Uchangiaji damu kwa hiyari

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amezindua uchangiaji damu na kuwataka wananchi wajitolee kutoa damu kwa lengo la kuwachangia wananchi wenzao wanaopatwa na shida

Tukumbuke kuwa UKIMWI unabaki kuwa tishio kubwa katika dunia.  Mpaka sasa hapa kwetu watu 6 kati ya kila watu 1000 (0.6%) wana UKIMWI.  Na iwapo kama Serikali isingechukua hatua hii ya Damu Salama na hatua nyenginezo zifaazo basi UKIMWI ungeweza kukua kwa kasi kubwa sana .    Hatua hii ina mchango mkubwa katika kudhibiti kasi ya ongezeko la maradhi haya thakili ya UKIMWI pamoja na maradhi mengine yanayoambuzikwa kwa njia ya damu kama vile homa ya ini (hepatitis) na kaswende (syphilis).

HOTUBA YA MHESHIMIWA MAKAMO WA KWANZA WA RAIS, MAALIM SEIF SHARIF HAMAD, ALIYOITAO KATIKA SIKU YA WACHANGIA DAMU DUNIANI TAREHE 14 JUNI 2011, NGOMBE KONGWE, ZANZIBAR .

Mheshimiwa Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya

Waheshimiwa Mawaziri na Viongozi mbali mbali wa Serikali

Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa

Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya

Waheshimiwa Wawakilishi

Waheshimiwa Mabalozi mnaowakilisha nchi mbali mbali

Waheshimiwa washirika wa maendeleo

Waheshimiwa wageni waalikwa, mabibi na mabwana

Assalaamu alaykum,

Hatunabudi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia Afya na Amani na kutuwezesha kuwa pamoja jioni hii ya leo ili kushuhudia tukio hili muhimu sana kwa afya na maisha yetu.

Kwanza kabisa kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar naanza kutoa shukurani zangu za dhati kwa wachangia damu wote hapa Zanzibar . Leo hii tumekusanyika hapa kuadhimisha siku yao duniani. Pongezi za wachangia damu zinaenda sambamba na kuishukuru Wizara ya Afya kwa kuchukuwa hatua muhimu sana ya kuipa uzito SIKU YA WACHANGIA DAMU DUNIANI.

Waheshimiwa waalikwa

Siku hii ni adhimu sana na inatambuliwa duniani kote. Kutambuliwa kwa siku hii kunakuja kutokana na umuhimu wake kwa afya, tiba na maisha ya binadamu. Kila binaadamu anaweza kuhitaji kutibiwa kwa kuongezwa damu, hivyo basi jambo hili linamgusa kila mmoja wetu, mwenye afya na siha njema vile vile aliemgonjwa. Inapokuja haja ya kutibiwa kwa kuchangiwa damu umuhimu wa wachangia damu unaonekana wazi. Kwani bila ya wachangia damu, tiba ya damu inaweza kuwa tabu au isiwezekane kabisa. Ili mtu mwenye kuhitaji damu aweze kupata nafuu ni lazima kupatiwa damu kwa wakati muafaka. Na ili damu iliyosalama iweze kupatikana kwa wakati, njia bora na ya haraka ni kupatikana kwa damu kupitia wachangiaji wa hiari.

Kwa ajili hii, sina budi kurejea kutoa pongezi za dhati na za kipekee kwa wachangia damu kwa khiari kwa nia ya kuokoa maisha ya wananchi wenzenu. Kitendo hiki ni kitendo cha Imani na ujasiri mkubwa usio kifani. Hasa ukizingatia kuwa wachangia damu kwa hiari wanajitokeza bila kujali damu hiyo atapewa mtu wa aina gani na wala kutegemea malipo yoyote ya kidunia. Malipo yenu yapo kwa Mungu na Inshaallah Mwenyezi Mungu awalipe kila lenye kheri, aziimarishe afya zenu na aziimarishe imani zenu muwe wachangiaji endelevu. Kwa kupitia juhudi zenu Taifa litaimarika na watu wake watakuwa na afya nzuri. Nachukua nafasi hii adhimu kuwapa jina la MASHUJAA wachangiaji damu wote.

Waheshimiwa wananchi

Kama tulivyokwisha elezwa ziko sababu nyingi zinazoweza kusababisha wagonjwa kuongezwa damu. Sababu hizi ni vigumu kuwa na hakika ya kuziepuka. Miongoni mwa sababu hizo zinazotajwa ni akina mama kutoka damu kwa wingi wakati wa kujifungua, ajali na operesheni za aina mbali mbali, upungufu wa damu kutokana na maradhi mbali mbali kama vile malaria, na nyengine nyingi.

Athari za vyanzo vya kupoteza damu zimejigawa kulingana na aina ya jamii inazoziathiri zaidi. Hili la kupoteza damu kwa wingi wakati wa kujifungua linachukua roho za akina mama wengi kwa hapa kwetu. Kwa upande mwengine vijana wengi, hasa wa kiume wanapoteza maisha yao kufuatia ajali zinazosababisha kupoteza damu kwa wingi. Upungufu wa damu ambao kwa kiasi kikubwa unasababishwa na lishe isiyokamili au maradhi, hasa malaria, inaongoza katika kutuweka wazazi katika hali ya wasiwasi wa afya na maisha ya watoto wetu wadogo, hasa chini ya miaka mitano. Hivyo basi kuwepo kwa utaratibu huu wa kukusanya damu kutoka kwa wachanginaji wa hiari utasaidia sana kupunguza vifo hivyo. Utaratibu huu unakubaliana kabisa na Dira ya Maendeleo ya Millenium ambapo lengo moja wapo ni kupunguza vifo vya akina mama na watoto.

Waheshimiwa wananchi

Kama ilivyoelezwa hapo awali Wizara ya Afya kwa kupitia Kituo cha Uchangiaji Damu imeanzisha Mpango wa Damu Salama. Wananchi wanaweza kujiuliza vipi damu inakuwa salama, hasa ukitilia maanani hadithi nyingi juu ya madhara yaliyowapata waliopokea damu hapo kabla. Naomba hapa niwatoe hofu kabisa juu ya hilo . Hivi sasa wanaopokea damu wapo salama. Mpango wa Damu Salama unahakikisha kwamba utoaji na upokeaji wa damu unaleta matokeo mazuri kwa pande zote mbili. Kwa kupitia mpango huu wa Damu Salama damu inakusanywa kwa utulivu na kufanyiwa vipimo vya hali ya juu hapa kutuoni. Wataalamu waliobobea wanaichunguza vema damu kabla ya kuhifadhiwa katika mahospitali kwa kusubiri watumiaji. Baadae damu iliyosafi na salama inasambazwa katika benki ya Hosipitali ili iwe tayari kutumika mara tu inapohitajika.

Tunapochangia damu mapema tunatoa fursa nzuri kwa uchunguzi huu wa damu na kuimarisha usalama wa damu inayotolewa kwa wagonjwa wetu.

Waheshimiwa wachangiaji damu na wageni waalikwa

Tukumbuke kuwa UKIMWI unabaki kuwa tishio kubwa katika dunia. Mpaka sasa hapa kwetu watu 6 kati ya kila watu 1000 (0.6%) wana UKIMWI. Na iwapo kama Serikali isingechukua hatua hii ya Damu Salama na hatua nyenginezo zifaazo basi UKIMWI ungeweza kukua kwa kasi kubwa sana . Hatua hii ina mchango mkubwa katika kudhibiti kasi ya ongezeko la maradhi haya thakili ya UKIMWI pamoja na maradhi mengine yanayoambuzikwa kwa njia ya damu kama vile homa ya ini (hepatitis) na kaswende (syphilis).

Waheshimiwa wageni waalikwa na wachangia damu kwa hiari

Kwa uapnde wa ukusanyaji damu, kama ilivyoelezwa makusanyo ya damu ya Unguja na Pemba yanatia moyo. Kuanzia mwaka 2009 karibu damu yote iliyokusanywa na kupimwa hapa kituoni imetokana na wachangiaji wa damu kwa hiari. Mafanikio haya yanatokana na kujitolea kwenu wachangaji damu. Hatuna budi ila kuiendeleza hali hii nzuri na ya kujivunia. Na ili kuiendeleza hali hii hatuna budi pia kuwa na wachangiaji wa hiari wengi na wa kudumu. Hapa natoa wito maalum kwenu enyi wachangiaji damu wa hiari kuwa MUENDELEE NA JAMBO HILI MUHIMU. Natoa wito kwa wananchi wengine wajitokeze kwa wingi kuanza kutoa damu kwa hiari.

****

Waheshimiwa wageni waalikwa

Kama ilivyotaarifiwa baadhi ya wananchi ambao ni wachangia damu wa kuendelea, wamejiunga pamoja na kuunda Jumuiya ya Wachangia Damu kwa Hiari Zanzibar (yaani JUWADAHIZ). Hii ni jumuiya muhimu sana katika kufanikisha suala hili la uchangiaji damu kwa hiari hapa kwetu Zanzibar . Jumuiya hii ikishirikaiana na Kituo cha Damu inasimamia uundaji wa vilabu vya uchangiaji damu (yaani “Donors Clubs”). Hili ni jambo la kupigiwa mfano kwani vilabu hivyo vitasaidia sana katika kuratibu shughuli za uchangiaji damu kwa wepesi na ufanisi zaidi. Panapokuwa na vilabu vilivyo madhubuti kiwango cha damu kinachohitajika ili kukidhi mahitaji ya kila siku na kujiwekea hakiba ya kutosha kitapatikana kwa haraka zaidi. Ndani ya vikundi hivi elimu juu ya uchangiaji damu salama unaojali afya ya mchangiaji na ya atakaepokea damu hutolewa. Lengo la wataalamu wa masuala ya damu ni kuongezeka afya na siha ya mchangiaji damu na atakaepokea damu hiyo. Ni wazi basi kujiunga katika vilabu hivyo kutapelekea kuwa na wachangiaji damu wa kudumu.

Waheshimiwa wananchi

Ili mtu awe mchangiaji damu wa kudumu ni lazima ajiangalie vizuri kiafya na aweze kuepukana na vitendo hatarishi ambayo vinaweza kupelekea kupata maambukizi kama vile UKIMWI, homa za maini, na maradhi mengine yanayohusika zaidi na damu. Kwa maana hiyo, kama tutakuwa na jamii kubwa ya wachangiajji damu endelevu basi tutaweza kuwa na sehemu kubwa ya jamii yenye afya nzuri. Kujitolea kuwa mchangiaji damu wa kudumu kwa maana nyengine ni kujiamulia kuwa na afya nzuri na maisha ya furaha. Nachukua fursa hii kutoa wito kwa wananchi wote kujiunga na jumuiya na vilabu hivi ili wajenge afya zao na waokoe maisha ya wengine.

Waheshimiwa

kila kinachoelea kimeundwa. Mafanikio haya katika huduma hii ya uchangiaji ni chombo kinachoelea vizuri hivi sasa, basi tukumbuke kuwa kimeundwa. Waundaji wa chombo hichi ni pamoja na wafanyakazi wa mpango huu wa Damu Salama. Wameunda. Wamecheza kwao. Ni lazima tuwapongeze. Tunawapongeza kwa shughuli ngumu wanayoifanya ya kushajihisha wananchi ili waweze kukusanya damu hapa kituoni na katika jamii. Wafanyakazi hawa wanachukua hatua za makusudi kuzipima damu kwa ufanisi ili zisiwe na viambukizi vya hatari kwa binaadamu mwengine. Tunawapongeza kwa jitihada zao za hali ya juu katika kuchunga afya za wachangiaji na wapokeaji damu na katika kufanikisha zoezi hili kiujumla. Tunajua kuwa, kama walivyo wafanyakazi wengine hapa nchini, mnafanyakazi katika hali ngumu – hili hatuwezi kulikataa wala kulipinga. Serikali yenu inalitafutia suluhisho.

Waheshimiwa waalikwa,

Natoa pongezi maalumu kwa Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mashirikiano yao makubwa katika Mpango wa Damu Salama kuhakikisha kuwa damu ya kutosha inapatikana wakati wote. Hawa ni mashujaa wetu.

Pamoja nao jambo hili la kuchangia damu linafanywa na mashujaa wengine kutoka katika maeneo mbali mbali. Miongoni mwao ni pamoja na wanafunzi wa sekondari, vyuo, taasisi za kidini, vilabu vya mpira, taasisi za sanaa, Jeshi la Wananchi Tanzania , taasisi mbali mbali za kiserikali na za kibinafsi na wananchi mmoja mmoja.

Waheshimiwa wananchi na wageni waalikwa,

Mafanikio yote haya ya shughuli hii ya uchangiaji damu kwa hiari yamepatikana kutokana na michango ya washiriki mbali mbali wa maendeleo, wa ndani ya nchi na wa kimataifa. Hatuna budi kuwashukuru washirika wetu wa maendeleo President Emergency Fund for Aids Releaf (PEPFAR) ya Marekani kwa kupitia Center for Disease Control (CDC) kwa msaada wao mkubwa wa kifedha na kihali katika ujenzi wa kituo hiki na uendeshaji wa shughuli za uchangiaji damu. Pia tunawapongeza kwa kuzipatia huduma hizi usimamizi mzuri wa kitaalamu kutoka kwa American Association of Blood Banks (AABB), University of Minnesota ya Marekani, Management Science for Health (MSH), na Phones for Health kwa kipindi chote ambacho huduma hizi zilianzishwa hapa Zanzibar na Tanzania Bara kiujumla.

Vile vile tunawapongeza washiriki wetu wengine wa maendeleo ambao wanahusika kwa njia moja au nyengine katika kuziboresha huduma hizi. Nao ni pamoja na DANIDA, Serikali ya Norway kupita FK Norway na Haukeland University , Serikali ya China , Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), pamoja na wengine ambao hapa hatujawataja lakini tunaelewa na kuthamini misaada yao . Tunawashukuru sana kwa misaada yao na mategemeo yetu ni kuwa tutakuwa na mashirikiano endelevu kuhakikisha kuwa haduma hizi zinaendelea na zitaendelea kuwa ubora wa hali ya juu.

Pia hatuna budi kupongeza makampuni ya kibinafsi ambayo yamejitokeza kujitolea ili huduma hizi ziwe bora na endelevu. Hizi ni pamoja na Zanair ambayo inatoa nafasi za bure za kusafirisha sampuli za damu kwa ajili ya kuzipima baina ya Unguja na Pemba , kampuni ya Zantel ambayo iliwahi kutoa msaada kipindi cha nyuma wakati wa siku ya wachangia damu, kampuni ya Zainab Bottlers na nyenginezo. Pia tunatoa pongezi kwa ZSSF kwa kwa michango yao kwa siku ya wachangia damu ya mwaka huu.

Tunatoa wito kwa wafanyabiashara wote na taasisi zote husika kuziunga mkono kwa njia moja au nyengine huduma za uchangiaji damu kwa khiari. Kufanya hivyo kutasaidia sana kuzifanya huduma hizi kuwa bora zaidi na endelevu.

Waheshimiwa wananchi

Ili tuweze kukidhi haja ya mahospitali yote ya Unguja na Pemba basi ni muhimu sana wananchi tujitokeze kwa wingi ili wakati wote tupate damu za kutosha. Serikali kupitia Wizara ya Afya inajitahidi kuhakikisha kuwa hospitali zote zinazotoa matibabu ya damu zina vifaa na umeme wa uhakika ili ziweze kutunza damu hizo katika mazingira yanayostahiki na kuweza kukidhi haja wakati wote damu inapohitajika. Sina budi kuipongeza Wizara ya Afya kwa juhudi zote kubwa katika kufanikisha hili na kuwatakia waendelee juhudi hizo na kuzidisha juhudi kwa lengo la mafanikio makubwa zaidi.

Na kwa hayo machache napenda kutoa wito kwa wananchi wote ambao afya zenu zinaruhusu mjiunge na wachangia damu ili muokoe maisha ya wale ndugu zetu ambao wamefikwa na matatizo na wanahitaji tiba ya damu.

Pia natoa wito kwa makundi mbali mbali, yakiwemo madhehebu mbali mbali ya kidini, waendelee kujitokeza kwa wingi na wawe wachangiaji wa damu wa kudumu.

Kauli mbiu ya mwaka huu inahimiza kujitokeza kwa wingi ili tuweze kuwa na damu ya kutosha kuokoa maisha ya wanohitaji tiba ya damu. Kauli hio inasema MORE BLOOD MORE LIVES yaani tuchangie damu kwa wingi tuokoe maisha ya wengi. Hivyo basi, mategemeo yetu ni kuwa wananchi ambao afya zenu zinaruhusu mtajitokeza kwa wingi kuchangia damu. Kwa taarifa tu hapo nje lipo basi la kisasa ambalo kazi yake ni kutoa huduma za uchangiaji damu. Hivyo natumai wengi wenu mtaanza kuchangia kuanzia leo. Na wale waliowahi kuchangia tunatoa wito kuwa waendelee kuchangia kila ambapo muda wao utafika.

Kwa mara nyengine tena napenda kuwapongeza wachangia damu wote kwa shughuli yao hii muhimu. Wao ni MASHUJAA na ushujaa huanza lakini haumaliziki.

Nakutakieni afya njema na muendelee kuwa wachangiaji damu wa kudumu.

CHANGIA DAMU OKOA MAISHA

TUCHANGIE DAMU KWA WINGI TUOKOE MAISHA YA WENGI.

Ahsanteni sana .

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s