaakzi wake.

“ Sote tunakumbuka ahadi za rais wa Zanzibar Dk Sheni siku aliyokuwa akihutubia kwa mra ya kwanza baraza la wawakilishi mara baada ya kuapishwa kuwa rais alitoa ahadi kwamba vyama vya wafanyakazi vitashirikishwa kikamilifu katika kujadili maslahi ya watumishi wa serikali ili kuona wanaishi katika maisha bora lakini ni jambo la kusikitisha sana kuona hata ile ahadi ya mheshimiwa rais haikuheshimiwa” alisema katibu huyo ambaye alioneshwa kuchukizwa na kitendo cha kutoshirikishwa katika bajeti hiyo.

Katibu huyo amesema kitu cha kufurahisha katika bajeti hiyo ni kuona serikali imezingatia suala la kutoongeza kodi ya aina yoyote kwa ajili ya kudhibiti mfumuko wa bei wa bidhaa mbali mbali nchini jambo ambalo linatoa faraja kwa wananchi ambao wengi wao kipato chao bado ni duni sana.

Ali Kombo Hamad ni mvuvi kutoka kisiwani Pemba akizungumza kwa njia ya simu amesema yeye na wenzake wamefurahishwa kusikia kwamba bajeti imegusa umoja wa kitaifa lakini hawajaona maelezo zaidi yaliopewa kipaumbele zaidi ya kutajwa tu kuwa serikali imezingatia suala la umoja wa kitaifa. “Hii bajeti sio mbaya lakini kusema serikali ya umoja wa kitaifa bila ya kutoa ufafanuzi kwamba mtaipa vipi umuhimu wa pekee huo umoja wa kitaifa sidhani kama serikali imewatendea haki wananchi wa Zanzibar” alisema na kuongeza kwamba suala la uvuvi halikutajwa kwa ufasaha na kupewa kipaumbele wakati wananchi wengi hasa vijijini wanategemea kipato chao kutokana na uvuvi.

Wakulima kutoka Mwera Kiongoni Aflah Said Masoud na Said Ahmed Said wamesema suala la kufanyika mapinduzi ya kilimo ni sawa lakini serikali haijazingatia umuhimu wa suala hilo kwa kuwa imesema aktika bajeti kuwa itaimarisha kilimo wakati ardhi ya kutosha ya kuendeleza kilimo chenyewe ni hapa hasa kwa kuzingatia hivi sasa mashamba mengi yanyotumiwa kwa kilimo yamevamiwa na kujengwa nyumba za kuishi huku vianzio vya maji navyo havipo salama kutokana na kuvamiwa jambo ambalo huhatarisha maisha ya wananchi wanaoishi karibu ya maeneo hayo.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mahoteli, Utalii na Mazingira (ZATHOCODAWU) Makame Launi alisema serikali ilitakiwa kuwa wazi zaidi katika suala la mishahara itaongezwa kwa kiwango gani na sio kusema itaongeza bila ya kutaja kiwango gani hasa kwa kuzingatia hali ya maisha ya wananchi wengi hapa Zanzibar ni ngumu hasa kwa kuwa mfumko wa bei umekuwa ukipata kila kukicha.

“Jambo la msingi serikali ingelifanya ingetaja viwango vya mishahara kwa sababu kama tunavyofahamu mshahara ndiyo silaha ya mfanyakazi yeyote inayomfanya kufanya kazi na kujiona kama yeye ni mfanyakazi, sasa kama unashindwa kufafanuwa kiasi gani serikali itaongeza kwa mwaka wa fedha ni tatizo kubwa hilo na hatua hiyo inaweza kuwavunja moyo wafanyakazi wengi” alisema Launi ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu wa shirikisho la vyama vya wafanayakazi.

Lauini alisema ukitoa kasoro hiyo ya mishahara mara hii serikali imejitahidi katika utengenezaji wa bajeti yake khasa kwa kuwa imejikita katika masuala muhimu kwa kuwa imegusa maeneo mbali mbali ya jamii, sekta ya kilimo, mifugo, elimu, afya na maendeleo ya ujenzi wa miundo mbinu wa barabara na kuwaondoshea umasikini wananchi wa Zanzibar.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazalishaji Karafuu Pemba (ZAPCO) Aboubakar Mohamed Ali ameshangazwa na serikali kuendelea kungangania uamuzi wake kumiliki kilimo cha zao la karafuu zaidi katika kipindi hiki cha soko huria ambapo walitarajia bajeti ya mwaka huu itatoa muangaza katika kuwaachia wananchi wauze karafuu zao sehemu watakazo na kuacha kinganganizi hicho..

Ali alisema zao la karafuu linahitaji kubinafasishwa na tayari tafiti kadhaa zinaonesha kuwa zao hilo basi kuendelea kushikiliwa na serikali kutokana na kuwa limeshindwa kuwanufaisha wananchi kwa kudhibitiwa na serikali.

“Tutaendelea kuishangaa serikali kwa tabia yake ya kuwa kinganganizi, mimi sioni sababu kwa nini serikali iendelee kudhibiti zao hili wakati tayari tafiti mbali mbali zilizofanywa ikiwemo ule utafiti wa mwaka 2003 unaonesha wazi kwamba zao hili linahitaji kubinafasishwa na wananchi wenyewe wapewe fursa hiyo” alisema Ali.

Alisema cha msingi kinachotakiwa kufanywa na serikali ni kujenga mazingira mazuri ya kuendesha biashara ya soko la karafuu pamoja na njia za kuimarisha kilimo cha mikarafuu ambapo kinyume na hivyo alisema suala la kuwepo kwa magendo ya karafuu kinachangiwa na serikali kushindwa kulibinafasisha zao hilo kwa kuwa wananchi wengi wanaona kwamba kuuza kwao nje ya nchi kunawaletea faida zaidi kuliko karafuu zao kuziuza serikali ambapo fedha wanayolipwa kutokana na mauzo hayo ni ndogo sana.

Serikali imesema itaendelea kuimarisha kilimo cha zao la karafuu lakini suala la kubinafasishwa kwa sasa bado jambo ambalo limewakera wananchi wengi hasa wananchi wa kisiwani Pemba amabo wanategemea kwa kiasi kikubwa zao hilo ambalo linaelezwa kuwa limeshika katika soko la dunia.
.
Zao la karafuu linaonekana kutokuwa na tija kwa kwa wananchi kutokana na fedha ndogo wanazozipata kutoka serikalini ambapo kilo moja shilingi 5,000 kiwango ambacho kinalalamikiwa kutolingana na kazi halisi ya uzalishaji na uuzaji wa zao hilo ambalo katika mwaka 1970 ilikuwa inaongoza duniani kwa uzalishaji wa zao la karafuu wakati hivi sasa limeanza kuchuka kwa kasi kubwa licha ya kuwa Zanzibar ndio iliyokuwa ikijulikana kwa kuzalisha kwa wingi zao hilo na lenye thamani kubwa kulinganishwa na nchi nyengine kama Indonesia na kisiwani Mauritius.

Kisiwa cha Pemba ndiyo kinachoongoza kwa uzalishaji wa zao la karafuu kwa asilimia 85% ambapo kasi ya magendo ya karafuu imekuwa ikiongezeka kwa wakulima kusafirisha zao hilo katika nchi za jirani ikiwemo Mombasa Kenya.

Wakitoa maoni yao wanasiasa wa vyama mbali mbali vya siasa wamesema kumeonekana udhaifu katika bajeti ya mwaka huu ambapo, Katibu Mkuu Zanzibar (TADEA) Juma Ali Khatib amesema bajeti hiyo haimugusi mwananchi moja kwa moja kwa sababu haijaweka wazi namna ya kuwasaidia wananchi katika kilimo hasa kwa kuzungatia Zanzibar haina ardhi ya kutosha ya kilimo ambapo alishauri serikali ingetafuta njia mbadala kwa kilimo ili wananchi waweze kuishi maisha mazuri hatua ambayo alisema haiwezi kuwaondoshea shida mwananchi wa kawaida na kama kweli serikali ina nia ya kusaidai wananchi absi ingeondosha kodi aktika bidhaa muhimu kama sukari, mchele na unga.

Amesema mishahara hata ikipandishwa chakula kwa mtu wa kawaida anahitaji elfu 15 kwa siku na huyo ni masikini wa kawaida hivyo mshahara ungeongezwa angalau kwa shilingi 25,000 kwa siku ndio serikali ingeweza kuwaisaida wananchi lakini kwa kuongeza mshahara wa mkia wa mbuzi ni kuongeza shida kwa wananchi katika kushindwa kujikimu.

Naye Mfanyabiashara Maafuru na Mkereketwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mohammed Raza amesema suala la kupanga bajeti sio tatizo lakini tatizo ni utekelezaji wa bajeti yenyewe ambao inapaswa kuwasaidia wananchi hasa walalahoi hasa watendaji wa serikali kufanya akzi zao kwa uadilifu, amabpo alisema yeye yupo tayari kutoa mikopo kwa wakulima na watu wengine wasio na uwezo lakini kwa masharti ya dhamana ya serikali.

Mwenyekiti wa Chama Cha Wakulima (AFP) Said Soud Said alisema bajeti sio mbaya lakini bado tatizo la wananchi kuwa na hali ngumu na kushindwa kumudu gharama za maisha lipo pale pale kwa kuwa bidhaa za vyakula bado ni ghali sana jambo ambalo wananchi wanashindwa kumudu gharama za maisha hadi hapo serikali itakapokuwa yatari kupunguza bei za vyakula kwa lengo la kuwasaidia wananchi hasa wa kawaida ambao kipato chao hakidizi dola moja kwa siku.

Advertisements

One response to “Maoni kuhusu bajeti ya SMZ

  1. Nakubaliana na kilio cha wafanyakazi juu ya kutojuilikana kiwango cha ongezeko la mishahara angalau kwa kutajwa asilimia inayotarajiwa. Suali la pili muhimu lakini halijapewa kipaumbele ni malipo ya pencheni kwa waliostaafu . Haieleweki kuona seriakali haijafikiria juu ya kuwaongeza malipo ya pencheni sambamba na ongezeko la mishahara. Wanaolipwa pencheni walikuwa watumishi wa serikali na wanaishi katika mazingira ya aina moja na watumishi wa serikali ambao hudai nyongeza kila mwaka. Haieleweki kwa nini seriakali isiweke uataratibu wa kuwaongezea posho wastaafu.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s