Serikali msiwe kama konokono


Kadhia ya moto Pwanimchangani ni matokeo

Kalamu ya Jabir Idrissa

NI Dk. Mohamed Gharib Bilal aliyenipa sababu ya kuendeleza mjadala wa kadhia ya moto Pwanimchangani.Nilikuwa nimetia tamati nilipojiridhisha kwamba ujumbe niliolenga ufike kwa serikali, umefika vizuri. Nimethibitishiwa viongozi wakuu na wasaidizi wao japo sijui idadi yao, wamesoma neno kwa neno.

Nia yangu ilikuwa kuelekeza ni vipi serikali inapaswa kutenda. Nashauri isitende kama mtu mwenye matende au konokono – kutembea polepole. Hapana. Serikali na hasa kipindi hiki ambacho wananchi wamejenga matumaini makubwa kwayo, lazima itembee haraka. Wengine waifuate.Kutembea kwa kasi kutahimiza wanaokufuata nao waamini katika kutenda vizuri, badala ya kutamka tu. Inatakiwa ijitahidi kuchukua hatua mapema kurekebisha kasoro mara tu inapojitokeza.

Isipofanya hivyo, inachelewesha ufanisi, inafinya utawala bora, inazorotesha maendeleo, na hapo itakuwa inachochea umasikini. Tukifika hapo, maana yake ile serikali iliyopewa imani na wananchi, imewaangusha wananchi hao.Dk. Bilal, kwa nafasi yake ya makamu wa rais wa Tanzania, amefika Pwanimchangani. Alipokutana na waathirika wa kadhia ya moto akawasilikiza, naye akasikilizwa.

Maelezo yake yalikuwa ya msisitizo kwamba serikali ya muungano na serikali ya mapinduzi Zanzibar, zitaharakisha taratibu za umilikaji wa ardhi ili kuwapatia waathirika sehemu za kudumu kwa ajili ya shughuli zao.Alisema, “Serikali inaendesha shughuli zake kwa kufuata katiba. Mtahudumiwa kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi, la msingi muwe wavumilivu. Kila mwananchi ana uhuru wa kufanya kazi mahali popote ilimradi tu havunji sheria na hakuna mwenye uwezo wa kumnyang’anya mwingine uhuru huo.”

Sawasawa. Kauli yake ni thabiti. Tatizo kwangu ni kwamba anatoa ahadi ninayodhani itakuja kusumbua serikali hasa Zanzibar.Dk. Bilal anatoa ahadi kwa mahitaji ambayo ni adimu sana. Ardhi kwa wananchi ili wajenge. Hili ni suala linaloleta mtafaruku serikalini. Ugawaji maeneo au viwanja kwa ajili ya shughuli za wananchi limekuwa tatizo kubwa Zanzibar.

Daktari anajua vizuri viwanja vilivyo mali sana Zanzibar. Anajua serikali ina deni kubwa kwa wananchi wengi ambao walivunjiwa nyumba zao kisheria na hawajalipwa fidia.
Anajua namna alipokuwa Waziri Kiongozi (1995-2000) yalitokea mengi yakiwemo ya kusikitisha na ambayo hadi sasa hayakurebishwa. Serikali iliyokuwa chini ya Dk. Salmin Amour Juma (Komandoo), ilivunja nyumba za wananchi eneo la Mtoni Kidatu pasina kulipa fidia yoyote.

Dk. Bilal anajua wananchi wale walivyovurugwa kimaisha. Labda alisikia baadaye kwamba baadhi ya waliovunjiwa nyumba, walifariki dunia siku zile.
Hebu aulize yuko wapi Mwalimu Omar, mwandishi wa habari aliyekuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi. Alikuwa na nyumba mbili eneo lile ambazo alijenga kwa shida akiwa mtumishi wa kawaida serikalini. Zote zilivunjwa.

Siku ya pili tu baada ya tukio, alipata kiharusi. Jitihada za kumsaidia apate nafuu zilishindikana. Haikuchukua muda alifariki dunia. Aliacha mke na watoto kadhaa ambao walikuwa wanakaribia kuhamia nyumba mpya Mtoni Kidatu. Walikuwa waondokane na madhila ya kupanga kwa miaka mingi.

Muda kabla ya uvunjaji, Omar alinihadithia matumaini yake ya kuhamia kwenye nyumba yake mpya. Kwa ile ya pili, alisema angeipangisha ili iwe kitegauchumi.Eneo lile limebaki msitu. Hakuna kilichofanyika. Walioathirika na janga lile hawakulipwa kitu. Na serikali ilieleza wazi kuwa haitalipa na ikathibitisha hivyo kwa kuvunja bila ya kulipa fidia wenyewe.

Nyumba zile zilijengwa wakati serikali inaona; haikuchukua hatua yoyote kuzuia ujenzi licha ya kueleza kuwa zilijengwa bila ya vibali halali vya kiserikali na kuendelea kuwepo kwake karibu na kituo cha umeme mkubwa, ni hatari inayochochea janga baadaye.

Utawala wa Dk. Salmin upo kwenye rekodi mbaya kuhusu matumizi ya ardhi. Haukuwahi kupima viwanja kwa ajili ya wananchi. Bali iliachia viongozi wagawane hadi maeneo yaliyokatwa eka tatu-tatu na kupewa wanyonge.Viongozi walichukua na kujigawia mpaka yaliyokuwa mashamba ya serikali maeneo ya Selem, Mkanyageni, Kizimbani na kwengineko.

Niliandika sana malalamiko ya wananchi wa Fuoni Kibondeni – na hawa wengi walitoka mikoa ya Tanzania Bara tangu miaka ya 1970 – waliokuwa wanaomba vibali vya kutumia ardhi waliyokuwa wakiishi.Walitaka ruhusa ya kujenga nyumba za kudumua kwa ajili ya kuishi na familia zao. Walinyimwa na kusisitizwa kwamba watumie kulima isipokuwa wasijenge nyumba za kudumu.

Wananchi wale walikuwa na familia zenye watoto wakubwa, wasichana na wavulana. Ilikuwa chusha kuishi katika vibanda vya makuti wakati wana uwezo wa kujenga nyumba nzuri. Walishindwa kwa sababu serikali iliwanyima vibali.Kabla ya uchaguzi mkuu 2010, ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi, chini ya maalim Abdalla Mwinyi Khamis, ilisimamia operesheni ya kuvunja nyumba za wananchi eneo la Tomondo.

Tukio lile lilikuwa la kuvunja sheria kwa sababu eneo lililodaiwa haramu kwa wananchi, lilikuwa na kesi na mahakama ilitoa amri ya kutofanyika uvunjaji mpaka uamuzi utakapotolewa. Hakuna simile, hakukuwa na fidia.Eneo la Kiwengwa na Pwanimchangani hakuna upimaji wa viwanja uliowahi kufanywa kwa miaka yote. Lakini wananchi waliomba zamani wapatiwe viwanja karibu na maeneo yaliyoko ufukweni. Walinyimwa.

Badala yake, wanashuhudia wakubwa katika serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiporomosha majumba ya fahari palepale wananchi wanapolilia kukatiwa viwanja.
Mwenendo huu umeendelea hadi serikali iliyotoka. Viongozi walinufaika sana na ardhi ya wananchi. waligawana viwanja kama ilivyothibitishwa na serikali yenyewe ndipo ikafuta ugawaji wa viwanja vilivyopimwa Tunguu.

Alichoanza kukipigia kelele Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, mara tu alipotulia ofisini baada ya kuteuliwa, ni matokeo ya ufisadi wa ardhi uliofanywa na viongozi wakuu na kuurithisha kwa waliokuwa chini yao.

Sasa ni ajabu kusikia katika wakati ambao wananchi mbalimbali wanahitaji viwanja vya kujenga nyumba, kiongozi wa ngazi ya juu kama Dk. Bilal anaahidi wajasiriamali walioko Pwanimchangani, eneo la makazi ya kudumu na la kuendesha biashara.
Nilitarajia ufumbuzi wa tatizo lao ukatafutwa kwa utaratibu ili kusije malalamiko kwamba serikali inabagua wananchi.

Iwapo kweli serikali imeamua kuwapatia viwanja, ijue inajitia kitanzi shingoni. Irudi kuzingatia mzigo wa deni la kuwapatia viwanja maelfu ya wananchi wakiwemo wale walioomba viwanja tangu miaka ya 1980.Hapo itaepuka lawama, shutuma na masimango. Hapo itakuwa imetenda haki sawa kwa wote kama katiba inavyohimiza. Ufumbuzi wa kudumu wa tatizo lolote unahitaji kupatikana kwa mipango endelevu na isiyojenga picha ya ubaguzi.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s