Sitakuelewa Dk Shein


Kwa hili sitakuelewa Dk Shein

Na Ally Saleh

Katikati ya wiki iliyopita waandishi wa habari tulialikkwa na Afisi ya
Umoja wa Mataifa iliyopo Zanzibar ili kukutana na uongozi huo katika
kile ambacho ni staftahi-habari ( hili ni neno ambalo nimelibuni kwa
maana ya kupata chai ya asubuhi lakini pia kupata habari).

Sababu ya staftahi-habari ile ilikuwa ni rahisi tu. Kwa kikombe cha
chai na kipande cha keki na sambusa unakutana na waandishi wa habari
bila gharama zaidi na kufikisha ujumbe wao kwao ili nawe ufikishiwe
kwa wananchi.

Hata jambo hili nobe Serikali ya Umoja wa Kitaifa haijalifanya wala
haijawzia kulifanya na huku Rais Dk Ali Muhammed Shein akihimiza
Serikali yake iwe wazi lakini hadi leo kwa kumbukumbu zangu ni Waziri
Ali Juma Shamhuna peke yake ambaye ndie aliiita waandishi wa habari
kuzungumza nao juu ya mambo mbali mbali ya Wizara yake.

Basi Mkurugenzi Mkuu wa Umoja wa Matifa kwa maana ya UNDP Bwana
Aliberic Kacou alitualika ili kutuarifu juu ya mabadiliko au tuseme
hatua mpya Umoja huo ambao sasa uanfanya kazi chini ya mwzmvuli mmoja
wa vitengo vyake, unakusudia kufanya katika kipindi cha 2011-2015.

Katika maelezo yake alielezea kuwa mpango wao utaweka vipa umbele
vyake kwa kutanguliza afya ambayo itatengewa asilimia 17, kisha eleimu
asilimia 14 na maeneo mengine kama ukuzaji uchumi, demokrasia na
utawala bora yakifuatia.

Nilimuuliza Bwana Kacou, jee ni kwa nini afya ikwekwa ndio kipaumbele
na sio sekta nyengine yoyote. Mkurugenzi Mkuu huyo alinipa maelezo
marefu ambapo mimi nikawa mbogo nikamwambia nataka maelezo mafupi tu
kwa nini afya ikawa mbele na sio chenginecho?

Kwa kweli tulishikana mashati kidogo katika hilo. Baadae akanieleza
kwamba hilo limefikiwa baada ya mashauriano, tena ya karibu kabisa,
baina ya wadau mbali mbali na Umoja wa Mataifa, jambo ambalo tokea
mwanzo nilijua ndivyo atavyonijibu.

Na kwa hakika nafsi yangu haikukubali wakati ule na hata wakati huu
kwmba kwa dhati yetu, sisi wadau tuliamua kuwa afya iwe mbele, na
mbele ikawekwa. Yeye hakunielewa hivyo, lakini mimi najua hilo halina
udhati.

Na kwa hakika haikuchukua muda hilo kujidhihirisha na naamini Kacou
anapaswa arudie tena mashauriano yake na wadau wake katika jamii ya
Zanzibar na Serikali ya Zanzibar juu ya vile vinavyoweza kuwa vipa
umbele vya uwekezaji wa UNDP katika harakati za maendeleo ya Zanzibar.

Hili limedhihrishwa na taarifa ya gazeti moja nchini kuw hospitali ya
Mnazi Mmoja, ambayo ni hosptiali ya rufaa kwa visiwa vya Unguja na
Pemba kwamba iko hoi bin taaban wakti Serikali yenyewe ina kipaumbele
cha afya katika mpango wake.

Taarifa zimesema kuwa kiwango kinachotakiwa kuiokoa hali mbaya iliopo
hivi sasa ni kiasi cha shillingi 80 millioni na hizo Serikali
haijazitoa hadi leo wakati hali inakuwa mbaya na tabaan kutahitajika
fedha kubwa zaidi iwapo hali hiyo itakabiliwa hapo baadae.

Kwa hakika kiasi cha shillingi 80 millioni ni kidogo kwa hali yoyote
ile kwa Serikali. Pia ni kidogo kwa kuwa zinahitajika katika sekta
nyeti ya afya ambayo pia ni sekta ambayo wenyewe tumeiambia UNDP kuwa
iwe ndio sekta kiongozi kwetu.

Pia haziwezi kuwa ziishinde Serikali kwa kuzipata kwa njia za dharura
hata iwapo zingeweza kutolewa kutoka mfuko mkuu wa Serikali, ikiwa ni
sekta kiongoiz tena katika hali ya dharura kama ambayo imejitokeza.

Lakini pia fedha hizo hazingeweza kushindkikana kupatikana wakati
tunajua kuwa fedha za kukarabati Ikulu ya Migombani zimepatikana
haraka, fedha za kukarabati nyumba ya Makamo wa Kwanza wa Rais
zilipatikana haraka.

Pia kila mwananchi ambaye amesikia habari kuwa shilllingi millioni 80
za kufanyia ukarabati Hospitaliya Rufaa ya Mnazi Mmoja zimekosekana
anajua kuwa viongozi wetu wa kitaifa wote watatu yaani Rais, Makamo wa
Kwanza na hata Makamo wa Pili wote wameshafanya ziara za nchi za nje.

Tunajua ukubwa wa msafara wa viongozi. Kuanzia kufuatana na wake zao,
mawaziri wao, wasaidizi wao na walinzi wao. Pia tunajua kuwa ni muhimu
wakae katika hoteli zenye uswalama ambazo kwa hakika ndizo ambazo zile
zilizoghali, mbali ya msururu wa matumizi ambao unaambatana na hadhi
ya viongozi.

Lakini pia tutamwambia vipi mtu kuwa Serikali inashindwa kupata
shillingi millioni 80 kukarabati hali mbaya ya Mnazi Mmoja wakati
tunajua kuwa Serikali ya Zanzibar imethubutu kununua msururu wa magari
ya kifakhari kwa ajili ya viongozi wanasiasa na viongozi watendaji,
tena kwa mkupuo mmoja.

Sasa angalau Hospitali ya Mnazi Mmoja imepata mtu wa kusemea, lakini
hakuna anaejua kuwa Kitengo cha Uzazi cha Hospitali ya Wete kiko
katika hali hoi pia na kinahitaji dharura kama ambayo inahitajika
Mnazi Mmoja.

Lakini kuhusu huko Wete Wazanzibari walio nje (Wazanje) wamejipanga
kinyume na Serikali. Ukitembelea mitandao ya Wazanzibari kama vile
http://www.zanzinet.net au http://www.mzalendo.net utaona jinsi ambavyo Wazanje hao
wanavyokamuana kwa kuchangishana visenti ili kukifanyia ukarabati
kitengo hicho.

Haipendezi na kwa hakika inachusha kuona kuwa utamaduni wetu wa
ukarabati na hata kushughulikia masuala ya dharura siku zote ni suala
lenye utata na ambalo halifanyiki mpaka hali tena iwe mbaya.

Sioni sababu kuwa shilingi millioni 80 zishindwe kupatikana, wengi
wetu tukijua mfumo wa kifedha wa Serikali unavyoweza kufanya kazi na
kwa hivyo kuweza kuhaulisha au kubinya vifungu ili kukabiliana na hali
hiyo ya dharura ambayo inahusu uhai wa wananchi.

Katika hili sitaki kabisa kulaumu ugeni wa Waziri na Naibu Waziri wa
Wizara hiyo kwa kuwa Wizara kama Wizara ilifanya wajibu wake kwa
kupeleka makisio yake Serikali, lakini naamini kinachotokea ni maamuzi
ya vipaumbele ambavyo Serikali inajipangia kwa muda mfupi na kwa muda
mrefu.

Katika hili siwezi kabisa kumuelewa Rais Dk Ali Muhammed Shein ikiwa
wiki hii hatafanya ziara ya dharura katika hospitali hiyo ili kufanya
tathmini yake mwenyewe juu ya hali ilivyo kwa kujua kuwa hiyo ndio
hospitali yetu kuu sisi wananchi.

Ningetaraji kuwa Dk. Shein atatumia nafasi yake kuwakutanisha viongozi
wa Wizara ya Afya na wa Wizara ya Fedha kuona suala la kupatikana
vijisenti hivyo vya shillingi millioni 80 vinapatikana bila ya
kungojea bajeti mpya, maana hii ni dharura.

Juzi juzi hapa kulipokuwa na dharura ya kuchomiwa vibanda vya biashara
watu walioko katika eneo la utalii la Pwani Mchangani, tuliona
Serikali ilivyohamia huko na jinsi ambavyo fedha zilipatikana kuwapa
ahueni waathirika.

Inatisha na ni aibu leo Serikali kuanikwa hadharani kwa tukio kama
hili la Mnazi Mmoja, jengo ambalo liko mbele ya macho ya Ikulu lakini
linapaswa kuwa mbele ya macho ya Rais na Serikali kwa maana ya afya ya
wananchi na jambo ambalo wadau na Serikali yenyewe wameiambia UNDP
kuwa ndio kipa umbele kikuu.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s