Hatutapandishi kodi yeyote

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha wa 2011/2012 Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar inakusudia kutumia jumla ya shilingi bilioni 613 kwa mwaka wa fedha 2011-2012 huku kipaumbele kikiwekwa kwenye utekelezaji wa miradi ya jamii na kupunguza umasikini.
Sambamba na hilo serikali imetangaza kutopandisha kodi yoyote katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/12, na kuahidi kuimarisha zaidi usimamizi na ukusanyaji wa mapato kwa vianzio vilivyopo na kuziba mianya inayotumika katika kuepuka, kupunguza au kukwepa kulipa kodi pamoja na kuendelea kufatilia matumizi mabaya ya misamaha ya kodi nchini.

Akisoma muelekeo wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2011/12 Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi jana kwmaba mwelekeo wa bajeti ya mwaka huu umelenga katika mwelekeo wa uchumi wa dira ya maendeleo 2020, mpango wa kukuza uchumi MKUZA 11 pamoja na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi.
“Kwa mwaka wa fedha 2011/12 serikali haikusudii kupandisha kodi yoyote. Serikali inakusudia kuimarisha zaidi usimamizi na ukusanyaji wa mapato kwa vianzio vilivyopo na kuziba mianya” alisema waziri huyo.
Waziri huyo amesema lengo la kufanya hivyo ni kuona kuwa kabla ya kuongeza kodi, juhudi zinachukuliwa kwanza katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji na uwajibikaji wa ulipaji kwenye vianzio vilivyopo na kuhakikisha kuwa misamaha inayotolewa inatumika kwa dhamira iliyokusudiwa ili kudhibiti mapato ya serikali.

Aidha amesema kuwa katika juhudi nyengine za kuongeza na kuimarisha mapato, Serikali katika mwaka ujao itaanza kupokea marejesho ya kodi ya mapato ya mtu binafsi kwa wafanyakazi wa taasisi za Muungano wanaofanyakazi Zanzibar, hatua ambayo imekuja kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya SMZ na SMT katika juhudi za kushughulikia kero za Muungano.

Waziri huyo alisema serikali imeweka kipaumbele katika mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi pamoja na kutoa mikopo nafuu kwa wananchi ikiwemo wajasiriamali kwa lengo la kupunguza umasikini hapa nchini na kuhakikisha wananchi wanaishi katika maisha yasio na dhiki.

Mzee alisema serikali ya mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kukusanya jumla ya shilingi 12.08 bilioni ikilinganishwa na shilingi 444.64 bilioni , ikiwa ziada ya shilingi 168.44 bilioni sawa na asilimia 38. Ambapo serikali imeweka mikakati madhubuti katika kuongeza mapato yake ikiwemo kuziba mianya yote ambayo ilikuwa ikivujisha mapato hayo kupitia taasisi zake zinazokusanya mapato hapa Zanzibar.

Alisema hatua kali zitachukuliwa kwa watendaji watakaofanya vitendo vya makusudi vya kuvujisha mapato huku serikali ikichukuwa hatua zote za matumizi mabaya ya misamaha ya kodi.
Alisema serikali inakusudia kukusanya jumla ya shilingi 221.24 bilioni katika vyanzo vyake mbali mbali vya mapato vya ndani na jumla ya shilingi 10.22 bilioni zinatokana katika vyanzo vya kodi na shilingi 11.02 bilioni vyanzo visivyokuwa vya kodi.

Akizungumzia suala la Mamlaka ya Mapato Tanzania ( TRA) inakusudia kukusanya jumla ya shilingi 100.58 bilioni wakati bodi ya mapato ya Zanzibar ZRB inakusudia kukusanya jumla ya shilingi 120.66 bilioni. Aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba katika bajeti ya serikali ya mwaka 2011-2012 hakuna ongezeko la kodi katika bidhaa zinazotumiwa na wananchi.

Lengo ni kuendelea kujaribu kudhibiti mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa mbali mbali ambao umekuwa mzigo mkubwa kwa wananchi katika kumudu maisha yao ya kila siku huku mfumuko wa bei umeongezeka kutoka asilimia 6.1 katika mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 7.9.

Aidha Mzee alisema serikali ya mapinduzi ya zanzibar imepata misaada ya kibajeti (GBS) yenye jumla ya shilingi 30.28 bilioni ikiwa ni asilimia 4.5 ya misada ya kibajeti kupitia serikali ya Muungano.

Mzee aliwaambia wajumbe wa barza la wawakilishi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekusudia kuimarisha zao la karafuu ili kulifanya kuwa tegemeo kwa taifa pamoja na wakulima kwa ujumla, Alisema kiwango cha usafirishaji wa zao la karafuu kimeshuka kutoka tani 2,9000 katika mwaka jana hadi kufikia tani 2,000,wakati bei ya karafuu iliongezeka katika soko la dunia na kufikia dola za kimarekani 3,559.8 kwa tani na kufikia dola za kimarekani 3,591.4 kwa tani katika kipindi hicho ambapo ustawi wa zao la karafuu umeathirika sana kwa magendo yanayofanywa na watu ambao sio waaminifu.

Mikakati inayokusudiwa kutumiwa katika kuimarisha zao hilo ambalo Zanzibar katika miaka ya mwaka 1970 ilikuwa ikiongoza kwa uzalishaji wake katika soko la dunia ikiwemo kupanda mikarafuu mipya ni kuwatafutia soko la uhakika wakulima wa zao la karafuu ili wapate bei nzuri na hivyo kuongeza tija kwa wakulima, kazi ambayo imepewa wizara tatu ikiwemo wizara ya kilimo, wizara ya biashara na wizara ya fedha.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inakusudia kuimarisha kilimo cha mwani kwa wakulima wa mwambao wa pwani ili kiwe mkombozi kwa wananchi toafauti na ilivyo sasa ambapo uzalishaji wa zao la mwani umeshuka kutoka dola za kimarekani 264.4 kwa tani katika mwaka 2010 hadi kufikia dola za kimarekani 255.7 katika mwaka 2011.

Mzee alisema serikali inakusudia kuimarisha huduma za utumishi wa umma kwa watumishi wake nchini ikiwemo maslahi bora na katika mipango hiyo Serikali inakusudia kuongeza mishahara kwa watumishi wake katika mwaka huu wa fedha 2011-2012 baada ya kufanyika kwa mapitio na mapendekezo mapya kwa watumishi wa serikali.

Viwango vipya na taratibu zake zitatolewa na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambapo viwango vipya vimezingatia vigezo vya elimu alivyonavyo mtumishi pamoja na uzoefu wa kazi katika kipindi chote cha kuwepo kazini, Mzee alisema serikali ya mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuwasiliana na serikali ya Muungano kuliondosha suala la mafuta katika mambo yaliopo katika orodha ya Muungano ambapo alisema katika mikakati hiyo serikali ipo katika mipango yake ya kuchimba mafuta na gesi Zanzibar kama ilivyopanga awali.

“SMZ inaendelea na mipango yake ya kuchimba mafuta na gesi pamoja na kuwasiliana na serikali ya Muungano kuliondosha suala la mafuta na gesi katika orodha ya mambo yaMuungano na serikali inaendelea na mipangop yake kama ilivyopangwa awali” alisema Mzee na kushangiriwa na wajumbe wote.

Akizungumzia suala la maridhiano ambayo yameunda serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar Waziri huyo alsiema kuna mafanikio makubwa yaliopatikana kutokana na utulivu uliopo ambao alisema unahitaji kuendelezwa kwa nguvu zote ili Zanzibar ipige hatua za kimaendeleo.
Alisema tangu zanzibar kuingia katika mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa washiriki wa maendeleo wameonesha nia ya kusaidia huku wawekezaji mbali mbali wakipiga hodi kutaka kuwekeza katika miradi mbali mbali ya maendeleo na uchumi kutokana na usalama na amani uliopo na wazanzibari walivyoancha tofauti zao na kuonesha wana dhamira ya kweli ya kuelekea katika maendeleo ya kuijenga nchi yao.
“Hapa natoa ombi maalumu kwa wanancgi wa Zanzibar kwamba hii amani tuliyonayo kwa sasa tunalazimika kuienzi kwa nguvu zote kwani imejenga misingi ya mapenzi na amani na nchi wafadhili wamepata moyo sana kutusaidia wameonesha nia ya kutusaidia kutokana na hali ilivyo sasa, hatuna budi kuendeleza nchi yetu ili tufikie maendeleo tunayoyataka” alisema Mzee.
Kuhusu suala la mishahara Waziri huyo amesema kuwa Serikali tayari imeshafanya mapitio na kuandaa mapendekezo mapya ya mishahara ya watumishi wa umma, ambayo itaanza kutumika mwaka wa fedha 2011/2012.

Amesema kuwa viango hivyo vipya na taratibu zake zitatolewa na Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ambapo mapendekezo hayo ya mishahara mipya yamezingatia vigezo mbali mbali ikiwa ni pamoja na elimu aliyonayo mtumishi, uzoefu na muda aliofanyakazi.

Hata hivyo amesema kuwa mbali na hatua hizo zinazochukuliwa Serikali itakuwa ikiongeza maslahi ya watumishi wa umma kila mwaka pale hali ya uchumi na mapato ya Serikali itakapokuwa nzuri. Serikali ya Zanzibar katika mwaka wa fedha 2011/2012 inatarajia kutumia shilingi bilioni 613.08 ambapo kati ya fedha hizo mapato ya ndani yanakadiriwa kufikia shilingi bilioni 221.24 wakati ruzuku pamoja na mikopo kutokana na misaada ya washirika ya maendeleo ni shilingi bilioni 340.96.

Bajeti ya mwaka huu ni mwendelezo wa jitihada za Serikali katika kufikia maendeleo ya Mpango wa Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA), malengo ya maendeleo ya Milenia na hatimae dira ya maendeleo ya 2020.

Serikali ya imependekeza mbele ya wajumbe wa baraza la wawakilishi kukusanya jumla ya shilingi 613,076 millioni pamoja na matumizi ya shilingi 23,175 millioni kwa kazi za kawaida na shilingi 378,901 millioni kwa kazi za maendeleo.

Advertisements

2 responses to “Hatutapandishi kodi yeyote

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s